Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 2 July 2013

Mswahili wetu Leo; Da'Tolly Ben..Alianzia wapi na yeye ni Nani?


039
Naitwa Akii Tolly Chawachi,najulikana kama Tolly Ben.Mtoto wa sita wa Mchungaji Benjamin Chawachi na Mama mchungaji Hezeline Chawachi.Nimezaliwa kwenye familia iliyosimama katika nguzo ya kumcha Mungu,Upendo,Umoja ,amani na furaha.Nguzo hizi husimamisha maisha yangu.
Tangu nikiwa mtoto, ni mtu wa kufurahi na kucheka wakati wote.Nilijisika vibaya na kuumia nilipoona mtu akiwa na sura ya huzuni.Niliamini kila mtu anapaswa kuwa na furaha,na nilipata shida kuelewa kwanini watu wengine hawawi na furaha.
Muda wa chakula ulikua muda maalum sana kwa familia yetu.kila mtu alikaa mezani kwaajili ya chakula.Tulikula na kufuraia chakula , Baba na Mama siku zote walikuwa na mambo mengi ya kutusimulia na kutuambia ambayo yalifanya tucheke sana na kufurahi.Kila mtu aliupenda muda wa kula na kuungoja kwa hamu.
Ilijengeka kichwani kwangu kwamba wakati wa kula ni wakati wa kufurahi na kucheka.Jambo ambalo lilinijengea mapenzi na chakula na kunifanya nipende kupika na kula chakula kizuri.Sikupenda kula chakula ambacho hakinifurahishi.
Ingawa nilipenda kupika,  sikujua kwamba nilikua na uwezo mkubwa kwenye sanaa ya chakula hadi pale nilipofika kidato cha tatu na kuchagua kusoma somo la chakula na virutubisho kama somo la ziada. Ujuzi wa awali nilioutoa jikoni kwa mama yangu,na uwezo wangu mkubwa jikoni uliongezeka na kukua kwa kasi ndani ya miaka niliyosoma somo hilo. Nilifanya vizuri sana katika somo hilo na kupata alama “A”katika mtihani wa Taifa.
Nilipokua mtu mzima na kuanza kutembea na kula katika nyumba na familia za ndugu, jamaa na marafiki Niligundua ambavyo watu wengi hupungukiwa na ujuzi wa sanaa ya chakula na ufahamu wa virutubisho vya vyakula.Jambo ambalo linachangia familia zao kutokufurahia chakula.
Ili kukuza furaha ya chakula Katika familia za kitanzania,nilianzisha blog rasmi “TOLLYZKITCHEN’’kwa ajili ya kufundisha sanaa ya chakula ,lengo kuu likiwa ni kuwasaidia watanzania kuboresha mapishi yao nyumbani na kuwaelimisha juu ya virutubisho na lishe ili kuleta furaha na vicheko katika familia kila waketipo kula na kuboresha afya zao
Leo,Kupitia “TOLLYZKITCHEN” nawafikia,nawafundisha na kuwaelimisha maelfu ya Watanzania na watu wengine wazungumzao lugha ya Kiswahili kote duniani.


MALENGO
Moja:Kuboresha mapishi nyumbani
Ingawa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kwa vyakula vingi, Ufahamu na ujuzi wa kuandaa chakula Bora chenye ladha nzuri,muonekano wakuvutia na wingi wa virutubisho ni mdogo miongoni mwa watanzania.Jiko hili liko hapa kutatua tatizo hilo
Mbili:Kuielimisha jamii juu ya virutubisho vya chakula na umuhimu wake katika mwili.
Elimu ndogo juu virutubisho vya chakula na umuhimu wake katika mwili huwafanya watanzania wengi wale mlo usio kamili,hivyo kusababisha ukosefu wa virutubisho muhim mwilini na kua chanzo cha magonjwa mbalimbali katika jamii.jiko hili hutoa elimu juu ya virutubisho vya chakula na umuhim wake katika mwili.
Tatu:Kukuza matumizi ya bidhaa za chakula zilizosindikwa na kuzalishwa hapa nchini.
Tanzania ni nchi inayozalisha bidhaa nyingi za chakula,bidhaa hizo ni nyingi sana sokoni,lakini Watanzania wengi hupenda kununua na kutumia bidhaa za chakula zitokazo nje ya nchi.Jiko hili linawahimiza watanzania kutumia bidhaa za chakula za hapa nchini kwani bidhaa hozo ni bora na fresh kuliko zile zitokazo nje.
DIRA
Dira ya Tollyzkitchen ni kua jiko linalotoa elimu na mafunzo bora ya upishi,chakula na virutubisho,na kuboresha upishi na ulaji wa virutubisho sahihi vya chakula kwa watanzania na watu watumiao lugha ya Kiswahili.Kuona watanzania wakitumia bidhaa za chakula zinazozalishwa hapa nchini.
DHIMA
  • Kutoa Elimu na mafunzo ya upishi,chakula na lishe bora kwa kupitia,tovuti ,simu,redio ,runinga ,vitabu na mafunzo kwa vitendo.
  • Kutoa ushauri na maelekezo juu ya chakula na lishe kwa makundi maalum
  • Kutoa Elimu juu ya chakula na virutubisho kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ,kwa kushirikiana na taasisi za elimu
  • Kufundisha na kuelimisha jamii juu ya upishi,vyakula na lishe bora kwa kutumia michezo,mashindano,muziki na sanaa mbalimbali.
  • Kukuza na kuboresha matumizi ya bidhaa za chakula zinazozalishwa hapa nchini kwa kutoa elimu ya uelewa na utambuzi wa bidhaa bora za chakula.
kumjua/kujua kazi zake ingia;

     "Swahili NA Waswahili" Wanawake Na Maendeleo/Kujituma.

No comments: