Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 4 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 26...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Mungu wetu yu mwema sana..Tumshukuru na kulisifu jina lake..
kwa maana pasipo yeye sisi si kitu kabisa..

Asante Baba wa Mbinguni kwa kutulinda usiku mzima na kutuamsha salama..Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tazama Jana imepita Baba Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine..
Tunashuka mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Jehovah...!
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua au kutojua Mfalme wa Amani..

Tunaomba utupe nasi Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..

Yahweh..! Tunaomba utulinde na kutuokoa na yule mwovu na kazi zake zote..

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Tunaomba ututakase Miili yetu na Akili zetu na kutufunika na Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Jehovah..! Tunaomba ukabariki Ridhiki zetu ziingiazo na zitokazo..zikawe baraka na tuweze kuwabariki na wengine wenye kuhitaji..
Mungu wetu tunaomba ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo,Vilaji/vinywaji,vyombo vya usafiri, tuingiapo/tutokapo,na tumbeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..!!


Baba tazama Yatima,Wajane,wenye shida/tabu,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,wanaogua rohoni,wagonjwa,wafiwa ukawe mfariji wao,waliokatika vifungo mbalimbali Baba tunaomba ukawafungue na kuwagusa na mkono wako wenye nguvu,ukawaponye kimwili na kiroho pia,ukaonekane kwenye shida zao Jehovah..!Ukasikie kulia kwao na ukapokee maombi yao,ukawanyanyue na kuwaongoza, ukawabariki na kuwafariji Yahweh..!!

Ndugu yangu mpendwa makabidhi Mungu shida zako yeye hatokuacha kamwe,Yeye anakujua zaidi ya yeyote,hakuna lililogumu kwakwe, Yeye hachoki binadamu anaweza kukuchoka na kukusimanga, binadamu anaweza kukuumiza zaidi,binadamu anaweza kukukwamisha zaidi,binadamu anaweza asikuelewe na kukuona mzigo,binadamu anaweza kukukatisha tamaa zaidi, binadamu anaweza asipende kuona maendeleo yako,Yupo mponyaji wa kweli, yeye anayependa na kufurahia maendeleo yako,yeye hufurahi zaidi ukimrudia na husamehe kabisa, Ukimwamini Mungu yote yanawezekana..Mtafute anapatikana,Mwite ataitika,Muombe atajibu, Muite atasikia..Kwa Mkono wake wenye nguvu atakugusa na kukubariki..


Tumtukuze Mungu wetu kwa nafasi tuliyonayo..
Kama muimbaji Muimbie na kumsifu kupitia uimbaji wako,kama mfinyanzi finyanga vyungu vya kuwekea maua tukapambe nyumba yake,Mungu ametupa vipawa tofauti, hakuna kidogo mbele zake..
hivyo ulivyo kuna karama Mungu amekupa, kwako unaweza  kuona ni ndogo lakini mbele za Mungu ni fahari na anamakusudi yake..Itumie vyema na kwa hiyari yako pasipo kulazimishwa..

Mwili una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake. Hali kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila mmoja ni kiungo cha mwenzake. Basi, tunavyo vipaji mbalimbali kadiri ya neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha unabii na akitumie kadiri ya imani yake. Mwenye kipaji cha utumishi na atumikie. Mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe. Mwenye kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.

Tukawe barua njema na tusomeke vyema..sawasawa na mapenzi yake..
Sifa na utukufu tumrudishie Mungu wetu,Tunayaweka haya yote mikononi mwako Baba wa Mbinguni..

Tukishukuru na kuamini wewe ni Mungu wetu Leo na hata milele..
Amina..!

Mungu akawaguse na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake,msipungukiwe katika mahitaji yenu na muweze kuwabariki na wengine..
Asanteni sana kwakupita hapa Mungu awabariki mno..
Nawapenda.



Hema la mkutano

(Kut 36:8-38)

1“Zaidi ya hayo yote, utatengeneza hema takatifu kwa mapazia kumi ya kitani safi iliyosokotwa, na kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu. Mapazia hayo utayapamba kwa michoro ya viumbe wenye mabawa waliotariziwa. 2Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 12 na upana wa mita 2. Mapazia hayo yawe ya kipimo kimoja. 3Utaunganisha mapazia matano yawe kipande kimoja na mapazia mengine matano yawe kipande cha pili. 4Utashonea vitanzi vya buluu upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, hali kadhalika utashonea vitanzi mwishoni mwa pindo la nje la kipande kingine cha pazia. 5Utatia vitanzi hamsini katika pazia moja na vitanzi vingine hamsini kwenye utepe wa pazia la pili; vitanzi vyote vielekeane. 6Kisha utatengeneza kulabu hamsini za dhahabu ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia, hivyo hema litakuwa kitu kimoja.
7“Pia utatengeneza kifuniko cha hema kwa mapazia kumi na moja ya manyoya ya mbuzi. 8Kila pazia litakuwa na urefu wa mita 13, na upana wa mita 2. Mapazia yote hayo 11 yatakuwa na kipimo kilekile. 9Utaunga mapazia matano pamoja, na mapazia sita pamoja. Pazia la sita utalikunja mara mbili mbele ya hema. 10Kisha utafanya vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha kwanza, na vitanzi hamsini upindoni mwa pazia la mwisho la kipande cha pili. 11Utatengeneza kulabu hamsini za shaba na kuziingiza katika vile vitanzi hamsini ili kuunganishia vile vipande viwili vya mapazia na hivyo kufanya pazia moja la hema. 12Ile nusu ya pazia iliyobaki utaitundika upande wa nyuma wa hema. 13Nusu mita ya urefu wa mapazia iliyo ya ziada utaikunja ininginie pande zote mbavuni mwa hema ili kulifunika. 14Utatengeneza pia kifuniko kingine cha hema kilichofanywa kwa ngozi laini ya kondoo dume na ngozi laini ya mbuzi.
15“Utatengeneza mbao za mjohoro za kusimama wima kwa ajili ya hema. 16Kila ubao utakuwa na urefu wa mita 4, na upana wa sentimita 66. 17Kila ubao utakuwa na ndimi mbili za kuunganishia. Utazifanyia mbao zote ndimi mbili. 18Basi, utatengeneza hizo mbao za hema hivi: Mbao ishirini kwa ajili ya upande wa kusini, 19na vikalio arubaini vya fedha chini ya hizo mbao ishirini, vikalio viwili chini kwa kila ubao ili kushikilia zile ndimi zake mbili na vikalio viwili viwe chini ya ubao mwingine ili kushikilia zile ndimi zake mbili. 20Upande wa kaskazini wa hema, utatengeneza mbao ishirini, 21na vikalio vyake arubaini vya fedha, vikalio viwili chini ya kila ubao. 22Kwa upande wa nyuma, ulio magharibi ya hema, utatengeneza mbao sita. 23Utatengeneza pia mbao mbili kwa ajili ya pembe za hema upande wake wa nyuma. 24Mbao hizo za pembeni ziachane chini lakini zishikamanishwe kwa juu kwenye pete ya kwanza. Mbao zote za pembeni zifanywe vivyo hivyo ili zifanye pembe mbili. 25Hivyo kutakuwa na mbao nane pamoja na vikalio vyake kumi na sita vya fedha: Vikalio viwili chini ya kila mbao na vikalio viwili chini ya ubao mwingine.
26“Utatengeneza pau za mjohoro; pau tano kwa ajili ya mbao za upande mmoja wa hema, 27na pau tano kwa ajili ya upande wa pili wa hema, na pau tano kwa ajili ya mbao za upande wa nyuma wa hema, ulio magharibi. 28Upau wa katikati uliofika nusu ya jengo la hema utapenya katikati toka mwisho huu hadi mwisho mwingine wa hema. 29Mbao zote utazipaka dhahabu na kuzifanyia pete za dhahabu zitakazoshikilia hizo pau, ambazo pia utazipaka dhahabu. 30Hivyo utalitengeneza hema hilo kulingana na mfano niliokuonesha mlimani.
31“Utatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu na kitani safi iliyosokotwa. Pazia hilo utalitarizi kwa ustadi kwa viumbe wenye mabawa. 32Utalitundika pazia kwenye nguzo nne za mjohoro zilizopakwa dhahabu, zenye kulabu za dhahabu na vikalio vinne vya fedha. 33Taz Ebr 6:19; 9:3-5 Utalitundika pazia hilo kwenye vifungo, kisha ulilete lile sanduku la ushuhuda humo ndani kukiwa na vibao viwili vya mawe, nyuma ya pazia hilo. Pazia hilo litatenga mahali patakatifu na mahali patakatifu sana. 34Ndani ya mahali patakatifu utakiweka kile kiti cha rehema juu ya sanduku la maamuzi. 35Ile meza ya mjohoro utaiweka upande wa nje wa pazia hilo, na kile kinara cha taa utakiweka upande wa kusini wa hema, mkabala wa meza. Meza hiyo itakuwa upande wa kaskazini.
36“Kwa ajili ya mlango wa hema utatengeneza pazia zito kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, na kutariziwa vizuri. 37Vilevile utatengeneza nguzo tano za mjohoro na kuzipaka dhahabu. Nguzo hizo zitakuwa na kulabu za dhahabu, na kila moja itakuwa na tako la shaba.

Kutoka26;1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

2 comments:

Jarusinga said...

Makala nzuri sana.Nimefaidika pakubwa.Naomba uchapishe makala nyingine!
baraka tele.(kiswahili.uonbi.ac.ke)

Rachel Siwa said...

Ameen..!!
Sifa na Utukufu tumrudishie Mungu wetu..
Asante kwa kutembelea..
Mungu aendelee kukubariki;Ndugu @Jarusinga.