Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 28 September 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 27 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana,Tumshukuru katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Uhimidiwe Jehovah..
Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa,Unatosha Baba wa Mbinguni..
Hakuna kama wewe Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo.
Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi,Muumba wa vyote
vinavyoonekana na visivyoonekana..
Matendo yako ni ya Ajabu..!



Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa hekalu pamoja na Masadukayo walifika. Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonesha wazi kwamba wafu watafufuka. Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake. Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu wanaume 5,000. Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na waalimu wa sheria walikusanyika pamoja huko Yerusalemu. Walikutana pamoja na Anasi kuhani mkuu, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa kuhani mkuu. Walipowasimamisha mitume mbele yao, waliwauliza, “Nyinyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?” Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, “Viongozi na wazee wa watu! Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima, basi, nyinyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye nyinyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka kwa wafu. Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: ‘Jiwe mlilokataa nyinyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.’ Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye.” Hao wazee wa Baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu. Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu. Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha. Wakaulizana, “Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba muujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo. Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu.” Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu. Lakini Petro na Yohane wakawajibu, “Amueni nyinyi wenyewe kama ni sawa mbele ya Mungu kuwatii nyinyi kuliko kumtii Mungu. Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia.” Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo. Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arubaini.

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako.
Mungu wetu tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya 
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mfalme wa Amani tunaomba utuepushe katika majaribu
Utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..


Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo! Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: ‘Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure? Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’ “Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.” Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga.



Mungu wetu tunaomba utubariki na ukabariki kazi za mikono yetu
Baba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahwe tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu
 ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu ukavitakase na ukavifunike kwa Damu ya
 Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..


Mfalme wa Amani tunakabidhi maisha yetu mikononi mwako..
Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na 
wote wanaotuzunguka,Mungu wetu Amani yako ikawe nasi..
Upendo wetu ukadumu,furaha na baraka zisitupite..
Utu wema na fadhili,Ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu..
Ukatupe ulinzi wako sisi na vyote tunavyovimiliki..
Ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wanaopitia
 magumu/majaribu mbalimbali,ukawaokoe na kuwaponya wote walio katika vifungo vya yule mwovu..
Ukawarudishe kundini wote waliopotea,Baba ukasikie kuomba kwetu,Baba ukawape neema ya kuweza kujiombea na kufuata njia zako ili wawe huru..
Utupe neema ya kusimamia Neno lako  Amri na Sheria zako 
siku zote za maisha yetu,Ee Baba utuhurumie..!



Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Asante Mungu wetu yote tunayaweka mikononi mwako..
Tukiamini wewe ni Mungu wetu hakuna mwingine kama wewe..
Sifa na Utukufu tunakurudisha Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakuwa nami na kunisoma
Mfalme wa Amani na baraka aendelee kutawala katika maisha yenu
Mkono wa Mungu ukawaguse na kuwatendea katika maisha yenu..
Nawapenda.


Sheria za Mungu zilizoandikwa kwenye mawe

1Basi, Mose akiwa pamoja na wazee wa Israeli aliwaambia watu hivi: “Shikeni amri zote ninazowapa leo. 2Siku ile mtakapovuka mto Yordani na kuingia katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewapeni, mtasimika mawe makubwa na kuyapiga lipu. 3Juu yake mtaandika maneno yote ya sheria zote hizi, mtakapoingia katika nchi inayotiririka maziwa na asali ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu, aliwaahidi. 4Mkiwa ngambo ya mto Yordani, mtasimika mawe hata juu ya mlima Ebali, kama ninavyowaamuru hivi leo, na kuyapiga lipu. 5Mtamjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, madhabahu mahali hapo palipo na mawe ambayo hayakuchongwa. 6Naam, madhabahu yoyote mtakayomjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lazima ijengwe kwa mawe yasiyochongwa. Juu ya madhabahu hiyo mtamtolea Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu sadaka za kuteketezwa. 7Mtamtolea sadaka za amani, na kula papo hapo na kufurahi mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 8Mtaandika waziwazi juu ya mawe hayo maneno yote ya sheria hii.”
9Basi, Mose pamoja na makuhani Walawi wakawaambia watu wote wa Israeli, “Nyamazeni mnisikilize enyi watu wa Israeli. Leo hii nyinyi mmekuwa watu wake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 10Kwa hiyo mtatii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mkizifuata amri zake na masharti yake ambayo ninawaamuru leo.”

Laana ya kutotii

11Siku hiyo Mose aliwaagiza watu na kusema, 12“Mkisha vuka Yordani, makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Gerizimu kuwabariki watu: Simeoni, Lawi, Yuda, Isakari, Yosefu na Benyamini. 13Na makabila yafuatayo yatasimama juu ya mlima Ebali wakati laana zitakapotolewa: Reubeni, Gadi, Asheri, Zebuluni, Dani na Naftali. 14Nao Walawi watawatangazia watu wote wa Israeli kwa sauti kubwa:
15“ ‘Alaaniwe mtu yeyote afanyaye sanamu ya kuchonga au ya kusubu na kuisimamisha kwa siri, kitu ambacho kimetengenezwa na mikono ya fundi na ambacho ni chukizo kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
16“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayemdharau baba yake au mama yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
17“ ‘Alaaniwe mtu yeyote aondoaye alama ya mpaka wa jirani yake.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
18“ ‘Alaaniwe mtu yeyote ampotoshaye kipofu njiani.’ Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
19“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayepotosha haki ya mgeni au yatima au mjane’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
20“ ‘Alaaniwe mwanamume alalaye na mke wa baba yake, maana amemwaibisha baba yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
21“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mnyama yoyote’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
22“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na dada yake awe ni binti ya baba yake au binti ya mama yake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
23“ ‘Alaaniwe mtu yeyote alalaye na mama mkwe wake’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
24“ ‘Alaaniwe mtu yeyote anayeua mtu kwa siri’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
25“ ‘Alaaniwe mtu yeyote apokeaye hongo ili aue mtu asiye na hatia’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’
26“ ‘Alaaniwe mtu yeyote asiyekubali maneno haya ya sheria na kuyatii’. Na watu wote wataitika, ‘Amina!’


Kumbukumbu la Sheria 27:1-26

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: