Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 1 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 8 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...
Mungu wetu Baba yetu,Baba wa Mbinguni,Muumba wetu,
Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vyote..
Mfalme wa Amani,Muweza wa yote,Alfa na Omega..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mungu wa Wajane,Baba wa Yatima,Baba wa Upendo..
Baba wa Faraja,Baba wa Baraka,Hakuna kama wewe Jehovah..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine..

Mungu aliweka siku nyingine ambayo inaitwa “Leo,” akasema baadaye kwa njia ya Daudi maneno yaliyokwisha tajwa: “Kama mkisikia sauti ya Mungu leo, msiwe wakaidi.” Kama Yoshua angekuwa amewapa watu hao hilo pumziko, Mungu hangalisema baadaye juu ya siku nyingine.

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Utuepushe katika majaribu Mungu wetu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote...
Ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu? Kama Abrahamu alikuwa amefanywa mwadilifu kutokana na bidii yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu. Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake. Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, akamkubali kuwa mwadilifu. Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu yule ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake: “Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa. Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.” Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Ukabariki Nyumba/Ndoa zetu, na ukawabariki Watoto/familia,wazazi/walezi,Ndugu/jamaa..
Na wote wanaotuzunguka..
Ukawaongoze na kuwalinda wakati wote..
Tukasimamie Neno lako,Shaeria na Amri zako..
Imani yetu na iwe nawe daima tukutukuze Mungu wetu..

Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu. Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu wanaoitii sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu. Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna sheria, haiwezekani kuivunja. Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi hiyo ni kwa ajili ya wote: Si kwa wale tu wanaoishika sheria, bali pia kwa wale waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote. Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.” Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu alimwamini-Mungu ambaye huwapa wafu uhai, na kwa amri yake, vitu ambavyo havikuwapo huwa. Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Wazawa wako watakuwa wengi kama nyota!” Alikuwa mzee wa karibu miaka 100, lakini imani yake haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe, Sara, alikuwa tasa. Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu. Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale aliyoahidi. Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu. Inaposemwa, “Alimkubali,” haisemwi kwa ajili yake mwenyewe tu. Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka kwa wafu. Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka ili tufanywe waadilifu.
Tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ubariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu..Mungu wetu ukatupe sawaswa na mapenzi yako..
Yahweh ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Krtisto vyote tunavyoenda kugusa/kutumia..
Na yote tunayoenda Kufanya/kutenda Jehovah tukatende kama ipasavyo..
Ukatufanye chombo chema Mungu Baba nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Mungu awabariki na kuwatendea katika yote..
Mkono wake wenye nguvu ukawaguse
Msipungukiwe katika mahitaji yenu..
Baba wa Rehema akawape kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.

Nchi nzuri ya kumilikiwa

1“Amri zote ninazowapeni leo, lazima mzifuate kwa uangalifu ili mpate kuishi na kuongezeka, mpate kuingia na kuimiliki ile nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliapa kuwapa babu zenu. 2Kumbukeni jinsi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyowaongoza katika safari ndefu kupitia jangwani kwa muda wa miaka hiyo arubaini, ili awatweze na kuwajaribu ili ajue mliyokuwa mnawaza mioyoni mwenu, na kama mngezishika amri zake au la. 3Aliwanyenyekesha, akawaacha muone njaa na baadaye akawapa mana mle, chakula ambacho hamkukijua, wala babu zenu hawajapata kukijua. Alifanya hivyo ili apate kuwafundisha kuwa binadamu haishi kwa mkate tu, bali kwa kila asemalo Mwenyezi-Mungu. 4Wakati huo wa miaka arubaini nguo zenu hazikuchakaa, wala miguu yenu haikuvimba. 5Kumbukeni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawarudi kama vile baba amrudivyo mwanawe. 6Hivyo, shikeni amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpate kuzifuata njia zake na kumcha yeye. 7Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anawaleteni kwenye nchi nzuri, nchi yenye vijito na chemchemi, na maji yabubujikayo kutoka bondeni na milimani; 8nchi yenye ngano na shayiri, mizabibu, mitini, mikomamanga, mizeituni na asali. 9Huko mtapata chakula tele na hamtapungukiwa kitu. Miamba yake ina chuma, na kwenye milima yake mnaweza kuchimba shaba. 10Mtakula na kushiba, mtamshukuru Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa nchi nzuri aliyowapa.

Onyo kuhusu kumsahau Mwenyezi-Mungu

11“Hakikisheni kwamba hamtamsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoshika amri zake, maagizo yake na masharti yake ninayowaamuru leo. 12Mkisha kula mkashiba, mkajijengea nyumba nzuri na kuishi humo, 13na wakati ambapo ng'ombe na kondoo wenu, dhahabu na fedha yenu, na kila kitu mlicho nacho kitakuwa kimeongezeka, 14msiwe na kiburi na kumsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, mahali mlipokuwa watumwa. 15Ndiye aliyewaongoza katika lile jangwa kubwa na la kutisha, lenye nyoka wenye sumu na nge; katika nchi ile kame isiyokuwa na maji, aliwatolea maji kutoka kwenye mwamba mgumu. 16Tena ndiye aliyewalisheni mana jangwani, chakula ambacho babu zenu hawakupata kukijua. Alifanya hayo yote ili awanyenyekeshe na kuwajaribu, ili kuwapima apate kuwajalia mema mwishowe. 17Hivyo jihadharini msije mkajisemea mioyoni mwenu: ‘Tumejitajirisha kwa uwezo na nguvu zetu wenyewe’. 18Kumbukeni kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye awapaye uwezo wa kupata utajiri. Anafanya hivyo ili kuimarisha agano alilofanya na babu zenu mpaka leo. 19Lakini mkimsahau Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuifuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, nawaonyeni vikali leo hii kuwa hakika mtaangamia. 20Msipomtii Mwenyezi-Mungu, mtaangamia kama mataifa ambayo anayaangamiza mbele yenu.



Kumbukumbu la Sheria 8:1-20

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: