1Sasa Balaamu alitambua kwamba Mwenyezi-Mungu alipenda kuwabariki Waisraeli, kwa hiyo hakwenda kupiga bao tena, akawa anaangalia jangwani. 2Alitazama juu akawaona Waisraeli wamepiga kambi, kila kabila mahali pake. Kisha roho ya Mungu ikamjia, 3naye akatamka kauli hii ya kinabii:
Kauli yangu mimi Balaamu mwana wa Peori
kauli ya mtu aliyefumbuliwa24:3 aliyefumbuliwa: Au aliyefumbwa, au aonaye vema. macho;
4kauli ya mtu aliyesikia maneno ya Mungu
mtu aliyeona maono ya Mungu Mwenye Nguvu,
mtu anayesujudu na kuona wazi.
5Hema zako zapendeza namna gani enyi watu wa Yakobo;
naam, kambi zenu enyi watu wa Israeli!
6Ni kama mabonde yanayotiririka maji,
kama bustani kandokando ya mto,
kama mishubiri aliyopanda Mwenyezi-Mungu,
kama mierezi kandokando ya maji.
7Watakuwa na hazina ya kutosha ya maji,24:7 Yatapata … kutosha: Kiebrania: Maji yatatiririka kutoka ndoo zake.
mbegu yao itapata maji mengi,
mfalme wao atakuwa mkuu kuliko Agagi,
na ufalme wake utatukuka sana.
8Mungu aliwachukua kutoka Misri,
naye huwapigania kwa nguvu kama nyati.
Atayateketeza mataifa yaliyo adui zao,
atavunjavunja mifupa yao,
atawachoma kwa mishale yake.
9Ataotea na kulala chini kama simba,
nani atathubutu kumwamsha?
Abarikiwe yeyote atakayewabariki nyinyi Waisraeli,
alaaniwe yeyote atakayewalaani.
10Balaki akawaka hasira dhidi ya Balaamu, akakunja mikono kwa ghadhabu na kumwambia, “Nilikuita uwalaani adui zangu, lakini mara hizi zote tatu umewabariki! 11Sasa! Nenda zako. Nilikuwa nimekuahidi kukupa zawadi nyingi, lakini Mwenyezi-Mungu hakukujalia kupata zawadi hizo, amekunyima!”
12Balaamu akamjibu Balaki, “Je, sikuwaambia wajumbe uliowatuma kwangu 13kwamba hata kama ungenipa nyumba yako imejaa fedha na dhahabu, mimi sitaweza kukiuka agizo la Mwenyezi-Mungu, kwa kufanya jambo lolote, jema au baya kwa hiari yangu mwenyewe? Nilisema, atakachosema Mwenyezi-Mungu ndicho nitakachokisema.
14“Sasa ninarudi kwa watu wangu, lakini kabla sijaondoka, acha nikuambie mambo ambayo watu hao watawatendea watu wako siku zijazo.” 15Basi, Balaamu akatamka kauli hii:
“Kauli yangu mimi Balaamu mwana wa Beori,
kauli ya mtu aliyefumbuliwa macho,
16kauli ya mtu aliyesikia maneno ya Mungu,
na mtu ajuaye maarifa ya Mungu Mkuu,
mtu aonaye maono ya Mungu Mwenye Nguvu,
mtu anayesujudu, macho wazi.
17Ninamwona, atakayekuja, lakini baadaye,
namwona, lakini hayuko karibu.
Nyota itatokea kwa wazawa wa Yakobo,
atatokea mfalme miongoni mwa Waisraeli.
Kwa fimbo yake atawachapa viongozi wa Wamoabu
atawaangamiza wazawa wote wa Sethi.
18Edomu itamilikiwa naye,
Seiri itakuwa mali yake,
Israeli itapata ushindi mkubwa.
19Mmoja wa wazawa wa Yakobo atatawala
naye atawaangamiza watakaonusurika wa Ari.”
20Kisha Balaamu akawaangalia Waamaleki, akatoa kauli hii:
“Amaleki ni taifa lenye nguvu kuliko yote,
lakini mwishoni litaangamia kabisa.”
21Kisha Balaamu akawaangalia Wakeni, akatoa kauli hii:
“Makao yenu ni salama, enyi Wakeni,
kama kiota juu kabisa mwambani.
22Lakini mtateketezwa, enyi Wakeni.
Mtachukuliwa mateka na Ashuru mpaka lini?”24:22 aya ya 22 makala ya Kiebrania si dhahiri.
23Tena Balaamu akatoa kauli hii:
“Lo! Nani ataishi, Mungu atakapofanya hayo?
24Meli zitafika kutoka Kitimu,
wataishambulia Ashuru na Eberi,
lakini nao pia wataangamia milele.”
25Basi, Balaamu akaondoka, akarudi nyumbani; Balaki pia akaenda zake.
Hesabu24;1-25
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment