Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday 17 July 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..10

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Ni siku/wiki nyingine tena Mungu ametuchagua na ametupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Mungu wetu yu mwema sana.Wema na fadhili zake kwetu ni za  ajabu...

Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu, na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya. Huniongoza katika njia sawa kwa hisani yake. Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda. Umeniandalia karamu mbele ya maadui zangu; umenipaka mafuta kichwani pangu; kikombe changu umekijaza mpaka kufurika. Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami, siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele.


Asante Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..wewe ni mlinzi wetu mkuu..
wewe hutulinda mchana/usiku na popote tuendako upo nasi...

Anayekaa chini ya ulinzi wa Mungu Mkuu, anayeishi chini ya kivuli cha Mungu Mwenye Nguvu, ataweza kumwambia Mwenyezi-Mungu: “Wewe ni kimbilio langu na ngome yangu; Mungu wangu, ninayekutumainia!” Hakika Mungu atakuokoa katika mtego; atakukinga na maradhi mabaya. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake; mkono wake utakulinda na kukukinga. Huna haja ya kuogopa vitisho vya usiku, wala shambulio la ghafla mchana; huna haja ya kuogopa baa lizukalo usiku, wala maafa yanayotokea mchana. Hata watu elfu wakianguka karibu nawe, naam, elfu kumi kuliani mwako, lakini wewe baa halitakukaribia. Kwa macho yako mwenyewe utaangalia, na kuona jinsi watu waovu wanavyoadhibiwa. Wewe umemfanya Mwenyezi-Mungu kuwa kimbilio lako; naam, Mungu aliye juu kuwa kinga yako. Kwa hiyo, hutapatwa na maafa yoyote; nyumba yako haitakaribiwa na baa lolote. Maana Mungu atawaamuru malaika zake, wakulinde popote uendapo. Watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe. Utakanyaga simba na nyoka, utawaponda wana simba na majoka. Mungu asema: “Nitamwokoa yule anipendaye; nitamlinda anayenitambua! Akiniita, mimi nitamwitikia; akiwa taabuni nitakuwa naye; nitamwokoa na kumpa heshima. Nitamridhisha kwa maisha marefu, nitamjalia wokovu wangu.”

Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni..tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Muumba wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizoziwaza,tulizozinena,tulizozitenda kwa kujua/kutojua..
Mungu Baba tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale walitukosea..
Utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu  kwa Damu ya Mwanao Mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukapate kutambua/kujitambua na tukawe na kiasi,Hekima,Upendo,Amani na utuwema..tusiionee haya Injili..

Tukawe chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yake..
Mungu Baba tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
tunaomba utubariki na kubariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda
na tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Tusipungukiwe kwenye mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji...

Ninawatakieni nyinyi ndugu amani, upendo na imani kutoka kwa Mungu Baba na kutoka kwa Bwana Yesu Kristo. Nawatakia neema ya Mungu wote wanaompenda Bwana wetu Yesu Kristo kwa mapendo yasiyo na mwisho.


Amina..!
Asanteni sana wapendwa /waungwana kwakuwa nami
Mungu ni pendo..
Nawapenda.





Tarumbeta za fedha

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Tengeneza tarumbeta mbili kwa fedha iliyofuliwa. Utazitumia tarumbeta hizo wakati wa kuwaita watu na wakati wa kuvunja kambi. 3Tarumbeta zote mbili zikipigwa pamoja, watu wote watakusanyika karibu nawe mbele ya lango la hema la mkutano. 4Lakini kama ikipigwa tarumbeta moja tu, basi ni viongozi tu wa makabila ya Israeli watakaokusanyika karibu nawe. 5Ishara hiyo ikitolewa kwa kupiga tarumbeta, wakazi wa kambi za mashariki wataanza safari. 6Ishara hiyo ikipigwa mara ya pili, wale wa kambi za upande wa kusini wataanza kuondoka. Ishara hiyo ya tarumbeta itatolewa kila wakati wa kuanza safari. 7Lakini wakati wa kuwaita watu wakusanyike pamoja, tarumbeta zitapigwa kwa njia ya kawaida. 8Wazawa wa Aroni, makuhani, ndio watakaopiga tarumbeta hizo. Utaratibu huo utafuatwa daima katika vizazi vyenu vyote.
9“Wakati wa vita nchini mwenu dhidi ya adui wanaowashambulia, mtatoa ishara ya vita kwa kupiga tarumbeta hizi ili Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu apate kuwakumbuka na kuwaokoa na adui zenu. 10Hali kadhalika katika siku zenu za furaha, kama vile sikukuu za mwandamo wa mwezi na sikukuu nyinginezo, mtazipiga tarumbeta hizi wakati mnapotoa sadaka zenu za kuteketezwa na tambiko za sadaka zenu za amani. Hapo mimi Mungu wenu nitawakumbukeni. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”

Waisraeli wanasafiri

11Mnamo siku ya ishirini ya mwezi wa pili, mwaka wa pili tangu wana wa Israeli walipoondoka Misri, wingu lililokuwa juu ya hema la maamuzi liliinuliwa, 12nao Waisraeli wakaanza safari yao kutoka jangwa la Sinai. Wingu hilo lilipaa na hatimaye likatua katika jangwa la Parani.
13Kwa mara ya kwanza Waisraeli walifunga safari hiyo kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama ilivyotolewa na Mose. 14Wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi cha kabila la Yuda, walitangulia, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Nashoni mwana wa Aminadabu. 15Nethaneli mwana wa Suari, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Isakari. 16Naye Eliabu mwana wa Heloni, alikuwa kiongozi wa kikosi cha kabila la Zebuluni.
17Kisha, hema lilishushwa, na watu wa ukoo wa Gershoni na wa Merari ambao walilibeba, walianza kuondoka.
18Halafu, watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Reubeni, walifuata kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri. 19Shelumieli mwana wa Suri-shadai, aliliongoza kabila la Simeoni. 20Naye Eliasafu mwana wa Deueli, aliliongoza kabila la Gadi.
21Kisha walifuata watu wa ukoo wa Kohathi, wakiwa wamebeba vyombo vitakatifu. Walipowasili, hema lilikuwa limekwisha simikwa.
22Baada ya hao, walifuata watu waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Efraimu, kundi moja baada ya jingine. Kiongozi wao alikuwa Elishama mwana wa Amihudi. 23Gamalieli mwana wa Pedasuri aliliongoza kabila la Manase, 24naye Abidani mwana wa Gideoni, aliliongoza kabila la Benyamini.
25Mwisho, wale waliokuwa chini ya bendera ya kikosi kilichoongozwa na kabila la Dani, waliokuwa kama walinzi nyuma ya vikosi vyote, walisafiri, kundi moja baada ya jingine. Hawa waliongozwa na Ahiezeri mwana wa Amishadai. 26Pagieli, mwana wa Okrani, aliliongoza kabila la Asheri. 27Naye Ahira mwana wa Enani, aliliongoza kabila la Naftali. 28Huu basi, ndio utaratibu walioufuata Waisraeli kulingana na makundi yao, kila wakati walipovunja kambi na kuanza kusafiri tena.
29Mose alimwambia shemeji yake, Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwe wake, “Sisi tunasafiri kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu amesema ‘Nitawapa nyinyi mahali hapo’. Basi, twende pamoja, nasi tutakutendea mema; maana Mwenyezi-Mungu ameahidi kutupa sisi Waisraeli fanaka.” 30Lakini Hobabu akajibu, “Mimi sitafuatana nanyi; ila nitarudi katika nchi yangu na kwa jamaa zangu.” 31Mose akamwambia, “Tafadhali usituache, maana wewe unajua mahali tunapoweza kupiga kambi jangwani, na unaweza kuwa kiongozi wetu. 32Tena ukiandamana nasi chochote chema atakachotutendea Mwenyezi-Mungu, ndicho utakachotendewa nawe pia.”

Safari inaanza

33Basi, watu wakasafiri toka Sinai, Mlima wa Mwenyezi-Mungu, mwendo wa siku tatu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwatangulia mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupiga kambi. 34Kila waliposafiri kutoka kambi moja hadi nyingine, wingu la Mwenyezi-Mungu lilikuwa juu yao mchana.
35 # Taz Zab 68:1 Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Mose alisema, “Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwatawanye adui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako.” 36Na kila wakati liliposimama, Mose alisema, “Warudie, ee Mwenyezi-Mungu, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.”#

Hesabu10;1-36


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: