Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 5 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 10 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema tumshukuru katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi..
Mlinzi wetu,Muweza wa yote,Alfa na Omega..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unasatahili ee Baba..
Utukuzwe Jehovah,Uinuliwa Yahweh,Uhimidiwe Mungu wetu..


Huu ni ufunuo aliotoa Yesu Kristo, ambao Mungu alimpa awaoneshe watumishi wake mambo ambayo yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe mtumishi wake Yohane mambo hayo. Naye Yohane ameshuhudia yote aliyoyaona kuhusu ujumbe wa Mungu na ushahidi wa Yesu Kristo. Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki chenye maneno ya ujumbe wa kinabii; na heri yao wanaosikia na kushika yaliyoandikwa humu, maana wakati wa mambo haya umekaribia. Mimi Yohane nayaandikia makanisa saba yaliyoko Asia. Nawatakieni neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi, na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa kutoka kwa wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia. Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya dhambi zetu, akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina. Tazama! Anakuja na mawingu! Kila mtu atamwona, na hata wale waliomtoboa. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina. “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Nguvu , aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.


Asante Baba wa Mbinguni kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi tumetenda mema sana na wala si kwa nguvu zetu walasi kwa uwezo/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo..
 Mungu wetu ni kwa neema na rehema zako tuu..
Baba wa Mbinguni tukakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako..
 Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Mungu wetu utuepushe katika majaribu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba Mungu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu na utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Baba wa Mbinguni tuomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu..
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu Baba ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Yahweh..!Tazama watoto wetu leo wameanza kurudi shule..
Baba wa Mbinguni tunaomba ulinzi wako,Baraka,Amani ikatawale..
Ukawalinde waingiapo/watokapo,vyote wanavyoenda kufanya Mungu wetu wakafanye sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni ukawaongoze katika masomo yao,wawe kichwa na si mkia,wapate kuelewa na kukumbuka yote wanayofundishwa..
Mungu wetu wewe ndiye mwalimu mkuu..
ukawalinde katika ujana wao wakujue wewe na kufuata Amri,sheria zako na wakasimamie Neno lako..

Mungu Baba tazama wenye shida/tabu,wagonjwa na wote wataabikao
waliokatika vifungo vya yule mwovu,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye nguvu..
ukawaponye kiroho na kimwili pia..



Kisha, nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuwako tena. Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa tayari kukutana na mumewe. Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema, “Tazama! Maskani ya Mungu kati ya watu. Atakaa kati yao, nao watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao. Yeye atayafuta machozi yao yote; maana kifo hakitakuwako tena, wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale imepita!” Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, “Tazama, nafanya yote mapya.” Tena akaniambia, “Andika jambo hili, maana maneno haya ni ya kuaminika na ya kweli!” Kisha akaniambia, “Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi ya maji ya uhai. Mshindi yeyote atapokea hicho, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa linalowaka moto na madini ya kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili.”

ukawape neema ya kusimamia neno lako nalo liwaweke huru..

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..


Kisha malaika akanionesha mto wa maji ya uhai maangavu kama kioo, yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo. Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji. Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uhai unaozaa matunda mara kumi na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya kuwaponya watu wa mataifa. Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo. Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo, na watumishi wake watamwabudu. Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso zao. Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele. Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika wake awaoneshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde. “Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii yaliyo katika kitabu hiki.” Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia na kuona, nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionesha mambo hayo, nikataka kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu hiki. Mwabudu Mungu!” Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia. Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema, na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.” “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi pamoja na tuzo nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake. Mimi ni Alfa na Omega, wa kwanza na wa mwisho, mwanzo na mwisho.” Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, wapate kuwa na haki ya kula tunda la mti wa uhai, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango yake. Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji. “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya asubuhi!” Roho na Bibi arusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na aseme, “Njoo!” Aliye na kiu na aje; anayependa, na achukue maji ya uhai bila malipo. Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki: Mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya, Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang'anya sehemu yake katika ule mti wa uhai, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa katika kitabu hiki. Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Kweli naja upesi.” Amina. Njoo Bwana Yesu! Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amina.

Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Asante Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Sifa na utukufu tunakurudishia wewe..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Mungu aendelee kuonekana katika maisha yenu...
Nawapenda


Mose anapokea tena amri kumi

(Kut 34:1-10)

1“Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, na sanduku la mbao, halafu uje kwangu huku juu mlimani, 2nami nitaandika maneno yaliyokuwa yameandikwa katika vibao vile ulivyovunja, kisha viweke vibao hivyo katika sanduku’.
3“Basi, nikatengeneza sanduku la mshita na vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nikavitwaa mkononi, nikapanda navyo mlimani. 4Mwenyezi-Mungu akaandika katika vibao hivyo maneno yaleyale kama ya hapo awali: Amri kumi10:4 Amri Kumi: Kiebrania: Maneno kumi. ambazo aliwapeni alipoongea kutoka katika moto siku ya mkutano. Halafu Mwenyezi-Mungu akanipa vibao hivyo. 5Niligeuka, nikashuka kutoka mlimani, na kama Mwenyezi-Mungu alivyoniagiza, niliviweka vibao hivyo ndani ya sanduku nililokuwa nimelitengeneza, na vimo ndani ya sanduku hilo, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.”
6(Watu wa Israeli walisafiri kutoka visima vya watu wa Yaakani hadi Mosera. Hapo, Aroni alifariki, akazikwa. Eleazari mwanawe, akachukua nafasi yake kama kuhani. 7Kutoka hapo, walisafiri hadi Gudgoda, na kutoka Gudgoda hadi Yot-batha, eneo lenye vijito vingi vya maji. 8Wakati huo, Mwenyezi-Mungu aliwateua watu wa kabila la Lawi wawe wakilibeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, wamtumikie kama makuhani na kubariki watu kwa jina lake hata hivi leo. 9Ndio maana kabila la watu wa Lawi halina sehemu ya nchi ya urithi pamoja na ndugu zao; walichopokea ni heshima ya kuwa makuhani wa Mwenyezi-Mungu, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alivyoahidi).
10“Nilikaa mlimani kwa muda wa siku arubaini, usiku na mchana, kama hapo awali. Mwenyezi-Mungu alinisikiliza kwa mara nyingine tena na akakubali kwamba hatawaangamiza. 11Kisha akaniambia ‘Ondoka uendelee na safari yako ukiwaongoza watu ili waweze kuingia na kuimiliki nchi niliyowaapia babu zenu ya kuwa nitawapa’.

Anachotaka Mungu

12“Sasa, enyi Waisraeli, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu anataka nini kwenu, ila kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuzifuata njia zake zote, kumpenda, kumtumikia Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na kwa roho zenu zote, 13na kuzitii amri na masharti ya Mwenyezi-Mungu ninayowawekea leo, kwa manufaa yenu wenyewe? 14Tazama, mbingu hata mbingu za mbingu ni mali yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; dunia na vyote vilivyomo ni mali yake. 15Tena Mwenyezi-Mungu aliwapenda babu zenu kwa dhati, akawachagua nyinyi wazawa wao kuwa watu wake badala ya watu wengine wote, kama ilivyo hivi leo. 16Kwa hiyo, takaseni mioyo yenu, msiwe wakaidi tena. 17Maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ndiye Mungu wa miungu na Bwana wa mabwana. Yeye ni Mungu mkuu na mwenye nguvu, na wa kuogofya; hapendelei wala hapokei rushwa. 18Huwapa haki yatima na wajane; huwapenda wageni na kuwapa chakula na nguo. 19Basi, wapendeni wageni kwa kuwa nanyi pia mlikuwa wageni nchini Misri. 20Mcheni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; mtumikieni; ambataneni naye na kuapa kwa jina lake. 21Yeye ni fahari yenu; ndiye Mungu wenu ambaye amewatendea haya mambo makubwa na ya kutisha mliyoyaona kwa macho yenu wenyewe. 22Babu zenu walipokwenda Misri, walikuwa watu sabini tu, lakini sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi kama nyota za mbinguni.



Kumbukumbu la Sheria 10:1-22

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: