Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 8 June 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Mambo Ya Walawi..10...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje Wapendwa/Waungwana?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo,Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Yahweh..!Jehovah..!Jehovah nissi..!Jehovah Shammah..!Jehovah Jireh..!Jehovah Rapha..! Jehovah Roi..!Jehovah Shalom..!!
Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni wewe ni Alfa na Omega,Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Unatosha Mungu wetu...!!

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako,
Asante kwa kutulinda usiku na wakati wote na umetuamsha salama..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..

Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachili mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwa kuwaza,kunena,kutenda,kujua/kutojua..Baba wa Mbinguni Tunaomba nasi utupe Neema ya kuiweza kuwasamehe waliotukosea..

Utuepushe na majaribu, utuokoe na yule mwovu na kazi zake..Mungu wetu ututakase na utufunike kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu tupate kutambua/kujitambua..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Mungu wetu tunaomba uwabariki na kuwatendea,Ukawaguse na mkono wako wenye nguvu Yatima na Wajane na ukawaponye kimwili na kiroho wote wanaotaabika kwa Shida/tabu,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokwenye vifungo mbalimbali Baba ukawafungue na wote waliokata tamaa,wenye hofu/mashaka wakapate tumaini na wakawe na Amani ya moyo na ukawatendee sawa sawa na mapenzi yako.


Wapendwa tumrudishie Sifa na Utukufu Mungu wetu,Tuwe na wakati wa kukumbuka na Kumshukuru Mungu kwa Mema meengi aliyotutendea/anayotutendea..Tusiwe watu wa kulalamika tuu kila siku na kusahau wema wa Mungu..Tunasahau mangapi ametenda kwenye maisha yetu,Tusiwe wepesi wa kukumbuka mapito/majaribu tuu na kumuasi Mungu wetu kwamba ametuacha..Tukumbuke wapi tulipotoka na wapi tunaenda,tukumbuke wema na fadhili zake,tukumbuke si kwamba mimi/wewe ni wema sana na tunaweza yote hayo kwa uwezo wetu..
Tukumbuke kwa Neema/Rehema zake ndiyo tunaishi,Tunapata mahitaji yetu wala si kwamba tuna nguvu ya kufanya kazi/biashara au kwa akili zetu wenyewe pasipo maarifa aliyotupa Mungu ndiyo tunafanikiwa..


Ee Mungu wetu Tunakushukuru katika yote,Tunakushukuru kwa uweza wako na kutupa sisi nafasi ya kufanya/kutenda yote haya..

Tusipo weza kumshukuru Mungu wetu kwa kidogo tulichonacho jee tutakumbuka kwa kikubwa..?Tusijilinganishe na maisha ya wengine na kulalamika Mungu mbona mimi hivi na huyu vile,Tumshukuru kwa hili kwanza na tumuombe na atupe maarifa,ubunifu na tukatumie vyema karama alizotupa...
Tumkabidhi maisha yetu na kuomba muongozo huku nasi tukijibidisha..


Ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe kutii masharti yako; nami nitayashika mpaka mwisho. Unieleweshe nipate kuishika sheria yako, niifuate kwa moyo wangu wote. Uniongoze katika njia ya amri zako, maana humo napata furaha yangu. Unipe ari ya kuzingatia maamuzi yako, na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa. Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi; unioneshe njia yako, unipe uhai. Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako; ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu. Uniokoe na lawama ninazoogopa; maana maagizo yako ni mema. Natamani sana kuzitii kanuni zako; unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.
Mungu wetu yu Mwema sana...!
Ee Mungu wetu ukatuongoze na kutuepusha na mambo yote yasiyokupendeza..
Ee Mungu wetu ukatupe kujua na kulielewa vyema Neno lako..

Ee Mwenyezi-Mungu, upokee sala yangu ya shukrani; na kunifundisha maagizo yako.
Asante Mungu wetu Tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tukiamini na kukusifu daima..
Kwakua Ufalme ni wako Nguvu na Utukukufu hata Milele..
Amina..!
Mungu aendelee kuwabariki..
Asanteni sana kwakunitembea/kunisoma..
Nawapenda sana.





Dhambi ya Nadabu na Abihu

1Nao Nadabu na Abihu, wanawe Aroni, walichukua kila mmoja chetezo chake, wakaweka moto na ubani, wakamtolea Mwenyezi-Mungu moto najisi, ambao haukulingana na agizo lake Mwenyezi-Mungu. 2Basi, moto ukatokea mbele ya Mwenyezi-Mungu, ukawateketeza hao vijana, wakafa mbele yake. 3Hapo, Mose akamwambia Aroni, “Kwa tukio hili Mwenyezi-Mungu amekuonesha maana ya kile alichosema: ‘Nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwa wale walio karibu nami; nitatukuzwa mbele ya watu wote!’” Aroni akanyamaza kimya.
4Basi, Mose akawaita Mishaeli na Elsafani, wanawe Uzieli, baba mdogo wa Aroni, akawaambia waje kuondoa maiti za ndugu zao maskani na kuzipeleka nje ya kambi. 5Wakachukua maiti za ndugu zao na kuzipeleka nje ya kambi wakiwa wamevaa mavazi yao, kama Mose alivyoamuru. 6Kisha Mose akamwambia Aroni na wanawe, Eleazari na Ithamari, “Msivuruge nywele zenu na wala msirarue mavazi yenu kuomboleza, la sivyo mtakufa na kuiletea jumuiya yote ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini ndugu zenu yaani jumuiya yote ya Israeli, wanaweza kuomboleza kwa sababu ya moto huo aliouleta Mwenyezi-Mungu. 7Msitoke nje ya mlango wa hema la mkutano, la sivyo mtakufa; kwani mafuta ya kupaka ya Mwenyezi-Mungu yangali juu yenu.” Aroni na wanawe wakafanya kama Mose alivyosema.
8Mwenyezi-Mungu aliongea na Aroni, akasema, 9“Mnapoingia ndani ya hema la mkutano, wewe na wanao msinywe divai wala kileo chochote, la sivyo mtakufa. Hii itakuwa sheria ya kudumu katika vizazi vyenu vyote. 10Ni lazima mtofautishe kati ya mambo matakatifu na mambo yasiyo matakatifu, kati ya mambo najisi na yasiyo najisi. 11Mtawafundisha Waisraeli masharti yote ambayo nimewaambia kwa njia ya Mose.”
12 # Taz Lawi 6:14-18 Mose akamwambia Aroni na wanawe waliosalia: Eleazari na Ithamari, “Chukueni ile sehemu ya sadaka ya nafaka iliyosalia kutoka sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto; muile karibu na madhabahu bila kutiwa chachu kwa sababu ni takatifu kabisa. 13Mtaila katika mahali patakatifu kwa sababu hiyo ni haki yako na wazawa wako kutoka katika sadaka anazotolewa Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hivyo ndivyo nilivyoamriwa. 14#Taz Lawi 7:30-34 Lakini kidari ambacho hufanywa nacho ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu na mguu unaotolewa sadaka kama ishara, mnaweza kula mahali popote pasipo najisi. Utakula wewe, na watoto wako wa kiume na wa kike. Vitu hivyo umepewa kama haki yako na ya wazawa wako kutoka sadaka za amani za watu wa Israeli. 15Ule mguu uliotolewa na kidari cha sadaka ya kufanyia ishara ya kumtolea Mwenyezi-Mungu watavileta pamoja na sadaka za mafuta zitolewazo kwa moto, ili kufanya ishara ya kuvitolea mbele ya Mwenyezi-Mungu, viwe sadaka ya kutolewa kwa ishara. Hivyo vitakuwa vyako pamoja na wanao; ni haki yenu milele kama Mwenyezi-Mungu alivyoamuru.”
16Basi, Mose alichunguza kwa makini kuhusu mbuzi mmoja aliyetolewa sadaka ya kuondoa dhambi, kumbe akagundua kuwa alikwisha teketezwa. Hivyo akawakasirikia sana Eleazari na Ithamari, wana wa Aroni waliosalia, akawauliza, 17#Taz Lawi 6:24-26 “Kwa nini hamkumla katika mahali patakatifu kwa vile huyo ni kitu kitakatifu kabisa na mlikuwa mmepewa huyo ili kuondoa hatia ya jumuiya na kuwafanyia ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu? 18Tena, kwa vile damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu, ni dhahiri iliwapasa kumla ndani ya mahali patakatifu kama nilivyoamuru.” 19Aroni akamwambia Mose, “Tazama, leo wametolea sadaka yao ya kuondoa dhambi na sadaka ya kuteketezwa mbele ya Mwenyezi-Mungu; hata hivyo mambo haya yamenipata! Tena kama ningekula ile sadaka ya kuondoa dhambi hivi leo, je, ingekubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu?” 20Mose aliposikia hayo, akaridhika.

Mambo Ya Walawi10;1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: