Uasi wa binadamu
1Nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa porini walioumbwa na Mwenyezi-Mungu. Basi, nyoka akamwambia huyo mwanamke, “Ati Mungu alisema msile matunda ya mti wowote bustanini?” 2Mwanamke akamjibu huyo nyoka, “Twaweza kula matunda ya mti wowote bustanini; 3lakini Mungu alisema, ‘Msile matunda ya mti ulio katikati ya bustani, wala msiuguse, msije mkafa.’” 4Nyoka akamwambia mwanamke, “Hamtakufa! 5Mungu alisema hivyo kwa sababu anajua kwamba mkila matunda ya mti huo mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.”
6Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe, naye pia akala. 7Mara macho yao yakafumbuliwa, wakatambua kwamba wako uchi; hivyo wakajishonea majani ya mtini, wakajifanyia mavazi ya kiunoni.
8Jioni, wakati wa kupunga upepo, huyo mwanamume na mkewe wakasikia hatua za Mwenyezi-Mungu akitembea bustanini, nao wakajificha kati ya miti ya bustani, Mwenyezi-Mungu asipate kuwaona. 9Lakini Mwenyezi-Mungu akamwita huyo mwanamume, “Uko wapi?” 10Naye akamjibu, “Nimesikia hatua zako bustanini, nikaogopa na kujificha, maana nilikuwa uchi.” 11Mwenyezi-Mungu akamwuliza, “Nani aliyekuambia kwamba uko uchi? Je, umekula tunda la mti nililokuamuru usile?” 12Huyo mwanamume akajibu, “Mwanamke uliyenipa akae pamoja nami ndiye aliyenipa tunda la mti huo, nami nikala.”
13Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza huyo mwanamke, “Umefanya nini wewe?” Mwanamke akamjibu, “Nyoka alinidanganya, nami nikala.”
Adhabu
14Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia nyoka,
“Kwa kuwa umefanya hivyo,
umelaaniwa kuliko wanyama wote wa kufugwa,
na kuliko wanyama wote wa porini.
Kwa tumbo lako utatambaa,
na kula vumbi siku zote za maisha yako.
15Nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke,
kati ya uzawa wako na uzawa wake;
yeye atakiponda kichwa chako,
nawe utamwuma kisigino chake.”
16Kisha akamwambia mwanamke,
“Nitakuzidishia uchungu wa kuzaa,
kwa uchungu utazaa watoto.
Hata hivyo utakuwa na hamu na mumeo,
naye atakutawala.”
17Kisha akamwambia huyo mwanamume,
“Kwa kuwa wewe umemsikiliza mkeo,
ukala matunda ya mti ambayo nilikuamuru usile;
kwa hiyo, kwa kosa lako ardhi imelaaniwa.
Kwa jasho utajipatia humo riziki yako,
siku zote za maisha yako.
18Ardhi itakuzalia michongoma na magugu,
nawe itakubidi kula majani ya shambani.
19Kwa jasho lako utajipatia chakula
mpaka utakaporudi udongoni ulimotwaliwa;
maana wewe ni mavumbi, na mavumbini utarudi.”
20Adamu akampa mkewe jina “Hawa”, kwani alikuwa mama wa binadamu wote. 21Mwenyezi-Mungu akawatengenezea Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.
Adamu na Hawa wanafukuzwa bustanini
22Kisha Mwenyezi-Mungu akasema, “Sasa, binadamu amekuwa kama mmoja wetu, anajua mema na mabaya. Lazima kumzuia kula lile tunda la mti wa uhai, kwani akilila ataishi milele!” 23Basi, Mwenyezi-Mungu akamfukuza Adamu nje ya bustani ya Edeni, ili akailime ardhi ambamo alitwaliwa. 24Alimfukuza nje, na kuweka mlinzi upande wa mashariki wa bustani ya Edeni na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia iendayo kwenye mti wa uhai.
Mwanzo 3;1-24
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (BHN):
Jifunze zaidi"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment