Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 4 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi Kumbukumbu la Sheria 31 (Kumbukumbu la Torati katika tafsiri nyingine)




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..
Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Utukuzwe Mungu wetu,Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa..
Baba wa yatima,Mume wa wajane,Mfalme wa Amani Muweza wa yote
Alfa na Omega,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Kimbilio letu,Faraja yetu,Baba wa Huruma hakuna kama wewe
Matendo yako ni ya ajabu,Matendo yako ni makuu mno..



Ni vema kukushukuru, ee Mwenyezi-Mungu, kuliimbia sifa jina lako, ee Mungu Mkuu. Ni vema kutangaza fadhili zako asubuhi, na uaminifu wako nyakati za usiku, kwa muziki wa zeze na kinubi, kwa sauti tamu ya zeze. Ee Mwenyezi-Mungu, matendo yako yanifurahisha; nitashangilia kwa sababu ya mambo yote uliyotenda. Matendo yako, ee Mwenyezi-Mungu, ni makuu mno! Mawazo yako ni mazito mno! Mtu mpumbavu hawezi kufahamu, wala mjinga hajui jambo hili:

Tunakuja mbele zako Baba wa Mbinguni tukijinyenyekeza,
tujikishusha na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Jehovah tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya..
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwajua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu
 na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba utufunike kwa Damu ya mwanao mpendwa Bwana na 
Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Biashara,masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda
tukatende sawasawa na mapenzi yako..
ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Yahweh nasi 
tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Tusipungukiwe katika mahitaji yetu 
Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba ukatawale katika maisha yetu..
Amani ikawe nasi katika nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka Mungu wetu ukawe
Mlinzi mkuu,ukatamalaki na kutuatamia,ukatubariki na 
ukatupe macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako
ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyo kupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi




Kumbuka kwamba, katika siku za mwisho kutakuwa na nyakati za taabu. Watu watakuwa na ubinafsi, wenye tamaa ya fedha, wenye majivuno, wenye kujiona, wenye kumtukana Mungu, wasiowatii wazazi wao, wasio na shukrani na waovu; watatokea watu wasio na upendo moyoni, wasio na huruma, wachongezi, walafi na wakali; watachukia chochote kilicho chema; watakuwa wahaini, wakaidi na waliojaa kiburi; watapenda anasa kuliko kumpenda Mungu. Kwa nje wataonekana kama watu wenye kumcha Mungu, lakini wataikana nguvu yake. Jiepushe kabisa na watu wa namna hiyo. Baadhi yao huenda katika nyumba za watu na huwateka wanawake dhaifu waliolemewa mizigo ya dhambi na ambao wanaongozwa na tamaa za kila aina; wanawake ambao wanajaribu daima kujifunza lakini hawawezi kuufikia ujuzi wa huo ukweli. Watu hao huupinga ukweli kama vile Yane na Yambre walivyompinga Mose. Hao ni watu wa akili potovu na imani ya uongo. Lakini hawataweza kuendelea zaidi kwa maana upumbavu wao utaonekana wazi kwa wote. Ndivyo ilivyokuwa kwa akina Yane na Yambre. Wewe, lakini, umeyafuata mafundisho yangu, mwenendo wangu, makusudi yangu katika maisha, imani yangu, uvumilivu wangu, upendo wangu, subira yangu, udhalimu na mateso. Unayajua mambo yaliyonipata huko Antiokia, Ikonio na Lustra. Nilivumilia udhalimu mkubwa mno! Lakini Bwana aliniokoa katika mambo hayo yote. Kila mtu anayetaka kuishi maisha ya kumcha Mungu katika kuungana na Kristo Yesu lazima adhulumiwe. Watu waovu na wadanganyifu wataendelea kuwa wabaya, wakidanganya wengine, na wao wenyewe wakidanganywa. Lakini wewe dumu katika ukweli ule uliofundishwa ukaukubali kabisa. Wawajua wale waliokuwa waalimu wako, wakumbuka kwamba tangu utoto wako umejua Maandiko Matakatifu ambayo yaweza kukupatia hekima iletayo wokovu kwa njia ya imani kwa Kristo Yesu. Maandiko yote Matakatifu yameandikwa kwa uongozi wa Mungu, na yanafaa katika kufundishia ukweli, kuonya, kusahihisha makosa, na kuwaongoza watu waishi maisha adili, ili mtu wa Mungu awe mkamilifu, na tayari kabisa kufanya kila kazi njema.

Baba wa Mbinguni ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote
wataabikao,wagonjwa,wenye njaa,shida/tabu,wali katika
vifungo vya yule mwovu,waliokata taama na wote walioanguka
Baba wa Mbinguni ukawaiunue na kuwapa uponyaji wa mwili
na roho,ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
ukawape neema ya kukujua wewe na kufuata njia zako
wakapate neema ya kujiombea Baba na ukapokee sala/maombi yao
ukasikie kulia kwao na ukawafute machozi yao..
eeh Baba tunaomba upokee sala/maombi ya watoto wako..



Kwa sababu hiyo, nampigia magoti Baba, aliye asili ya jamaa zote duniani na mbinguni. Namwomba Mungu, kadiri ya utajiri wa utukufu wake, awajalieni kwa uwezo wa Roho wake, nguvu ya kuwa imara ndani yenu, naye Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani. Namwomba mpate kuwa na mzizi na msingi katika mapendo kusudi muweze kufahamu pamoja na watu wote wa Mungu jinsi upendo wa Kristo ueneavyo kwa mapana na marefu, kwa kimo na kina. Naam, mpate kujua upendo wa Kristo upitao elimu yote, mjazwe kabisa utimilifu wote wa Mungu. Kwake yeye ambaye kwa nguvu yake ifanyayo kazi ndani yetu aweza kufanya mambo makuu zaidi ya yale tuwezayo kuomba au kufikiria; kwake Mungu uwe utukufu katika kanisa na katika Kristo Yesu, nyakati zote, milele na milele! Amina.
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami
Baraka,Amani,Furaha na upendo visipungue katika maisha yenu
Mungu aendelee kuwabariki na kuwafadhili..
Nawapenda.

Yoshua anachukua mahali pa Mose

(Hes 27:12-23)

1Mose aliendelea kuongea na Waisraeli wote, 2akawaambia, “Mimi sasa nina umri wa miaka 120, na sina nguvu ya kufanya kazi zaidi. Tena Mwenyezi-Mungu, ameniambia kuwa sitavuka mto Yordani. 3Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawatangulia na kuyaangamiza mataifa yanayoishi huko, ili muimiliki nchi yao. Yoshua atakuwa kiongozi wenu kama alivyosema Mwenyezi-Mungu. 4Mwenyezi-Mungu atayaangamiza mataifa hayo kama vile alivyowaangamiza Sihoni na Ogu, wafalme wa Waamori, na nchi yao. 5Mwenyezi-Mungu atawapeni ushindi juu yao nanyi mtawatendea kama nilivyowaamuru. 6Muwe imara na hodari, wala msiwaogope au kutishwa nao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu ndiye anayekwenda pamoja nanyi. Yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa.”
7Kisha Mose akamwita Yoshua, akamwambia mbele ya watu wote wa Israeli, “Uwe Imara na hodari, maana wewe utawaongoza watu hawa kwenda kuimiliki nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaahidi babu zao; nawe utawakabidhi waimiliki. 8Mwenyezi-Mungu ndiye anayewaongoza; yeye atakuwa pamoja nanyi; yeye hataacha kuwasaidia na hatawatupa. Hivyo, msiogope wala msifadhaike.”

Kukumbuka sheria kila mwaka wa saba

9Basi, Mose aliandika sheria hiyo, akawapa makuhani wa ukoo wa Lawi ambao walikuwa na jukumu la kubeba agano la Mwenyezi-Mungu, na wazee wote wa Israeli. 10Kisha akawaamuru akasema, “Kila mwaka wa saba utakuwa mwaka wa mafungulio. Katika sikukuu ya vibanda, mwaka huo, 11wakati watu wa Israeli wanapokuja mbele ya Mwenyezi-Mungu mahali pale atakapochagua mtawasomea watu wote wa Israeli sheria hii. 12Wakusanye watu: Wanaume, wanawake, watoto na wageni wanaoishi katika miji yenu, ili kila mmoja asikie maneno haya ya kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kuwa waangalifu kutekeleza maneno ya sheria hii. 13Nao wazawa wao ambao hawajasikia sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, wapate kuisikia na kujifunza kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, muda wote mtakaoishi katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki ngambo ya mto Yordani.”
14Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Siku yako ya kuaga dunia imekaribia. Mwite Yoshua, mje pamoja katika hema la mkutano ili nimpe maagizo.” Basi, Mose na Yoshua wakaenda katika hema la mkutano, 15naye Mwenyezi-Mungu akawatokea humo katika nguzo ya wingu ambayo ilisimama kwenye mlango wa hema.
16Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Umekaribia sasa kuaga dunia, na baada ya kufariki, watu wataanza kuniacha na kuiendea miungu mingine ya nchi hiyo ambamo watakwenda kuishi; wataniacha na kuvunja agano nililoagana nao. 17Hapo hasira yangu itawawakia siku hiyo, nami nitawaacha na kuuficha uso wangu mbali nao, wataangamizwa. Maovu mengi na taabu zitawavamia hata watambue kwamba maovu hayo yamewapata kwa kuwa Mungu wao hayupo miongoni mwao. 18Hakika nitawaficha uso wangu kwa sababu wamefanya mambo maovu na kuigeukia miungu mingine.
19“Sasa, andika wimbo huu, uwafundishe watu wa Israeli ili uwe ushahidi wangu juu yao. 20Nitakapowapeleka katika nchi inayotiririka maziwa na asali, kama nilivyowaapia babu zao, nao wakala wakashiba na kunenepa, wataigeukia miungu mingine na kuitumikia; watanidharau na kulivunja agano langu. 21Watakapovamiwa na maafa mengi na taabu, wimbo huu utawakabili kama ushahidi kwani hautasahauliwa na wazawa wao. Na hata sasa, kabla sijawapeleka katika nchi niliyoapa kuwapa, naijua mipango ambayo wanapanga.”
22Basi, Mose aliandika wimbo huo siku hiyohiyo, akawafundisha Waisraeli.
23Kisha Mwenyezi-Mungu akamwagiza Yoshua, mwana wa Nuni, akamwambia, “Uwe imara na hodari, maana utawaongoza Waisraeli katika nchi ambayo nimewaapia kuwapa, nami nitakuwa pamoja nawe.”
24Mose alipomaliza kuandika maneno ya sheria hiyo tangu mwanzo mpaka mwisho, 25aliwaambia Walawi, waliokuwa na jukumu la kubeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, 26“Chukueni kitabu hiki cha sheria, mkiweke karibu na sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili kiwe ushahidi dhidi yenu. 27Maana najua mlivyo waasi na wakaidi. Ikiwa mmemwasi Mwenyezi-Mungu wakati niko hai pamoja nanyi, itakuwaje baada ya kifo changu? 28Wakusanye mbele yangu wazee wote wa makabila yenu na maofisa wenu nipate kusema maneno haya wasikie, nazo mbingu na dunia zishuhudie juu yao. 29Maana ninajua kuwa baada ya kifo changu hakika mtakuwa waovu na kuiacha ile njia niliyowaamuru mwifuate. Na katika siku zijazo mtakumbwa na maafa kwa kuwa mtafanya maovu mbele ya Bwana na kumkasirisha kwa matendo yenu.”

Wimbo wa Mose

30Halafu, Mose akakariri maneno ya wimbo huu mbele ya kusanyiko lote la Waisraeli.



Kumbukumbu la Sheria 31:1-30


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: