Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 22 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 23 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu, Baba yetu,Muumba wetu na Muumba wa Vyote..
Mfalme wa Amani,Muweza wa yote,Mwenyezi-Mungu
Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo..
Hakuna kama wewe,hakuna lililogumu kwako..
Tumaini letu lipo kwako Jehovah,Amani ina wewe.
Uponyaji unawewe,Wokovu unapatika kwako..
Upendo wa kweli una wewe Mungu wetu,Ulinzi upo nawe Yahweh..!
Wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho,Alfa na Omega..!!

Baadaye mwanasheria mmoja alisimama, akamwuliza akitaka kumtega, “Mwalimu, nifanye nini ili nipate uhai wa milele?” Yeye akamwuliza, “Imeandikwa nini katika sheria? Unaelewaje?” Akamjibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.” Yesu akamwambia, “Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi.” Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, “Na jirani yangu ni nani?” Yesu akamjibu, “Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyanganya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu. Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando. Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali hapo akamwona, akapita kando. Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma. Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai na kuyafunga; halafu akampandisha juu ya punda wake, akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamwuguza. Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, ‘Mwuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi.’” Kisha Yesu akauliza, “Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?” Yule mwalimu wa sheria akamjibu, “Ni yule aliyemwonea huruma.” Yesu akamwambia, “Nenda ukafanye vivyo hivyo.”



Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Tazama Jana imepita Mungu wetu Leo ni siku mpya
 na Kesho ni siku nyingine Jehovah..
Tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu
  utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh ututakase miili yetu na akili zetu Baba utufunike
kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi! Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake. Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!

Baba wa Mbinguni tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
 wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe sawasawa
na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Tunaomba ulinzi wako na Amani yako katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,
Wazazi,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe....



Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja aitwaye Martha, akamkaribisha nyumbani kwake. Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake. Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, “Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie.” Lakini Bwana akamjibu, “Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi. Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyanganya.”
Yahwe tazama wenye shida/tabu,wote wanaotaabika,
walio katika vifungo vya yule mwovu,waliokata tamaa..
Tazama wanaotafuta watoto Mungu wetu tunaomba ukawaguse na mkono
wako wenye nguvu,ukawafungue na kuwaponya kimwili na kiroho pia..
ukasikie kilio chao, maombi/sala zetu ,ukaonekane katika mapito/magumu yao..

ukawape neema ya kukujua wewe,wakasimamie Neno lako Amri na sheria zako..
Baba wa Mbinguni unayajua mahitaji yao na unayeona sirini..
Ukawape kinachowafaa sawasawa na mapenzi yako..


Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu, na mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu, sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu, ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua. Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu ni sawa na nguvu ile kuu mno aliyomfufua nayo Kristo kutoka kwa wafu, akamketisha upande wake wa kulia mbinguni. Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote. Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami..
Baba wa rehema na Baraka akawe nanyi daima..
Nawapenda.

Kutengwa na watu wa Mungu

1“Mwanamume yeyote aliyehasiwa au aliyekatwa uume wake haruhusiwi kujiunga na kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu.
2“Na mwana haramu yeyote, wala mzawa wake hata kizazi cha kumi, haruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu.
3“Mwamoni au Mmoabu yeyote, wazawa wao wote hata kizazi cha kumi, hawaruhusiwi kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu, 4kwa sababu walikataa kuwapatia chakula na maji mlipokuwa njiani kutoka Misri, na kwa kuwa walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori kule Mesopotamia, awalaani. 5Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, hakumsikiliza Balaamu; badala yake laana hiyo iligeuka kuwa baraka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliwapenda. 6Kwa hiyo, kamwe msiwasaidie hao wapate amani na fanaka.
7“Msiwachukie Waedomu; hao ni ndugu zenu. Na msiwachukie Wamisri, kwani mlikaa katika nchi yao kama wageni. 8Wazawa wao, kuanzia kizazi cha tatu, wataruhusiwa kuingia katika kusanyiko la watu wa Mwenyezi-Mungu.

Usafi kambini

9“Mkienda vitani, mkapiga kambi, kila mmoja ajihadhari na kitu chochote kiovu. 10Kama miongoni mwenu kuna mtu yeyote ambaye ni najisi kwa sababu ya kutokwa mbegu usiku, huyo atatoka nje ya kambi; hatakaa karibu na kambi. 11Lakini ikifika jioni ataoga, na jua likitua anaweza kurudi kambini.
12“Lazima muwe na mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda haja. 13Kati ya vifaa vyenu mtakuwa na jembe, na hilo mtatumia kuchimba shimo na kufukia kinyesi chenu. 14Kambi yenu lazima iwe takatifu kwa kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anatembea kambini mwenu ili awaokoe na kuwatia adui zenu mikononi mwenu. Kwa hiyo msimwache aone kitu chochote kisichofaa miongoni mwenu, la sivyo atawaacheni.
15“Mtumwa akikimbilia kwako usimrudishe kwa bwana wake. 16Ataishi pamoja nawe mahali atakapochagua katika mojawapo ya makao yako, mahali panapompendeza. Usimdhulumu.
17“Mwisraeli yeyote, mwanamume au mwanamke, haruhusiwi kamwe kuwa kahaba wa kidini. 18Fedha yoyote iliyopatikana kwa vitendo vya ukahaba huo, isipelekwe hekaluni kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kulipia nadhiri, maana mwanamume au mwanamke aliye kahaba wa kidini ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu.
19“Usimkopeshe ndugu yako Mwisraeli kitu kwa riba; usimtoze riba juu ya mkopo wa fedha, chakula, au chochote ambacho watu hukopesha kwa riba. 20Unaweza kutoza riba unapomkopesha mgeni, lakini ndugu yako Mwisraeli usimtoze riba, naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, atakubariki katika shughuli zako zote utakazofanya katika nchi ambayo unakwenda kuimiliki. 21Unapoweka nadhiri kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, usichelewe kuitekeleza, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wako ataidai kwako, nawe utakuwa na kosa. 22Lakini ukiacha kuweka nadhiri hutakuwa na dhambi. 23Uwe mwangalifu kutimiza nadhiri uliyotamka kwa mdomo wako, maana ulimwahidi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, kwa hiari yako.
24“Ukipitia katika shamba la mzabibu la jirani yako unaweza kula zabibu kadiri uwezavyo, lakini usichume na kuchukua zabibu zozote kikapuni mwako. 25Ukipitia katika shamba la jirani yako lenye nafaka unaweza kukwanyua masuke kwa mkono na kula, lakini usichukue mundu kukata mazao yake.



Kumbukumbu la Sheria 23:1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: