Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 13 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 16 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)


Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..
Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
si kwamba sisi tumetenda mema sana,si kwa nguvu/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo ni kwa Neema/rehema zako Mungu wetu..
Tunakushukuru Mungu wetu,Tunakuabudu Jehovah..
Uhimidiwe Yahweh,Unastahili sifa Jehovah..
unatosha Baba wa upendo,Baba wa Baraka,Baba wa Huruma..
Muweza wa yote,Mponyaji,Mfaji,Alfa na Omega..
Hakuna kama wewe...

Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu  wetu..!



Kisha, kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.” Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Asifiwe Mungu! Maana Bwana Mungu wetu Mwenye Nguvu ametawala! Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa harusi ya Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari. Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na yenye kung'aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watakatifu). Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa kwenye karamu ya harusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni maneno ya kweli ya Mungu.” Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako; sote tunamshuhudia Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio unaowaangazia manabii.”

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mfalme wa Amani tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..





“Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi: “Mimi niitwaye Amina, shahidi mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba Mungu nasema hivi. Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: Baridi au moto. Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika! Wewe unajisema, ‘Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya kitu chochote;’ kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi! Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona. Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa hiyo uwe na bidii na kutubu. Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula pamoja naye, naye atakula pamoja nami. “Mshindi nitamjalia kuketi pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi. “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia makanisa!”

Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Mungu wetu tunaomba ukatubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo ...
Jehova nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..

Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
 Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mungu wetu tunaomba ukabariki Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi/wazee wetu,Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Baba wa Mbinguni ukatulinde na ukatupe Amani,kupendana,kusaidiana,kuhurumiana,kuchukuliana na kuonyana kwa  hekima na busara..

Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..




Kisha, nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: Watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. Wakapaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!” Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na wale viumbe hai wanne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu, wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!” Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?” Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa. Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda. Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena, kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”

Mungu wetu ukatufanye Barua njema na tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mfalme wa Amani tunaomba ukawaponye na kuwagusa wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa,wenye shida/tabu na wote wanaoteseka na yule mwovu..
ukawape uponyaji wa mwili na roho pia,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako ili wawe huru..

Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa pamoja..
Mungu aendelee kuwabariki katika yote yampendezezayo..
Nawapenda.

Pasaka

(Kut 12:1-20)

1“Adhimisheni mwezi wa Abibu na kufanya Pasaka kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Maana katika mwezi huo wa Abibu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu aliwatoa Misri wakati wa usiku. 2Mtatoa sadaka ya Pasaka kutoka mifugo yenu ya kondoo au ng'ombe kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atachagua likae jina lake. 3Msile sadaka hiyo na mikate iliyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso – kwa sababu mlitoka Misri kwa haraka; kwa hiyo, muda wote mtakaoishi mtakumbuka ile siku mlipotoka Misri. 4Kwa muda wa siku saba mtu yeyote katika nchi yenu asiweke chachu nyumbani mwake; na nyama ya yule mnyama aliyechinjwa jioni ya siku ya kwanza isibaki mpaka asubuhi. 5Msitolee sadaka ya Pasaka katika mji wowote ambao Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, 6bali mtaitolea pale mahali ambapo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atapachagua likae jina lake, hapo ndipo mtakapotolea sadaka ya Pasaka jioni, jua linapotua, wakati uleule mlipotoka Misri. 7Hiyo nyama mtaichemsha na kuila mahali pale Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atakapochagua; asubuhi yake mtageuka na kurudi mahemani mwenu. 8Kwa siku sita mtakula mikate isiyotiwa chachu; na mnamo siku ya saba utakuwapo mkutano mkubwa wa kumwabudu Mwenyezi-Mungu, na msifanye kazi yoyote siku hiyo.

Sikukuu ya mavuno

(Kut 34:22; Lawi 23:15-21)

9“Mtahesabu majuma saba; mtaanza kuyahesabu tangu mnapoanza kuvuna nafaka. 10Halafu mtaadhimisha sikukuu ya majuma kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kutoa sadaka ya hiari, mtakayotoa kadiri awabarikiavyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 11Mtafurahia mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi pamoja na wana wenu na binti zenu, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao wanaishi pamoja nanyi. Fanyeni haya katika mahali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapochagua likae jina lake. 12Mkumbuke kuwa mlikuwa watumwa kule Misri; basi muwe waangalifu kufuata masharti haya.

Sikukuu ya vibanda

(Lawi 23:33-43; Hes 29:12-39)

13“Baada ya kupura nafaka yenu yote na kukamua zabibu zenu, adhimisheni sikukuu ya vibanda kwa muda wa siku saba. 14Mtafanya sherehe hiyo, nyinyi na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu, Walawi, wageni, yatima na wajane ambao huishi katika miji yenu. 15Kwa siku saba mtamfanyia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, sherehe mahali ambapo Mwenyezi-Mungu atapachagua; kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu atawabariki kwa mazao yenu yote na katika shughuli zenu zote nanyi hakika mtafurahi.
16“Wanaume wote wa taifa lenu watakuja mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mara tatu kila mwaka, mahali atakapopachagua: Wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, sikukuu ya kuvuna majuma na wakati wa sikukuu ya vibanda. Wasiende mbele ya Mwenyezi-Mungu mikono mitupu. 17Wote watatoa kadiri wanavyoweza kulingana na baraka Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowajalia.

Mwongozo juu ya haki za watu

18“Mtateua waamuzi na maofisa kutoka makabila yenu katika miji yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapa, nao watatoa hukumu za haki kwa watu. 19Msipotoshe haki; msiwe na upendeleo, wala msikubali kupokea rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha macho ya watu wenye hekima na kupotosha kesi ya mtu mwadilifu. 20Mtazingatia haki tu, ili mpate kuishi na kuimiliki nchi mnayopewa na Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
21“Msipande mti wowote uwe nguzo ya mungu wa uongo karibu na meza ya madhabahu sadaka mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 22Wala msisimamishe nguzo ambayo Mwenyezi-Mungu Mungu wako anaichukia.




Kumbukumbu la Sheria 16:1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: