Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 24 July 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..15



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba yetu Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuamsha salama na wenye afya njema ..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
na kutupa nguvu ya kuendelea na majukumu yetu..
Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni tukinjinyenyekeza,tukijishusha
na tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mungu wetu..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mfalme wa Amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea..
Utuepushe katika majaribu Jehovah utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..Ututakase Miili yetu na Akili zetu kwa Damu ya Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..yeye aliteseka ili sisi tupate kupona...

Yesu anasulubiwa
(Mat 27:32-44; Marko 15:21-32; Yoh 19:17-27)
Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu. Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia. Yesu akawageukia, akasema, “Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu. Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: ‘Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!’ Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: ‘Tuangukieni!’ Na vilima, ‘Tufunikeni!’ Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?” Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye. Walipofika mahali paitwapo, “Fuvu la Kichwa,” ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura. Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!” Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.” Vilevile maandishi haya yalikuwa yamewekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.” Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.” Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo. Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.” Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamjibu, “Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.” Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaifunika nchi yote mpaka saa tisa, na pazia lililokuwa limetundikwa hekaluni likapasuka vipande viwili. Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho. Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.” Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni. Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.

Yahwe tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Tunaomba utubariki na kubariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda
Jehovah tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Roho Matakatifu akatuomngoze tukapate kutambua/kujitambua
tukasimamie Neno lako Sheria na Amri zako Mungu ..
tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji...

Mwenyezi-Mungu asema: “Piga kelele, wala usijizuie; paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazie watu wangu makosa yao, waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao. Siku hata siku wananijia kuniabudu, wanatamani kujua mwongozo wangu, kana kwamba wao ni taifa litendalo haki, taifa lisilosahau sheria za Mungu wao. Wananitaka niamue kwa haki, na kutamani kukaa karibu na Mungu. “Nyinyi mnaniuliza: ‘Mbona tunafunga lakini wewe huoni? Mbona tunajinyenyekesha, lakini wewe hujali?’ “Ukweli ni kwamba wakati mnapofunga, mnatafuta tu furaha yenu wenyewe, na kuwakandamiza wafanyakazi wenu! Mnafunga, na kugombana na kupigana ngumi. Mkifunga namna hiyo maombi yenu hayatafika kwangu juu. Mfungapo, nyinyi mnajitaabisha; mnaviinamisha vichwa vyenu kama unyasi, na kulalia nguo za magunia na majivu. Je, huo ndio mnaouita mfungo? Je, hiyo ni siku inayokubaliwa nami? “La! Mfungo ninaotaka mimi ni huu: Kuwafungulia waliofungwa bila haki, kuziondoa kamba za utumwa, kuwaachia huru wanaokandamizwa, na kuvunjilia mbali udhalimu wote! Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao, kuwavalisha wasio na nguo, bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu. “Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko, mkiwa wagonjwa mtapona haraka. Matendo yenu mema yatawatangulia, nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu. Ndipo mtakapoomba, nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia; mtalia kwa sauti kuomba msaada, nami nitajibu, ‘Niko hapa!’ “Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu, mkiacha kudharau wengine na kusema maovu, mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa, mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki, mwanga utawaangazia nyakati za giza, giza lenu litakuwa kama mchana. Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe. Magofu yenu ya kale yatajengwa; mtajenga upya juu ya misingi iliyoachwa zamani. Nanyi mtaitwa watu waliotengeneza upya kuta, watu waliozifanya barabara za mji zipitike tena.

Asante Mungu wetu..Sifa na Utukufu tunakurudishia wewe..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa kwakuwa nami
Mungu awe nanyi daima..
Nawapenda.

Sheria kuhusu sadaka
1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 2“Waambie Waisraeli kwamba mtakapofika katika nchi ninayowapeni ambamo mtaishi, 3mkanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka kutoka katika mifugo yenu, sadaka ya kuteketezwa au tambiko, ili mtu atimize nadhiri aliyoweka au kutoa sadaka ya hiari au sadaka ya wakati wa sikukuu zenu zilizowekwa, na kufanya harufu nzuri ya kunipendeza mimi Mwenyezi-Mungu, 4basi, yule atoaye sadaka yake, atamletea pia Mwenyezi-Mungu sadaka ya nafaka ya kilo moja ya unga laini uliokandwa na kuchanganywa na lita moja ya mafuta; 5pamoja na divai ya sadaka ya kinywaji, lita moja, vitu hivyo vitaandamana na kila mnyama wa tambiko ya kuteketezwa: Kondoo au mbuzi. 6Wakati wa kutoa sadaka ya kondoo dume, kilo mbili za unga uliokandwa na lita moja u nusu ya mafuta vitatolewa kama sadaka ya nafaka, 7pamoja na sadaka ya kinywaji ya lita moja u nusu ya divai, na kufanya harufu nzuri ya sadaka haya kumpendeza Mwenyezi-Mungu. 8Wakati mtakapomtolea Mwenyezi-Mungu fahali kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa au tambiko ili kutimiza nadhiri au kwa ajili ya sadaka za amani, 9mtu atamtoa kama sadaka pamoja na sadaka ya nafaka ya unga wa kilo tatu ulio mzuri na lita 2 za mafuta, 10pamoja na sadaka ya kinywaji ya lita 2 za divai, na kufanya harufu nzuri ya sadaka ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu.
11“Hivyo ndivyo vitu vitakavyotolewa pamoja na kila fahali, kondoo dume au mbuzi. 12Hesabu ya vitu hivyo itaongezwa kulingana na hesabu ya wanyama watakaotolewa. 13Kila mwananchi Mwisraeli atafuata maagizo hayo wakati anapotoa tambiko, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu. 14Na kama kuna mgeni anayeishi pamoja nanyi kwa muda au daima, akitaka kutoa sadaka yake kwa kuiteketeza, harufu impendezayo Mwenyezi-Mungu, mtu huyo atafanya kama mnavyofanya nyinyi. 15Katika vizazi vyote vijavyo, kanuni zilezile mtakazofuata nyinyi ndizo atakazofuata mgeni yeyote atakayeishi pamoja nanyi; mbele ya Mwenyezi-Mungu mtakuwa sawa; 16#Taz Lawi 24:22 nyinyi na yeye mtakuwa chini ya sheria ileile moja na maagizo yaleyale.”
17Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Waeleze 18Waisraeli kwamba wakati watakapoingia katika nchi ninayowapeleka 19kila mtakapokula mazao ya nchi hiyo, mtatenga kiasi fulani na kunipa mimi Mwenyezi-Mungu. 20Mtakapooka mikate, mkate wa kwanza wa mazao ya kwanza ya nafaka yenu utatolewa kama sadaka kutoka mahali pa kupuria nafaka. 21Mtanitolea mimi Mwenyezi-Mungu sadaka hii maalumu katika vizazi vyenu vyote vijavyo.
22“Lakini ikiwa mtakosa kuzifuata amri zote ambazo mimi Mwenyezi-Mungu nimewapa kwa njia ya Mose, 23kama siku zijazo watu hawatafuata yote ambayo mimi Mwenyezi-Mungu nimemwamuru Mose, 24basi, ikiwa kosa hilo limefanyika bila kukusudia, bila jumuiya kujua, jumuiya yote itatoa fahali mmoja mchanga kuwa sadaka ya kuteketezwa, harufu nzuri ya kumpendeza Mwenyezi-Mungu, pamoja na sadaka yake ya nafaka na ya divai kufuatana na maagizo yake. Kadhalika watu watatoa beberu mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. 25Kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya jumuiya yote ya Waisraeli, nao watasamehewa kwa sababu si kosa lililokusudiwa, na wameleta sadaka yao, sadaka ya kuteketeza kwa Mwenyezi-Mungu kama tambiko na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya kosa lao. 26Jumuiya yote ya Waisraeli, pamoja na wageni wanaoishi nao, watasamehewa kwa sababu wote walihusika na kosa hilo.
27“Mtu mmoja akifanya dhambi bila kujua, atatoa mbuzi jike wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuondoa dhambi. 28#Taz Lawi 4:27-31 Kuhani atafanya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu, kwa ajili ya huyo mtu aliyekosa bila kujua, naye atasamehewa. 29Mtafuata sheria moja kila mtu atakayekosea bila kukusudia, awe ni mwananchi Mwisraeli au ni mgeni anayeishi pamoja nanyi.
30“Lakini mtu yeyote atakayekosa kwa makusudi, awe mwananchi au mgeni, atakuwa anamdhihaki Mwenyezi-Mungu, na ni lazima akatiliwe mbali miongoni mwa watu wake. 31Maana amekataa yale aliyosema Mwenyezi-Mungu na kuvunja mojawapo ya amri zake. Mtu huyo atakatiliwa mbali kabisa; na lawama ya kifo chake itakuwa juu yake mwenyewe.”

Uvunjaji wa Sabato
32Siku moja, wakati Waisraeli walipokuwa jangwani, walimwona mtu mmoja akiokota kuni siku ya Sabato. 33Basi, mtu huyo akapelekwa mbele ya Mose, Aroni na jumuiya yote. 34Wao wakamweka kifungoni kwa sababu haikuwa bado imesemwa wazi namna ya kumfanya mtu wa namna hiyo. 35Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtu huyo lazima auawe; jumuiya yote itampiga mawe nje ya kambi.” 36Basi, watu wakamtoa nje ya kambi, wakampiga mawe mpaka akafa, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
Vishada katika ncha za nguo
37Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose: 38#Taz Kumb 22:12 “Waambie watu wa Israeli, uwaagize wajifanyie vishada katika ncha za mavazi yao, na kutia nyuzi za buluu juu ya kila kishada. Waambie wafanye hivyo katika vizazi vyao vyote vijavyo. 39Vishada hivyo vitakuwa kumbukumbu kwenu. Kila mtakapoviona, mtazikumbuka amri zangu zote na kuzifuata, ili msije mkafuata matakwa yenu na yale mnayoyaona kwa macho yenu wenyewe. 40Vishada hivyo vitawakumbusha amri zangu zote na mtazifuata zote kikamilifu, nanyi mtakuwa watakatifu wangu. 41Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa nchini Misri ili niwe Mungu wenu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”
Hesabu15;1-41



Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: