Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 29 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 28 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..! Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Baba wa Mbinguni,Baba wa Upendo..
Baba wa Faraja,Baba wa Baraka,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote..
Jehovah Jireh..!,Jehovah Nissi..!,Jehovah Shammah..!
Jehovah Shalom...!,Jehovah Raah..!Emanuel..!
Mungu pamoja nasi...!!



Mimi mzee nakuandikia wewe Bimkubwa mteule pamoja na watoto wako ninaowapenda kweli. Wala si mimi tu ninayewapenda, bali pia wote wanaoujua ule ukweli wanawapenda nyinyi, kwa sababu ukweli unakaa nasi milele. Neema na huruma na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwana wa Baba, zitakuwa pamoja nasi katika ukweli na upendo. Nilifurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanaishi katika ukweli kama Baba alivyotuamuru. Basi, Bimkubwa, ninalo ombi moja kwako: Tupendane. Ombi hili si amri mpya, bali ni amri ileile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Upendo maana yake ni kuishi kwa kuzitii amri zake Mungu. Amri mliyoisikia tangu mwanzo ndiyo hii: Mnapaswa nyote kuishi katika upendo. Wadanganyifu wengi wamezuka duniani, watu ambao hawakiri kwamba Yesu Kristo amekuja kwetu, na mwili wa kibinadamu. Mtu asemaye hivyo ni mdanganyifu na ni mpinzani wa Kristo. Basi, jihadharini nyinyi wenyewe ili msije mkapoteza kile mlichokishughulikia, bali mpate tuzo lenu kamili. Asiyezingatia na kudumu katika mafundisho ya Kristo, bali anayakiuka, hana Mungu. Lakini anayedumu katika mafundisho hayo anaye Baba na Mwana. Basi, kama mtu akija kwenu bila kuwaleteeni mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu. Maana anayemsalimu mtu huyo, anashirikiana naye katika matendo yake maovu. Ninayo mengi ya kuwaambieni, lakini sipendi kufanya hivyo kwa karatasi na wino; badala yake, natumaini kuwatembeleeni na kuzungumza nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ikamilike.
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona siku hii..
Si kwamba tumekutenda mema sana,si kwa nguvu wala uwezo wetu..
Ni kwa neema/rehema zako tuu sisi kuwa hivi tulivyo..

Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Mfalme wa Amani tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu..
Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale na kutamalaki 
katika Nyumba/ndoa zetu,


Nanyi wake, jiwekeni chini ya mamlaka ya waume zenu, ili kama wako waume wowote wasioamini neno la Mungu, wapate kuamini kwa kuuona mwenendo wenu. Haitakuwa lazima kwenu kusema neno, kwani wataona jinsi mwenendo wenu ulivyo safi na wa kumcha Mungu. Katika kujipamba kwenu msitegemee mambo ya njenje, kama vile mitindo ya kusuka nywele, kujivalia vitu vya dhahabu na nguo maridadi. Bali, uzuri wenu unapaswa kutokana na hali ya ndani ya utu wa kweli, uzuri usioharibika wa wema na utulivu wa roho, ambao ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu. Ndivyo walivyojipamba hapo kale wanawake waadilifu waliomtumainia Mungu; walijiweka chini ya mamlaka ya waume zao. Sara kwa mfano alimtii Abrahamu na kumwita yeye bwana. Nyinyi mmekuwa sasa binti zake kama mkitenda mema bila kuogopa tisho lolote. Kadhalika nanyi waume, katika kuishi na wake zenu mnapaswa kutambua kwamba wao ni dhaifu na hivyo muwatendee kwa heshima; maana nao pia watapokea pamoja nanyi zawadi ya uhai anaowapeni Mungu. Hapo sala zenu hazitatiliwa kizuizi.
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka Mungu wetu ukawe mlinzi mkuu..
Baba wa Mbinguni ukatubariki,ukatutakase na kutufunika kwa 
Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Ukatupe neema ya kufuata njia zako,tukasimamie Neno lako
Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..


Mwisho nasema hivi: Mnapaswa kuwa na moyo mmoja, na fikira moja; mnapaswa kupendana kindugu, kuwa wapole na wanyenyekevu nyinyi kwa nyinyi. Msiwalipe watu ovu kwa ovu, au tusi kwa tusi; bali watakieni baraka, maana nyinyi mliitwa na Mungu mpate kupokea baraka. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Anayetaka kufurahia maisha, na kuona siku za fanaka, ajizuie asiseme mabaya aepe kusema uongo. Ajiepushe na uovu, atende mema, atafute amani na kuizingatia. Maana Bwana huwatazama kwa wema waadilifu na kuzisikiliza sala zao. Lakini huwapa kisogo watu watendao maovu.” Ni nani atakayeweza kuwadhuru nyinyi kama mkizingatia kutenda mema? Lakini, hata kama itawapasa kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, basi, mna heri. Msimwogope mtu yeyote, wala msikubali kutiwa katika wasiwasi. Lakini mtukuzeni Kristo kama Bwana mioyoni mwenu. Muwe tayari kumjibu yeyote atakayewaulizeni juu ya matumaini yaliyo ndani yenu, lakini fanyeni hivyo kwa upole na heshima. Muwe na dhamiri njema, kusudi mnapotukanwa, wale wanaosema ubaya juu ya mwenendo wenu mwema kama Wakristo, waone aibu. Maana ni afadhali kuteseka kwa sababu ya kutenda mema, kama Mungu akipenda, kuliko kuteseka kwa sababu ya kutenda uovu.

Tukawe barua njema nasi tukasoke kama inavyokupendeza wewe..
Roho mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Mkono wako wenye nguvu ukawaguse na kuwaponya wote
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Mungu wetu ukawaokoe
wote wali katika vifungo vya yule mwovu..
wakapate uponyaji wa mwili na roho pia..
ukawape neema ya kujiombea na ukapokee sala/maombi yao
ukaonekane katika mapito yako na ukawape sawasawa na mapenzi yako..



Kwa maana Kristo mwenyewe alikufa kwa ajili ya dhambi zenu; alikufa mara moja tu na ikatosha, mtu mwema kwa ajili ya waovu, ili awapeleke nyinyi kwa Mungu. Aliuawa kimwili lakini akafanywa hai kiroho; na kwa maisha yake ya kiroho alikwenda kuwahubiria wale roho waliokuwa kifungoni. Hao ndio wale waliokataa kumtii Mungu alipowangoja kwa saburi wakati Noa alipokuwa anatayarisha ile safina. Ndani ya chombo hicho ni watu wachache tu, yaani watu wanane, waliookolewa katika maji, ambayo yalikuwa mfano wa ubatizo unaowaokoa nyinyi sasa. Ubatizo si shauri la kuondoa uchafu mwilini, bali ni ahadi kwa Mungu inayofanyika katika dhamiri njema. Huwaokoeni kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo ambaye alikwenda mbinguni na sasa amekaa upande wa kulia wa Mungu, anatawala juu ya malaika, wakuu na wenye enzi.
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki katika yote yampendezayo..
Muwe na wakati mwema..
Nawapenda.


Baraka kwa wanaotii

(Lawi 26:3-13; Kumb 7:12-24)

1“Kama mkiitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu na kuzingatia kwa uangalifu amri ambazo ninawaamuru leo, yeye atawaweka juu ya mataifa yote duniani. 2Kama mkitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mtapewa baraka zifuatazo;
3“Miji yenu itabarikiwa na mashamba yenu.
4“Mtabarikiwa mpate wazawa wengi, mavuno mengi, ng'ombe na kondoo wengi.
5“Vikapu vyenu vya nafaka vitabarikiwa na vyombo vyenu vya kukandia. 6Mtabarikiwa mnaporudi nyumbani na mnapotoka nje. 7Maadui zenu wakiwashambulia, Bwana atawapeni ushindi juu yao. Wakija kuwashambulia kwa njia moja watawakimbieni kwa njia saba. 8Baraka za Mwenyezi-Mungu zitakuwa katika ghala zenu za nafaka na katika shughuli zenu zote. Atawabariki katika nchi ambayo anawapeni.
9“Mwenyezi-Mungu atawafanyeni kuwa watu wake watakatifu kama alivyowaahidi, kama mkizitii amri zake yeye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata njia zake. 10Mataifa yote duniani yakiona kwamba nyinyi mnaitwa kwa jina la Mwenyezi-Mungu yatawaogopa. 11Mwenyezi-Mungu atawafanikisha kwa wingi: Watoto, mifugo na mavuno shambani katika nchi aliyowaapia wazee wenu kuwa atawapeni, 12Mwenyezi-Mungu atawafungulieni hazina yake nzuri kutoka mbinguni na kunyesha mvua katika nchi kwa wakati wake, na kubariki kazi zenu. Mtayakopesha mataifa mengi, lakini nyinyi hamtakopa. 13Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawafanya kuwa wa kwanza kwa nguvu na sio wa mwisho. Mtaendelea mbele na sio kurudi nyuma kama mkishika amri zake ambazo ninawapeni leo na kuwa waangalifu kuzitekeleza, 14bila kugeuka kulia au kushoto kuifuata miungu mingine na kuitumikia.

Kukosa utii

(Lawi 26:14-46)

15“Lakini kama hamtaitii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, au msipokuwa waangalifu kutekeleza amri zake zote na masharti ninayowaamuru leo, basi mtapatwa na laana hizi zote: 16Mtapata laana katika miji yenu na mashamba yenu. 17Vikapu vyenu vya nafaka vitalaaniwa na vyombo vyenu vya kukandia mkate. 18Watoto wenu watalaaniwa na mazao yenu ya nchi; mifugo yenu italaaniwa isiongezeke. 19Mtalaaniwa mnapoingia na mnapotoka.
20“Mwenyezi-Mungu atawaleteeni maafa, vurugu na kukata tamaa katika shughuli zenu zote mpaka mmeangamia upesi kwa sababu ya uovu wa matendo yenu na kwa sababu ya kumwacha Mwenyezi-Mungu. 21Atawaleteeni maradhi mabaya mpaka wote muangamie kabisa katika nchi ambayo mnaenda kuimiliki. 22Mwenyezi-Mungu atawashambulia kwa kifua kikuu, homa, majipu, joto kali, ukame, dhoruba na ukungu; mambo hayo yatawaandama mpaka mmeangamia. 23Mbingu zitakauka kama shaba nyeusi bila mvua, na nchi itakuwa kama chuma. 24Mwenyezi-Mungu ataifanya vumbi na mchanga kuwa mvua yenu, vumbi litawanyeshea mpaka mmeangamizwa.
25“Mwenyezi-Mungu atawafanya mshindwe na adui zenu. Nyinyi mtakwenda kuwakabili kwa njia moja, lakini mtawakimbia kwa njia saba. Nanyi mtakuwa kinyaa kwa watu wote duniani. 26Maiti zenu zitakuwa chakula cha ndege wala hapatakuwa na mtu atakayewafukuza. 27Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa majipu yaliyowapata Wamisri, atawapeni vidonda, upele na kuwashwa ambavyo hamwezi kuponywa. 28Mwenyezi-Mungu atawapiga kwa pigo la kuwa na wazimu, mtakuwa vipofu na kuvurugika akili. 29Mtakwenda kwa kupapasapapasa mchana kama vipofu wala hamtafanikiwa katika shughuli zenu. Mtakuwa mkidhulumiwa kila mara na hakutakuwa na mtu wa kuwasaidieni.
30“Mtachumbia wasichana lakini watu wengine watalala nao. Mkijenga nyumba watu wengine watakaa ndani yake. Mkipanda mizabibu watu wengine watavuna. 31Ngombe wenu watachinjwa mbele ya macho yenu lakini hamtaonja hata kipande cha nyama yao. Punda wenu watachukuliwa kwa nguvu mbele ya macho yenu wala hamtarudishiwa. Kondoo wenu watapewa adui zenu, na hakuna mtu atakayeweza kuwasaidia. 32Watoto wenu wa kiume na wa kike watatolewa kwa watu wengine huku mkikodoa macho mchana kutwa kuwatazamia warudi, lakini hamtakuwa na nguvu ya kufanya chochote.
33“Taifa msilolijua litachukua mazao yote ya nchi yenu na matunda ya jasho lenu, nanyi mtadhulumiwa na kuteswa daima, 34hata mtapata wazimu kwa mambo mtakayoona kwa macho yenu wenyewe. 35Mwenyezi-Mungu atayashambulia magoti yenu na miguu yenu kwa majipu mabaya ambayo hamtaweza kuponywa; yatawaenea tangu utosini mpaka nyayo za miguu.
36“Mwenyezi-Mungu atawapeleka nyinyi na mfalme wenu mtakayejichagulia, mpaka kwa taifa ambalo nyinyi hamkulijua wala wazee wenu. Na huko mtatumikia miungu mingine ya miti na mawe. 37Nanyi mtakuwa kinyaa, dharau na mshangao miongoni mwa watu wote wa nchi ambako Mwenyezi-Mungu atawapeleka. 38Mtapanda mbegu nyingi lakini mtavuna kidogo tu kwa kuwa nzige watakula mazao yenu. 39Mtapanda mizabibu na kuitunza, lakini hamtavuna mizabibu hiyo wala kunywa divai yake, maana wadudu wataila. 40Mtakuwa na mizeituni mahali pote nchini mwenu, lakini hamtakuwa na mafuta ya kujipaka; kwa sababu zeituni hizo zitapukutika. 41Mtazaa watoto wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wenu, watachukuliwa uhamishoni. 42Matunda yenu yote na mazao yenu mashambani vitamilikiwa na nzige.
43“Wageni waishio katika nchi yenu watazidi kupata nguvu huku nyinyi mkizidi kufifia zaidi na zaidi. 44Wao watawakopesha nyinyi, lakini nyinyi hamtakuwa na uwezo wa kuwakopesha. Wao watakuwa wa kwanza kwa nguvu nanyi mtakuwa wa mwisho.
45“Hayo yote yatawapateni nyinyi na kuwaandama mpaka muangamizwe kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu kuhusu kushika amri zake na masharti aliyowapa. 46Lakini hizo zitakuwa ushahidi wa hukumu ya Mwenyezi-Mungu kwenu na wazawa wenu milele.
47“Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwabariki katika kila njia, lakini nyinyi hamkumtumikia kwa moyo wa furaha na mkunjufu. 48Kwa hiyo mtawatumikia maadui zenu ambao Mwenyezi-Mungu atawatuma dhidi yenu, kwa njaa, kiu na uchi, na kutindikiwa kila kitu. Atawafungeni nira ya chuma mpaka awaangamize.
49“Mwenyezi-Mungu ataleta kutoka mbali taifa moja liwavamie kasi kama tai, taifa ambalo lugha yake hamuielewi. 50Taifa hilo lenye watu wa nyuso katili halitajali wazee wala kuwahurumia vijana; 51litakula ng'ombe wenu na mazao yenu, mpaka mmeangamizwa. Halitawaachieni nafaka, divai, mafuta, ng'ombe au kondoo mpaka liwaangamize. 52Watu hao watawazingira katika miji yenu yote, mpaka kuta zenu za ngome ambazo mlitegemea zimeporomoshwa chini kila mahali katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni. 53Wakati wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui wenu, mtakula watoto wenu ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapeni. 54Hata mtu mpole kabisa na aliyelelewa vizuri sana atamnyima chakula ndugu yake, mkewe ampendaye na mtoto wake atakayesalia; 55wala hatamgawia hata mmoja wao nyama ya watoto wake atakaowala. Hamtabakiwa na chochote wakati huo wa kuzingirwa na kutaabishwa na maadui katika miji yenu yote. 56Hata mwanamke yule ambaye ni mpole sana na aliyelelewa vizuri na mwororo hata hajawahi kukanyaga udongo kwa kisigino chake hataweza kufanya vingine. Wakati huo wa kuzingirwa kutakuwa na njaa hata 57atamla mtoto wake mchanga na kile kinachotoka baada ya kuzaliwa mtoto bila hata mumewe mpenzi au mmoja wa watoto wake kutambua.
58“Kama msipokuwa waangalifu kutekeleza maneno yote ya sheria hii iliyoandikwa katika kitabu hiki na msipoliheshimu na kulitukuza jina tukufu la kuogofya la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, 59basi, Mwenyezi-Mungu atawaleteeni nyinyi na wazawa wenu mateso yasiyo ya kawaida, mateso makali yasiyoponyeka na ya kudumu, na magonjwa makali ya kudumu. 60Atawaleteeni tena yale magonjwa mliyoyaogopa nchini Misri, nayo yatawaandama daima. 61Atawaleteeni magonjwa ya kila aina na mateso mengine ambayo hayakutajwa katika kitabu hiki cha sheria mpaka muangamie. 62Ijapokuwa nyinyi ni wengi kama nyota za mbinguni, lakini mtakuwa wachache tu kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 63Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyopendezwa kuwafanikisha na kuwafanya kuwa wengi, vivyo hivyo Mwenyezi-Mungu atapendezwa kuwaletea maafa na kuwaangamiza. Nanyi mtaondolewa katika nchi hiyo ambayo mnakwenda kuimiliki. 64Mwenyezi-Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka pembe moja ya dunia hadi nyingine na huko mtaitumikia miungu mingine ya miti na mawe, miungu ambayo nyinyi wala wazee wenu hawakuijua. 65Hamtakuwa na raha yoyote mahali penu wenyewe pa kutulia wala miongoni mwa mataifa hayo. Ila Mwenyezi-Mungu atawapeni huko wasiwasi wa moyo, kufifia kwa macho na mahangaiko ya rohoni.
66“Maisha yenu yatakuwa mashakani, mchana na usiku mtakuwa na hofu na hamtakuwa na usalama wa maisha. 67Mioyo yenu itajaa woga wa kila mtakachoona. Asubuhi mtasema, ‘Laiti ingekuwa jioni,’ jioni itakapofika mtasema, ‘Laiti ingekuwa asubuhi.’ 68Mwenyezi-Mungu atawarudisheni Misri kwa meli, safari ambayo aliahidi kwamba hamngeifanya tena. Huko mtajaribu kujiuza kwa maadui zenu kuwa watumwa, lakini hakuna mtu atakayewanunua.”



Kumbukumbu la Sheria 28:1-68

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Thursday, 28 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 27 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana,Tumshukuru katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unatosha Baba wa Mbinguni..
Hakuna kama wewe Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.
Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vyote
vinavyoonekana na visivyoonekana..
Matendo yako ni ya Ajabu..!



Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?” Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: ‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’ Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.” Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu. Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.” Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini.

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako.
Mungu wetu tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya 
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mfalme wa Amani tunaomba utuepushe katika majaribu
Utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo! Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: ‘Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure? Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’ “Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.” Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga.



Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Baba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahwe tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
 ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na ukavifunike kwa Damu ya
 Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Mfalme wa Amani tunakabidhi maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka,Mungu wetu Amani yako ikawe nasi..
Upendo wetu ukadumu,furaha na baraka zisitupite..
Utu wema na fadhili,Ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu..
Ukatupe ulinzi wako sisi na vyote tunavyovimiliki..
Ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia
 magumu/majaribu mbalimbali,ukawaokoe na kuwaponya wote walio katika vifungo vya yule mwovu..
Ukawarudishe kundini wote waliopotea,Baba ukasikie kuomba kwetu,Baba ukawape neema ya kuweza kujiombea na kufuata njia zako ili wawe huru..
Utupe neema ya kusimamia Neno lako  Amri na Sheria zako 
siku zote za maisha yetu,Ee Baba utuhurumie..!



Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Asante Mungu wetu yote tunayaweka mikononi mwako..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu hakuna mwingine kama wewe..
Sifa na Utukufu tunakurudisha Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami na kunisoma
Mfalme wa Amani na baraka aendelee kutawala katika maisha yenu
Mkono wa Mungu ukawaguse na kuwatendea katika maisha yenu..
Nawapenda.


Sheria za Mungu zilizoandikwa kwenye mawe

1Basi, Mose akiwa pamoja na wazee wa Israeli aliwaambia watu hivi: “Shikeni amri zote ninazowapa leo. 2Siku ile mtakapovuka mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni, mtasimika mawe makubwa na kuyapiga lipu. 3Juu yake mtaandika maneno yote ya sheria zote hizi, mtakapoingia katika nchi inayotiririka maziwa na asali ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu, aliwaahidi. 4Mkiwa ngambo ya mto Yordani, mtasimika mawe hata juu ya mlima Ebali, kama ninavyowaamuru hivi leo, na kuyapiga lipu. 5Mtamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, madhabahu mahali hapo palipo na mawe ambayo hayakuchongwa. 6Naam, madhabahu yoyote mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lazima ijengwe kwa mawe yasiyochongwa. Juu ya madhabahu hiyo mtamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu sadaka za kuteketezwa. 7Mtamtolea sadaka za amani, na kula papo hapo na kufurahi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 8Mtaandika waziwazi juu ya mawe hayo maneno yote ya sheria hii.”
9Basi, Mose pamoja na makuhani Walawi wakawaambia watu wote wa Israeli, “Nyamazeni mnisikilize enyi watu wa Israeli. Leo hii nyinyi mmekuwa watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 10Kwa hiyo mtatii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mkizifuata amri zake na masharti yake ambayo ninawaamuru leo.”

Laana ya kutotii

11Siku hiyo Mose aliwaagiza watu na kusema, 12“Mkisha vuka Yordani, makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Gerizimu kuwabariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yosefu na Benyamini. 13Na makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Ebali wakati laana zitakapotolewa: Reubeni, Gadi, Asheri, Zebuluni, Dani na Naftali. 14Nao Walawi watawatangazia watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
15“ ‘Alaaniwe mtu yeyote afanyaye sanamu ya kuchonga au ya kusubu na kuisimamisha kwa siri, kitu ambacho kimetengenezwa na mikono ya fundi na ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
16“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayemdharau baba yake au mama yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
17“ ‘Alaaniwe mtu yeyote aondoaye alama ya mpaka wa jirani yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
18“ ‘Alaaniwe mtu yeyote ampotoshaye kipofu njiani.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
19“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayepotosha haki ya mgeni au yatima au mjane’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
20“ ‘Alaaniwe mwanamume alalaye na mke wa baba yake, maana amemwaibisha baba yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
21“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mnyama yoyote’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
22“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na dada yake awe ni binti ya baba yake au binti ya mama yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
23“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mama mkwe wake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
24“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayeua mtu kwa siri’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
25“ ‘Alaaniwe mtu yeyote apokeaye hongo ili aue mtu asiye na hatia’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
26“ ‘Alaaniwe mtu yeyote asiyekubali maneno haya ya sheria na kuyatii’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’


Kumbukumbu la Sheria 27:1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

Wednesday, 27 September 2017

Kifo cha Mtanzania Hispania - Mwanasarakasi



KIFO CHA MWANASARAKASI MOHAMMED IDI MOHAMMED (“MOHDY”)
Na Freddy Macha




Sarakasi ni kati ya sanaa hatari na za kusisimua sana.
Kwa sasa Ulaya wapo vijana na watu wa makamo mbalimbali waliohamia toka Afrika Mashariki (hasa Kenya na Tanzania) wakitumbuiza kadamnasi kwa sarakasi, Uingereza, Ureno, Ujerumani na Hispania.
Nchini Hispania kuna visiwa vya Grand Canary ambapo Watanzania wachache huruka ruka kuvutia maelfu ya watalii.
Moja yake ni Lanzarote. Hapa Mtanzania Mohammed Idi Mohamed aliyehamia baada ya kuishi Ujerumani kwa kipindi. Mohdy, Muddy au Modi (wanavyomjua wengi) aliwahi pia kufanya kazi Tanzania, Ureno na Uingereza.
Alifariki Jumatatu 18 Septemba, 2017, asubuhi. Sababu za kifo chake zimeelezwa na waganga ni kuvuja damu kutoka mfereji wa koo kwenda mapafu na kutokea tumboni. Alipasukwa mshipa huu wa damu ghafla na kuanguka bafuni akipiga mswaki. Bahati nzuri Muddy alijikatia bima ya maisha ambayo imeondoa tatizo la kusafirisha mwili wake nyumbani kuzikwa. Michango iiliyoombwa kutolewa itasaidia familia yake na gharama nyingine za mazishi. Tuma kupitia Western Union. Huwa bei nafuu zikitumwa zifike kesho yake badala ya siku hiyo hiyo... Marehemu ameacha watoto wawili na wajukuu. Mungu aiweke roho yake pema peponi.

Kwa walio Ujerumani, ni Malimbo Saidi Malimbo, simu (+49 ) 1522-4082848.

Uingereza, Saidi Kanda (+44) 4040-66607. Tanzania, Eddy Sengo, (+255) 656 210 725.

Picha ihsani ya Fab Moses, Lanzarote, Hispania


-London, 26 Septemba 2017

-Bpepe: gmacha52@gmail.com
-Tovuti: www.freddymacha.com

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 26 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii na kua tayari kuendelea na majukumu yetu..
Si kwamba sisi ni wema sana,Si kwa nguvu zetu wala ujuzi wetu
sisi kuwa hivi tulivyo hapana ni kwa neema/rehema zako Mungu..

Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Yahweh,Usifiwe Jehovah..
Unastahili kuabudiwa Mfalme wa Amani,Unatosha Mungu wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane
Hakuna kama wewe Mungu wetu,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho
Matendo yako ni ya Ajabu,wewe ndiye Ndimi Mwenyezi-Mungu..
Baba wa upendo,Baba wa faraja,Baba wa huruma,Baba wa Baraka
wewe ukisema ndiyo nani aseme siyo?



Kwa hiyo, sasa hakuna hukumu kwa wale ambao katika maisha yao wameungana na Kristo. Maana, sheria ya Roho iletayo uhai kwa kuungana na Kristo Yesu imenikomboa kutoka katika sheria ya dhambi na kifo. Mungu ametekeleza jambo lile ambalo sheria haikuweza kutekeleza kwa sababu ya udhaifu wa binadamu. Mungu alimtuma Mwanae akiwa mwenye mwili sawa na miili yetu sisi wenye dhambi, ili aikabili dhambi, na kwa mwili huo akaiangamiza dhambi. Mungu alifanya hivyo kusudi matakwa ya haki ya sheria yatekelezwe kikamilifu ndani yetu sisi ambao tunaishi, si kwa nguvu za kibinadamu, bali kwa nguvu ya Roho. Maana, wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya mwili, hutawaliwa na fikira za mwili. Lakini wale wanaoishi kufuatana na matakwa ya Roho Mtakatifu, hutawaliwa na fikira za Roho. Fikira za mwili huleta kifo; fikira za Roho huleta uhai na amani. Maana, mwenye kutawaliwa na fikira za mwili ni adui wa Mungu; haitii sheria ya Mungu, wala hawezi kuitii. Watu wanaotii matakwa ya mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini nyinyi hamuishi kufuatana na matakwa ya mwili, bali kufuatana na matakwa ya Roho, ikiwa Roho wa Mungu anaishi ndani yenu. Yeyote asiye na Roho wa Kristo, huyo si wake Kristo. Lakini kama Kristo yumo ndani yenu, ingawa miili yenu imekufa kwa sababu ya dhambi, kwenu Roho ndiye uhai kwa sababu mmefanywa kuwa waadilifu. Ikiwa Roho wa Mungu aliyemfufua Kristo kutoka wafu anaishi ndani yenu, basi huyo aliyemfufua Kristo kutoka kwa wafu ataipa uhai miili yenu yenye hali ya kufa; atafanya hivyo kwa njia ya Roho wake akaaye ndani yenu. Hivyo basi, ndugu zangu, tunalo jukumu, lakini si la kuishi kufuatana na maumbile ya kibinadamu. Kwa maana, kama mkiishi kufuatana na matakwa ya maumbile ya kibinadamu, hakika mtakufa. Lakini, kama kwa njia ya Roho mnayaua matendo yenu maovu, basi, mtaishi. Wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu ni watoto wa Mungu. Kwa maana, hamkumpokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watumwa tena na kuwatia hofu, bali mmempokea Roho mwenye kuwafanya nyinyi watoto wa Mungu, na kwa Roho huyo, sisi tunamwita Mungu, “Aba,” yaani “Baba!” Naye Roho mwenyewe anathibitisha na roho zetu kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Basi, kwa vile sisi ni watoto wa Mungu, tutapokea baraka zote Mungu alizowawekea watu wake, na tutashiriki urithi huo pamoja na Kristo; maana, tukiyashiriki mateso yake Kristo, tutaushiriki pia utukufu wake.



Mfalme wa Amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishushana kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizo zifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
 wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na
 yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu 
na utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo 
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Naona kuwa mateso ya wakati huu wa sasa si kitu kamwe kama tukiyalinganisha na ule utukufu utakaodhihirishwa kwetu. Viumbe vyote vinangojea kwa hamu Mungu awadhihirishe watoto wake. Kwa maana, viumbe viliwekwa katika hali ya kutojiweza kabisa, si kwa hiari yao, ila vilifanywa hivyo kwa mapenzi ya Mungu. Hata hivyo yapo matumaini, maana hivyo viumbe navyo vitaokolewa kutoka katika utumwa wa uharibifu, vishiriki uhuru mtukufu wa watoto wa Mungu. Kwa maana tunajua kwamba mpaka hivi sasa, viumbe vyote vinalia kwa maumivu kama ya kujifungua mtoto. Wala si hivyo viumbe peke yake, bali hata sisi tulio na huyo Roho, aliye wa kwanza wa zawadi za Mungu; sisi pia tunalalamika ndani yetu, tukingojea tufanywe watoto wa Mungu, nazo nafsi zenu zikombolewe. Maana kwa matumaini hayo sisi tumekombolewa. Lakini tumaini halina maana ikiwa tunakiona kile tunachotumainia. Maana ni nani anayetumaini kile ambacho tayari anakiona? Kama tunakitumaini kile ambacho hatujakiona bado, basi, tunakingojea kwa uvumilivu. Hali kadhalika, naye Roho anatusaidia katika udhaifu wetu. Maana hatujui inavyotupasa kuomba; lakini Roho mwenyewe anatuombea kwa Mungu kwa mlio wa huzuni usioelezeka. Naye Mungu aonaye mpaka ndani ya mioyo ya watu, anajua fikira ya huyo Roho; kwani huyo Roho huwaombea watu wa Mungu kufuatana na mapenzi ya Mungu. Tunajua kwamba, katika mambo yote, Mungu hufanya kazi na kuifanikisha pamoja na wote wampendao, yaani wale aliowaita kadiri ya kusudi lake. Maana hao aliowachagua tangu mwanzo, ndio aliowateua wapate kufanana na Mwanae, ili Mwana awe wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Basi, wale ambao Mungu aliwateua ndio hao aliowaita; na hao aliowaita ndio hao aliowafanya kuwa waadilifu na hao aliowafanya waadilifu ndio hao aliowashirikisha pia utukufu wake.

Baba wa Mbinguni tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuwabariki wenyekuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu 
Baba ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,Familia/ndugu 
na wote wanaotuzunguka Mfalme wa Amani tunaomba amani yako
ikatawale,ulinzi wako ukawe nasi,Upendo ukatawale,furaha, 
hekima na busara vikatawale katika maisha yetu..
Yahweh ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amari na Sheria zako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Kutokana na hayo, tuseme nini zaidi? Ikiwa Mungu yuko upande wetu, nani awezaye kutupinga? Mungu hakumhurumia hata Mwanae wa pekee, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote. Ikiwa amefanya hivyo, je, hatatujalia pia mema yote? Ni nani atakayewashtaki wateule wa Mungu? Mungu mwenyewe huwaondolea hatia! Ni nani atakayewahukumu? Hakuna! Maana Kristo ndiye aliyekufa, tena alifufuka kutoka kwa wafu na anakaa upande wa kulia wa Mungu. Yeye anatuombea! Ni nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je, ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo? Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Kwa ajili yako, twakikabili kifo kutwa kucha; tunatendewa kama kondoo wa kuchinjwa.” Lakini, katika mambo haya yote, tumepata ushindi mkubwa kwa msaada wake yeye aliyetupenda. Maana ninajua hakika kwamba hakuna kitu kiwezacho kututenganisha na upendo wake: Wala kifo, wala uhai; wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni; wala yanayotokea sasa, wala yatakayotokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa. Hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu katika Kristo Yesu Bwana wetu.



Tazama wenye shida/tabu,wote wanaopitia magumu/majaribu
waliokatika vifungo vya yule mwovu,wagonjwa ..
Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu..
Ukawaponye kimwili na kiroho pia..
Baba ukawape neema ya kuweza kujiombea na kukujua wewe
wakafuate yaliyo yako na kuamini kuwa wewe ndiye mponyaji..
ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe..
ukapokee sala/maombi yao ukasikie kulia kwao,ukawafute machozi yao,ukawainue na kuwaongoza,ukawatakase na kuwafunika kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana wetu Yesu Kristo..
 wafiwa ukawe mfariji wao na ukawape nguvu,imani katika kipindi kigumu kwao..


Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu nani muweza wa yote..
Hakuna lililogumu kwako..
Sifa na utukufu ni wako Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo asanteni sana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na mkadumu katika pendo lake..
Amani ya Kristo iwe nanyi daima..
Nawapenda.


Matoleo ya mavuno

1“Baada ya kufika na kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawapa iwe yenu na kuishi huko, 2baadhi ya malimbuko ya mazao utakayovuna katika nchi anayokupa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, utayachukua katika kikapu mpaka pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amepachagua pawe makao yake. 3Utamwendea kuhani anayehudumu wakati huo, na kumwambia, ‘Leo ninakiri mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, kuwa nimeingia katika nchi aliyowaapia wazee wetu kuwa atatupa.’
4“Naye kuhani atakapochukua kikapu hicho mikononi mwako na kukiweka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, 5utatamka maneno haya mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako: ‘Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyetangatanga huko na huko, kisha akashuka kwenda Misri akaishi huko kama mgeni. Yeye na jamaa yake walikuwa watu wachache tu walipokuwa huko, lakini wakawa taifa kubwa lenye nguvu na watu wengi. 6Wamisri walitutendea kwa ukatili wakatutesa na kutulazimisha kufanya kazi ngumu ya watumwa. 7Kisha tukamlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wetu, akasikia kilio chetu, na kuyaona mateso yetu, kazi ngumu na dhuluma tulizozipata. 8Basi, Mwenyezi-Mungu akatutoa huko Misri kwa mkono wake wa nguvu ulionyoshwa, kwa vitisho, ishara na maajabu. 9Alituleta hapa na kutupatia nchi hii inayotiririka maziwa na asali. 10Na sasa ninamletea Mwenyezi-Mungu malimbuko ya mazao ya nchi ambayo amenipa.’
“Kisha utaweka kikapu chini, mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, na kuabudu mbele zake. 11Nawe utafurahia mema yote ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, amekujalia wewe na jamaa yako. Nao watafurahi pamoja nawe. 12Kila baada ya miaka mitatu, kila mmoja wenu atatoa sehemu moja ya kumi ya mazao yake yote kwa ajili ya Walawi na wageni, yatima na wajane, ili wapate chakula chote wanachohitaji wanapokuwa katika miji yenu. 13Kisha utasema mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, hivi: ‘Nimelitoa nyumbani kwangu fungu takatifu, nikawapa Walawi, wageni, yatima na wajane, kama ulivyoniamuru nifanye. Sijavunja amri zako wala sijasahau. 14Sikula zaka yoyote nilipokuwa ninaomboleza; sikuitoa nje ya nyumba yangu nilipokuwa najisi na sikutoa zaka hiyo kwa wafu. Nimekutii ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoamuru. 15Uangalie chini kutoka makao yako matakatifu mbinguni, uwabariki watu wako Israeli na nchi uliyotupatia kama ulivyowaapia wazee wetu; nchi inayotiririka maziwa na asali.’

Watu wa Mwenyezi-Mungu

16“Leo hii, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaamuru kuyashika masharti na maagizo haya. Muwe waangalifu kuyatekeleza kwa moyo wote na roho yote. 17Leo hii mmekiri Mwenyezi-Mungu, kuwa Mungu wenu, na kwamba mtafuata njia zake na kushika masharti, amri zake na maagizo yake na kutii sauti yake. 18Naye Mwenyezi-Mungu ametamka rasmi leo hii kwamba nyinyi ni watu wake yeye mwenyewe kama alivyowaahidi na kwamba mnatakiwa kushika amri zake zote. 19Atawafanyieni nyinyi kuwa taifa kubwa kuliko mataifa yote aliyoyaumba. Nanyi mtalitetea jina lake, sifa yake na heshima yake. Nyinyi mtakuwa watu wake, walio mali yake, kama alivyoahidi.”



Kumbukumbu la Sheria 26:1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.