Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday 24 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 39...


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mngu wetu katika yote..
Mtakatifu.!Mtakatifu.!Mtakatifu.! Baba wa Mbinguni..Tunakushukuru na kukusifu daima..

Asante kwa wema na fadhili zako Mungu wetu, Asante kwa ulinzi wako na kutuamsha salama Mungu wetu..Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tunashuka mbele zako tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Yahweh..!
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mungu wetu kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Baba tunaiweka siku hii na maisha yetu mikononi mwako..Tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo,Vyombo vya usafiri,Tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Jehovah..Ukabariki vilaji/vinywaji,Kazi zetu,Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mfalme wa Amani ukavitakase kwa Damu ya mwanao Mpendwa Bwana wetu na mwokozi wetu Yesu Kristo yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..
Ukatuokoe na yule mwovu na kazi zake..


Ukatutakase Miili yetu na Akili zetu ..tupate kutambua na kujitambua..

Ukatupe ufahamu, Busara na hekima,Utuwema na Upendo..
Kila mmoja akatumike sawasawa na karama uliyompa na akaijitoe kwa kazi yako Mungu wetu Sifa na utukufu ukurudie wewe Mungu wetu..
Mungu wetu ukaonekane tuwapo Kazini,Shuleni na katika yote tunayoenda kufanya
Tukawe chombo chema tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Wapendwa Ndugu zangu Mungu wetu yu Mwema sana na kupitia yeye tumebarikiwa vipaji/karama mbalimbali na nilichonacho mimi pengine wewe huna na ulichonacho wewe mimi sina au siwezi kufanya hivyo/hicho kitu..Yote hiyo ni makusudi yake ili kuwe na mgawanyiko wa kazi zake...
Tumuombe Mungu atuongoze katika kazi zake na kutupa moyo wa kuifanya hiyo kazi..hakuna kazi ndogo mbele za Mungu..

Kama wewe nimshonaji unaweza kushona hata vitambaa vya kutandika/kupambia Nyumba ya Mungu[Tabitha-Matendo 9:36-43],kama wewe ni mfagiaji kafagie na kusafisha Nyumba ya Mungu,kama wewe ni mpambaji Pamba Nyumba ya Mungu,kama wewe ni mpishi pika hata chai na unaweza kukusanya wawili watatu mkaongea Neno la Mungu na kusaidiana kutafakari kila mmoja ataondoka na kitu..Kama wewe una pesa hayaaa kunamahitaji mengi yanahitaji pesa Bariki wengine nawe uendelee kubarikiwa, Angalia nini kimepungua kwenye Nyumba za ibada au kwa watu wa Mungu ili uwasaidie na Mungu akuongezee zaidi ya hizo utakazo toa..
kwenye maisha haya ya kila siku kuna vitu vingi vya kufanya/kumfanyia Mungu ili watu wauone wema,Utukufu wa Mungu..
Kila mmoja afanye kwa nafasi yake aliyopewa na Mungu..nasi kwakubishana au kugombania kazi moja..Baraka za Mungu zipo na zinapatikana hata kama wewe si kiongozi Kanisani..Na silazima ukafanye kazi inayoonekana na watu wengi ili upate sifa hapa Duniani..Kazi yako inawezekana isionekane zaidi machoni mwa Wanadamu na hata ikaonekana haifai na wakaidharau..Lakini Mungu wetu Baba wa Mbinguni yeye akiibariki nawe utabarikiwa..Mungu alitupa bure nasi tukatumike na kujitoa sawasawa na mapenzi yake..Tukawe wakarimu na wanyenyekevu katika kujitoa kwetu..



Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.” Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; wema wake wadumu milele.” Na Mungu ampaye mkulima mbegu na mkate kwa chakula, atawapa nyinyi pia mbegu mnazohitaji, na atazifanya ziote, zikue na kuwapa mavuno mengi ya ukarimu wenu. Yeye atawatajirisha nyinyi daima kwa kila kitu, ili watu wapate kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi zenu wanazozipokea kwa mikono yetu. Maana huduma hii takatifu mnayoifanya si kwamba itasaidia mahitaji ya watu wa Mungu tu, bali pia itasababisha watu wengi wamshukuru Mungu. Kutokana na uthibitisho unaooneshwa kwa huduma hii yetu, watu watamtukuza Mungu kwa sababu ya uaminifu wenu kwa Habari Njema ya Kristo mnayoiungama, na pia kwa sababu ya ukarimu mnaowapa wao na watu wote. Kwa hiyo watawaombea nyinyi kwa moyo kwa sababu ya neema ya pekee aliyowajalieni Mungu. Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi yake isiyo na kifani!

Tazama wenye shida/tabu,waliomagerezani pasipo na hatia,waliokatika vifungo vya mwovu,wagonjwa, wafiwa ukawe mfariji wao..waliokataliwa,waliokata tamaa,wenye hofu/mashaka,wanaougua rohoni,Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu, UKawaponye na kuwaokoa.. wapate kupona kimwili na kiroho pia..Baba wa mbinguni ukaonekane kwenye mapito yao..

Tunaweka haya yote mikononi mwako Baba wa mbinguni..
kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata milele..

Amina..!
Asanteni wote kwakupita hapa..
Mungu akawabariki katika yote na akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.


Mavazi ya makuhani: Kizibao

(Kut 28:1-14)
1Kwa kutumia sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu walifuma sare za kuvaa wakati wa kuhudumu mahali patakatifu. Walimshonea Aroni mavazi matakatifu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
2Walitengeneza kizibao kwa nyuzi za dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. 3Waliifua dhahabu na kuikata katika nyuzi nyembamba ili kuzifuma pamoja na sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa kwa ustadi. 4Kizibao hicho kilivaliwa kwa kamba mbili mabegani zilizoshonewa kwenye ncha zake mbili. 5Mkanda uliofumwa kwa ustadi juu yake ili kuifungia ulikuwa kitu kimoja na kizibao hicho, na ulitengenezwa kwa vitu hivyohivyo: Dhahabu, sufu ya buluu, zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
6Kisha waliandaa vito vya sardoniki na kuvipanga katika vijalizo vya dhahabu; navyo vilichorwa, kama mtu achoravyo mhuri, majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. 7Waliviweka vito hivyo katika kanda za mabegani za kile kizibao ili kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Kifuko cha kifuani

(Kut 28:15-30)

8Mafundi walitengeneza kifuko cha kifuani kama vile walivyokitengeneza kile kizibao, kwa dhahabu, kwa sufu ya rangi ya buluu, rangi zambarau na nyekundu, na kwa kitani safi iliyosokotwa. 9Kifuko hicho kilikuwa cha mraba, sentimita 22 kwa sentimita 22 nacho kilikunjwa. 10Kifuko hicho kilipambwa kwa safu nne za mawe ya thamani; safu ya kwanza ilikuwa ya akiki, topazi na almasi nyekundu; 11safu ya pili ilikuwa ya zumaridi, na johari ya rangi ya samawati na almasi; 12safu ya tatu ilikuwa ya yasintho, ya akiki nyekundu na amethisto; 13na safu ya nne ilikuwa ya zabarajadi, ya shohamu na yaspi; yote yalimiminiwa vijalizo vya dhahabu. 14Basi, palikuwa na mawe kumi na mawili yaliyochorwa majina kumi na mawili ya wana wa Israeli. Yalikuwa yamechorwa kama wachoravyo mhuri, kila moja limechorwa jina kuwakilisha makabila kumi na mawili. 15Walikitengenezea kile kifuko cha kifuani mikufu ya dhahabu safi. 16Walitengeneza vijalizo viwili vya dhahabu safi na pete mbili za dhahabu, na kuzitia pete hizo kwenye ncha mbili za juu za kifuko hicho. 17Mikufu hiyo miwili ya dhahabu waliifunga kwenye pete hizo za kifuko cha kifuani. 18Zile ncha mbili za mikufu ya dhahabu walizitia kwenye vile vijalizo viwili wakazishikamanisha na vile vipande viwili vya mabegani vya kizibao, upande wa mbele. 19Walitengeneza pete mbili za dhahabu, wakazitia penye ncha mbili za chini upande wa ndani wa kifuko hicho cha kifuani karibu na kizibao. 20Walitengeneza pete nyingine mbili za dhahabu na kuzitia mbele katika ncha za chini za vipande vya kizibao, mahali kinapoungana na ule mkanda uliofumwa kwa ustadi. 21Walifunga kifuko cha kifuani kwenye kizibao kwa kufunganisha pete zake na kizibao kwa kamba ya rangi ya buluu, ili kifuko hicho kisilegee ila kikalie ule mkanda uliofumwa kwa ustadi, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Mavazi mengine ya kikuhani

(Kut 28:31-43)

22Alitengeneza kanzu ya kuvaa ndani ya kizibao ya rangi ya buluu. 23Joho hilo lilikuwa na nafasi ya kupitishia kichwa katikati, nayo ilizungushiwa utepe uliofumwa ili isichanike. 24Kwenye upindo wa chini wa kanzu walifuma mapambo ya makomamanga ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu, na kitani safi iliyosokotwa. 25Kisha walitengeneza njuga za dhahabu, na kila baada ya komamanga walitia njuga kwenye upindo wa joho. 26Hivyo, njuga na komamanga vilifuatana kuuzunguka upindo wa joho hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
27Kisha wakawafumia Aroni na wanawe vizibao vya kitani safi, 28kilemba cha kitani safi, kofia za kitani safi, suruali za kitani safi iliyosokotwa, 29na mikanda ya kitani safi iliyosokotwa kwa sufu ya rangi ya buluu, ya zambarau na nyekundu na kuitarizi vizuri, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
30Kisha walitengeneza pambo la dhahabu safi kwa ajili ya taji takatifu na kuchora juu yake kama wachoravyo mhuri, “Wakfu kwa Mwenyezi-Mungu.” 31Kisha wakalifunga mbele ya kile kilemba kwa ukanda wa rangi ya buluu, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

Kukamilika kwa kazi

(Kut 35:10-19)

32Basi, kazi yote ya hema la mkutano ikamalizika. Waisraeli walifanya yote kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. 33Wakamletea Mose hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote, vikonyo vyake, mbao zake, pau zake, nguzo zake na vikalio vyake; 34kifuniko cha ngozi za kondoo dume na mbuzi kilichotiwa rangi nyekundu, pazia la mahali patakatifu, 35sanduku la agano, mipiko yake na kiti cha rehema; 36meza na vyombo vyake vyote, mikate iliyowekwa mbele ya Mungu; 37kinara cha taa cha dhahabu safi, taa zake, vyombo vyake vyote pamoja na mafuta kwa ajili ya taa hizo; 38madhabahu ya dhahabu; mafuta ya kupaka, ubani wenye harufu nzuri, na pazia la mlango wa hema; 39madhabahu ya shaba na wavu wake wa shaba, mipiko yake na vyombo vyake vyote; bakuli, birika na tako lake; 40vyandarua vya ua, nguzo zake na vikalio vyake; pazia la mlango wa ua, kamba zake na vigingi vyake; vyombo vyote vilivyohitajika katika huduma ya hema takatifu, yaani hema la mkutano; 41na mavazi yote yaliyofumwa vizuri kabisa kwa ajili ya huduma ya mahali patakatifu, yaani mavazi matakatifu ya kuhani Aroni, na ya wanawe kwa ajili ya huduma ya ukuhani. 42Waisraeli walifanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. 43Mose alikagua kila kitu, akaridhika kwamba walikuwa wamefanya kila kitu kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru. Hivyo Mose akawabariki.


Kutoka39;1-43

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: