Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 30 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 6 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Alfa na Omega,Yahweh..!Jehovah..!El Shaddai..Emanuel..!
Elohim..!El Elyon..!El Elom..!Adonai..!
Unatosha Mungu wetu,Unastahili sifa,Unastahili Kuabudiwa..
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Hakuna kama wewe,Matendo yako ni ya Ajabu..!

Asante Baba wa Mbinguni kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii..

Si kwamba tumekutenda mema sana,wala si kwamba ni wenye nguvu
si kwa uwezo wetu wala  utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo..
Nikwa mapenzi yako Baba wa Mbinguni..

Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Baba wa Mbinguni
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..

“Lakini nawaambieni nyinyi mnaonisikiliza, wapendeni maadui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni. Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya. Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie pia la pili. Mtu akikunyanganya koti lako mwachie pia shati lako. Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyanganya mali yako usimtake akurudishie. Jinsi mnavyotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. “Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda nyinyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao. Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya hayo. Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile. Ila nyinyi wapendeni maadui zenu na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia kurudishiwa, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya. Muwe na huruma kama Baba yenu alivyo na huruma. “Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa. Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho atakachotumia Mungu kwenu.” Akawaambia mfano huu: “Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni. Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake. Kwa nini wakiona kibanzi jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako? Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ na huku huioni boriti iliyomo katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyomko jichoni mwako, na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako.

Ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Mfalme wa Amani tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabari wenye kuhitaji..
Jehova ukabariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Baba wa Mbinguni ukavitakase na ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..

Yahweh tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
ukatamalaki na kutuatamia ,Ukawalinde na ukabariki Nyumba/ndoa zetu,watoto/familia,ndugu/jamaa na wote wanaotuzunguka..
Mfalme wa Amani Amani ikatawale hapa tunapoishi na duniani pote..
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo..
ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama ipasavyo..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


“Mti mzuri hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri. Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili. Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyomo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya kutoka katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake. “Mbona mwaniita ‘Bwana, Bwana,’ na huku hamtimizi yale ninayosema? Nitawapeni mfano unaofaa kuonesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza: Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara. Lakini yeyote anayesikia maneno yangu asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!”

Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Baba wa rehema na Baraka aendelee kuwabariki..
Na akawaguse na mkono wake wenye nguvu..
Nawapenda.

Amri kuu

1“Hizi ndizo amri, masharti na maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliniamuru niwafundishe, ili muyatekeleze katika nchi mnayokwenda kuimiliki. 2Wakati wote mlipo hai, mtapaswa kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuzitii kanuni zote na amri ninazowapeni nyinyi na wazawa wenu ili mpate kuishi maisha marefu. 3Kwa hiyo enyi Waisraeli, muwe waangalifu kuzitekeleza ili mfanikiwe na kuongezeka sana katika nchi hiyo inayotiririka maziwa na asali kama alivyowaahidi.
4“Basi sikilizeni enyi Waisraeli! Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ni Mwenyezi-Mungu mmoja.6:4 Mwenyezi-Mungu – Mwenyezi-Mungu mmoja: Au Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ndiye Mungu pekee. 5Mpendeni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa moyo wenu wote, kwa roho yenu yote na kwa nguvu zenu zote. 6Wekeni mioyoni mwenu maneno hayo ninayowaamuru leo 7na kuwafundisha kwa uangalifu watoto wenu. Mtawasimulia muwapo mnakaa nyumbani au mlipo safarini au mnapolala au mnapoamka. 8Yafungeni katika mikono yenu na kuyavaa katika vipaji vya nyuso zenu kama ukumbusho. 9Yaandikeni kwenye miimo ya milango yenu na malango ya miji yenu.

Onyo kwa watu wasiotii

10“Kama vile Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, yeye atawapeni nchi yenye miji mikubwa na mizuri iliyostawi ambayo nyinyi hamkuijenga. 11Nyumba zitakuwa zimejaa vitu vizuri ambavyo nyinyi hamkuviweka, kutakuwa na visima ambavyo hamkuvichimba na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hamkuyapanda. Mwenyezi-Mungu atakapowapeleka kwenye nchi hiyo ambako mtakuwa na chakula chote mnachohitaji, 12hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu aliyewatoa Misri ambako mlikuwa watumwa. 13Mtamcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtamtumikia yeye peke yake na kuapa kwa jina lake peke yake. 14Msiabudu miungu mingine, miungu ya watu walio jirani nanyi, 15hasira ya Mwenyezi-Mungu isije ikawaka juu yenu, naye akawafutilia mbali kutoka duniani, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliye kati yenu, ni Mungu mwenye wivu.
16“Msimjaribu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu kule Masa. 17Hakikisheni kwamba mnazitii amri zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, maamuzi na masharti yake ambayo amewaamuru. 18Fanyeni yale yanayompendeza Mwenyezi-Mungu, ili mpate kufanikiwa. Mtaweza kuimiliki nchi ile nzuri ambayo Mwenyezi-Mungu aliapa kuwapa babu zenu, 19na kwamba Mwenyezi-Mungu atawafukuza adui zenu kama alivyoahidi.
20“Siku zijazo, watoto wenu wakiwauliza, ‘Nini maana ya maamuzi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, aliwaamuru kutenda?’ 21Nyinyi mtawajibu hivi: ‘Sisi tulikuwa watumwa wa Farao, mfalme wa Misri, na Mwenyezi-Mungu akatuokoa kwa mkono wake wenye nguvu. 22Kwa macho yetu wenyewe tulimwona akifanya ishara na miujiza na mambo ya kutisha na ya ajabu dhidi ya Wamisri, mfalme wao na wakuu wake. 23Alitutoa Misri, akatuleta hapa na kutupa nchi hii, kama alivyoapa kwamba atawapa babu zetu. 24Basi, Mwenyezi-Mungu alituamuru kuzitii kanuni hizi zote na kumcha kwa faida yetu wenyewe; apate kutulinda daima kama hivi leo. 25Tena tutakuwa waadilifu kama tukitimiza kwa uangalifu amri hizi zote mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kama alivyotuamuru’.



Kumbukumbu la Sheria 6:1-25


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: