Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday 29 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 5 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ....!Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu katika yote..

Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu,Mlinzi wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Mungu wa Wajane na Yatima..
Alfa na Omega,Muweza wa yote,Hakuna kama wewe Baba wa Mbinguni..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Uhimidiwe Mfalme wa Amani..
Wewe ni msaada kwetu,Wewe ni kimbilio letu,Wewe ni mtetezi wetu..
Matendo yako ni ya ajabu,Unatosha Mungu wetu..!


Nitakutukuza, ee Mungu wangu na mfalme wangu; nitalitukuza jina lako daima na milele. Nitakutukuza kila siku; nitalisifu jina lako daima na milele. Mwenyezi-Mungu ni mkuu, astahili sifa nyingi; ukuu wake hauwezi kuchunguzika. Kizazi hata kizazi, sifa za matendo yako zitasimuliwa, watu watatangaza matendo yako makuu. Nitanena juu ya utukufu na fahari yako, nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Watu watatangaza ukuu wa matendo yako ya ajabu, nami nitatangaza ukuu wako. Watatangaza sifa za wema wako mwingi, na kuimba juu ya uadilifu wako. Mwenyezi-Mungu ni mwenye huruma na rehema; hakasiriki ovyo, amejaa fadhili. Mwenyezi-Mungu ni mwema kwa wote, ni mwenye huruma kwa viumbe vyake vyote. Viumbe vyako vyote vitakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, nao waaminifu wako watakutukuza. Watasema juu ya utukufu wa ufalme wako, na kutangaza juu ya nguvu yako kuu, ili kila mtu ajue matendo yako makuu, na fahari tukufu ya ufalme wako. Ufalme wako ni ufalme wa milele; mamlaka yako yadumu vizazi vyote. Mwenyezi-Mungu ni mwaminifu katika ahadi zake zote, ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu huwategemeza wote wanaoanguka; huwainua wote waliokandamizwa. Viumbe vyote vinakutazama kwa hamu, nawe wavipa chakula chao kwa wakati wake. Waufumbua mkono wako kwa ukarimu, watosheleza mahitaji ya kila kiumbe hai. Mwenyezi-Mungu ni mwadilifu katika njia zake zote; ni mwema katika matendo yake yote. Mwenyezi-Mungu yuko karibu na wote wanaomwomba, wote wanaomwomba kwa moyo mnyofu. Huwapatia mahitaji yao wote wanaomcha; husikia kilio chao na kuwaokoa. Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wanaompenda; lakini atawaangamiza waovu wote. Nitatangaza sifa za Mwenyezi-Mungu; viumbe vyote vilisifu jina lake takatifu, milele na milele.


Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa  kibali cha kuendelea kuiona siku hii..

Si kwamba sisi ni wema sana au sisi ni wenye nguvu,si kwa nguvu zetu wala utashi wetu ni kwa Neema/rehema zako Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo..

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote walio tukosea..
Ututakase miili yetu na akili zetu,Utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote,

Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Yaweh tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikonoi yetu..
ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
yote tunayokwenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..

Jishughulishe na biashara hata kama kwa kubahatisha; yawezekana baadaye ukapata chochote kile. Wagawie watu saba hata wanane sehemu yako, maana, hujui balaa litakalofika duniani. Mawingu yakijaa maji, mvua hunyesha; mti ukiangukia kusini au kaskazini, hapo uangukiapo ndipo ulalapo. Anayengoja upepo hatapanda mbegu, anayesubiri mawingu yatoweke, hatavuna kitu. Usivyojua jinsi uhai unavyoingia katika mifupa ya mtoto tumboni mwa mamake, kadhalika huwezi kuelewa matendo ya Mungu, ambayo hufanya kila kitu. Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri. Mwanga wafaa, na kuliona jua kwapendeza macho. Mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie miaka hiyo yote; lakini akumbuke kuwa siku za giza zitakuwa nyingi, na kwamba yote yatakayofuata ni bure. Ewe kijana, furahia ujana wako, moyo wako, uchangamke wakati ungali kijana. Fuata mapenzi ya moyo wako na upeo wa macho yako. Lakini kumbuka kwamba Mungu atakuhukumu kadiri ya hayo yote. Ondoa mahangaiko moyoni mwako, jikinge, usipate maumivu mwilini kwa sababu ujana na mwisho wa maisha ni bure kabisa.

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Ukatamalaki na kutuatamia,ukatulinde katika yote..
Baba wa mbinguni ukatufinyange na kutupa macho ya rohoni..
Ukatupe masikio ya kusikia sauti yako...
Jehovah ukatupe  neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako
tukapate kutambua/kujitambua,ukatupe neema ya Hekima,Busara,Upendo na tukadumu katika Pendo lako..


Ukatufanye chombo chema na tukatumike kama ipasavyo..


Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..




Baada ya hayo yote yaliyokwisha semwa bado kuna hili linalotakiwa: Mche Mungu, na uzishike amri zake; kwa sababu hilo ndilo jukumu aliloumbiwa binadamu. Maana, Mungu atahukumu matendo yetu yote, hata yale yanayotendwa kwa siri, yawe mema au mabaya.

Tazama wenye shida /tabu Mungu wetu na wote wanaotaabika..
Walio katika vifungo vya yule mwovu,waliokata tamaa,waliokataliwa..
wagonjwa na wenye Njaa..Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye nguvu,ukawaponye kimwili na kiroho pia,ukawape neema ya kusimamia Neno lako na ukawape maarifa na ufumbuzi..

ukaonekane Mungu katika mapito/majaribu yao..
Wafiwa ukawafiri Baba wa Mbinguni..

Nitawasimulia ndugu zangu matendo yako; nitakusifu kati ya kusanyiko lao: Enyi mnaomcha Mwenyezi-Mungu, msifuni! Mtukuzeni enyi wazawa wote wa Yakobo! Mcheni Mungu enyi wazawa wote wa Israeli! Maana yeye hapuuzi au kudharau unyonge wa mnyonge; wala hajifichi mbali naye, ila humsikia anapomwomba msaada. Kwa sababu yako ninakusifu katika kusanyiko kubwa la watu; nitatimiza ahadi zangu mbele yao wakuchao. Maskini watakula na kushiba; wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu watamsifu. Mungu awajalie kuishi milele! Ulimwengu wote utakumbuka na kumrudia Mwenyezi-Mungu; jamaa zote za mataifa zitamwabudu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mfalme; yeye anayatawala mataifa. Wenye kiburi wote duniani watasujudu mbele yake; wote ambao hufa watainama mbele yake, wote ambao hawawezi kudumisha uhai wao. Vizazi vijavyo vitamtumikia; watu watavisimulia habari za Mwenyezi-Mungu, watatangaza matendo yake ya wokovu. Watu wasiozaliwa bado wataambiwa: “Mwenyezi-Mungu ndiye aliyefanya hayo!”

Sifa na utukufu tunakurushia Mungu wetu..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Jehovah tuliyoyanena na tusiyoyanena yote  unayajua Mungu wetu..


Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Baba wa Upendo aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda..




Amri kumi

(Kut 20:1-17)

1Mose aliwaita pamoja Waisraeli, akawaambia: “Enyi Waisraeli, sikilizeni masharti na maagizo ambayo ninayatamka mbele yenu leo. Jifunzeni hayo na kuyatekeleza kwa uangalifu. 2Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alifanya agano nasi mlimani Horebu. 3Hakufanya agano hilo na wazee wetu tu, bali alifanya na sisi sote ambao tuko hai hivi leo. 4Mwenyezi-Mungu aliongea nanyi ana kwa ana huko mlimani katikati ya moto. 5Wakati huo mimi nilisimama kati yenu na Mwenyezi-Mungu, nikawatangazieni yale aliyoyasema, kwa kuwa nyinyi mliogopa ule moto na hamkupanda mlimani. Mwenyezi-Mungu alisema hivi,
6“ ‘Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako niliyekutoa katika nchi ya Misri, ambako ulikuwa mtumwa.
7“ ‘Usiwe na miungu mingine ila mimi.5:7 Usiwe … mimi: Au Usiwe na miungu mingine zaidi yangu.
8“ ‘Usijifanyie sanamu za miungu za kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.
9“ ‘Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu. Nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wale wanichukiao. 10Lakini nawafadhili maelfu ya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.
11“ ‘Usilitaje bure jina langu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako; maana mimi ni Mwenyezi-Mungu sitaacha kumwadhibu yeyote afanyaye hivyo. 12Adhimisha siku ya Sabato na kuiweka wakfu, kama mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nilivyokuamuru. 13Siku sita fanya kazi na tenda mambo yako yote, 14lakini siku ya saba ni siku ya Sabato ambayo imetengwa kwa ajili yangu. Siku hiyo wewe usifanye kazi yoyote, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako wa kiume na wa kike wapate kupumzika vilevile kama wewe. 15Usisahau kwamba wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, nami Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, nikakutoa huko kwa mkono wenye nguvu na mkono ulionyoshwa; ndiyo maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nimekuamuru kuiadhimisha siku ya Sabato.
16“ ‘Waheshimu baba yako na mama yako, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako nilivyokuamuru; fanya hivyo ili uishi siku nyingi na kufanikiwa katika nchi ambayo ninakupatia.
17“ ‘Usiue.
18“ ‘Usizini.
19“ ‘Usiibe.
20“ ‘Usimshuhudie jirani yako uongo.
21“ ‘Usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba yake, wala shamba lake, wala mtumwa wake wa kiume au wa kike, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu chochote alicho nacho jirani yako.’
22“Hizi ndizo amri Mwenyezi-Mungu alizowaambieni nyote kwa sauti kubwa kutoka katika moto na lile wingu zito na giza nene. Aliwaambieni mlipokuwa mmekusanyika kule mlimani na hakuongeza hapo amri nyingine. Kisha akaziandika juu ya vibao viwili vya mawe, akanipatia.

Mose msemaji wa Mungu

(Kut 20:18-21)

23“Wakati mliposikia hiyo sauti kutoka katikati ya lile giza, juu ya ule mlima uliokuwa unawaka moto, viongozi wote wa makabila yenu na wazee walinijia 24wakasema, ‘Sikiliza! Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametufunulia utukufu na ukuu wake; tumeisikia sauti yake kutoka katikati ya ule moto. Leo hivi tumemwona Mungu akiongea na binadamu, naye binadamu badala ya kufa akaendelea kuishi! 25Lakini ya nini kujitia katika hatari ya kufa kwa kuteketezwa na ule moto mkubwa? Tukiisikia tena sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, tutakufa! 26Je, ni binadamu gani aliyepata kumsikia Mungu aliye hai akiongea kutoka katikati ya moto kama tulivyomsikia sisi halafu akaweza kubaki hai? 27Heri wewe Mose uende karibu, ukasikilize yote atakayosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kisha uje kutuambia mambo hayo yote atakayokuambia. Sisi tutayasikiliza na kuyatekeleza’.
28“Mwenyezi-Mungu alisikia maneno yenu hayo, akaniambia ‘Nimesikia maneno waliyokuambia watu hawa; yote waliyosema ni sawa. 29Laiti wangekuwa daima na mawazo kama haya wakaniheshimu na kushika amri zangu! Mambo yao yote yangewaendea vyema daima wao wenyewe na wazawa wao milele. 30Nenda ukawaambie warudi mahemani mwao. 31Lakini wewe Mose usimame hapa karibu nami; mimi nitakuambia amri zote na masharti na maagizo ambayo utawafundisha, ili nchi ambayo ninawapa iwe mali yao.’
32“Nyinyi muwe waangalifu mkafanye kama Mwenyezi-Mungu alivyowaamuru; tekelezeni kila kitu barabara. 33Mtafuata njia yote Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyowaamuru kufuata ili mambo yenu yawaendee vyema na mpate kuishi muda mrefu katika nchi mtakayotwaa iwe mali yenu.




Kumbukumbu la Sheria 5:1-33


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: