Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 21 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 17...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwakuwa yeye ni mwema sana..

“Muwe tayari mmejifunga mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka; muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka harusini, ili wamfungulie mara atakapobisha. Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia. Hata kama atarudi usiku wa manane au alfajiri na kuwakuta wanakesha, heri yao watumishi hao! Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe. Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia.”
Asante Baba wa Mbinguni kwa Neema/Rehema hii kwa kutupa tena kibali cha kuendelea kuiona siku hii...
Tunaomba ikawe yenye Amani,Upendo,utuwema,Fadhili na Furaha..

Tunaomba ukaibariki katika yote,Maisha yetu tunayaweka mikononi mwako Baba wa Mbingu..
Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale na kutamalaki katika maisha yetu..Ukatuatamie na kututakasa Miili yetu na Akili zetu..
Ukatuokoe na yule Mwovu na kazi zake zote..
Ukatufunike na Damu ya mwanao mpendwa Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Utusamehe Baba pale tulipokwenda kinyume nawe kwakuwaza,kunena,kutenda,kwakujua,kutojua..

Mfalme wa Aamni ukatupe neema yakuweza kuwasamehe nasi waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Baba wa Mbingu tunaomba ukawaponye na kuwagusa wote wanaopitia Magaumu/majaribu mbalimbali,shida/tabu,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao..
Mkono wako ukawaguse na kuwaponya wote wanaogua moyoni kwa kisasi,kutosamehe,wivu,chuki,kuumizwa,wametendwa vibaya na Imani yao imepotea,Mashaka,Hofu na kutaka kujitoa uhai..Mungu Baba ukawape uponyaji na Amani ya moyo..
Mungu Baba ukawaponye na kuwaongoza  wale ambao kila wanalolifanya halifanikiwi..Ikiwa kazi,Biashara,Masomo..
Wenye Laana,Mikosi,kukataliwa,kutengwa na kunyanyaswa kimwili na kiroho pia..
Tunaomba Baba ukaonekane nao wapate kupona na kujua wewe ni Mungu mwenye Upendo,Haki na ni Mungu wa masikini,Mtajiri na wote wanaokutegemea wewe wapo huru..
Neema yako na Fadhili zako zatutosha Baba..Hakuna kama wewe na hata kuwepo..wewe ukisema ndiyo nani aseme hapana?
Kukutegemea wewe kuna faida kubwa,Amani na Imani,Furaha na Upendo wa kweli vipo nawe Jehovah..!!

Sifa na Utukutufu ni wako Daima..Tunashukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu Leo kesho na hata Milele..
Amina..!!

3Mtumainie Mwenyezi-Mungu na kutenda mema,
upate kuishi katika nchi na kuwa salama.
4Uitafute furaha yako kwa Mwenyezi-Mungu,
naye atakujalia unayotamani moyoni.
5Mkabidhi Mwenyezi-Mungu maisha yako;
mtumainie yeye naye atafanya kitu.
6Ataufanya wema wako ungae kama mwanga,
na uadilifu wako kama jua la adhuhuri.[Zaburi 37;3-6]

Wote mliopita hapa nawatakia Amani na Asanteni sana..
Mungu aendelee kuwabariki katika yote yaliyo mema..
Nawapenda.



Maji kutoka mwambani
(Hes 20:1-13)

1Kutoka jangwa la Sini, jumuiya yote ya Waisraeli ilisafiri hatua kwa hatua kama alivyoamuru Mwenyezi-Mungu, watu wakapiga kambi huko Refidimu. Lakini huko hakukuwa na maji ya kunywa. 2Kwa hiyo watu wakamnungunikia Mose wakisema, “Tupe maji ya kunywa.” Mose akawauliza, “Mbona mnaninungunikia? Mbona mnamjaribu Mwenyezi-Mungu?” 3Lakini wote walikuwa na kiu, wakamnungunikia Mose wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri utuue kwa kiu sisi sote na watoto wetu na mifugo yetu?”
4Basi, Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu akisema, “Nitawafanyia nini watu hawa? Wako karibu kunipiga mawe!” 5Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Pita mbele ya watu hawa ukiwachukua wazee wao kadhaa; chukua pia mkononi mwako ile fimbo uliyoipiga nayo mto Nili. 6Tazama mimi nitasimama mbele yako mwambani pale Horebu, nawe utaupiga huo mwamba na maji yatabubujika kutoka humo ili watu wote wapate kunywa.” Basi, Mose akafanya hivyo mbele ya wazee wa Waisraeli. 7Mahali hapo Mose akapaita “Masa”17:7 Masa: Kiebrania maana yake: Jaribu. na “Meriba”,17:7 Meriba: Kiebrania maana yake: Kunung'unika. kwa sababu Waisraeli walimnungunikia na kumjaribu Mwenyezi-Mungu wakisema, “Je, kweli Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi?”

Vita na Waamaleki
8Waamaleki walikuja na kupigana na Waisraeli huko Refidimu. 9Mose akamwambia Yoshua, “Chagua wanaume uende ukapigane na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilele cha kilima, nikiishika mkononi mwangu ile fimbo ya Mungu.” 10Basi, Yoshua akafanya kama Mose alivyosema, akaenda kupigana na Waamaleki. Mose, Aroni na Huri wakapanda kilele cha kilima. 11Ikawa wakati wote Mose alipoinua mkono wake juu, Waisraeli walishinda, na alipouteremsha, Waamaleki walishinda. 12Lakini baada ya muda, mikono ya Mose ilichoka. Kwa hiyo Aroni na Huri walichukua jiwe wakaliweka karibu na Mose naye akaketi. Kisha wakaishika na kuiinua mikono yake, mmoja akauinua mkono wa kulia na mwingine mkono wa kushoto. Hivyo mikono ya Mose ikabaki imara ikiwa imeinuliwa juu hadi jua lilipotua. 13Yoshua akawakatakata Waamaleki.
14 Taz Kumb 25:17-19; 1Sam 15:2-9 Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Liandike jambo hili katika kitabu, liwe ukumbusho. Tena kariri masikioni mwa Yoshua kwamba nitawafuta kabisa Waamaleki duniani.” 15Mose akajenga madhabahu na kuiita, “Mwenyezi-Mungu ni Bendera Yangu”,17:15 Mwenyezi-Mungu … Yangu: Kiebrania “Yahweh-nisi.” 16akisema, “Inueni juu bendera ya Mwenyezi-Mungu!17:16 Inueni … ya Mwenyezi-Mungu: Makala ya Kiebrania si dhahiri. Mwenyezi-Mungu atapigana na Waamaleki kizazi hata kizazi!”
Kutoka17;1-16

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: