Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 25 May 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Kutoka 40- Mwisho wa kitabu cha Kutoka...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu....

Mungu wetu, Baba yetu, Muumba wetu, Muumba Mbingu na Nchi na Vyote vilivyomo ni mali yako..Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Yahweh.!Jehovah..!El shaddai..!Muweza wa yote, Alfa na Omega,Wewe ni Mwanzo na wewe ni mwisho,Hakuna kama wewe..!!


Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako.
Asante kwa ulinzi wako na kutuamsha salama..

Asante kwakutuchagua tena  na umetupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa nguvu zetu wala Akili zetu,si kwamba sisi ni wema sana,si kwamba sisi wazuri mno..hapana ni kwa Neema/Rehema zako sisi kuiona leo hii...
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,kujishusha na kujiachilia mikononi mwako Mfalme wa Amani ..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe kwa kuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua,kutojua..
Baba wa mbinguni tunaomba nasi utupe Neema ya kuweza kuwasamehe waliotukosea..
Utuepushe na majaribu Baba wa mbinguni na utuokoe na yule mwovu na kazi zake..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Mungu Baba tunaomba ukatutakase Miili yetu na Akili zetu tupate kutambua na kujitambua..

Tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo,vyombo vya usafiri, tutembeapo hatua zetu ziwe nawe Yahweh..Mungu wetu ukabariki Kazi zetu,Biashara,Masomo,vilaji/vinywaji na vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Mfalme wa Amani ukavitakase kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu na kuwaponya wote wanaopitia majaribu mbalimbali,shida/tabu,wafiwa ukawe mfariji wao,wagonjwa na wote walio katika vifungo mbalimbali Baba ukawafungue na kuwaokoa, wakapate kupona kimwili na kiroho pia,Baba ukaonekane kwenye shida zao wote wanaokuomba na kukulilia Mungu wetu ukawafute machozi yao..

Tunakushuru Mungu wetu kwa uwezo wako na kutupa Neema hii ya kuweza kusoma Neno Lako Baba wa Mbinguni..

leo tumemaliza kusoma Neno lako kwenye kitabu hiki..Baba wa mbinguni isiwe mwisho na iwe ndiyo mwanzo tukawe na Shauku ya kusoma Neno lako..
 Tunaomba utubariki na kutupa mwangaza zaidi kwenye neno lako..na tusomapo tuondoke na faida na tupate kuelewa na kulitunza likapate kutusaidia sisi na wengine..
Yesu anafafanua mfano wa mpanzi
(Mat 13:18-23; Luka 8:11-15)



Basi, Yesu akawauliza, “Je, nyinyi hamwelewi mfano huu? Mtawezaje basi, kuelewa mfano wowote? Mpanzi hupanda neno la Mungu. Watu wengine ni kama walio njiani ambapo neno lilipandwa. Lakini mara tu baada ya kulisikia, Shetani huja na kuliondoa neno hilo lililopandwa ndani yao. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa penye mawe. Mara tu walisikiapo hilo neno hulipokea kwa furaha. Lakini haliwaingii na kuwa na mizizi ndani yao; huendelea kulizingatia kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya hilo neno, mara wanakata tamaa. Watu wengine ni kama zile mbegu zilizoanguka penye miti ya miiba. Huo ni mfano wa wale wanaosikia hilo neno, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu, anasa za mali na tamaa za kila namna huwaingia na kulisonga hilo neno, nao hawazai matunda. Lakini wengine ni kama zile mbegu zilizopandwa katika udongo mzuri. Hawa hulisikia hilo neno, wakalipokea, wakazaa matunda: Wengine thelathini, wengine sitini na wengine mia.”

Mungu wetu ukatupe masikio tusikie na macho ya kuona.. Tukawe kama zile mbegu zilizopandwa kwenye udongo mzuri..
Tukawe barua njema na tukasomeke popote tutakapo pita sawasawa na mapenzi yako...


Mfano wa mbegu inayoota


Yesu akaendelea kusema, “Ufalme wa Mungu ni kama ifuatavyo. Mtu hupanda mbegu shambani. Usiku hulala, mchana yu macho na wakati huo mbegu zinaota na kukua; yeye hajui inavyofanyika. Udongo wenyewe huiwezesha mimea kukua na kuzaa matunda: Kwanza huchipua jani changa, kisha suke, na mwishowe nafaka ndani ya suke. Nafaka inapoiva, huyo mtu huanza kutumia mundu wake, maana wakati wa mavuno umefika.”
Mungu wetu ukatupe Neema ya kupanda  mbegu njema na tupate kukua kiimani/kiroho na kuvuna yaliyo mema..
 Mungu wetu tunapanda mbegu zako kwa wote wasioamini na wapate kujua wewe Mungu wetu na wema wako..Sifa na utukufu tunakurudishia wewe Daima..


Asante Mungu wetu katika yote.
Tunayaweka haya yote mikononi mwako tukiamini wewe ni Mungu wetu na Tumaini letu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele..
Amina..!
Mungu wetu yu mwema sana wapendwa..

kwa uwezo wake na mapenzi yake kwetu leo tumemaliza kitabu hiki..
ninaimani kuna tuliokuwa nao sambamba tangu mwanzo..
Mungu aendele kukupa shauku ya kuendelea kusoma Neno lake..

haijalishi uko busy kiasi gani lakini huwezi kukosa muda kidogo kwa ajili yake yeye Mungu aliyekupa hiyo shughuli ya kukufanya ukawa Busy..
kusikiliza Neno kanisani tuu haitoshi lazima tujibidishe na kujipa msukumo wa kujisomea katika mazingira yoyote tunayopitia tuweke  Mungu kwanza..
Mungu aendelee kutufunulia na kutupa mwanga zaidi..
tunachokipanda kipate kumea/kukua vyema..
Asanteni sana kwakutembelea hapa..
Mungu awabariki na kuwapa Amani ya Moyo..
Nawapenda sana. 

Hema lasimikwa na kuwekwa wakfu

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, utalisimika hema takatifu la mkutano. 3Ndani ya hema hilo utaweka lile sanduku la ushuhuda, kisha weka pazia mbele yake. 4Utaiingiza meza na kupanga vyombo vyake juu. Utaingiza kile kinara pia na kuziweka taa zake juu yake. 5Madhabahu ya dhahabu ya kufukizia ubani utaiweka mbele ya sanduku la ushuhuda, kisha utatundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu. 6Ile madhabahu ya kuteketezea sadaka utaiweka mbele ya mlango wa hema takatifu la mkutano. 7Birika la kutawadhia utaliweka katikati ya hema la mkutano na madhabahu na kulijaza maji. 8Utazungushia ua na kutundika pazia penye lango lake.
9“Kisha, utaliweka wakfu hema takatifu pamoja na vyombo vyake vyote kwa kuvipaka yale mafuta ya kupaka, nalo litakuwa takatifu. 10Halafu, utaiweka wakfu madhabahu ya kuteketezea sadaka na vyombo vyake vyote kwa kuipaka mafuta, nayo itakuwa takatifu kabisa. 11Birika la kutawadhia na tako lake pia utaliweka wakfu kwa namna hiyohiyo.
12“Utamwita Aroni na wanawe waje mlangoni mwa hema la mkutano, kisha uwatawadhe. 13Mvike Aroni yale mavazi matakatifu; utampaka mafuta na kumweka wakfu, ili aweze kunitumikia kama kuhani. 14Waite wanawe na kuwavisha zile kanzu. 15Kisha uwapake mafuta kama ulivyompaka baba yao, ili nao pia wanitumikie kama makuhani. Kupakwa mafuta huku kutawaingiza katika ukuhani wa kudumu katika vizazi vyao vyote.”
16Basi, Mose alitekeleza kikamilifu kabisa maagizo yote ya Mwenyezi-Mungu.
17Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza mwaka wa pili baada ya kutoka Misri, hema la mkutano lilisimikwa. 18Mose aliweka vikalio vyake, akainua mbao zake, akashikamanisha pau zake na kusimamisha nguzo zake. 19Alitandaza pazia juu ya hema takatifu na kuweka kifuniko cha hema juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 20Kisha alichukua vile vibao viwili vya mawe na kuviweka katika lile sanduku. Aliipitisha ile mipiko katika vikonyo vya sanduku na kukiweka kiti cha rehema juu yake. 21Kisha akaliweka lile sanduku la maamuzi ndani ya hema na kutundika pazia, na kwa namna hiyo akalisitiri sanduku la maamuzi, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu.
22Aliweka meza ndani ya hema la mkutano, upande wa kaskazini, sehemu ya nje ya pazia, 23na juu yake akaipanga mikate iliyotolewa kwa Mwenyezi-Mungu, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 24Alikiweka kinara ndani ya hema la mkutano, upande wa kusini, mkabala wa meza. 25Humo, mbele ya Mwenyezi-Mungu, akaziwasha taa zake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 26Aliiweka ile madhabahu ya dhahabu katika hema, mbele ya pazia, 27na kufukiza ubani wenye harufu nzuri juu yake, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 28Alitundika pazia kwenye mlango wa hema takatifu, 29akaweka hapo langoni mwa hema takatifu madhabahu ya sadaka za kuteketezwa, akatolea juu yake sadaka ya kuteketezwa na sadaka ya nafaka, kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 30Aliliweka birika la kutawadhia katikati ya hema la mkutano na madhabahu, na kutia maji ya kutawadha. 31Mose, Aroni na wanawe, wote walinawa mikono na miguu yao humo. 32Kila walipoingia ndani ya hema au walipokaribia ile madhabahu, walinawa, kama Mose alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. 33Mwishowe Mose akatengeneza ua kulizunguka hema takatifu na madhabahu, na kuweka pazia kwenye lango la ua. Hivyo,
Mose akaikamilisha kazi yote.


Wingu juu ya hema la mkutano

34Kisha, lile wingu likalifunika lile hema la mkutano, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukalijaza hema. 35Mose alishindwa kuingia ndani ya hema la mkutano kwa sababu hilo wingu lilikaa juu yake, na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukajaa humo. 36Katika safari zao zote Waisraeli hawakuanza safari kamwe isipokuwa wakati wingu hilo lilipoinuliwa kutoka juu ya hema. 37Kama wingu hilo halikuinuliwa wao hawakuanza safari; walingoja mpaka wakati lilipoinuliwa. 38Katika safari zao zote, Waisraeli waliweza kuliona lile wingu la Mwenyezi-Mungu juu ya hema wakati wa mchana na ule moto ukiwaka juu yake usiku.

Kutoka40;1-38

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: