Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 10 July 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..5



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Baba wa Rehema,Baba wa Upendo, Alpha na Omega..!
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuamsha salama na wenye afya..
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana au niwajuaji sana..
Si kwanguvu au uwezo wetu hapana Mungu wetu ni kwa Neema/Rehema zako tuu..kuwa hivi tulivyo...

Natazama juu milimani; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu watoka kwa Mwenyezi-Mungu, aliyeumba mbingu na dunia. Hatakuacha uanguke; mlinzi wako hasinzii. Kweli mlinzi wa Israeli hasinzii wala halali. Mwenyezi-Mungu ni mlinzi wako; yuko upande wako wa kulia kukukinga. Mchana jua halitakuumiza, wala mwezi wakati wa usiku. Mwenyezi-Mungu atakukinga na baya lolote; atayalinda salama maisha yako. Mwenyezi-Mungu atakulinda katika shughuli zako zote tangu sasa na hata milele.

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu
Tulizoziwaza,tulizozinena,tulizozitenda kwakujua/kutojua..
Baba wa Rehema tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea...

Basi, habari tuliyoisikia kwake Yesu na tunayowahubirieni ndiyo hii: Mungu ni mwanga na hamna giza lolote ndani yake. Tukisema kwamba tuna umoja naye, na papo hapo tunaishi gizani, tutakuwa tumesema uongo wala hatuishi kwa ukweli kwa maneno na matendo. Lakini tukiishi katika mwanga, kama naye alivyo katika mwanga, basi, tutakuwa na umoja sisi kwa sisi, na damu yake Yesu Kristo, Mwanae, inatutakasa dhambi zote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, tunajidanganya wenyewe, na ukweli haumo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, basi, Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote. Tukisema kwamba hatujatenda dhambi, tutakuwa tumemfanya Mungu mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.
Roho Mtakati akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako tunaomba utubariki na ukabariki nyumba zetu/Ndoa zetu,Familia,Ndugu na jamaa zetu..
Baba wa Upendo ukaonekane katika maisha yetu na tusipungukiwe katika mahitaji yetu..Basi ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Mfalme wa Amani ukabariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Ukatufanye chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..

Tazama wenyeshida/tabu,wanaopitia magumu/majaribu,waliokatika vifungo mbalimbali na wote wataabikao..Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye nguvu..ukawape uponyaji wa mwili na roho pia..
Ukawape Neema ya kukujua wewe na kufuata sheria zako..
wakasimamie neno lako nalo liwaweke huru...

Tumaini lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida, na kusali daima. Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu. Watakieni baraka wote wanaowadhulumu nyinyi; naam, watakieni baraka na wala msiwalaani. Furahini pamoja na wenye kufurahi, lieni pamoja na wenye kulia. Ishini kwa kupatana vema nyinyi kwa nyinyi. Msijitakie makuu, bali jishughulisheni na madogo. Msijione kuwa wenye hekima sana. Msilipe ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote. Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na watu wote.

Tunayaweka haya yote mikononi mwako Mungu wetu..
Sifa na utukufu tunakurudishia wewe..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wote mnaopitia hapa..
Mungu akawe nanyi daima na msipungukiwe katika mahitaji yenu..
Akawape kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.




Watu najisi

1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 2“Waamuru Waisraeli wamtoe nje ya kambi kila mtu mwenye ukoma, kila mtu anayetokwa usaha, na kila aliye najisi kwa kugusa maiti. 3Mtawatoa nje ya kambi watu wote hawa, wanaume kwa wanawake, ili wasije wakaitia najisi kambi yangu ninamokaa.” 4Waisraeli walifanya hivyo, wakawafukuza nje ya kambi. Kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Mose, ndivyo Waisraeli walivyofanya.

Toba baada ya kufanya makosa

5Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 6“Waambie Waisraeli kuwa: Mtu yeyote, mwanamume au mwanamke akitenda dhambi dhidi ya mtu, akakosa uaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, mtu huyo ana hatia; 7itambidi aungame dhambi yake aliyotenda. Lazima atoe fidia kamilifu kwa kosa lake, akiongeza asilimia ishirini ya fidia hiyo; atampa fidia hiyo yule aliyemkosea. 8Lakini ikiwa mtu huyo amefariki na hana jamaa wa karibu ambaye anaweza kupokea fidia hiyo, basi, fidia ya kosa itatolewa kwa Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya makuhani; malipo haya ni pamoja na kondoo dume wa upatanisho ambaye atatumiwa kumfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake. 9Michango yote na matoleo yote ambayo Waisraeli wataweka wakfu kwa Mungu na kumletea kuhani itakuwa yake huyo kuhani. 10Kila kitu kilichowekwa wakfu kwa Mungu na kupelekwa kwa kuhani kitakuwa chake.”#5:10 tafsiri si dhahiri na makala ya Kiebrania si dhahiri pia.

Kesi za wake wasio waaminifu kwa waume zao

11Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 12“Waambie Waisraeli: Kama mke wa mtu yeyote amepotoka akakosa uaminifu kwa mumewe, 13akalala na mtu mwingine bila ya mumewe au mtu mwingine yeyote kujua; amejitia najisi lakini hakuna mtu aliyeshuhudia kitendo chake kwa kuwa hakufumaniwa. 14Basi, mumewe akiingiwa na shaka na kuwa na wivu juu ya mkewe aliyejitia najisi; au kama amekuwa na wivu juu ya mke wake ingawa mkewe hakujitia najisi, 15basi wote wawili watakwenda kwa kuhani na kupeleka sadaka inayotakiwa, yaani sehemu ya kumi ya unga wa shayiri; lakini bila kuitia mafuta au ubani, kwa kuwa ni sadaka ya nafaka ya mume anayemshuku mkewe, sadaka inayotolewa kuhusu kosa ambalo linabainishwa.
16“Kuhani atampeleka huyo mwanamke karibu, na kumsimamisha mbele ya Mwenyezi-Mungu. 17Kisha, atamimina maji matakatifu katika chombo cha udongo na kutwaa vumbi kutoka sakafuni mwa hema takatifu na kuitia katika maji hayo ili kuyafanya machungu. 18Kuhani atamweka mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumfunua nywele na kumpa sadaka hiyo ya nafaka itolewayo kwa sababu ya shuku ya mumewe. Kuhani mwenyewe atashikilia kile chombo chenye maji machungu yaletayo laana. 19Halafu kuhani atamwapisha mwanamke huyo akisema: ‘Ikiwa hukulala na mwanamume mwingine, ukajitia najisi hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, basi, hutapatwa na laana iletwayo na maji haya machungu. 20Lakini kama umepotoka hali uko chini ya mamlaka ya mumeo, ukajitia najisi kwa kulala na mwanamume mwingine asiye mume wako, 21#5:21 Aya hii katika Kiebrania inaanza na: Kuhani na amwapishe kiapo cha laana na kumwambia huyo mwanamke.Mwenyezi-Mungu na akuadhibu hata uwe laana na apizo miongoni mwa watu wako, uwe tasa na tumbo lako livimbe. 22Maji haya yaletayo laana na yaingie tumboni mwako na kukufanya tasa na tumbo lako livimbe.’ Naye mwanamke ataitikia, ‘Amina, Amina.’
23“Kisha kuhani ataandika laana hizi kitabuni na kuzioshea katika maji machungu; 24naye atamnywesha mwanamke hayo maji machungu yaletayo laana nayo yataingia ndani yake na kumletea maumivu makali; 25kisha kuhani atachukua ile sadaka ya nafaka ya wivu mikononi mwa mwanamke huyo na kuitikisa mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuipeleka madhabahuni. 26Halafu, atatwaa konzi moja ya sadaka hiyo ya nafaka kwa ukumbusho na kuiteketeza madhabahuni. Hatimaye atamnywesha mwanamke maji hayo. 27Akisha kunywa, kama amejitia najisi na hakuwa mwaminifu kwa mume wake, maji hayo yaletayo laana yatamletea maumivu makali sana; mwili wake utavimba na tumbo lake la uzazi litaharibika. Mwanamke huyo atakuwa laana miongoni mwa watu wake. 28Lakini kama mwanamke huyo hajajitia unajisi na hana hatia, basi hatadhurika na ataweza kupata watoto.
29“Basi, hii ndiyo sheria kuhusu kesi za wivu iwapo mwanamke, ingawa yu chini ya mamlaka ya mumewe, atapotoka na kujitia unajisi, 30au wakati mwanamume ashikwapo na wivu na kumshuku mkewe. Atamsimamisha mwanamke huyo mbele ya Mwenyezi-Mungu, na kuhani atatekeleza masharti yote ya sheria hii. 31Mumewe hatakuwa na hatia yoyote, lakini mwanamke atawajibika kwa uovu wake.”

Hesabu5;1-31


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: