Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 14 August 2017

Kikombe Cha Asubuhi;kitabu cha Hesabu..30



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!
Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu..
Muumba wa Mbingu na Nchi,Mwenyezi-Mungu,
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Yahwe..!Jehovah..!Mungu wa Wajane,Baba wa Yatima..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Usifiwe Muumba wetu..
Uhimidiwe Mungu wetu,Unatosha Mungu wetu..
Hakuna kama wewe,Baba wa Upendo,Mfalme wa Amani..

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana,Si kwamba sisi tunajua sana,Si kwamba sisi ni wazuri mno,Wala si kwa nguvu zetu wala si kwa utashi wetu..
Ni kwa Neema/Rehema zako Mungu wetu sisi leo hii kuwa hivi tulivyo..

Tunajishusha na kujiachilia mikononi mwako Muumba wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa rehema tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wote waliotukosea..
Utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Ututakase miili yetu na Akili zetu kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Mfalme wa Amani ukatawale maisha yetu..
Tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende kama itakavyo kupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mfalme wa Amani ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mungu Baba tunayaweka maisha yetu mikononi mwako,Ndoa/Nyumba zetu ,watoto wetu/familia,ndugu na wote wanao tuzunguka Mungu wetu ukawalinde na kuwafunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..


Mungu asema hivi: “Enyi wakazi wa mbali nyamazeni mnisikilize! Enyi mataifa jipeni nguvu; jitokezeni mkatoe hoja zenu, na tuje pamoja kwa hukumu. “Nani, ila mimi, aliyemwita shujaa toka mashariki, mtu ambaye hupata ushindi popote aendako? Mimi huyatia mataifa makuchani mwake, naye huwaponda wafalme chini ya miguu yake! Upanga wake huwafanya kuwa kama vumbi, kwa upinde wake huwapeperusha kama makapi. Yeye huwafuatia na kupita salama; huenda kasi kana kwamba hagusi chini. Nani aliyefanya yote haya yatendeke? Ni nani aliyepanga wakati wa kila tukio? Mimi Mwenyezi-Mungu nipo tangu mwanzo, mimi nitakuwapo hata milele. “Wakazi wa mbali wameona niliyotenda, wakaogopa; dunia yote inatetemeka kwa hofu. Watu wote wamekusanyika, wakaja. Kila mmoja anamhimiza mwenzake akisema, ‘Haya! Jipe moyo!’ Fundi anamhimiza mfua dhahabu, naye alainishaye sanamu kwa nyundo, anamhimiza anayeiunga kwa misumari. Wote wanasema, ‘Imeungika vizuri sana!’ Kisha wanaifunga kwa misumari isitikisike. “Sikiliza ewe Israeli, mtumishi wangu, wewe, Yakobo ambaye nimekuchagua, wewe mzawa wa Abrahamu, rafiki yangu; wewe niliyekuleta toka miisho ya dunia, wewe niliyekuambia: ‘Wewe u mtumishi wangu; mimi sikukutupa, bali nilikuchagua.’ Basi, usiogope, mimi nipo pamoja nawe. Usifadhaike, mimi ni Mungu wako. Nitakuimarisha na kukusaidia; nitakulinda kwa mkono wangu wa ushindi. “Naam! Wote waliokuwakia hasira, wataaibishwa na kupata fedheha. Wote wanaopingana nawe, watakuwa si kitu na kuangamia. Utawatafuta hao wanaopingana nawe, lakini watakuwa wameangamia. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ndimi ninayetegemeza mkono wako. Mimi ndimi ninayekuambia: ‘Usiogope, nitakusaidia.’” Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Enyi watu wa Yakobo dhaifu kama mdudu, enyi Waisraeli, msiogope! Mimi Mwenyezi-Mungu nasema nitawasaidia. Mimi ni Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli. Nitawafanya muwe kama chombo cha kupuria, chenye meno mapya na makali. Mtaipura milima na kuipondaponda; vilima mtavisagasaga kama makapi. Mtaipepeta milima hiyo, nao upepo utaipeperushia mbali, naam, dhoruba itaitawanya huko na huko. Nanyi mtafurahi kwa sababu yangu Mwenyezi-Mungu; mtaona fahari kwa sababu yangu Mungu Mtakatifu wa Israeli. “Maskini na fukara wakitafuta maji wasipate, wakiwa wamekauka koo kwa kiu, mimi Mwenyezi-Mungu nitawajibu; mimi Mungu wa Israeli, sitawaacha. Nitabubujisha mito kwenye milima mikavu, na chemchemi katika mabonde. Nitaigeuza nyika kuwa bwawa la maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Nitapanda miti huko nyikani: Mierezi, mikakaya, mijohoro, na mizeituni; nitaweka huko jangwani: Miberoshi, mivinje na misonobari. Watu wataona jambo hilo, nao watatambua na kuelewa kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nimetenda hayo, mimi Mtakatifu wa Israeli nimefanya jambo hilo.”

Isaya 41:1-20



Tazama wenye Shida/tabu na wote wanaotaabika,waliokatika majaribu mbalimbali Mungu wetu tunaomba ukawaguse na mkono wako wenye nguvu wakapate uponyaji wa mwili na roho,Ukawape neema ya kusimamia Amri,Sheria na Neno lako nalo likawaweke huru..

Asante Mungu wetu katikayote..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako,Tuliyoyanena na tusiyo yanena Baba wa Mbinguni unayajua na kutujua sisi zaidi ya tunavyojijua..
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapenda/waungwana kwakuwa nami..
Mungu akawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.


Mwongozo kuhusu nadhiri

1 Taz Kumb 23:21-23; Mat 5:33 Kisha Mose alizungumza na viongozi wa makabila ya Israeli, akawaambia, “Hili ndilo neno lililoamriwa na Mwenyezi-Mungu:
2“Mtu akiweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu au akiahidi kwa kiapo na kujifunga nafsi yake kwa ahadi, ni lazima atimize ahadi yake; ni lazima atekeleze yote yale aliyotamka kwa kauli yake.
3“Msichana ambaye bado anaishi nyumbani kwa baba yake akiweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu na kujifunga mwenyewe kwa ahadi, 4na baba yake akawa amesikia ahadi hiyo, asimpinge, basi, nadhiri zake alizoweka zitambana na kila ahadi aliyotoa itambana. 5Lakini kama baba yake akisikia juu ya nadhiri hiyo, akampinga, basi nadhiri zake na ahadi yake havitambana. Mwenyezi-Mungu atamsamehe kwa sababu baba yake amelipinga jambo hilo.
6“Ikiwa msichana ataolewa baada ya kuweka nadhiri, au kuahidi bila ya kufikiri vizuri kwanza, na akajifunga mwenyewe, 7halafu mumewe akasikia jambo hilo asimpinge, basi nadhiri zake zitambana na ahadi zake zitambana. 8Lakini kama mume wake akisikia jambo hilo akampinga, basi huyo mumewe atabatilisha nadhiri ya mkewe na tamko lake alilotoa bila kufikiri; naye Mwenyezi-Mungu atamsamehe.
9“Lakini nadhiri au ahadi yoyote aliyoiweka mama mjane au mwanamke aliyepewa talaka ambayo kwayo amejifunga, ni lazima imbane.
10“Mwanamke aliyeolewa akiweka nadhiri au akiahidi kwa kiapo akiwa nyumbani kwa mumewe, 11kisha mume wake akasikia jambo hilo lakini asimpinge, wala kumwambia kitu, basi, nadhiri zake zote zitambana; kadhalika na ahadi zake zote zitambana. 12Lakini kama mumewe atakaposikia habari zake, akizitangua na kuzibatilisha, basi, hata kama alitaka kutimiza nadhiri au ahadi zake, hatawajibika kuzitimiza; mumewe atakuwa amezitangua na Mwenyezi-Mungu atamsamehe. 13Mumewe anaweza kuthibitisha au kutangua nadhiri au ahadi yoyote inayomfunga. 14Lakini ikiwa mumewe hatasema neno lolote tangu siku atakaposikia habari za nadhiri au ahadi za mkewe, basi atakuwa amezithibitisha siku hiyo alipopata habari zake kwa sababu hakusema chochote. 15Lakini akizibatilisha na kuzitangua muda fulani baada ya kusikia habari zake, basi yeye atakuwa na lawama kwa kosa la mkewe.”
16Hizi ndizo kanuni ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya mume na mkewe; baba na binti yake, huyo binti akiwa bado kijana na anakaa nyumbani kwa baba yake.



Hesabu30;1-16



Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: