Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 4 July 2017

Kikombe Cha Asubuhi;Leo tunaanza kitabu cha Hesabu..1



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu..
Asante Mungu wetu, Baba yetu kwa ulinzi wako na kutuamsha salama..
Asante kwa kutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tunakuja mbele zako Mungu wetu,Tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizoziwaza,tulizozinena,tulizozitenda,tunazozijua/tusizozijua..
Jehovah tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukoasea..
Utuepushe na majaribu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu kwa Damu ya Mwanao Mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu..
Aliumizwa kwasababu ya maovu yetu...
Kwakuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai..
Kwakupigwa kwake sisi tumepona...!!!
Mwanadamu yupi anayeweza kujitoa kiasi hiki?
Nani anaweza kuvumilia haya yote kwa sababu wewe upate kupona/usamehewe dhambi?..

Si kwamba sisi tulikuwa tunampenda Mungu kwanza..
Bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kuondolea dhambi zetu..
Wapenzi wangu ikiwa Mungu alitupenda hivyo,basi nasi tunapaswa kupendana...[1Yohane 4:10-11]

Nani aliyeamini mambo tuliyosikia? Nani aliyetambua kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu ulihusika? Maana, mbele yake Mwenyezi-Mungu, mtumishi wake alikua kama mti mchanga, kama mzizi katika nchi kavu. Hakuwa na umbo wala sura ya kutupendeza, wala hakuwa na uzuri wowote wa kutuvutia. Alidharauliwa na kukataliwa na watu, alikuwa mtu wa uchungu na huzuni. Alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu; alidharauliwa na tukamwona si kitu. Hata hivyo alivumilia majonzi yetu, na kubeba huzuni zetu. Sisi tulifikiri amepata adhabu, amepigwa na Mungu na kuteswa. Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu, aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu. Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai; kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote tumepotea kama kondoo, kila mmoja wetu ameelekea njia yake. Lakini Mwenyezi-Mungu alimtwika adhabu, ambayo sisi wenyewe tuliistahili. Alidhulumiwa na kuteswa, lakini alivumilia kwa unyenyekevu, bila kutoa sauti hata kidogo. Alikuwa kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni, kama kondoo akaavyo kimya anapokatwa manyoya. Hakutoa sauti hata kidogo. Alidhulumiwa, akahukumiwa na kupelekwa kuuawa; na hakuna mtu aliyejali yanayompata. Alifukuzwa kutoka nchi ya walio hai, kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Walimzika pamoja na wahalifu; katika kifo aliwekwa pamoja na matajiri, ingawa hakutenda ukatili wowote, wala hakusema neno lolote la udanganyifu. Mwenyezi-Mungu alipenda kumwumiza na kumweka katika huzuni. Alijitoa mhanga kwa ajili ya kuondoa dhambi. Mtumishi wa Mungu atakuwa na wazawa; ataishi maisha marefu. Yeye ndiye atakayetimiza mpango wa Mwenyezi-Mungu. Mungu asema: “Baada ya kutaabika sana, mtumishi wangu atafurahi. Kwa kuwajibika kwake kikamilifu, atatosheka na matokeo hayo. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwadilifu atawafanya wengi wawe waadilifu Yeye atazibeba dhambi zao. Kwa hiyo, nitamweka katika cheo cha wakuu, atagawa nyara pamoja na wenye nguvu; kwa kuwa alijitolea mwenyewe kufa, akawekwa katika kundi moja na wakosefu, alizibeba dhambi za watu wengi, akawaombea msamaha hao wakosefu.”

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na Upendo wa kweli,Utuwema,Fadhili,Hekima,Busara,kuchukuliana,Upole na kiasi..

Jehovah..! tunakabidhi nyumba zetu,Ndoa na familia vyote mikononi mwako..
Ukatubariki na kubariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende sawasawa na mapenzi yako...

Asante Mungu wetu kwa neema ya kusoma Neno lako..
Tumemaliza/tumepitia na kujifunza mengi katika kitabu cha walawi na Leo tunaanza Kitabu hiki cha Hesabu..Mungu wetu tunaomba tukaelewe na kusimamia yote tunayojifunza..isiwe tunasoma tuu kama gazeti au hadithi..
Mungu wetu tunaomba Neno lako likakae ndani yetu na likawe kinga..
likatufae sisi na wengine pia..
Tukapate shauku/hamu ya kujifunza zaidi na kujua ukuu wako Mungu wetu...
Na tuendane/tufuate Amri na sheria zako Mungu wetu..
Ukatupe macho ya kuona zaidi,Masikio ya kusikia na akili ya kutambua/kujitambua katika mema na mabaya...
Tunakushukuru na kukusifu daima..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Wapendwa/waungwana asanteni sana..
Mungu aendelee kuwabariki..
Asanteni kwakuwa pamoja na Mungu akatuongoze
Msipungukiwe katika mahitaji yenu na Mungu akawape sawasawa na mapenzi yake...
Nawapenda.

Hesabu ya kwanza ya Waisraeli

1 # Taz Hes 26:1-51 Mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa pili, mwaka wa pili baada ya wana wa Israeli kutoka Misri, Mwenyezi-Mungu aliongea na Mose ndani ya hema la mkutano jangwani Sinai, akamwambia hivi: 2“Wewe na Aroni fanyeni sensa ya jumuiya yote ya Waisraeli, familia mojamoja kwa kufuata koo zao na idadi ya majina yao kila mwanamume mmojammoja; 3wale wote katika Israeli wanaoweza kwenda vitani, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, mtawaweka katika orodha ya vikosi vikosi. 4Tena mwanamume mmoja wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi, kila mmoja aliye kiongozi wa jamaa za kabila lake. 5Haya ndiyo majina ya watu watakaokusaidia:
Kabila la Reubeni: Elisuri, mwana wa Shedeuri;
6Kabila la Simeoni: Shelumieli mwana wa Suri-shadai;
7Kabila la Yuda: Nashoni mwana wa Aminadabu;
8Kabila la Isakari: Nethaneli mwana wa Suari;
9Kabila la Zebuluni: Eliabu mwana wa Heloni;
10Kabila la Efraimu: Elishama mwana wa Amihudi;
Kabila la Manase: Gamalieli mwana wa Pedasuri;
11Kabila la Benyamini: Abidani mwana wa Gideoni;
12Kabila la Dani: Ahiezeri mwana wa Amishadai;
13Kabila la Asheri: Pagieli mwana wa Okrani;
14Kabila la Gadi: Eliasafu mwana wa Deueli;
15Kabila la Naftali: Ahira mwana wa Enani.”
16Hawa ndio viongozi waliochaguliwa miongoni mwa jumuiya yote ya watu wa Israeli, kama viongozi wakuu wa makabila yao na viongozi wa koo za Israeli.
17Basi, Mose na Aroni wakawachukua watu hawa waliotajwa, 18na mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa pili, wakaikusanya jumuiya yote ya watu waliokuwa wamehesabiwa kila mmoja kulingana na familia yake na ukoo wake. Kufuatana na majina ya watu waliokuwa na umri wa miaka ishirini na zaidi, mmojammoja, 19kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose. Mose akawahesabu watu hawa kule jangwani Sinai.
20Watu waliotoka katika kabila la Reubeni aliyekuwa mzaliwa wa kwanza wa Israeli, kwa kufuata vizazi vyao, kulingana na familia zao na jamaa zao, kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, kila mwanamume aliyekuwa na umri wa miaka ishirini na zaidi, aliyefaa kuingia jeshini, 21walikuwa watu 46,500.
22Kutoka kabila la Simeoni kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 23walikuwa watu 59,300.
24Kutoka kabila la Gadi kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 25walikuwa watu 45,650.
26Kutoka kabila la Yuda kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 27walikuwa watu 74,600.
28Kutoka kabila la Isakari kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 29walikuwa watu 54,400.
30Kutoka kabila la Zebuluni kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 31walikuwa watu 57,400.
32Kutoka kabila la Efraimu, mwanawe Yosefu, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 33walikuwa watu 40,500.
34Kutoka kabila la Manase, mwanawe Yosefu, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi waliofaa kuingia jeshini, 35walikuwa watu 32,200.
36Kutoka kabila la Benyamini, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 37walikuwa watu 35,400.
38Kutoka kabila la Dani kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 39walikuwa watu 62,700.
40Kutoka kabila la Asheri, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina yao mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 41walikuwa watu 41,500.
42Kutoka kabila la Naftali, kwa kufuata vizazi vyao kulingana na familia zao na jamaa zao kadiri ya jumla ya majina ya mmojammoja, wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini, 43walikuwa watu 53,400.
44Hawa ndio watu waliokuwa wamehesabiwa ambao Mose na Aroni waliwahesabu wakisaidiwa na wale viongozi kumi na wawili wa Israeli, kila kiongozi akiwakilisha ukoo wake. 45Hivyo jumla ya wanaume wote wa Israeli wenye umri kuanzia miaka ishirini na zaidi, waliofaa kuingia jeshini nchini Israeli 46ilikuwa watu 603,550.
47Lakini Walawi hawakuhesabiwa pamoja na yale makabila mengine, 48kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, 49“Usihesabu kabila la Lawi wala usiwafanyie sensa kati ya watu wa Israeli; 50bali utawateua wawe waangalizi wa hema la ushuhuda, vyombo vyake vyote na kila kitu kilichomo ndani yake; watakuwa wakilibeba pamoja na vyombo vyake vyote. Watahudumu humo ndani na kupiga kambi yao kwa kulizunguka. 51Tena wakati wa hema kungolewa Walawi ndio watakaolingoa na wakati wa hema kusimikwa Walawi ndio watakaolisimamisha. 52Waisraeli wengine wote watapiga kambi zao makundimakundi, kila mtu katika kundi lake na chini ya bendera yake. 53Lakini Walawi watapiga kambi zao kulizunguka hema la maamuzi, wakililinda ili mtu yeyote asije akalikaribia na kusababisha ghadhabu yangu kuwaka dhidi ya jumuiya ya watu wa Israeli; basi Walawi watalitunza hema la maamuzi.” 54Kwa hiyo Waisraeli wakafanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.
Hesabu1;1-54


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: