Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 25 July 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..16

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Mungu yu wetu yu mwema sana..tumshukuru na kumsifu ..!
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!
Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Baba yetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Jehovah,Yahweh,Alpha na Omega,Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni..
Tunakusifu na kukuabudu..Utukuzwe Baba wa Mbinguni..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Neema/Rehema zako Baba ni za Ajabu..!

Sio sisi, ee Mwenyezi-Mungu, sio sisi; bali wewe peke yako utukuzwe, kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako. Kwa nini mataifa yaseme: “Mungu wenu yuko wapi?” Mungu wetu yuko mbinguni; yeye hufanya yote anayotaka. Miungu yao ni ya fedha na dhahabu; imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu. Ina vinywa, lakini haisemi. Ina macho, lakini haioni. Ina masikio, lakini haisikii. Ina pua, lakini hainusi. Ina mikono, lakini haipapasi. Ina miguu, lakini haitembei. Haiwezi kamwe kutoa sauti. Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo, kadhalika na wote wanaoitumainia. Enyi Waisraeli, mtumainieni Mwenyezi-Mungu; yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Enyi wazawa wa Aroni, mtumainieni Mwenyezi-Mungu; yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, mtumainini, yeye ndiye msaada wenu na ngao yenu. Mwenyezi-Mungu atukumbuka na atatubariki; atawabariki watu wa Israeli, atawabariki wazawa wa Aroni. Atawabariki wote wamchao, atawabariki wakubwa na wadogo. Mwenyezi-Mungu awajalieni muongezeke; awajalieni muongezeke nyinyi na wazawa wenu! Mbarikiwe na Mwenyezi-Mungu, aliyeziumba mbingu na dunia. Mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu, bali dunia amewapa binadamu. Wafu hawamsifu Mwenyezi-Mungu, wala wale wanaoshuka katika nchi ya kimya. Lakini sisi tulio hai twamsifu Mwenyezi-Mungu; tutamsifu sasa na hata milele. Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Mfalme wa Amani,Baba wa Upendo,Baba wa Rehema,Muweza wa yote..
Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizoziwaza,tulizozinena,tulizozitenda kwa kujua/kutojua..
Jehovha nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea..Utuepushe katika majaribu Mungu wetu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase Miili yetu na Akili zetu kwa damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tupate kutambua/kujitambua...
Tusimamie Neno lako  Sheria na Amri zako Mungu Baba..
Tukapate kupendana na kuhurumiana,ukatuepushe na visasi na magomvi,chuki,wivu,uongo,ugombanishi na mabishano yasiyo na maana...


Basi, wakumbushe watu wako mambo haya na kuwaonya mbele ya Mungu waache ubishi juu ya maneno. Ubishi huo haufai, ila huleta tu uharibifu mkuu kwa wale wanaousikia. Jitahidi kupata kibali kamili mbele ya Mungu kama mfanyakazi ambaye haoni haya juu ya kazi yake na ambaye hufundisha sawa ule ujumbe wa kweli. Jiepushe na majadiliano yasiyofaa na ya kipumbavu; kwani hayo huzidi kuwatenga watu mbali na Mungu. Mafundisho ya aina hiyo ni kama donda linalokula mwili. Miongoni mwa hao waliofundisha hayo ni Humenayo na Fileto. Hawa wamepotoka kabisa mbali na ukweli, na wanatia imani ya watu wengine katika wasiwasi kwa kusema ati ufufuo wetu umekwisha fanyika. Lakini msingi thabiti uliowekwa na Mungu uko imara, na juu yake yameandikwa maneno haya: “Bwana anawafahamu wale walio wake,” na “Kila asemaye yeye ni wa Bwana, ni lazima aachane na uovu.” Katika nyumba kubwa kuna mabakuli na vyombo vya kila namna: Vingine ni vya fedha na dhahabu, vingine vya mbao na udongo, vingine vya matumizi ya heshima na vingine kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Basi, kama mtu atajitakasa kwa kujitenga mbali na mambo hayo yote maovu, atakuwa chombo cha matumizi ya pekee, kwa sababu amewekwa wakfu, anamfaa Bwana wake na yupo tayari kwa kila kazi njema. Jiepushe na tamaa za ujana, fuata uadilifu, imani, upendo, amani, pamoja na watu wote ambao wanamwomba Bwana kwa moyo safi. Epuka ubishi wa kijinga na kipumbavu; wajua kwamba hayo huleta magomvi. Mtumishi wa Bwana asigombane. Anapaswa kuwa mpole kwa watu wote, mwalimu mwema na mvumilivu, ambaye ni mpole anapowaonya wapinzani wake, kwani huenda Mungu akawajalia nafasi ya kutubu, wakapata kuujua ukweli. Hapo fahamu zao zitawarudia tena, wakaponyoka katika mtego wa Ibilisi aliyewanasa na kuwafanya wayatii matakwa yake.

Mungu wetu ukatufanye barua njema na tukasome sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba utubariki na kubariki yote tunayoenda kufanya/kutenda na tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu na ukatupe sawasaswa na mapenzi yako..Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi utupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji..
Asante Baba wa Mbinguni yote tutayaweka mikononi mwako Mungu wetu tuliyoyanena na tusiyoyanena Baba wa Mbinguni yote unayajua na kutujua vyema kuliko tujijuavyo sisi..
Sifa na utukufu utunakurudishia Muumba wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asante sana wapendwa/waungwana kwa kuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki katika yote..
Mkono wake wenye nguvu na uponyaji ukawaguse..
Msipungukiwe katka mahitaji yenu Mungu akawape kama itakavyompendeza yeye..
Nawapenda.



Uasi wa Kora, Dathani na Abiramu

1 # Taz Yuda 11 Baadaye Kora mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu pamoja na watu watatu wa ukoo wa Reubeni: Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, 2hao wote waliungwa mkono na viongozi mashuhuri 250 waliochaguliwa na jumuiya yote, wakamwasi Mose. 3Walikusanyika mbele ya Mose na Aroni, wakawaambia, “Nyinyi mmepita kikomo! Jumuiya yote ni takatifu na kila mtu katika jumuiya hii ni mtakatifu, na Mwenyezi-Mungu yu pamoja nasi sote. Mbona sasa nyinyi mnajifanya wakuu wa jumuiya ya Mwenyezi-Mungu?”
4Mose aliposikia hayo, alijitupa chini kifudifudi. 5Kisha akamwambia Kora na wafuasi wake, “Kesho asubuhi, Mwenyezi-Mungu ataonesha ni nani aliye wake na ni nani aliye mtakatifu, naye atakayemchagua, atamwezesha kukaribia madhabahuni. 6Basi, fanyeni hivi: Asubuhi, wewe pamoja na wafuasi wako, mtachukua vyetezo, 7mweke makaa ya moto ndani na kutia ubani juu yake, kisha mtavipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu. Halafu tutaona ni nani aliyechaguliwa na Mwenyezi-Mungu. Nyinyi Walawi mmepita kikomo!”
8Mose akaendelea kumwambia Kora, “Sikilizeni, enyi Walawi! 9Je, mnaona ni jambo dogo kwenu kwamba Mungu wa Israeli amewateua nyinyi miongoni mwa jumuiya ya Israeli, ili muweze kumkaribia, mhudumie katika hema la Mwenyezi-Mungu na kuihudumia na kuitumikia jamii yote? 10Amewatunukia heshima ya kuwa karibu naye, nyinyi pamoja na Walawi wenzenu wote. Sasa mnataka kunyakua hata ukuhani? 11Kwa hiyo wewe na kundi lako mnamshambulia Mwenyezi-Mungu. Nyinyi mnamnungunikia Aroni, lakini ukweli ni kwamba mnanungunika dhidi ya Mungu.”
12Mose alituma ujumbe kwa Dathani na Abiramu wana wa Eliabu ili waitwe, lakini wao wakasema, “Hatutakuja! 13Je, ni jambo dogo kwamba umetutoa Misri, nchi inayotiririka maziwa na asali, ili uje kutuua humu jangwani? Tena, unajifanya mkuu wetu! 14Zaidi ya hayo, hukutuleta kwenye nchi inayotiririka maziwa na asali, wala kutupatia urithi wa mashamba na mashamba ya mizabibu. Unafikiri utawafanya hawa watu kuwa vipofu? Hatutakuja!”
15Mose alikasirika mno, akamwambia Mwenyezi-Mungu “Usizikubali sadaka za watu hawa. Mimi sijachukua punda wa mtu yeyote, wala sijamdhuru mtu!”
16Mose akamwambia Kora, “Kesho usikose kuja pamoja na wafuasi wako mbele ya Mwenyezi-Mungu. Aroni pia atakuwapo. 17Kila mmoja wenu achukue chetezo chake, na kutia ubani, kisha atakipeleka mbele ya Mwenyezi-Mungu; kwa jumla vitakuwa vyetezo 250; wewe pia na Aroni, kila mmoja atakuwa na chetezo chake.”
18Basi, kila mmoja wao akachukua chetezo chake, akatia makaa ya moto na ubani, kisha wakaenda na kusimama mlangoni mwa hema la mkutano, pamoja na Mose na Aroni. 19Naye Kora akawakusanya watu wote pamoja, wakasimama mbele ya Mose na Aroni ambao walikuwa mlangoni mwa hema la mkutano. Ndipo utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea watu wote! 20Hapo Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, 21“Jitengeni na watu hawa, niwaangamize sasa hivi.”
22Lakini Mose na Aroni wakajitupa chini kifudifudi na kusema, “Ee Mwenyezi-Mungu uliye asili ya uhai wa binadamu wote. Je, mtu mmoja akikukosea, utaikasirikia jumuiya nzima?” 23Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 24“Waambie watu waondoke karibu na makao ya hema ya Kora, Dathani na Abiramu.”
25Basi, Mose akaenda kwa Dathani na Abiramu, akifuatwa na wazee wa Israeli. 26Alipofika, akawaambia watu, “Tafadhalini ondokeni kwenye hema za watu hawa waovu na msiguse kitu chao chochote, msije mkaangamizwa pamoja nao kwa sababu ya dhambi zao zote.” 27Watu wakaondoka kwenye makao ya Kora, Dathani na Abiramu.
Dathani na Abiramu wakatoka mahemani mwao na kusimama mlangoni wakiandamana na wake zao na watoto wao wote hata wale wanaonyonya. 28Hapo Mose akawaambia watu, “Hivi ndivyo mtakavyotambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyenituma kufanya mambo haya yote, wala siyo kwa matakwa yangu mwenyewe. 29Watu hawa wakifa kifo cha kawaida, au wakipatwa na maafa kama watu wengine, basi jueni kuwa Mwenyezi-Mungu hakunituma. 30Lakini Mwenyezi-Mungu akifanya jambo ambalo halijapata kutendeka, ardhi ikafunuka na kuwameza watu hawa pamoja na kila kitu chao, wakaenda kuzimu wakiwa hai, basi mtajua kuwa watu hawa wamemdharau Mwenyezi-Mungu.”
31Mara tu alipomaliza kusema maneno hayo yote, ardhi chini ya Dathani na Abiramu ikafunuka 32kuwameza watu hao, jamaa zao, pamoja na wafuasi wote wa Kora na mali zao zote. 33Basi, wao, pamoja na vyote vilivyokuwa vyao wakashuka kuzimu hali wangali hai. Ardhi ikawafunika, wote wakatoweka. 34Waisraeli wote wengine waliokuwa karibu waliposikia vilio vyao walikimbia wakisema, “Tukimbie, ardhi isije ikatumeza na sisi pia.”
35Kisha Mwenyezi-Mungu akapeleka moto ukawateketeza wale watu 250 waliokwenda kufukiza ubani.

Vyetezo

36Baada ya hayo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 37“Mwambie Eleazari mwana wa kuhani Aroni avitoe hivyo vyetezo penye moto, akautapanye mbali moto uliomo ndani, maana vyetezo hivyo ni vitakatifu. 38Vimekuwa vitakatifu kwa sababu watu hawa walivileta madhabahuni pa Mwenyezi-Mungu. Basi, vichukue vyetezo vya watu hao waliouawa kwa sababu ya dhambi zao, vifuliwe kuwa vyembamba ili viwe kifuniko cha madhabahu. Hili litakuwa onyo kwa Waisraeli wote.” 39Basi, kuhani Eleazari alivichukua vyetezo hivyo vya shaba ambavyo vililetwa mbele ya Mwenyezi-Mungu na wale watu walioteketezwa vikafuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu. 40Hili lilikuwa onyo kwa Waisraeli kwamba mtu yeyote ambaye si kuhani, yaani asiye wa ukoo wa Aroni asiende madhabahuni kumfukizia Mwenyezi-Mungu ubani. La sivyo ataangamizwa kama Kora na wafuasi wake. Haya yote yalitendeka kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Eleazari kwa njia ya Mose.

Aroni awaokoa watu

41Kesho yake, Waisraeli wote walimnungunikia Mose na Aroni wakisema, “Mmewaua watu wa Mwenyezi-Mungu.” 42Walipokusanyika mbele ya Mose na Aroni ili kutoa malalamiko yao, waligeuka kuelekea hema la mkutano, wakaona kuwa wingu limeifunika hema na utukufu wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa umetokea hapo. 43Mose na Aroni walikwenda, wakasimama mbele ya hema la mkutano, 44na Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 45“Jitenge na watu hawa, niwaangamize mara moja!”
Lakini wao wakajitupa chini kifudifudi. 46Mose akamwambia Aroni, “Chukua chetezo chako, kitie moto na kukiweka kando ya madhabahu, kisha ukitie ubani halafu uende nacho haraka kwa watu na kuwafanyia upatanisho. Fanya haraka! Ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imekwisha wafikia na pigo limeanza kuwashambulia.” 47Basi, Aroni akafanya kama alivyoambiwa na Mose. Alichukua chetezo chake na kukimbia hadi katikati ya watu waliokuwa wamekusanyika pamoja. Alipoona kwamba pigo limekwisha anza, alitia ubani katika chetezo na kuwafanyia watu upatanisho. 48Alipofanya hivyo, pigo hilo lilikoma, naye akabaki katikati ya waliokufa na walio hai. 49Idadi ya watu waliokufa kwa pigo ilikuwa 14,700, bila kuhesabu wale waliokufa kutokana na uasi wa Kora. 50Pigo lilipokoma, Aroni alirudi kwa Mose mlangoni mwa hema la mkutano.
Hesabu16;1-50


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: