Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 9 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..27




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu...
Asante Mungu wetu Baba yetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..!
Utukuzwe Mungu wetu wakati wote,Uabudiwe daima,
Usifiwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah..!

Njoni kumsifu Mwenyezi-Mungu enyi watumishi wake wote, enyi nyote mnaotumikia usiku nyumbani mwake. Inueni mikono kuelekea mahali patakatifu, na kumtukuza Mwenyezi-Mungu! Mwenyezi-Mungu awabariki kutoka Siyoni; yeye aliyeumba mbingu na dunia.

Asante Mungu wetu  kwaulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Tunakuja mbele zako Mungu Baba tukijinyeyekeza,tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako Jehovah..
Mfalme wa Amani tunaomba utusamehe dhambi zetu zote..
Tulizoziwaza,tulizozinena,tulizozitenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Upendo nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh utuepushe katika majaribu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..

Akafunga siku arubaini mchana na usiku, na mwishowe akaona njaa. Basi, mshawishi akamjia, akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, amuru mawe haya yawe mikate.” Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno asemalo Mungu.’” Kisha Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, mji mtakatifu, akamweka juu ya mnara wa hekalu, akamwambia, “Ikiwa wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini; maana imeandikwa: ‘Mungu atawaamuru malaika wake kwa ajili yako; watakuchukua mikononi mwao, usije ukajikwaa kwenye jiwe.’” Yesu akamwambia, “Imeandikwa pia: ‘Usimjaribu Bwana, Mungu wako.’” Kisha Ibilisi akamchukua mpaka juu ya mlima mrefu, akamwonesha falme zote za ulimwengu na fahari zake, akamwambia, “Hivi vyote nitakupa kama ukipiga magoti na kuniabudu.” Hapo, Yesu akamwambia, “Nenda zako Shetani! Imeandikwa: ‘Utamwabudu Bwana Mungu wako na kumtumikia yeye peke yake.’” Basi, Ibilisi akamwacha, na malaika wakaja, wakamhudumia.



Ututakase Akili zetu na Miili yetu kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Binadamu hupanga mipango yake, lakini kauli ya mwisho ni yake Mwenyezi-Mungu. Matendo ya mtu huonekana kwake kuwa sawa, lakini Mwenyezi-Mungu hupima nia ya mtu. Mwekee Mwenyezi-Mungu kazi yako, nayo mipango yako itafanikiwa. Mwenyezi-Mungu ameumba kila kitu kwa kusudi lake; hata waovu kwa ajili ya siku ya maangamizi. Kila mwenye kiburi ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; hakika mtu wa namna hiyo hataacha kuadhibiwa. Kwa utii na uaminifu mtu huondolewa dhambi, kwa kumcha Mwenyezi-Mungu huepuka uovu. Mwenyezi-Mungu akipendezwa na mwenendo wa mtu, huwageuza hata adui zake kuwa marafiki. Afadhali mali kidogo kwa uadilifu, kuliko mapato mengi kwa udhalimu. Mtu aweza kufanya mipango yake, lakini Mwenyezi-Mungu huongoza hatua zake. Mfalme huamua kwa maongozi ya Mungu; anapotoa hukumu hakosei. Mwenyezi-Mungu hutaka kipimo na mizani halali; mawe yote mfukoni ya kupimia ni kazi yake. Ni chukizo kubwa wafalme kutenda uovu, maana msingi wa mamlaka yao ni haki. Mfalme hupendelea mtu asemaye kwa unyofu; humpenda mtu asemaye ukweli. Hasira ya mfalme ni kama mjumbe wa kifo; mtu mwenye busara ataituliza. Uso wa mfalme ukingaa kuna uhai; wema wake ni kama wingu la masika. Kupata hekima ni bora kuliko dhahabu; kupata akili ni chaguo bora kuliko fedha. Njia ya wanyofu huepukana na uovu; anayechunga njia yake huhifadhi maisha yake. Kiburi hutangulia maangamizi; majivuno hutangulia maanguko. Afadhali kuwa mnyenyekevu na kuwa maskini, kuliko kugawana nyara na wenye kiburi. Anayezingatia mafundisho atafanikiwa; heri mtu yule anayemtumainia Mwenyezi-Mungu. Mwenye hekima moyoni huitwa mwenye akili; neno la kupendeza huwavutia watu. Hekima ni chemchemi ya uhai kwake aliye nayo, bali upumbavu ni adhabu ya wapumbavu. Moyo wa mwenye hekima humwezesha kusema kwa busara; huyafanya maneno yake yawe ya kuvutia. Maneno mazuri ni kama asali; ni matamu rohoni na yenye kuupa mwili afya. Mtu aweza kuona njia yake kuwa sawa, lakini mwishowe humwongoza kwenye kifo. Hamu ya chakula humhimiza mfanyakazi, maana njaa yake humsukuma aendelee. Mtu mwovu hupanga uovu; maneno yake ni kama moto mkali. Mtu mpotovu hueneza ugomvi, mfitini hutenganisha marafiki. Mtu mkatili humshawishi jirani yake; humwongoza katika njia mbaya. Anayekonyeza jicho kwa hila amepanga maovu; anayekaza midomo amekwisha nuia mabaya. Kuwa na mvi za uzee ni taji la utukufu; hupatikana kwa maisha ya uadilifu. Asiye mwepesi wa hasira ni bora kuliko mwenye nguvu; aitawalaye nafsi yake ni bora kuliko autekaye mji. Kura hupigwa kujua yatakayotukia, lakini uamuzi ni wake Mwenyezi-Mungu.


Tukasimamie Neno lako Amri na Sheria zako..
Mungu wetu ukatufanye chombo chema na tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Jehovah tunaomba ukatubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki vyote tunavyoenda kufanya/kutenda na tukatende kama itakavyokupendeza wewe..
Mungu wetu ukabariki na kuvitakase ,ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi ukatupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji..
Asante Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa pamoja..
Mungu aendelee kuwabariki..
Nawapenda.



Haki ya kurithi kwa wanawake

1Mala, Noa, Hogla, Milka na Tirza walikuwa binti zake Selofehadi. Naye Selofehadi alikuwa mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase mwanawe Yosefu. 2Basi, hao binti wanne walimwendea Mose, wakasimama mbele yake na kuhani Eleazari na viongozi wote wa jumuiya ya Waisraeli, kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasema, 3“Baba yetu alifia jangwani nyikani na bila mtoto yeyote wa kiume. 4Yeye hakuwa miongoni mwa wafuasi wa Kora waliokusanyika dhidi ya Mwenyezi-Mungu, bali alikufa kutokana na dhambi yake mwenyewe. Kwa nini basi jina la baba yetu lifutwe katika ukoo wake kwa sababu hakuwa na mtoto wa kiume? Tupe urithi pamoja na ndugu zake baba yetu.”
5Mose akaleta lalamiko lao mbele ya Mwenyezi-Mungu. 6Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, 7Taz Hes 36:2 “Wanachosema binti za Selofehadi ni kweli; wape urithi pamoja na ndugu za baba yao, wachukue urithi wake. 8Kisha waambie Waisraeli kwamba mtu yeyote akifa bila kuacha mtoto wa kiume, urithi wake atapewa binti yake. 9Ikiwa hana binti, basi urithi huo watapewa ndugu zake wa kiume. 10Na ikiwa hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utawaendea baba zake, wakubwa na wadogo. 11Na ikiwa baba yake hana ndugu wa kiume, basi urithi wake utakuwa wa jamaa yake wa karibu, naye ataumiliki kama mali yake. Hii itakuwa kanuni na sheria kwa Waisraeli, kama vile mimi Mwenyezi-Mungu nilivyokuamuru.”

Yoshua ateuliwa kuwaongoza Waisraeli
(Kumb 31:1-8)
12 Taz Kumb 3:23-27; 32:48-52; Marko 6:34 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Panda juu ya Mlima huu wa miinuko ya Abarimu uitazame nchi ambayo nimewapa Waisraeli. 13Ukisha iona, nawe pia utafariki kama ndugu yako Aroni alivyofariki, 14kwa sababu hamkuitii amri yangu kule jangwani Sini. Wakati jumuiya yote ya watu walipolalamika juu yangu kule Meriba, hamkuacha utukufu wangu uonekane mbele yao walipotaka wapewe maji.” (Meriba ni chemchemi ya maji ya Kadeshi katika jangwa la Sini).
15Naye Mose akamwomba Mwenyezi-Mungu, 16“Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu uliye asili ya uhai wote,27:16 Mungu uliye asili ya uhai wote: Neno kwa neno: Mungu wa roho za wanaadamu wote. nakuomba umteue mtu wa kuisimamia jumuiya hii, 17Taz 1Fal 22:17; Eze 34:5; Mat 9:36 ambaye atawatangulia na kuwaongoza katika shughuli zao zote, ili wasije wakawa kama kondoo wasio na mchungaji.”
18 Taz Kut 24:13 Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mtwae Yoshua mwana wa Nuni, mtu mwenye roho nzuri, kisha umwekee mikono, 19na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote, umkabidhi jukumu hilo. 20Mpe sehemu ya mamlaka yako ili jumuiya yote ya Waisraeli imtii. 21Taz Kut 28:30; 1Sam 14:41; 28:6 Yeye atamtegemea kuhani Eleazari ambaye atamjulisha matakwa yangu kwa kutumia jiwe la kauli.27:21 jiwe la kauli: Kiebrania: Urimu, moja ya mawe mawili yaliyotumiwa na kuhani kujua matakwa ya Mungu. Kwa njia hii, Eleazari atamwongoza Yoshua na jumuiya yote ya Waisraeli wanapotoka na wanapoingia.” 22Mose akafanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Alimtwaa Yoshua na kumsimamisha mbele ya kuhani Eleazari na jumuiya yote ya Waisraeli. 23Taz Kumb 31:23 Kisha akamwekea mikono kichwani na kumpa mamlaka kama alivyoagizwa na Mwenyezi-Mungu.


Hesabu27;1-23


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: