Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 15 April 2016

Kisa cha Leo na Tweve Hezron



Bosi wangu alikuwa akitembelea gari nzuri sana na kila siku ilikuwa ni kazi yangu kumfungulia mlango na kumsalimia.

Lakini tokea niajiliwe na mke wake kuwa kama mlinzi pale kwao hakuwahi kupokea salamu yangu hata siku moja. Nilimuona ananidharau sana ila sikuwa na jinsi.

Siku moja wakati akitoka ndani aliniona nje nikitafuta kama kuna chakula kilichobaki katika dustbean. Lakini kama kawaida yake alinitizama mara moja akaendelea na shughuli zake.

Siku iliyofuata niliona mfuko wa rambo palepale kwenye zile dustbean (ndoo za takataka), ila mifuko ile ilikuwa misafi mno na ndani kulikuwa kuna chakula kizuri tu ambacho pasina shaka nilijua tu kitakuwa kimetoka supermarket.

Sikujiuliza ni nani ametupa me nilifurahi kukipata. Kila siku nikawa nikiona mfuko wa rambo hapo kwenye dustbean ukiwa na vyakula vizuri. Hii ikawa ni utaratibu wa kila siku. Nami sikuuliza ni nani amekuwa akiweka.

Jioni ninaporudi nyumban kwenye makazi duni niliyokuwa nikiishi na familia yangu, nilirudi nacho na nikawa nakula na kushare hicho chakula na familia yangu.

Nikashangaa sana ni nani mpumbavu ambae anatupa chakula kizuri kama kile kila siku? Ila nikajijibu mwenyewe kwamba kuna gepu kubwa sana kati ya masikini na tajiri, wala sikujihangaisha kuuliza.

Siku moja kulikuwa na tatizo kubwa mahala nilipokuwa nikifanya kazi. Niliambiwa kuwa bosi wangu amefariki. Kulikuwa na wageni wengi sana waliokuja pale nyumbani na siku hiyo sikupata chakula katika zile dustbean kama kawaida.

Hivyo nikajua labda mmoja wa wageni labda alikiona na akachukua. Ila hali hiyo ikaendelea kujitokeza baada ya shughuli za msiba kuisha na hata week zingine zilizoendelea sikupata kitu. Na nikaona hali imekuwa ngumu tena kuihudumia familia yangu chakula kwa kuwa nilishakuwa nimewazoesha kuwaletea kila jioni.

Hivyo nikaamua kumuomba mke wa marehemu bosi wangu kwamba aniongezee mshahara ama vinginevyo niache tu kazi maana hali ilikuwa ngumu.

Baada ya kumueleza hilo alilalamika kwanini sikulalamika suala la mshahara miaka miwili sasa imeshapita nije nilalamike leo, kwanini mshahara usitoshe leo? Nilimpa sababu nyingi ila hazikumshawishi hata kidogo.

Mwishoni nikaamua kumueleza ukweli, nikamueleza ishu nzima ya mimi kupata chakula cha bure pale kwenye dustbean na kwa jinsi gani kilinisupport kuilisha familia yangu. Pia nikamueleza kukikosa kwa muda sasa.

Akaniuliza ni lini ilikuwa mwisho wa kukipata hicho chakula katika dustbean? Nikamueleza kuwa baada ya kifo tu cha mumewe sikupata tena chakula.

Nikajiuliza kimyakimya mbele yake, Je inamaana bosi wangu ndio alikuwa akinikiwekea kile chakula kila siku? Hapana sidhani maana kwa jinsi alivyokua akinidharau kwa kutopokea salamu zangu asingekuwa na ubinadamu wa kunipa chakula.

Mke wa bosi wangu akaanza kulia, nikamuomba anyamaze na nikamuomba radhi kwa kumuomba aniongezee mshahara.

Mke wa bosi akaniambia, ninalia kwa sababu nimempata mtu wa saba ambae mume wangu alikuwa akimsaidia kumpa chakula fresh toka supermarket kila siku.

Nilikuwa najua mume wangu anawasaidia chakula watu saba wasiojiweza kila siku, ila nilipata kuwafahamu sita tu. Na siku zote nilikuwa nikitaka nimjue wa saba alikuwa nani ili niendelee kutoa huduma ambayo mume wangu amekuwa akiifanya. Nimefurahi kwa kuwa kumbe ndio wewe!

Kuanzia siku ile nikaanza kupokea chakula tena kama kawaida, ila safari hii mwanae wa kiume ndio alikuwa akituletea nyumbani.

Ila kila nilipokuwa nikimshukuru hakuwahi kunijibu! Kama baba yake tu!

Siku moja alinipa chakula pale nyumbani kwao nikamwambia AHSANTEE kwa sauti ya juu sana, akabaki ananishangaa. Mama yake akatoka nje akaniambia usijisikie vibaya akiwa hakujibu ni kiziwi kama baba yake alivyokuwa kiziwi. Akanieleza kuwa mumewe alikuwa ni bubu pia kiziwi na huyo mwanae nae yuko hivyohivyo.

Nilisikitika sana kwa jinsi nilivyokuwa nikiwawazia vibaya, tofauti na jinsi walivyo.

_______________________________________

Oh! Tumekuwa tukikosea mara nyingi sana kuwahukumu wenzetu bila kujua ni nini nyuma ya kile wanachokifanya. Kuwa na busara katika kuishi na wanadamu wenzako, huwezi jua kila mmoja wetu anapigana vita ngumu.

Kuwa makini, sio kila kitu unajitizama wewe peke yako kabla huja assume mambo ni bora ukauliza. Usikimbilie kutoa maamuzi kabla hujachunguza jambo, huenda siku ukaumia au kupatwa jambo lolote lile baya.

Matatizo mengi katika jamii zetu yanasababishwa na jinsi sisi wenyewe tunavyowachukulia wenzetu. Usihukumu hali fulani ambayo hujawahi kuipitia. Kuwa na busara ya kujifunza, huwezi kujua vyote.

Kuanzia leo tubadili fikra mbaya juu yetu na kwa wenzetu. Kuna vitu viwili katika hadithi hii mosi, usiamini kila unachoambiwa, chunguza zaidi. Na cha pili tambua kwamba kila mmoja unaekutana nae anapigana vita ambayo wewe huijui.

Hima, tuifanye Dunia kuwa mahala salama pa kuishi.

Share

Tweve Hezron

No comments: