Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 24 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 2 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi..
Mfalme wa Amani,Mlinzi wetu,Muweza wa Yote..
Baba wa Yatima Mume wa Wajane,Alfa na Omega..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Usifiwe Mungu wetu,Uhimidimiwe Baba..
Hakuna kama wewe,Matendo yako ni ya Ajabu Unatosha Mungu wetu..

Sikieni mafundisho yangu, enyi watu wangu; yategeeni sikio maneno ya kinywa changu. Nitasema nanyi kwa mafumbo, nitasema mambo yaliyofichika tangu kale; mambo tuliyoyasikia na kuyajua, mambo ambayo wazee wetu walitusimulia. Hatutawaficha watoto wetu; ila tutakisimulia kizazi kijacho matendo matukufu ya Mwenyezi-Mungu na uwezo wake; tutawaambia maajabu yake aliyotenda. Aliwapa wazawa wa Yakobo masharti, aliweka sheria katika Israeli, ambayo aliwaamuru wazee wetu wawafundishe watoto wao; ili watu wa kizazi kijacho, watoto watakaozaliwa baadaye, wazijue, nao pia wawajulishe watoto wao, ili wamwekee Mungu tumaini lao, wasije wakasahau matendo ya Mungu, bali wazingatie amri zake.


Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena kuendelea kuiona Leo hii..
Si kwa nguvu zetu wala si kwa ujuzi/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo..
Ni kwa neema /rehema zako Muumba wetu..

Tunakuja mbele zako Baba yetu tukijishusha,tukijinyenyekeza na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mungu wetu..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale walio tukosea..
Utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Ututakase Miili yetu na Akili zetu Baba utufunike na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Yahweh tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu tukatumike kama ipasavyo.

Mwimbieni kwa sauti Mungu, nguvu yetu, mshangilieni Mungu wa Yakobo; vumisheni wimbo wa shangwe, pigeni ngoma, chezeni zeze na kinubi cha sauti nzuri. Pigeni tarumbeta kutangaza mwezi mwandamo, na pia mwezi mpevu, wakati wa sikukuu yetu. Hiyo ndiyo kanuni katika Israeli; hilo ndilo agizo la Mungu wa Yakobo. Aliwapa watu wa Israeli agizo hilo, alipoishambulia nchi ya Misri. Nasikia sauti nisiyoitambua ikisema: “Mimi nilikutua mizigo yako mabegani, nilikuondolea matofali uliyochukua mikononi. Ukiwa shidani uliniita, nami nikakuokoa. Nilikujibu nikiwa mafichoni katika ngurumo. Nilikujaribu kwenye maji ya Meriba. Enyi watu wangu, sikieni onyo langu. Laiti ungenisikiliza, ee Israeli! Asiwepo kwako mungu wa kigeni; usiabudu kamwe mungu mwingine. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri. Fumbua kinywa chako, nami nitakulisha. “Lakini watu wangu hawakunisikiliza; Israeli hakunitaka kabisa. Hivyo, nikawaacha wabaki na ukaidi wao; wafuate mashauri yao wenyewe. Laiti watu wangu wangenisikiliza! Laiti Israeli angefuata njia yangu! Ningewashinda maadui zao haraka; ningenyosha mkono dhidi ya wadhalimu wao. Wanichukiao wangenipigia magoti kwa hofu, na adhabu yao ingekuwa ya milele. Lakini wewe ningekulisha kwa ngano bora, ningekushibisha kwa asali ya mwambani.”


Tazama wenye shida/tabu na wote wanaopitia magumu/majaribu..
Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye nguvu,ukawaponye kimwili na kiroho pia..
ukawape neema ya kukujua wewe na kusimamia Neno lako..
Baba wa Mbinguni ukaonekane kwenye taabu zao..

Jinsi gani yanavyopendeza makao yako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi! Nafsi yangu yatamani mno maskani ya Mwenyezi-Mungu! Moyo na mwili wangu wote wamshangilia Mungu aliye hai. Hata shomoro wamepata makao yao, mbayuwayu wamejenga viota vyao, humo wameweka makinda yao, katika madhabahu zako, ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu! Heri wale wanaokaa nyumbani mwako, wakiimba daima sifa zako. Heri watu wanaopata nguvu zao kwako, wanaotamani kwenda kuhiji mlimani kwako. Wapitapo katika bonde kavu la Baka, hulifanya kuwa mahali pa chemchemi, na mvua za vuli hulijaza madimbwi. Wanaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi; watamwona Mungu wa miungu huko Siyoni. Usikie sala yangu ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi; unitegee sikio, ee Mungu wa Yakobo. Ee Mungu, umwangalie kwa wema ngao yetu mfalme, umtazame huyo uliyemweka wakfu kwa mafuta. Siku moja tu katika maskani yako, ni bora kuliko siku elfu mahali pengine; afadhali kusimama mlangoni pa nyumba yako, kuliko kuishi nyumbani kwa watu waovu. Mwenyezi-Mungu ni jua letu na ngao yetu; yeye hutuneemesha na kutujalia fahari. Hawanyimi chochote kilicho chema, wale waishio kwa unyofu. Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, heri mtu yule anayekutumainia wewe!

Tumaini,Amani,Upendo,Uzima, Maarifa,Hekina na Busara vina wewe Mungu wetu..
Asante Mungu wetu,Sifa na utukufu tunakurudishia wewe..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana sana wapendwa/waumgwa kwakuwa nami
Mungu andelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.



Miaka kadhaa jangwani

1“Kisha, tuligeuka, tukasafiri jangwani kwa kupitia njia ya Bahari ya Shamu, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniambia; tulitangatanga karibu na mlima Seiri kwa muda mrefu. 2Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, 3‘Mmetangatanga vya kutosha katika nchi hii ya milima; sasa geukeni mwelekee kaskazini. 4Mko karibu kupita katika nchi ya milima ya Seiri, nchi ya ndugu zenu wazawa wa Esau. Hao watawaogopeni, lakini muwe na tahadhari, 5msipigane nao kwa sababu sitawapeni sehemu yoyote ya nchi yao. Sitawapeni hata mahali padogo pa kukanyaga. Nchi hiyo ya milima ya Seiri nimewapa wazawa wa Esau iwe mali yao. 6Mkitaka chakula au maji kutoka kwao, lazima mnunue.’
7“Basi, kumbukeni jinsi Mwenyezi-Mungu Mungu wenu alivyowabariki katika kila jambo mlilofanya. Aliwatunza mlipokuwa mnatangatanga katika jangwa hili kubwa. Amekuwa pamoja nanyi miaka hii yote arubaini na hamkupungukiwa kitu chochote.
8“Hivyo tuliendelea na safari yetu, tukawapita ndugu zetu, wazawa wa Esau ambao waliishi Seiri, tukaiacha nyuma ile njia ya Araba na pia miji ya Elathi na Esion-geberi. Kisha tukageuka tukafuata njia ya kupitia nyika ya Moabu. 9Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Usiwasumbue watu wa Moabu, wala usipigane nao maana sitawapeni sehemu yoyote ya nchi yao. Ila eneo hilo la Ari nimewapa hao wazawa wa Loti liwe mali yao.’ 10(Hapo zamani hiyo nchi ya Ari ilikuwa imekaliwa na watu wengi, wenye nguvu na ambao walikuwa warefu kama Waanaki. 11Kama vile Waanaki, watu hawa walijulikana pia kama Warefai, lakini Wamoabu waliwaita Waemi. 12Wahori pia waliishi huko Seiri hapo awali, lakini wazawa wa Esau waliwafukuza na kuwaangamiza, kisha wao wenyewe wakakaa katika eneo hilo badala yao. Waisraeli walifanya vivyo hivyo katika nchi ile ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa iwe mali yao).
13“Mwenyezi-Mungu akatuambia: ‘Ondokeni sasa, mvuke kijito Zeredi’. Basi, tukavuka kijito cha Zeredi. 14Miaka thelathini na nane ilikuwa imepita tangu kuondoka Kadesh-barnea mpaka kuvuka kijito cha Zeredi. Wakati huo, kizazi chote cha wale watu wa umri wa kwenda vitani kilikuwa kimetoweka kulingana na jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowaapia. 15Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwakabili ili kuwaangamiza huko kambini, hata wote wakaisha.
16“Basi, watu hao wote wenye umri wa kwenda vitani walipokwisha aga dunia, 17Mwenyezi-Mungu aliniambia, 18‘Leo hii mtauvuka mpaka wa Moabu kwa kupitia nchi ya Ari. 19Mtaifikia nchi ya Waamoni. Msiwasumbue wala msipigane nao kwa kuwa sitawapeni sehemu yoyote ya hao wazawa wa Amoni; iwe mali yenu. La! Hao ni wazawa wa Loti, na nimewapa hiyo nchi iwe mali yao.’”
20(Nchi hiyo inajulikana pia kama nchi ya Warefai. Warefai walikuwa wanaishi huko hapo zamani; Waamoni waliwaita hao Wazamzumi. 21Walikuwa watu wengi, wenye nguvu na warefu kama Waanaki. Lakini Mwenyezi-Mungu aliwaangamiza walipofika Waamori ambao walichukua nchi yao wakaishi humo badala yao. 22Mwenyezi-Mungu alifanya kama alivyowafanyia wazawa wa Esau, Waedomu, ambao wanaishi katika nchi ya Seiri. Aliwaangamiza Wahori wakati Waedomu walipofika huko, wakainyakua nchi yao na kuishi humo hadi leo. 23Waavi walikuwa hapo awali wakiishi katika vijiji vya mwambao wa Mediteranea mpaka Gaza. Wakaftori kutoka kisiwa cha Kaptori wakawaangamiza, wakaishi humo badala yao).
24“Kisha Mwenyezi-Mungu alituamuru: ‘Haya! Anzeni safari. Vukeni bonde la Arnoni. Mimi nimemtia mikononi mwenu Sihoni, mfalme wa Waamori wa Heshboni na nchi yake. Mshambulieni na kuanza kuimiliki nchi yake. 25Leo nitaanza kuwafanya watu wote duniani wawe na woga na hofu juu yenu; watasikia habari zenu nao watatetemeka na kufadhaika.’

Waisraeli wamshinda mfalme Sihoni

(Hes 21:21-30)

26“Basi, nikatuma watu kutoka jangwa la Kedemothi waende kwa mfalme Sihoni wa Heshboni na ujumbe ufuatao wa amani: 27‘Turuhusu tupite katika nchi yako. Tutapitia barabarani na kwenda moja kwa moja bila kugeuka kulia wala kushoto. 28Chakula chetu tutakinunua kwako na maji ya kunywa pia. Tunachoomba tu ni ruhusa ya kupita kwa miguu nchini mwako, 29tuvuke mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu anatupatia. Wazawa wa Esau wanaoishi Seiri na Wamoabu waishio Ari walituruhusu pia kupita katika nchi yao’.
30“Lakini Sihoni, mfalme wa Heshboni, hakuturuhusu tupite nchini mwake. Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alimfanya awe na kichwa kigumu na mkaidi wa moyo, ili tumshinde na kuchukua nchi yake ambayo tunaimiliki hadi leo.
31“Halafu Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Tazama, nimeanza kumtia mfalme Sihoni na nchi yake mikononi mwenu; anzeni kuichukua nchi yake na kuimiliki’. 32Kisha Sihoni alitoka na watu wake wote kupigana nasi karibu na mji wa Yahasa. 33Naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, akamtoa, tukamshinda yeye, watoto wake na watu wake wote. 34Tukaiteka na kuiharibu miji yake yote, tukaua wanaume na wanawake na watoto; hatukumwacha mtu yeyote hai. 35Nyara zetu zilikuwa tu mifugo na mali yote tuliyokuta mijini. 36Kuanzia Aroeri, mji ulio ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ulio ndani ya bonde hili mpaka Gileadi, hakuna mji wowote uliokuwa imara hata tukashindwa kuuteka. Mwenyezi-Mungu aliitia yote mikononi mwetu. 37Lakini hatukukaribia nchi ya Waamoni au ukingoni mwa mto Yaboki wala katika miji ya nchi ya milima wala sehemu yoyote ile ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alitukataza.


Kumbukumbu la Sheria 2:1-37

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: