Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 4 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 9 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Mungu wetu yu mwema sana..
Ni mwezi/wiki/siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Asante Mungu wetu,Baba yetu,Muumba wetu..
Muumba wa Mbingu na Nchi na vyote vilivyomo..
Asante Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Baba wa Amani..
Mungu mwenye uponyaji,Unayefariji,Unayeokoa..
Mungu wa Wajane,Baba wa Yatima,Muweza wa yote..
Alfa na Omega,Hakuna kama wewe,Matendo yako ni ya Ajabu..
Unatosha Mungu wetu,Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa..
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Jehovah...!!

Enyi mataifa yote, msifuni Mwenyezi-Mungu! Enyi watu wote mhimidini! Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu; uaminifu wake Mwenyezi-Mungu wadumu milele! Msifuni Mwenyezi-Mungu!
Asante Mungu Baba kwa ulinzi wako kwetu..
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Tazama Jana imepita Mungu wetu Leo ni siku Mpya na Kesho ni siku nyingine..
Jehova tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe pale tulipokwenda kinyume nawe Mungu wetu..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..

Heri watu wanaoishi bila kosa, wanaozingatia sheria ya Mwenyezi-Mungu. Heri wanaozingatia matakwa yake, wanaomtafuta kwa moyo wao wote, watu wasiotenda uovu kamwe, bali daima hufuata njia zake. Ee Mungu, umetupatia kanuni zako ili tuzishike kwa uaminifu. Laiti mwenendo wangu ungeimarika, kwa kuyafuata masharti yako! Nikizingatia amri zako zote, hapo kweli sitaaibishwa. Nitakusifu kwa moyo mnyofu, nikijifunza maagizo yako maadilifu. Nitayafuata masharti yako; usiniache hata kidogo.
Mungu wetu utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Ututakase miili yetu na akili zetu utufunike kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..

Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki nyumba/ndoa zetu..
tukaishi kwa upendo na kufuata Neno lako..
watoto wetu ukawape ulinzi wako,wakue kimwili,kiakili,kiroho na kimo..
Ukawalinde na kuwaongoza katika masomo na  ujana wao, wakakutegemee wewe Mungu katika yote


Kijana atatunzaje maisha yake kuwa safi? Kwa kuyaongoza kadiri ya neno lako. Najitahidi kukutii kwa moyo wote; usiniache nikiuke amri zako. Nimeshika neno lako moyoni mwangu, nisije nikakukosea. Utukuzwe, ee Mwenyezi-Mungu! Unifundishe masharti yako. Nitayarudia kwa sauti maagizo yako yote uliyotoa. Nafurahi kufuata maamuzi yako, kuliko kuwa na utajiri mwingi. Nazitafakari kanuni zako, na kuzizingatia njia zako. Nayafurahia masharti yako; sitalisahau neno lako.
familia,wazazi/wazee wetu ukawape umri mrefu na ukawape neema ya kukujua,kukutafuta na kusimamia Neno lako Sheria na Amri zako..


Unitendee mimi mtumishi wako kwa ukarimu, nipate kuishi na kushika neno lako. Uyafumbue macho yangu, niyaone maajabu ya sheria yako. Mimi ni mkimbizi tu hapa duniani; usinifiche amri zako. Roho yangu yaugua kwa hamu kubwa ya kutaka kujua daima maagizo yako. Wewe wawakemea wenye kiburi, walaanifu, ambao wanakiuka amri zako. Uniepushe na matusi na madharau yao, maana nimeyazingatia maamuzi yako. Hata kama wakuu wanakula njama dhidi yangu; mimi mtumishi wako nitayatafakari maamuzi yako. Masharti yako ni furaha yangu; hayo ni washauri wangu.
Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa na wote wanaopitia majaribu mbalimbali,walio katika vifungo vya yule mwovu..


Nagaagaa chini mavumbini; unipe tena uhai kama ulivyoahidi. Nimeungama niliyotenda, nawe ukanijibu; unifundishe masharti yako. Unifundishe namna ya kushika kanuni zako, nami nitayatafakari matendo yako ya ajabu. Niko hoi kwa uchungu; unirudishie nguvu kama ulivyoahidi. Uniepushe na njia za upotovu; unifundishe kwa wema sheria yako. Nimechagua njia ya uaminifu; nimezingatia maagizo yako. Nazingatia maamuzi yako, ee Mwenyezi-Mungu; usikubali niaibishwe! Nitafuata maelekezo ya amri zako, maana unanipa maarifa zaidi.

Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye nguvu,wote wakutafutao na kukuomba Mungu wetu ukawajibu ,ukawape neema ya kusimamia Neno lako na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..


Ee Mwenyezi-Mungu, unifundishe kutii masharti yako; nami nitayashika mpaka mwisho. Unieleweshe nipate kuishika sheria yako, niifuate kwa moyo wangu wote. Uniongoze katika njia ya amri zako, maana humo napata furaha yangu. Unipe ari ya kuzingatia maamuzi yako, na si kwa ajili ya kupata faida isiyofaa. Uniepushe, nisifuate mambo ya upuuzi; unioneshe njia yako, unipe uhai. Unitimizie mimi mtumishi wako ahadi yako; ahadi unayowapa wale wanaokuheshimu. Uniokoe na lawama ninazoogopa; maana maagizo yako ni mema. Natamani sana kuzitii kanuni zako; unijalie uhai maana wewe ni mwadilifu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..
Mungu wetu maisha yetu yapo mikononi mwako..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana Wapendwa/waungwana kwa kuwa nami..
Mungu andelee kuwabariki na kuwatendea kama ipasavyo..
Nawapenda.


Kutotii kwa watu

1“Sikilizeni enyi Waisraeli! Hivi leo mmekaribia kuvuka mto Yordani, kwenda kumiliki nchi ya mataifa makubwa na yenye nguvu kuliko nyinyi. Miji yao ni mikubwa na ina kuta zifikazo mawinguni. 2Watu wenyewe ni warefu na wenye nguvu; ni Waanaki ambao kama mjuavyo na kama mlivyosikia watu husema juu yao ‘Nani awezaye kuwakabili?’ 3Jueni leo hii kwamba anayewatangulia kama moto uteketezao miti ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Yeye atawaangamiza hao na kuwashinda mbele yenu; kwa hiyo mtawafukuza na kuwaangamiza mara moja, kama Mwenyezi-Mungu alivyowaahidi.
4“Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuwafukuza watu hao mbele yenu, msiseme moyoni mwenu kuwa, ‘Ni kwa sababu ya uadilifu wetu Mwenyezi-Mungu ametuleta tuimiliki nchi hii,’ ambapo Mwenyezi-Mungu amewafukuza watu hawa mbele yenu kwa sababu wao ni waovu. 5Mnaweza kuimiliki nchi yao si kwa sababu nyinyi ni watu wema au wenye mioyo safi; bali Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawafukuza watu hao mbele yenu kwa sababu ni waovu na anataka kuliweka imara lile neno alilowaapia babu zenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo. 6Basi, jueni ya kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, anawapeni nchi hii nzuri mwimiliki si kwa sababu mnastahili kuimiliki, maana nyinyi ni watu wakaidi.
7“Kumbukeni na msisahau jinsi mlivyomkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kule jangwani. Tangu siku ile mlipotoka nchi ya Misri mpaka siku mlipofika mahali hapa, nyinyi mmekuwa mkimwasi Mwenyezi-Mungu. 8Hata huko mlimani Horebu, mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, naye alikasirika sana, kiasi cha kutaka kuwaangamiza. 9Nilipopanda mlimani kupokea vibao vya mawe ambavyo viliandikwa agano ambalo Mwenyezi-Mungu alifanya nanyi, nilikaa huko siku arubaini, usiku na mchana; sikula wala kunywa chochote. 10Kisha Mwenyezi-Mungu alinipa vibao viwili vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole chake Mungu; vilikuwa vimeandikwa maneno yote ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaambieni mlimani kutoka kwenye moto siku ya mkutano. 11Naam, baada ya siku hizo arubaini, usiku na mchana, Mwenyezi-Mungu alinipa vibao hivyo viwili vya mawe ambavyo viliandikwa agano.
12“Basi, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Ondoka, ushuke chini ya mlima upesi, kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamepotoka. Wameiacha upesi njia niliyowaamuru wafuate na wamejifanyia sanamu ya kusubu’.
13“Kadhalika, Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Nimewaona watu hawa, ni watu wakaidi sana; 14niache niwaangamize, nilifutilie mbali jina lao duniani; nami nitakufanya wewe kuwa taifa lenye nguvu na kubwa kuliko wao.’
15“Basi, niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, nikiwa nimebeba vile vibao viwili vya mawe, nao moto ulikuwa unawaka mlimani. 16Nilitazama, nikaona kwamba tayari mmekwisha kutenda dhambi dhidi ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mlikwisha jitengenezea sanamu ya ndama ya kusubu; bila kukawia mlikwisha iacha njia ya Mwenyezi-Mungu ambayo aliwaamuru. 17Hivyo, nilivishika vile vibao viwili nikavitupa chini, nikavivunja mbele yenu. 18Kisha nikalala chini kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu, kama hapo awali, kwa muda wa siku arubaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji, kwa sababu ya dhambi mliyokuwa mmetenda kwa kufanya maovu mbele yake Mwenyezi-Mungu kwa kumkasirisha. 19Niliogopa kwamba hasira na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu dhidi yenu, ingewaangamiza; lakini Mwenyezi-Mungu alinisikiliza pia wakati huo. 20Hali kadhalika, Mwenyezi-Mungu alikuwa amemkasirikia sana Aroni, kiasi cha kumwangamiza; hivyo, nikamwombea Aroni wakati huohuo. 21Kile kitu kiovu, yaani yule ndama mliyejitengenezea, nilikichukua, nikakiteketeza motoni, nikakipondaponda na kukisagasaga, kikawa mavumbi laini; halafu nikayatupa hayo mavumbi kwenye kijito kilichotiririka chini ya mlima huo.
22“Pia mlimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, huko Tabera, Masa na Kibroth-hataava. 23Na Mwenyezi-Mungu alipowatuma kutoka Kadesh-barnea akisema, ‘Nendeni mkaimiliki nchi ambayo nimewapatia,’ mlimwasi; hamkusadiki wala hamkutii yale aliyowaambia. 24Nyinyi mmekuwa waasi dhidi ya Mwenyezi-Mungu tangu siku nilipowajua.
25“Kwa hiyo, nililala kifudifudi mbele ya Mwenyezi-Mungu siku hizo arubaini, usiku na mchana, kwa sababu Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema atawaangamiza. 26Nilimwomba Mwenyezi-Mungu, nikisema. ‘Ee Mwenyezi-Mungu, usiwaangamize watu wako na urithi wako, watu uliowakomboa na kuwatoa katika nchi ya Misri kwa uwezo na nguvu yako kubwa. 27Wakumbuke watumishi wako, Abrahamu, Isaka na Yakobo, wala usiujali ukaidi, uovu na dhambi za watu hawa. 28Watu wa kule ulikotutoa wasije wakasema, Mwenyezi-Mungu aliwatoa ili awaue jangwani kwa sababu hakuweza kuwaingiza katika nchi aliyowaahidi na kwa sababu aliwachukia. 29Maana, hawa ni watu wako na urithi wako; watu ambao uliwatoa kutoka Misri kwa nguvu na uwezo wako mkuu.’


Kumbukumbu la Sheria 9:1-29

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: