Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 2 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 29 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Haleluyah..!Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Ni Mwezi/wiki/siku nyingine tena Baba wa Mbinguni umetuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa Ulinzi wako wakati wote..



Basi, tukiwa wafanyakazi pamoja na Mungu, tunawasihi msikubali ile neema mliyopokea kutoka kwa Mungu ipotee bure. Mungu asema hivi: “Wakati wa kufaa nimekusikiliza, wakati wa wokovu nikakusaidia.” Basi, sasa ndio wakati wa kufaa; sasa ndiyo siku ya wokovu! Kusudi tusiwe na lawama yoyote katika utumishi wetu, hatupendi kumwekea mtu yeyote kizuizi chochote. Badala yake, tunajionesha kuwa kweli watumishi wa Mungu kwa kila kitu: Kwa uvumilivu mwingi wakati wa mateso, shida na taabu. Tumepigwa, tumetiwa gerezani na kuzomewa hadharani; tumefanya kazi tukachoka; tumekesha na kukaa bila kula. Tunajionesha kuwa watumishi wa Mungu kwa usafi wa moyo, elimu, uvumilivu na wema; kwa Roho Mtakatifu, kwa upendo usio na unafiki, kwa ujumbe wa kweli na kwa nguvu ya Mungu. Uadilifu ndiyo silaha yetu kila upande. Tuko tayari kupata heshima na kudharauliwa, kulaumiwa na kusifiwa. Twadhaniwa kuwa waongo, kumbe twasema kweli; kama wasiojulikana, kumbe twajulikana kwa wote; kama waliokufa, lakini mwonavyo, sisi ni hai kabisa. Ingawa tumeadhibiwa, hatukuuawa; ingawa tunayo huzuni, twafurahi daima; ingawa tu maskini, twatajirisha watu wengi; twaonekana kuwa watu tusio na chochote, kumbe tuna kila kitu. Ndugu Wakorintho, tumezungumza nanyi kwa unyofu; mioyo yetu iko wazi kabisa. Kama mnaona kuna kizuizi chochote kile, kizuizi hicho kiko kwenu nyinyi wenyewe, na si kwa upande wetu. Sasa nasema nanyi kama watoto wangu: Wekeni mioyo yenu wazi kama nasi tulivyofanya.
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba  wa Nchi na Mbingu
Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Muweza wa yote,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..
Hakuna kama wewe Mungu wetu,Matendo yako ni ya ajabu..
Unatosha Mungu wetu,Unastahili kuwabudiwa,Unastahili sifa..
Uhimidiwe Baba wa Mbinguni,Utukuzwe Jehovah..

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe makosa yetu tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..



Msiambatane na watu wasioamini. Je, wema na uovu vyapatana kweli? Mwanga na giza vyawezaje kukaa pamoja? Kristo anawezaje kupatana na Shetani? Mwaamini ana uhusiano gani na asiyeamini? Hekalu la Mungu lina uhusiano gani na sanamu za uongo? Maana sisi ni hekalu la Mungu aliye hai. Kama Mungu mwenyewe alivyosema: “Nitafanya makao yangu kwao, na kuishi kati yao. Nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.” Kwa hiyo Bwana asema pia: “Ondokeni kati yao, mkajitenge nao; msiguse kitu najisi, nami nitawapokea. Mimi nitakuwa Baba yenu, nanyi mtakuwa wanangu, waume kwa wake, asema Bwana Mwenye Nguvu.”
Baba wa Mbinguni tumaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie, ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya. Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu. Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote, lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aoneshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uhai wa milele. Kwake yeye aliye Mfalme wa milele, asiyekufa, asiyeonekana na aliye Mungu pekee – kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina. Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri, na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao. Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahita yetu Mungu wetu ukatupe
 sawasawa na mapenzi yako..


Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako..
Tunaomba ukabariki Nyumba/Ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,Amani ikatawale,
ukatamalaki na kutuatamia,ukatuguse kwa mkono wako
baraka,Furaha,upendo,utuwema na fadhili ziwe nasi..
Ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako
siku zote za maisha yetu..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama 
inavyokupendeza wewe..




Basi, ueni chochote kilicho ndani yenu ambacho ni cha kidunia: Uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu). Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi. Wakati mmoja nyinyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo. Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: Hasira, tamaa na uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwani nyinyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote, mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu. Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote. Nyinyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo, basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe nyinyi. Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo, kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili. Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo nyinyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani! Ujumbe wa Kristo na ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni Zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani. Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.


Roho Mtakatifu akatuongoze na tukapate kutambua/kujitambua
tukanene yaliyo yako Mungu wetu na tukawe na kiasi..


Yahweh tazama wenye shida/tabu,wagonjwa na wenye njaa
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio katika vifungo vya 
yule mwovu na waliokata tamaa..
Mungu wetu ukawaguse na mkono wako wenye wenye nguvu..
ukawaponye kimwili na kiroho pia,Ukawape neema ya kujua njia zako
waweze kujiombea na kukutafuta wewe Mungu,ukasikie kulia kwao na ukawafute machozi yao,Ukapokee sala/maombi yao na ukawatendee
kama inavyokupendeza wewe..


Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu. Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni. Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo. Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri wakati mlio nao. Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na yaliyokolezwa kwa chumvi na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.


Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu Baba..

Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa/waungwana kwa kuwa nami..
Mungu wetu aendelee kutubariki katika yote yampendezayo
Amani na Upendo ukatawale katika maisha yenu..
Nawapenda.


Agano la Mwenyezi-Mungu na Waisraeli nchini Moabu

1Haya ni maneno ya agano ambalo Mwenyezi-Mungu aliwaamuru Mose kufanya na Waisraeli katika nchi ya Moabu, licha ya agano Mwenyezi-Mungu alilofanya nao mlimani Horebu. 2Mose aliwaita pamoja Waisraeli wote akawaambia, “Mliona nyinyi wenyewe jinsi Mwenyezi-Mungu alivyomtendea mfalme wa Misri, maofisa, watumishi wake na nchi yake yote. 3Mliona maafa makubwa, ishara na maajabu aliyotenda. 4Lakini mpaka leo Mwenyezi-Mungu hajawapa akili ya kuelewa, macho ya kuona, wala masikio ya kusikia!
5“Kwa muda wa miaka arubaini, mimi niliwaongoza jangwani, nguo zenu mlizovaa hazikuchakaa wala viatu vyenu havikuchakaa miguuni mwenu. 6Hamkula mkate wala kunywa divai au kileo chochote kile, mpate kujua kwamba Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu.
7“Na mlipofika mahali hapa, mfalme Sihoni wa Heshboni na mfalme Ogu wa Bashani walikuja kupigana nasi; lakini tukawashinda, 8tukaichukua nchi yao, tukayagawia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu kabila la Manase iwe mali yao. 9Kwa hiyo muwe waangalifu kushika maneno yote ya agano hili ili mpate kufanikiwa katika kazi zenu zote.
10“Leo, mmesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nyinyi nyote viongozi wa makabila, wazee wenu, maofisa wenu, 11watoto wenu na wake zenu, wageni wanaoishi miongoni mwenu ambao hukata kuni na kuwatekea maji. 12Mko hapa leo ili kufanya agano hili ambalo Bwana Mungu wenu anafanya leo, 13kwamba atawathibitisha leo kuwa watu wake naye atakuwa Mungu wenu, kama alivyowaapia nyinyi na babu zenu: Abrahamu, Isaka na Yakobo. 14Wala sifanyi agano hili leo kwa niaba yenu tu na kutamka laana zake; sifanyi kwa niaba ya wale tu walio pamoja nasi leo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, 15bali pia kwa niaba ya wale ambao hawapo pamoja nasi leo.
16“Mnajua jinsi tulivyoishi nchini Misri na jinsi tulivyosafiri katika nchi za mataifa mengine. 17Mliona sanamu zao za kuchukiza, miungu ya miti na mawe, ya fedha na dhahabu. 18Chukueni hadhari kwamba hakuna mwanamume, mwanamke, jamaa au kabila lolote linalosimama hapa leo litakalomwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwenda kutumikia miungu ya mataifa mengine. Jambo hili litakuwa kama mzizi utakaomea na kuzaa matunda machungu yenye sumu. 19Kama baada ya kusikia maneno ya agano hili ambayo mmeapishwa, halafu mtu akajiamini mwenyewe moyoni mwake na kusema atakuwa salama, hata kama atafuata ukaidi wake mwenyewe, hiyo itawaangamiza wote, wabaya na wema. 20Mwenyezi-Mungu hatasamehe mtu huyo, nayo hasira ya Mwenyezi-Mungu na wivu wake vitamwakia mtu huyo; laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki zitamjia, naye Mwenyezi-Mungu atalifuta kabisa jina la mtu huyo kutoka duniani. 21Mwenyezi-Mungu atamtenga kutoka miongoni mwa makabila yote ya Israeli apatwe na maafa kufuatana na laana zote za agano zilizoandikwa katika kitabu hiki. 22Katika vizazi vijavyo, wazawa wenu na wageni kutoka nchi ya mbali wataona jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoiletea nchi hii maafa na mateso: 23Imejaa madini ya kiberiti na chumvi, imeteketea na kuwa tupu, haikupandwa mbegu na haioti chochote. Ni kama ilivyokuwa wakati Mwenyezi-Mungu alipoangamiza Sodoma na Gomora, Adma na Seboimu, kwa hasira yake kali. 24Naam, mataifa yote yatasema: ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu ameitendea hivyo nchi hii? Hasira hii kubwa inamaanisha nini?’ 25Na jibu litatolewa: ‘Ni kwa sababu walivunja agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wao ambalo alifanya nao alipowatoa katika nchi ya Misri, 26wakaenda kuitumikia na kuiabudu miungu mingine, ambayo hawakuijua hapo awali, wala Mwenyezi-Mungu hakuwa amewapa. 27Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka dhidi ya nchi hii, na kuiletea laana zote zilizoandikwa katika kitabu hiki. 28Naye Mwenyezi-Mungu, akawangoa kutoka katika nchi yao kwa hasira na ghadhabu kubwa, akawatupa katika nchi nyingine kama ilivyo leo.’
29“Mambo ya siri ni ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, lakini yale ambayo ameyafunua ni yetu na wazawa wetu milele, ili tutekeleze maneno yote ya sheria hii.”



Kumbukumbu la Sheria 29:1-29


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: