Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 21 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 22 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa
kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana zaidi ya wengine waliotangulia/fariki
Si kwa nguvu zetu wala uwezo wetu sisi kuwa hivi tulivyo..
Ni kwa neema/rehema zako Mungu wetu..
Asante Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Nchi na vyote vilivyomo..
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa Mfalme wa Amani..


Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ngambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa. Watu waliotembea gizani wameona mwanga mkubwa. Watu walioishi katika nchi ya giza kuu, sasa mwanga umewaangazia. Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa, umeiongeza furaha yake. Watu wanafurahi mbele yako, wana furaha kama wakati wa mavuno, kama wafurahivyo wanaogawana nyara. Maana nira nzito walizobeba, nira walizokuwa wamefungwa, na fimbo ya wanyapara wao, umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani. Viatu vyote vya washambulizi vitani na mavazi yote yenye madoa ya damu yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto. Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu, tumepewa mtoto wa kiume. Naye atapewa mamlaka ya kutawala. Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”. “Mungu Mwenye Nguvu”, “Baba wa Milele”, “Mfalme wa Amani”. Utawala wake utastawi daima, amani ya ufalme wake haitakoma. Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi na kutawala juu ya ufalme wake; ataustawisha na kuuimarisha, kwa haki na uadilifu, tangu sasa na hata milele. Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

Mfalme wa Amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu na Utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga Kristo zishindwe katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo..



Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu atakayemtambika mtoto wake wa kiume au wa kike kwa moto, wala mtu apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu. Maana yeyote atendaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu; na kwa ajili ya mambo haya ya kuchukiza, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu wa namna hiyo mbele yenu. Muwe wakamilifu mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Yaweh tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Jehovah tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba zetu/Ndoa,watoto wetu,wazazi,Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Tunaomba ulinzi wako,Amani,Hekima na Busara..
Upendo,fadhili zako na tukasimamie Neno lako Amri na sheria zako siku zote..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..


Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda. Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake. Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma nyinyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwamwitu. Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani. Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: ‘Amani iwe katika nyumba hii!’ Kama akiwako mpenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni. Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile. Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni. Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.’ Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni: ‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunayapangusa dhidi yenu. Lakini, jueni kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.’ Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa kuliko ile ya watu wa Sodoma.

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na Amani iwe nanyi..
Nawapenda.

1“Ukimwona ng'ombe au kondoo wa ndugu yako amepotea, usimwache, bali mrudishe kwa ndugu yako. 2Lakini kama nyumbani kwa huyu ndugu si karibu au kama humjui mwenyewe, basi, utamchukua mnyama huyo nyumbani kwako, akae kwako mpaka mwenyewe atakapokuja, nawe umrudishie. 3Utafanya vivyo hivyo kuhusu punda au vazi au kitu chochote ambacho nduguyo amekipoteza. Kamwe usiache kumsaidia.
4“Ukiona punda au ng'ombe wa nduguyo ameanguka njiani, usiache kumsaidia nduguyo; utamsaidia kumwinua.
5“Wanawake wasivae nguo za wanaume, na wanaume wasivae nguo za wanawake. Anayefanya hivyo ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
6“Ukikuta kiota cha ndege mtini au njiani, kina makinda au mayai na mamandege ameyafunika hayo makinda au mayai, usimchukue mamandege na makinda yake. 7Utamwacha mamandege aende zake, lakini unaweza kuchukua makinda. Ukifanya hivyo utafanikiwa na kuishi maisha marefu.
8“Unapojenga nyumba, jenga ukingo pembeni mwa paa, usije ukalaumiwa kama mtu akianguka kutoka huko, akafa.
9“Usipande mizabibu yako pamoja na mimea mingine, la sivyo mazao yote yatakuwa haramu, siyo tu yale uliyopanda bali pia matunda ya mizabibu.
10“Usilime shamba kwa kutumia ng'ombe na punda pamoja.
11“Usivae mavazi yaliyofumwa kwa sufu na kitani.
12“Funga vishada katika pembe nne za vazi lako.

Heshima kuhusu mambo ya mume na mke

13“Mwanamume akioa mwanamke, halafu baadaye akate shauri kumwacha, 14na kumshtaki kwamba ametenda mambo ya aibu, na kumharibia sifa kwa kusema kwamba hakupata ushahidi wa ubikira wakati alipomwoa, 15basi, wazazi wa mwanamke huyo watachukua ushahidi wa ubikira wa binti yao kwa wazee kwenye lango la mji na kuwaambia, 16‘Tulimwoza binti yetu kwa mtu huyu, lakini sasa hamtaki tena, 17na ajabu ni kwamba amemshtaki mambo ya aibu na kusema ati hakumkuta na ushahidi wowote wa ubikira. Hata hivyo ushahidi wa ubikira wa binti yetu ni huu.’ Halafu atakunjua nguo yenye huo ushahidi mbele ya wazee wa mji. 18Hapo wazee wa mji watamchukua yule mwanamume na kumpiga viboko. 19Pia watamtoza mtu huyo faini ya vipande 100 vya fedha na kupewa baba wa huyo mwanamke kwa kuwa mwanamume huyo amemharibia sifa binti wa Israeli. Na huyo mwanamke ataendelea kuwa mke wake na hataweza kumpa talaka maisha yake yote. 20Lakini kama mashtaka hayo ni ya kweli, na hakuna ushahidi wa ubikira wake, 21watampeleka kwenye mlango wa nyumba ya baba yake na wanaume wa mji huo watampiga mawe afe, kwa sababu amefanya ufidhuli katika Israeli kwa kufanya umalaya akiwa nyumbani kwa baba yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu.
22“Mwanamume akifumaniwa na mke wa mtu mwingine, wote wawili, mwanamume na mwanamke, lazima wauawe. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu.
23“Mwanamume akimkuta msichana aliyechumbiwa, akalala naye, 24mtawatoa wote wawili nje ya mji na kuwapiga mawe mpaka wafe. Msichana huyo lazima auawe kwa kuwa hakupiga kelele asaidiwe ingawa alikuwa mjini; naye mwanamume lazima auawe kwa kuwa amemchafua mchumba wa jirani yake. Ndivyo mtakavyokomesha uovu huo miongoni mwenu.
25“Lakini kama mwanamume amekutana na msichana aliyechumbiwa akamshika kwa nguvu, basi ni huyo mwanamume tu atakayeuawa. 26Msimtendee huyo msichana chochote; yeye hana kosa linalostahili adhabu ya kifo. Tukio hili ni sawa na la mtu anayemshambulia mtu mwingine na kumwua, kwa sababu 27mwanamume huyo alimshika kwa nguvu huyo msichana huko mbugani, na ingawa alipiga kelele kuomba msaada hapakuwa na mtu wa kumsaidia.
28“Mwanamume akikutana na msichana ambaye hajachumbiwa, akamshika kwa nguvu, wakafumaniwa, 29mwanamume huyo atamlipa baba yake msichana huyo vipande hamsini vya fedha kwa sababu amemnajisi, na msichana huyo atakuwa mke wake, wala hana ruhusa ya kumwacha maisha yake yote.
30“Mwanamume yeyote kamwe asilale na mke wa baba yake.


Kumbukumbu la Sheria 22:1-30

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: