Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 24 April 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 18...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Ni siku nyingine tena Mungu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii..Tunamshukuru Mungu katika yote,ametulinda wiki nzima na usiku umepita, tumeamka tena..Asante kwa Neema/Rehema hii..
Tazama Jana imepita Baba Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine Jehovah..
Tunakuja mbele zako na tukijinyenyekeza, Tukishukuru na kukusifu Daima..
Tunaomba ukatulinde,ukatuponye,ukatutakase na kutufunika kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti.Maisha yetu yawe mikononi mwako Yahweh..
Roho Mtakatifu akatuongoze kwenye Kunena/kutenda na tukawe na kiasi..
Baba ukabariki kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba ukavitakase kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Baba ukabariki Vilaji /vinywaji tuingiapo/tutokapo,tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..

Baba tazama wenye Shida/Tabu,Wanaopitia magumu/majaribu,Wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao..Tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu na ukawaponye na kuwaokoa wapate kupona kimwili na kiroho pia..
Jehovah..Utusamehe pale tulipo kwenda kinyume nawe..kwakujua/kutojua,kwakunena/kwakutenda,kwakuwaza..
Baba tunaomba nasi ukatupe Neema ya kuweza kuwasamehe wote waliotukosea..
Tunakwenda kinyume na yule Mwovu na kazi zake zote..

Baba ukatuokoe na kutulinda katika safari yetu ya maisha..
tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Baba tunaiweka Nchi hii tunayoishi mikononi mwako..Ukaibariki na kutubariki wote tunaoishi humu..ukawe mlinzi mkuu na ukatawale katika yote..
Tunaiweka Tanzania na watanzania wote  mikononi mwako ukawabariki na kuwabariki watu wake popote walipo..ukaonekane juu yao.. ukawe mtalawa mkuu..
Afrika na Dunia nzima iwe mikononi mwako, ukawe mtawala mkuu na ukawaongoze wanaotuongoza wakatuongoze katika haki kweli.
Tazama watoto wetu Leo wamerudi shule Baba ukaonekane kwenye masomo yako..wapate kuelewa na kukumbuka yote wanayofundishwa..

Ukawalinde katika ujana wao na wakawe na hofu yako Mungu..
waje kuwa watu wema mbele zako na jamii pia.
Neema yako yatutosha Yahweh..Furaha na Amani vipo kwako, Upendo wa kweli una wewe..Fadhili na wema ukokwako Jehovah..Uzima wa milele unapatikana kwako Mungu wetu, Muumba wetu, Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!!
Tunayaweka haya yote mikononi mwako.. tunakuabudu na Kuamini  wewe ni Mungu wetu na hatuna Mungu mwingine Leo kesho na hata Milele..
Amina..!
Asante kwa wote mliopita hapa natumaini hamtotoka watupu..
Mungu aendelee kuwaBariki..
Nawapenda.


Yethro anamtembelea Mose
(Kumb 1:9-18)
1Yethro, kuhani wa Midiani, baba mkwe wa Mose, alisikia juu ya mambo yote ambayo Mwenyezi-Mungu alimtendea Mose na Waisraeli alipowatoa katika nchi ya Misri. 2Taz Kut 2:21-22 Kwa hiyo Yethro, akiwa na Sipora, mkewe Mose, ambaye Mose alikuwa amemrudisha kwa baba yake, alimwendea Mose, 3Taz Mate 7:29 pamoja na watoto wawili wa Mose. Mtoto wa kwanza aliitwa Gershomu. Mose alimpa jina hili kwa vile alisema, “Nimekimbilia18:3 Nimekimbilia: Au nimekuwa mgeni, au mkimbizi Kiebrania: Ger. katika nchi ya kigeni.” 4Wa pili aliitwa Eliezeri,18:4 Eliezeri: Kiebrania “Eli” maana yake “Mungu wangu,” na “ezeri” maana yake “msaada.” kwa vile Mose alisema, “Mungu wa baba yangu ndiye aliyenisaidia nisiuawe na Farao.”
5Yethro, mkwewe Mose, alikuja pamoja na binti yake, yaani mkewe Mose, pamoja na watoto, akamkuta Mose jangwani alikokuwa amepiga kambi kwenye mlima wa Mungu. 6Mose alipoambiwa kuwa baba mkwe wake pamoja na mkewe na wanawe wawili wanakuja, 7alitoka kwenda kumlaki baba mkwe wake, akamwinamia na kumbusu. Wakasalimiana, kisha wakaingia hemani. 8Mose akamweleza mkwewe mambo yote Mwenyezi-Mungu aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Waisraeli. Alimwambia pia juu ya shida zote zilizowapata safarini na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaokoa. 9Yethro akafurahishwa na yote aliyotenda Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Waisraeli, kwa kuwaokoa mikononi mwa Wamisri. 10Yethro akasema, “Na atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewaokoa mikononi mwa Wamisri na kutoka utumwa wa Farao. 11Sasa najua kwamba Mwenyezi-Mungu ni mkuu kuliko miungu yote, kwani amewakomboa watu hawa mikononi mwa Wamisri ambao waliwatendea ujeuri.” 12Hapo Yethro, baba mkwe wa Mose, akamtolea Mungu sadaka za kuteketezwa na tambiko. Naye Aroni akaja pamoja na wazee wa Israeli ili kula chakula pamoja na Yethro, mbele ya Mwenyezi-Mungu.

Kuteuliwa kwa waamuzi
(Kumb 1:9-18)

13Kesho yake, Mose aliketi kuamua matatizo ya Waisraeli, nao wakasimama wakiwa wamemzunguka, tangu asubuhi mpaka jioni. 14Yethro, baba mkwe wa Mose, alipoyaona mambo yote ambayo Mose aliwafanyia Waisraeli, alimwuliza, “Kwa nini unawafanyia watu mambo haya? Mbona unaketi peke yako huku watu wamekuzunguka tangu asubuhi mpaka jioni?” 15Mose akamjibu mkwewe, “Kwa sababu watu huja kwangu kuuliza matakwa ya Mungu. 16Wakiwa na ugomvi wowote ule wao huja kwangu nami huamua kati ya mtu na mwenzake, na kuwafunza amri za Mungu na maamuzi yake.” 17Basi, Yethro akamwambia Mose, “Unavyofanya si vizuri! 18Utajidhuru mwenyewe na hawa watu kwa uchovu, kwani hii ni kazi ngumu usiyoweza kuifanya peke yako. 19Sikiliza shauri langu kwako, na Mungu awe pamoja nawe. Wewe utawawakilisha watu mbele ya Mungu na kumletea Mungu matatizo yao. 20Hali kadhalika utawafundisha amri na maamuzi ya Mungu na kuwaonesha jinsi inavyowapasa kuishi na kufanya. 21Lakini kuhusu mambo mengine, chagua miongoni mwa watu wote, watu wanaostahili, watu wanaomcha Mungu, waaminifu na wanaochukia kuhongwa. Wape hao mamlaka, wawe na jukumu la kuwasimamia watu katika makundi ya watu elfu, mia, hamsini na kumikumi. 22Hao ndio watakaokuwa na vikao kila siku kutatua matatizo ya watu. Matatizo magumu watakuletea wewe, lakini yale madogomadogo watayaamua wenyewe. Kwa njia hiyo utaweza kurahisisha kazi yako kwa vile watashirikiana nawe katika jukumu hilo. 23Ukifanya hivyo, na kama ndivyo atakavyo Mungu, utaweza kustahimili na watu hawa wote wataweza kurudi makwao kwa amani.”
24Mose alilisikiliza shauri hilo la mkwewe na kufanya kama alivyoshauriwa. 25Basi, akawateua watu wenye uwezo kati ya Waisraeli, akawafanya kuwa viongozi wa makundi ya watu elfu, watu mia, watu hamsini na watu kumikumi. 26Nao wakawa wanaamua matatizo ya watu kila wakati. Matatizo magumu walimletea Mose, lakini yale madogomadogo waliyatatua wao wenyewe. 27Baada ya kufanya hivyo, Mose na mkwewe wakaagana naye Yethro akarudi nchini kwake.
Kutoka18;1-27

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: