Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 26 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 25 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mfalme wa Amani,Muweza wa yote..
Utukuzwe Jehovah,Uabudiwe Yahweh,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..


Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana. Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia. Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu. Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.



Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na tukijiachilia mikononi mwako..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
 kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Jehovah tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi
tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.
Mfalme wa Amani tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Baba wa Mbinguni ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao, na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji. Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa. Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.

Baba wa Mbinguni tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi,famili/ndugu na wote wanaotuzunguka
Ukatamalaki na kutuatamia,tunaomba ulinzi wako, Amani na Upendo
Hekima na Busara vikatawale katka familia zetu..
Tuhurumiane na kusaidiana,tuelekezane kwa upendo na tuchukuliane..
Tukanene yaliyoyako Mungu wetu,Ukatupe kutambua/kujitambua
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Tukasimamie Neno lako Amri na Sheria zako siku zote.
Ukatufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yetu Kristo...
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi

Siku moja Yesu alikuwa anamfukuza pepo aliyemfanya mtu mmoja kuwa bubu. Basi, huyo pepo alipomtoka, yule mtu akaweza kuongea, hata umati wa watu ukashangaa. Lakini baadhi ya watu hao wakasema, “Anawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, mkuu wa pepo.” Wengine, wakimjaribu, wakamtaka afanye ishara kuonesha kama alikuwa na idhini kutoka mbinguni. Lakini yeye, akiwa anayajua mawazo yao, akawaambia, “Ufalme wowote uliogawanyika vikundi vinavyopingana hauwezi kudumu; kadhalika, jamaa yoyote iliyo na mafarakano huangamia. Kama Shetani anajipinga mwenyewe, utawala wake utasimamaje? Mnasemaje, basi, kwamba ninawafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli? Kama ninafukuza pepo kwa uwezo wa Beelzebuli, wafuasi wenu huwafukuza kwa uwezo wa nani? Kwa sababu hiyo, wao ndio watakaowahukumu nyinyi. Lakini ikiwa ninafukuza pepo kwa uwezo wa Mungu, basi jueni kwamba ufalme wa Mungu umekwisha fika kwenu. “Mtu mwenye nguvu anapolinda jumba lake kwa silaha, mali yake yote iko salama. Lakini akija mwenye nguvu zaidi akamshambulia na kumshinda, huyo huziteka silaha zake alizotegemea na kugawanya nyara. Yeyote asiyejiunga nami, ananipinga; na yeyote asiyekusanya pamoja nami, hutawanya.


Yahweh ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu,
wagonjwa,waliokata tamaa,waliokataliwa wanao taabika..
wanaopitia magumu/majaribu,walio katika vifungo vya yule mwovu
Baba wa mbinguni ukawape uponyaji wa mwili na roho pia
wakapate tumaini lako na ukawasimamishe tena..
Ukawape neema ya kuweza kujiombea na kusimamia Neno lako
Ukawafungue na kuwaongoza katika yote,Ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukaonekane katika mapito yao

“Pepo mchafu akifukuzwa kwa mtu, huzururazurura jangwani kukavu akitafuta mahali pa kupumzika. Asipopata, hujisemea: ‘Nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka.’ Anaporudi, huikuta ile nyumba imefagiwa na kupambwa. Basi, huenda na kuwachukua pepo wengine saba wabaya kuliko yeye; wote huenda, wakamwingia mtu huyo. Hivyo, hali ya mtu huyo sasa huwa mbaya zaidi kuliko hapo mwanzo.” Alipokuwa akisema hayo, mwanamke mmoja katika lile kundi la watu, akasema kwa sauti kubwa: “Heri mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!” Lakini Yesu akasema, “Lakini heri zaidi wale wanaolisikia neno la Mungu na kulishika.”

Baba wa Faraja ukawafariji Wafiwa,ukawape amani na uvumilivu..
Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Tuliyoyanena na tusiyoyanena Baba yote unajua na kutujua sisi
zaidi ya tujijuavyo..
Tumaini la kweli lipo kwako,Amani ina wewe..
Upendo wa kweli una wewe Mungu wetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!


Asanteni sana wapendwa katika Kristo,Mungu aendelee kuwabariki
Mungu akawe nanyi na kuwalinda,msipungukiwe katika mahitaji yenu
Baba wa Mbinguni akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.



 

1“Ikiwa kuna ugomvi kati ya watu wawili, wakaenda kuamuliwa mahakamani, mmoja akaonekana hana hatia, na mwingine akahukumiwa, 2kama yule aliyehukumiwa amepewa adhabu ya kuchapwa viboko, hakimu atamwamuru huyo alale chini na kuchapwa viboko kulingana na kosa lake. 3Mwenye hatia anaweza kuchapwa viboko arubaini lakini si zaidi. Mkizidisha kiasi hicho mtakuwa mmemfedhehesha ndugu yenu.
4“Usimfunge ng'ombe kinywa anapopura nafaka.

Jukumu la kaka kwa ndugu yake marehemu

5“Kama ndugu wawili wa kiume wanaishi mahali fulani na mmoja wao akafariki bila kuacha mtoto wa kiume, mkewe marehemu asiolewe na mtu mwingine nje ya jamaa hiyo. Ni wajibu wa ndugu wa marehemu kumwoa mjane huyo. 6Mtoto wa kwanza wa kiume atakayezaliwa nao atahesabiwa kuwa mtoto wa marehemu, ili jina lake lisifutwe nchini Israeli. 7Lakini kama huyo ndugu wa marehemu hamtaki huyo mwanamke mjane, basi, mwanamke huyo atakwenda mbele ya wazee wa mji na kusema, ‘Kaka wa mume wangu marehemu anakataa kuendeleza jina la kaka yake marehemu katika Israeli; hapendi kunitimizia jukumu lake la kaka wa mume wangu marehemu.’ 8Kisha wazee wa mji watamwita huyo mwanamume kuongea naye. Kama bado atasisitiza kwamba hataki kumwoa, 9huyo mwanamke mjane atamwendea mbele ya hao wazee wa mji, atamvua kiatu chake kimoja na kumtemea mate usoni na kumwambia, ‘Hivi ndivyo anavyopaswa kutendewa mtu anayekataa kuidumisha nyumba ya kaka yake.’ 10Na jina la nyumba yake katika Israeli litakuwa: ‘Nyumba ya mtu aliyevuliwa kiatu.’”

Sheria nyingine

11“Wanaume wawili wakipigana na mke wa mmoja wao akamsaidia mumewe kwa kumkamata sehemu za siri yule anayepigana na mumewe, 12mtaukata mkono wa kulia wa huyo mwanamke; msimhurumie.
13“Msiwe na vipimo vya kupimia vya namna mbili: Kimoja kizito na kingine chepesi. Msitumie mizani za udanganyifu. 14Wala msiwe na aina mbili za vipimo vya kupimia, kubwa na ndogo.
15“Tumieni mizani na vipimo vyenye uzito sahihi ili mpate kuishi maisha marefu katika nchi anayowapa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 16Wote wanaofanya mambo hayo, wote wanaotenda kwa udanganyifu ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Amri ya kuwaua Waamaleki

17“Kumbukeni kitendo cha Waamaleki mlipokuwa safarini kutoka Misri. 18Kumbukeni walivyowashambulieni huko njiani mkiwa wanyonge na kuwapiga wale wote waliokuja nyuma yenu wamechoka. Waamaleki hawakumwogopa Mungu. 19Kwa hiyo wakati Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atakapowapumzisha kutokana na mashambulio ya adui zenu wote wanaowazunguka katika nchi ambayo amewapa mwimiliki na kuishi humo, ni lazima muwaangamize Waamaleki wote.


Kumbukumbu la Sheria 25:1-19

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: