Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 12 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 31...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu kwa mema yote aliyotutendea na anayoendelea kututendea..
Tunakushukuru Mungu wetu  kwa wema na fadhili zako, umetulinda usiku kucha na kutuamsha salama, Umetuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani..Mungu wetu, Nuru na mwanga wetu,Jehova nissi..!, Jehovah shammah..!, Jehovah rapha..!, Jehovah Shalom..!,Jehovah rohi..!,Jehovah jireh..!Mungu unayeponya, Mungu unayetenda, Mungu unayejibu, Mungu unayebariki na wewe ni Mungu wa Rehema..

Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe, kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.
Baba nasi ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea.

ukatupe macho ya rohoni tupate kutambua/kujitambua..tukawe na 
  hekima,busara,utuwema,upendo wa kweli na upole kiasi..
tuweze kuachilia na kuchukuliana..
Utuepeshe na chuki,hasira na kisasi, makwazo na kukwaza wengine..

Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha. Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa. Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, muonye; akitubu, msamehe. Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema, ‘Nimetubu,’ lazima umsamehe.”
Roho Mtakatifu akatuongoze na tukawe na kiasi..

Baba wa Mbinguni tunaiweka siku hii na maisha yetu mikononi mwako, tunaomba ukaibariki na kutubariki katika yote tunayoenda kufanya/kutenda, ukatuongoze na kutulinda, ukatutakase Miili yetu na Akili zetu na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa mbinguni ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti.. Yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..
Kwa imani na tumaini la kweli tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Sifa na utukufu ni wako Baba wa Mbinguni,Tunashukuru na kuku abudu siku zote za maisha yetu,,Ehh Mungu utuongoze..


Msifuni Mwenyezi-Mungu! Umsifu Mwenyezi-Mungu, ee nafsi yangu! Nitamsifu Mwenyezi-Mungu maisha yangu yote; nitamwimbia Mungu wangu muda wote niishipo. Msiwategemee wakuu wa dunia; hao ni binadamu tu, hawawezi kuokoa. Binadamu akitoa pumzi yake ya mwisho, anarudi mavumbini alimotoka; na hapo mipango yake yote hutoweka. Heri mtu anayesaidiwa na Mungu wa Yakobo, mtu aliyeweka tumaini lake kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, aliyeumba mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo. Yeye hushika ahadi yake milele. Yeye huwapatia wanaoonewa haki zao, huwapa wenye njaa chakula. Mwenyezi-Mungu huwapa wafungwa uhuru, huwafungua macho vipofu. Mwenyezi-Mungu huwainua waliokandamizwa; huwapenda watu walio waadilifu. Mwenyezi-Mungu huwalinda wageni, huwategemeza wajane na yatima; lakini huipotosha njia ya waovu. Mwenyezi-Mungu atawala milele, Mungu wako, ee Siyoni, ni mfalme vizazi vyote! Msifuni Mwenyezi-Mungu!
                                           Amina..
Asanteni sana wote mnaotembelea hapa Mungu akawabariki katika yote..muwe salama Rohoni
Nawapenda.



Mafundi wa kutayarisha hema la mkutano

(Kut 35:30–36:1)

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 2“Mimi nimemteua Bezaleli, mwana wa Uri, mjukuu wa Huri, wa kabila la Yuda 3na kumjaza roho wangu. Nimempatia uzoefu na akili, maarifa na ufundi, 4ili abuni kazi za usanii na kufanya kazi za kufua dhahabu, fedha na shaba. 5Nimempatia ujuzi wa kuchonga mawe ya kupambia, kuchonga mbao, na ujuzi wa kila aina ya ufundi. 6Vilevile nimemteua Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, afanye kazi pamoja naye. Hali kadhalika nimewapa uwezo mkubwa watu wengine kwa ajili ya kazi mbalimbali, ili watengeneze vifaa vyote nilivyoagiza vifanywe: 7Hema la mkutano, sanduku la ushuhuda na kiti cha ushuhuda juu yake, pamoja na vifaa vyake vyote; 8meza na vyombo vyake, kinara safi cha taa na vyombo vyake, madhabahu ya kufukizia ubani, 9madhabahu ya sadaka za kuteketezwa na vyombo vyake vyote, birika la maji pamoja na tako lake, 10mavazi matakatifu ya kuhani Aroni na wanawe ambao watafanya huduma ya ukuhani, 11mafuta ya kupaka na ubani wenye harufu nzuri kwa ajili ya mahali patakatifu. Vitu hivyo vyote vitatengenezwa kulingana kabisa na jinsi nilivyokuamuru.”

Siku ya kupumzika

12Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 13“Waambie Waisraeli hivi: Nyinyi mtaadhimisha Sabato zangu, kwa sababu hizo ni ishara kati yenu na mimi kwa vizazi vyote kwamba mimi ndimi ninayewatakasa. 14Mtaiadhimisha Sabato, nayo itakuwa kwenu siku takatifu. Yeyote atakayeitia unajisi siku hiyo lazima auawe. Na mtu atakayefanya kazi yoyote siku hiyo atatengwa mbali na watu wake. 15Taz Kut 20:8-11; 23:12; 34:21; 35:21; Lawi 23:3; Kumb 5:12-14 Mtafanya kazi zenu kwa muda wa siku sita, lakini siku ya saba ni siku rasmi ya mapumziko, ni siku yangu takatifu. Mtu yeyote atakayefanya kazi yoyote siku hiyo lazima atauawa. 16Kwa hiyo Waisraeli wataiadhimisha siku ya Sabato katika vizazi vyao vyote kama ishara ya agano la milele. 17Taz Kut 20:11 Jambo hili litakuwa ishara ya kudumu kati ya Waisraeli na mimi, maana mimi Mwenyezi-Mungu nilifanya mbingu na dunia kwa muda wa siku sita, lakini siku ya saba niliacha kufanya kazi, nikapumzika.”
18Mwenyezi-Mungu alipomaliza kuongea na Mose mlimani Sinai, alimpatia Mose vile vibao viwili vya mawe ambavyo yeye Mungu aliviandika zile amri kwa kidole chake mwenyewe.

Kutoka31;1-18

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: