Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje? Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona Leo hii.. Tumshukuru Mungu katika yote..
Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake zadumu milele! Semeni hivyo, enyi mliokombolewa na Mwenyezi-Mungu, watu ambao aliwaokoa katika taabu, akawakusanyeni kutoka nchi za kigeni: Kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini. Baadhi walitangatanga katika jangwa tupu, wasiweze kufikia mji wa kukaa. Waliona njaa na kiu; wakavunjika moyo kabisa. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwaongoza katika njia iliyonyoka, mpaka wakaufikia mji wa kukaa. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huwatosheleza walio na kiu; na wenye njaa huwashibisha mema. Baadhi waliishi katika giza na ukiwa, wafungwa katika mateso na minyororo, kwa sababu waliasi maagizo ya Mungu, na kuyapuuza mashauri yake Mungu Mkuu. Walikuwa hoi kwa kazi ngumu, wakaanguka chini, pasiwe na wa kuwasaidia. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Aliwatoa katika giza na ukiwa, na minyororo yao akaivunjavunja. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Yeye huvunja na kufungua milango ya shaba, na kukatakata fito za chuma. Baadhi walipumbaa kwa sababu ya dhambi zao, waliteseka kwa sababu ya uovu wao; chakula kikawa kinyaa kwao, wakawa nusura wafe. Ndipo katika taabu yao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso yao. Kwa neno lake aliwaponya, akawaokoa wasiangamie. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Wamtolee tambiko za shukrani; wasimulie matendo yake kwa nyimbo za shangwe. Baadhi walisafiri baharini kwa meli, na kufanya shughuli zao humo baharini. Waliyaona matendo ya Mwenyezi-Mungu, mambo ya ajabu aliyotenda huko. Aliamuru, akazusha dhoruba kali, ikarusha juu mawimbi ya bahari. Walitupwa juu angani, kisha chini vilindini; uhodari wao ukawaishia katika mkasa huo. Waliyumbayumba na kupepesuka kama walevi; maarifa yao ya uanamaji yakawaishia. Ndipo katika taabu zao wakamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akawaokoa katika mateso zao. Aliifanya ile dhoruba kali itulie, nayo mawimbi yakanyamaza. Hapo wakafurahi kwa kupata utulivu; akawafikisha kwenye bandari waliyoiendea. Mshukuruni Mwenyezi-Mungu kwa fadhili zake; kwa sababu ya maajabu aliyowatendea binadamu. Mtukuzeni katika kusanyiko la watu, na kumsifu katika baraza la wazee. Mungu aliigeuza mito kuwa jangwa, chemchemi akazikausha kabisa. Ardhi yenye rutuba akaifanya udongo wa chumvi, kwa sababu ya uovu wa wakazi wake. Aligeuza majangwa kuwa mabwawa ya maji, na nchi kame kuwa chemchemi za maji. Akawahamishia huko wenye njaa, nao wakajenga mji wa kukalika. Walilima mashamba na kupanda mizabibu, wakavuna mazao kwa wingi. Aliwabariki watu wake, wakaongezeka; na idadi ya wanyama wao akaizidisha. Kisha walipopungua na kuwa wanyonge, kwa kukandamizwa, kuteswa na huzuni, aliwadharau wakuu waliowatesa, akawazungusha jangwani kusiko na njia. Lakini aliwaokoa wahitaji katika taabu zao, akaongeza jamaa zao kama kundi la kondoo. Waadilifu waonapo jambo hilo wanafurahi, lakini waovu wote wananyamazishwa. Wenye hekima na wayafikirie mambo haya, wazitambue fadhili zake Mwenyezi-Mungu.
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu.. Asante kwa ulinzi wako wakati wote.. Tazama jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya na Kesho ni siku nyingine.. Mfalme wa Amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba.. Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.. Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Mungu wetu utepusha katika majaribu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote.. Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti.. Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.. Baba wa Mbinguni tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu.. Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Jehovah tunaomba nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako.. Yahweh Tazama watoto/vijana wetu wanaoenda kuanza maisha mapya kuanza vyuo[University] na hawaishi nyumbani kwa wazazi wameanza maisha yao peke yao katika miji/Nchi nyingine mbali na wazazi/walezi wao.. Mungu wetu tunaomba ukawalinde,ukawaongoze katika maisha yao mapya,katika ujana wao,katika masomo yao,Ukaonekane Mungu wetu katika yote,wazingatie kilichowapeleka,wakawe werevu na si wajinga wakapate kuelewa na kukumbuka yote wanayofundishwa.. Wakawe Baraka kwa watu wote,wakasimamie Neno lako Amri na sheria zako siku zote za maisha yao.. Wakawe kichwa na si mkia.. Hakuna tunayemjua huko na kumkabidhi maisha ya watoto wetu.. Lakini tuna imani na matumaini kwa sababu Mungu wetu mwenye Nguvu na ulinzi upo nao.. Hizi ni methali za Solomoni mfalme wa Israeli, mwana wa Daudi. Methali hizi zawapatia watu hekima na nidhamu; zawafanya waelewe maneno ya busara, zawafanya kuwa na nidhamu, utaratibu, uadilifu, haki na kutenda kwa usawa. Huwapatia wajinga werevu na vijana maarifa na hadhari. Mwenye hekima azisikie na kuongeza elimu yake, naye mwenye busara apate mwongozo. Mtu aelewe methali na mifano, maneno ya wenye hekima na vitendawili vyao. Kumcha Mwenyezi-Mungu ni msingi wa maarifa, lakini wapumbavu hudharau hekima na adabu. Mwanangu, sikiliza mwongozo wa baba yako, wala usiyapuuze mafundisho ya mama yako; hayo yatakupamba kilemba kichwani pako, kama mkufu shingoni mwako. Mwanangu, usikubali kushawishiwa na wenye dhambi. Wakisema: “Twende tukamvizie mtu na kumuua; njoo tukawashambulie wasio na hatia! Tutawameza kama Kuzimu wakiwa hai, watakuwa kama wale washukao Shimoni. Tutajitwalia mali zote za thamani, nyumba zetu tutazijaza nyara. Njoo ushirikiane nasi, vyote tutakavyopata tutagawana.” Wewe mwanangu usiandamane nao, uzuie mguu wako usifuatane nao. Maana wao wako mbioni kutenda maovu, haraka zao zote ni za kumwaga damu. Mtego utegwao huku ndege anaona, mtego huo wategwa bure. Wao huvizia na kujiangamiza wao wenyewe, hutega mtego wa kujinasa wao wenyewe. Ndivyo zilivyo njia za waishio kwa ukatili; ukatili huyaangamiza maisha ya wakatili. Methali 1:1-19 wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho.. Alfa na Omega,Unatosha Baba wa Mbinguni...
Malaika wa Mwenyezi-Mungu huwalinda wote wamchao, na kuwaokoa katika hatari. Jaribuni mwone Mwenyezi-Mungu alivyo mwema. Heri mtu anayekimbilia usalama kwake. Mcheni Mwenyezi-Mungu enyi watakatifu wake; maana wenye kumcha hawatindikiwi na kitu. Hata wanasimba hutindikiwa na kuona njaa; lakini wanaomtafuta Mwenyezi-Mungu hawakosi chochote chema. Njoni enyi vijana mkanisikilize, nami nitawafundisha kumcha Mwenyezi-Mungu. Je, watamani kufurahia maisha, kuishi maisha marefu na kufurahia mema? Basi, acha kusema mabaya, na kuepa kusema uongo. Jiepushe na uovu, utende mema; utafute amani na kuizingatia.
Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako.. Nyumba/Ndoa zetu,watoto wetu,wazazi/wazee wetu,Familia/Ndugu na wote waliotuzunguka Baba wa Mbinguni ukawe mlinzi mkuu,ukabariki na kutupa neema ya kusimamia Neno lako Amri na sheria zako.. Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe.. Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi.. Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu.. Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele.. Amina..!! Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa nami.. Baba wa Upendo akawabariki katika yote yampendezayo.. Pendo lenu likadumu milele.. Nawapenda. |
Miji ya kukimbilia usalama
(Hes 35:9-34; Yos 20:1-9)
1“Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuwaangamiza watu wale ambao nchi yao anawapeni, na baada ya kuimiliki na kuishi katika nyumba zao, 2mtatenga miji mitatu katika nchi atakayowapatia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, muimiliki. 3Mtatengeneza barabara na kugawa katika sehemu tatu nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapatia muimiliki ili kila anayemuua mtu bila kukusudia apate kukimbilia huko.
4“Mtu akimuua mwenzake bila kukusudia, naye hakuwa adui yake, anaweza kukimbilia mmojawapo wa miji hii, akayaokoa maisha yake. 5Kwa mfano, mtu aendaye na mwenzake msituni kukata kuni naye wakati anakata mti, shoka likachomoka kutoka kwenye mpini wake, likamuua yule mwingine, mtu huyo anaweza kukimbilia kwenye mji mmojawapo, akayaokoa maisha yake. 6Lakini kama umbali wa mji huo ni mkubwa mno, huyo mwenye kulipiza kisasi, kwa hasira kali anaweza kumfuatia, akamkamata na kumuua huyo aliyesababisha kifo, ingawaje hakupewa hukumu ya kifo na hao wahusika wawili hawakuwa maadui hapo awali! 7Kwa hiyo mimi nawaamuru mtenge miji mitatu.
8“Tena kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ataipanua mipaka ya nchi yenu, kama alivyowaapia babu zenu, naye akawapatia nchi yote ambayo aliahidi kuwapatia hao babu zenu 9ikiwa mtakuwa waangalifu kushika amri hizi zote ninazowaamuru hivi leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata siku zote njia zake – basi, mtaongeza miji mingine mitatu zaidi ya hii mitatu, 10ili mtu asiye na hatia asije akauawa katika nchi yenu ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawapatia kuwa yenu, na hivyo kuwasababisha kuwa na hatia ya mauaji.
11“Lakini mtu akiwa adui wa mwenzake, akamvizia akamshambulia na kumuua, kisha akakimbilia kwenye mji mmojawapo wa miji hiyo, 12hapo wazee wa mji huo watatuma watu wamtoe huko na kumkabidhi kwa mwenye kulipiza kisasi cha umwagaji damu, auawe. 13Msimwonee huruma, bali mtaukomesha uovu wa mauaji ya mtu asiye na hatia katika Israeli, ili mpate kuishi kwa amani.
Mipaka ya zamani
14“Msiondoe alama ya mipaka ya jirani zenu, ambayo iliwekwa hapo zamani katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu wenu anawapatieni mwimiliki.
Mashahidi
15“Ushahidi wa mtu mmoja hautoshi kumhukumu mtu juu ya kosa lolote la jinai au uovu kuhusu kosa lolote alilofanya. Ni ushahidi wa watu wawili au watatu tu ndio utakaothaminiwa. 16Ikiwa shahidi mdhalimu atatokea kumshtaki mtu yeyote juu ya kosa fulani, 17basi yeye na mshtakiwa kuhusu mzozo huo watakwenda mbele ya Mwenyezi-Mungu, mbele ya makuhani na waamuzi ambao wako katika ofisi wakati huo; 18waamuzi watachungua kwa uangalifu kesi hiyo na ikiwa mshahidi ni mshahidi wa uongo na amemshtaki mwenzake kwa uongo, 19basi, mtamtendea alivyokusudia kumtendea ndugu yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu kati yenu. 20Nao watu wengineo watasikia na kuogopa, na uovu kama huo hautafanyika tena kati yenu. 21Msiwaonee huruma watu wa aina hiyo. Uhai utalipwa kwa uhai, jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono na mguu kwa mguu.
Kumbukumbu la Sheria 19:1-21
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment