Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 23 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 10...





Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Mungu wetu yu mwema sana..
Ni wiki/siku nyingine tena Mungu wetu ametupa Kibali cha
kuendelea kuiona Leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu kwa mema mengi aliyotutendea/anayotutendea

Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa uzima/pumzi, afya na kutuamsha salama na
tukiwa tayari kwa majukumu yetu..




Shangilieni kwa sababu ya Mwenyezi-Mungu enyi waadilifu! Kumsifu Mungu ni wajibu wa watu wanyofu. Msifuni Mwenyezi-Mungu kwa zeze; mwimbieni kwa kinubi cha nyuzi kumi. Mwimbieni wimbo mpya; pigeni kinubi vizuri na kushangilia. Neno la Mwenyezi-Mungu ni la kweli; na matendo yake yote ni ya kuaminika. Mungu apenda uadilifu na haki, dunia imejaa fadhili za Mwenyezi-Mungu. Mbingu ziliumbwa kwa neno la Mwenyezi-Mungu, na vyote vilivyomo kwa pumzi ya mdomo wake. Alikusanya maji ya bahari kama katika chupa, vilindi vya bahari akavifunga ghalani. Dunia yote na imwogope Mwenyezi-Mungu! Wakazi wote duniani, wamche! Maana alisema na ulimwengu ukawako; alitoa amri nao ukajitokeza. Mwenyezi-Mungu hupangua mipango ya mataifa, na kuyatangua mawazo yao. Mpango wa Mwenyezi-Mungu hudumu milele; maazimio yake yadumu vizazi vyote. Heri taifa ambalo Mungu wake ni Mwenyezi-Mungu; heri wale aliowachagua kuwa watu wake mwenyewe! Mwenyezi-Mungu huangalia chini kutoka mbinguni, na kuwaona wanadamu wote. Kutoka kwenye kiti chake cha enzi, huwaangalia wakazi wote wa dunia. Yeye huunda mioyo ya watu wote, yeye ajua kila kitu wanachofanya. Mfalme hawezi kuokolewa kwa kuwa na jeshi kubwa; wala shujaa hapati ushindi kwa nguvu zake kubwa. Farasi wa vita hafai kitu kwa kupata ushindi; nguvu zake nyingi haziwezi kumwokoa mtu. Mwenyezi-Mungu huwaangalia wale wamchao, watu ambao wanatumainia fadhili zake. Yeye huwaokoa katika kifo, huwaweka hai wakati wa njaa. Mioyo yetu yamtumainia Mwenyezi-Mungu. Yeye ni msaada wetu na ngao yetu. Naam twafurahi kwa sababu yake; tuna matumaini katika jina lake takatifu. Fadhili zako zikae nasi, ee Mwenyezi-Mungu, kwani sisi tumekuwekea tumaini letu.
Utukuzwe ee Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Unastahili sifa Jehovah,Unastahili kuabudiwa Yahweh..
Matendo yako ni ya ajabu mno,Matendo yako ni makuu sana..
Hakuna kama wewe ee Mungu wetu,Unatosha Jehovah..!

Tazama jana imepita Leo ni siku mpya na kesho ni siku nyingine
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyeyekeza,
tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako Yahweh..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,wakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mfalme wa amani nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu
Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
 wa Nazareti..
Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..





Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala, akatawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka hamsini na mitano. Alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kuiga mienendo miovu ya mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyafukuza wakati watu wake wa Israeli walipokuwa wanaingia nchini. Kwa maana alirekebisha mahali pa kuabudia miungu mingine palipokuwa pamebomolewa na Hezekia baba yake; akajenga madhabahu za kuabudia Mabaali, akatengeneza na sanamu za Maashera. Isitoshe, aliabudu vitu vyote vya mbinguni na kuvitumikia. Alijenga madhabahu katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu mahali ambapo Mwenyezi-Mungu alikuwa amesema, “Jina langu litaabudiwa milele katika Yerusalemu.” Alijenga madhabahu za kuabudia vitu vyote mbinguni kwenye nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Pia aliwatoa wanawe kama sadaka ya kuteketeza katika bonde la mwana wa Hinomu. Alipiga ramli, alibashiri na alitumia hirizi; hata alishirikiana na waaguzi wa mizimu na wachawi. Alitenda maovu mengi mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamkasirisha. Nayo sanamu aliyoitengeneza, aliiweka katika nyumba ya Mungu mahali alipopazungumzia, mbele ya Daudi na Solomoni mwanawe: “Katika nyumba hii na katika Yerusalemu kati ya makabila kumi na mawili ya Israeli, ndipo mahali nitakapoabudiwa milele. Na iwapo watu wa Israeli watajali kutenda yote niliyowaamuru, wakatii sheria zote, masharti, na maagizo yaliyotolewa kwa mkono wa Mose, basi kamwe sitawaacha wafukuzwe kutoka katika nchi hii ambayo niliwapa babu zao.” Lakini Manase aliwapotosha watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu, wakatenda maovu zaidi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu aliyaangamiza mbele ya watu wa Israeli.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende
sawasawa na mapenzi yako..
Yahweh ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu tunaomba nasi utupe neema ya kuwabariki wenye kuhitaji
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe kama
inavyokupendeza wewe..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na
wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,Baraka,utuwema,fadhili
Baba ukatupe neema ya hekima,busara,heshima,upendo wa kweli
tukasaidiane,tukachukuliane na tukaonyane/kuelimishana kwa upendo
Baba wa Mbinguni pendo lako likadumu,Nuru ikaangaze katika maisha
yetu,tukawe na kiu/shauku ya kukutafuta wewe Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba utupe neema ya kusimamia Neno
lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..



Mwenyezi-Mungu alimwonya Manase na watu wake, lakini hawakumsikia. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu akawaleta makamanda wa jeshi la mfalme wa Ashuru. Hao makamanda walimkamata Manase kwa kulabu wakamfunga pingu za shaba, wakampeleka hadi Babuloni. Wakati alipokuwa taabuni, alimwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, akajinyenyekesha sana mbele ya Mungu wa babu zake. Alimsihi, naye Mungu akapokea ombi lake na sala yake akamrudisha Yerusalemu katika ufalme wake. Ndipo Manase akatambua kuwa Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.

Ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote,
tupate kutambua/kujitamnbu na tukawe na kiasi..

Tazama wenye shida/tabu Mungu wetu,wagonjwa,wenye njaa,
waliokatika vifungo vya yule mwovu,wanaopitia magumu/majaribu
mbalimbali,waliokata tamaa,waliokataliwa,wanaotafuta watoto,
wanaotafuta wenza mke/mume mwema na wote waliopotea/anguka
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kiroho na kimwili
Mfalme wa amani ukatawale kwenye maisha yao na mwanga wako
ukaangaze katika mapito yao,Jehovah nukawape neema ya kujiombea
na wakafuate njia zako nazo zikawaweke huru..
Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale wote waliokwenda kinyume nawe
Yahweh ukawatendee wenye njaa,Baba ukawape maarifa na ubunifu
katika maisha yao,kazi,biashara,kilimo na wote wakutafutao kwa bidii
Baba ukaonekane katika shida zao,Mungu wetu ukasikie kulia kwao
Baba ukawafute machozi ya watoto wako,Mungu wetu ukapokee
Maombi/sala zetu,wafiwa ukawe mfarinji wao..




Baada ya haya, Manase alijenga ukuta mwingine upande wa nje wa mji wa Daudi, magharibi mwa Gihoni, bondeni, akauendeleza hadi Lango la Samaki, akauzungusha hadi Ofeli; akauinua juu sana. Pamoja na hayo, aliweka makamanda wa majeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome. Alitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu miungu yote ya kigeni na sanamu pamoja na madhabahu zote alizokuwa amezijenga kwenye mlima wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu na katika Yerusalemu; alivitupa nje ya mji. Alirudisha madhabahu ya kumwabudia Mwenyezi-Mungu, na juu yake akatoa tambiko za amani na za shukrani, akawaamuru watu wa Yuda wamwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Hata hivyo watu waliendelea kutoa sadaka mahali pa kufanyia ibada, lakini kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao tu.
Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako
tukiamini na kushukuru daima..
Sifa na utukufu ni wako Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele
Amina...!


Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwakuwa nami
Baba wa upendo aendelee kuwabariki na kuwatendea
sawasawa na mapenzi yake,Amani ya Kristo iwe nanyi daima
Nawapenda.

Waamori wanashindwa

1Mfalme Adoni-sedeki wa Yerusalemu10:1 Yerusalemu: Wakati huo mji huu ulikuwa wa Wayebusi. alipata habari juu ya jinsi Yoshua alivyouteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa akiutendea mji huo na mfalme wake kama alivyoutendea Yeriko na mfalme wake. Pia alipata habari kwamba wakazi wa Gibeoni walikuwa wamefanya mkataba wa amani na Waisraeli na kwamba sasa wanaishi miongoni mwao. 2Habari hizo zilisababisha hofu kubwa huko Yerusalemu kwa sababu mji wa Gibeoni ulikuwa maarufu miongoni mwa miji ya kifalme. Isitoshe, mji huu ulikuwa maarufu kuliko Ai na wanaume wake wote walikuwa askari hodari mno. 3Basi, Mfalme Adoni-sedeki akapeleka ujumbe kwa mfalme Hohamu wa Hebroni, mfalme Piramu wa Yarmuthi, mfalme Yafia wa Lakishi na mfalme Debiri wa Egloni, akawaambia, 4“Njoni mnisaidie tuwaangamize Wagibeoni, maana wamefanya mkataba wa amani na Yoshua pamoja na Waisraeli.” 5Kisha wafalme hao watano wa Waamori: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni, wakaunganisha majeshi yao, wakaenda nayo mpaka Gibeoni; wakapiga kambi kuuzingira mji huo, wakaushambulia.
6Wagibeoni wakapeleka ujumbe kwa Yoshua huko kambini Gilgali, wakamwambia, “Tafadhali, usitutupe sisi watumishi wako; njoo upesi utusaidie na kutuokoa kwa maana wafalme wote wa Waamori kutoka nchi ya milimani wamekuja kutushambulia.”
7Basi, Yoshua pamoja na jeshi lake lote na mashujaa wakaondoka Gilgali. 8Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Usiwaogope hata kidogo maana nimewatia mikononi mwako, wala hakuna hata mmoja atakayeweza kukukabili.” 9Baada ya kutembea kutoka Gilgali usiku kucha, Yoshua akawatokea ghafla. 10Naye Mwenyezi-Mungu akawatia hofu kuu mbele ya Waisraeli ambao waliwaua watu wengi huko Gibeoni wakiwakimbiza kwenye njia ya mteremko wa Beth-horoni mpaka Azeka na Makeda ambako pia waliwaua watu wengi sana. 11Walipokuwa wakiwakimbia Waisraeli kwenye mteremko wa Beth-horoni, Mwenyezi-Mungu akawanyeshea mvua ya mawe makubwa kutoka mbinguni wakiwa njiani mpaka Azeka hata waliouawa kwa mawe hayo wakawa wengi kuliko waliouawa kwa silaha za Waisraeli.
12Wakati Mwenyezi-Mungu alipowatia Waamori mikononi mwa Waisraeli, Yoshua alimwomba Mwenyezi-Mungu mbele ya Waisraeli wote, akasema,
“Wewe jua, simama kimya juu ya Gibeoni,
wewe mwezi, katika bonde la Aiyaloni.”
13 Taz 2Sam 1:18 Jua likasimama kimya na mwezi ukasimama mpaka taifa la Israeli lilipolipiza kisasi maadui wake. Kama alivyoandika katika kitabu cha Yashari, jua lilisimama kimya katikati ya mbingu, likakatiza safari yake ya kwenda kutua kwa siku nzima. 14Siku kama hiyo haijawahi kuwako kamwe wala haijapata kuonekana tena, siku ambayo Mwenyezi-Mungu amemwitikia binadamu kwa namna hiyo; maana Mwenyezi-Mungu mwenyewe aliwapigania Waisraeli.
15Kisha Yoshua akarudi kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote.

Yoshua anawaua wafalme watano wa Waamori

16Wale wafalme watano walikimbia na kujificha katika pango la Makeda. 17Yoshua akapata habari kwamba wafalme hao wamegunduliwa walikojificha katika pango la Makeda. 18Yoshua akasema, “Vingirisheni mawe makubwa mlangoni mwa pango na kuweka walinzi hapo. 19Lakini nyinyi msikae huko, bali muwafuatie adui zenu. Muwapige kutoka upande wa nyuma, wala musiwaache waingie mijini mwao, maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.” 20Yoshua pamoja na Waisraeli waliwapiga na kuwaangamiza wote, na wachache wao walionusurika walikimbilia kwenye miji yao yenye ngome. 21Baada ya hayo Waisraeli wote walirudi salama kwa Yoshua huko kambini Makeda; na hakuna tena mtu aliyethubutu kusema lolote dhidi ya Waisraeli.
22Kisha Yoshua akasema, “Fungueni mlango wa pango mniletee kutoka humo wale wafalme watano.” 23Wakafanya hivyo, wakamletea Yoshua wale wafalme watano: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni. 24Wafalme hao walipoletwa, Yoshua akawaita Waisraeli wote na wakuu wa majeshi waliokwenda naye vitani, akawaambia, “Njoni karibu mwakanyage wafalme hawa shingoni mwao.” Nao wakasogea na kuwakanyaga shingoni. 25Yoshua akawaambia “Msiogope, wala msiwe na wasiwasi, muwe imara na hodari, maana hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyowatendea adui zenu ambao mtapigana nao. Kwa hiyo, muwe imara na hodari.” 26Baadaye, Yoshua aliwanyonga kwa kuwaangika kwenye miti mitano ambako walitundikwa mpaka jioni. 27Wakati jua lilipokuwa karibu kutua, Yoshua aliamuru waondolewe juu ya miti walipokuwa wameangikwa na kutupwa pangoni walimokuwa wamejificha. Kisha wakaweka mawe makubwa kwenye mlango wa pango, nayo mawe hayo yako huko mpaka leo.

Yoshua anateka miji ya kusini

28Siku hiyo Yoshua alipouteka mji wa Makeda, alimuua mfalme wake na wakazi wake wote bila kumbakiza hata mtu mmoja. Alimtendea mfalme wa Makeda kama vile alivyomtendea mfalme wa Yeriko.
29Kutoka Makeda, Yoshua pamoja na Waisraeli wote walikwenda Libna wakaushambulia. 30Mwenyezi-Mungu akautia mji huo pamoja na mfalme wao mikononi mwa Waisraeli, wakawaua wakazi wake bila kumbakiza hata mtu mmoja. Walimtendea mfalme wa Libna kama walivyomtendea mfalme wa Yeriko.
31Kisha kutoka Libna Yoshua na Waisraeli wote walikwenda Lakishi, wakauzingira na kuushambulia. 32Naye Mwenyezi-Mungu akautia mji huo mikononi mwa Waisraeli, wakauteka mnamo siku ya pili. Waliwaua wakazi wote wa mji huo kama walivyofanya kule Libna.
33Hapo, mfalme Horamu wa Gerezi akaamua kuja kuwasaidia watu wa Lakishi. Lakini Yoshua alimuua pamoja na watu wake wote, hakumbakiza hata mtu mmoja.
34Kisha kutoka Lakishi, Yoshua na Waisraeli wote walikwenda mpaka Egloni, wakauzingira na kuushambulia. 35Wakauteka siku hiyohiyo na kuwaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Lakishi.
36Halafu kutoka Egloni Yoshua na Waisraeli wote wakaenda mpaka Hebroni, wakaushambulia 37na kuuteka. Wakawaua wakazi wake wote pamoja na mfalme wao; waliiharibu kabisa miji mingine iliyouzunguka, wakawaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Egloni.
38Kisha, Yoshua na Waisraeli wote wakarudi Debiri, wakaushambulia. 39Waliuteka mji huo na mfalme wake pamoja na miji mingine yote iliyouzunguka na kuwaangamiza wote waliokuwamo bila kumbakiza hata mtu mmoja. Waliutendea mji huo kama walivyoutendea mji wa Hebroni na mji wa Libna na wafalme wao.
40Basi, Yoshua aliiteka nchi yote; aliwashinda wafalme wa sehemu za milimani, eneo la Negebu, na sehemu za nchi tambarare na miteremko. Hakuacha chochote chenye uhai ila aliangamiza kila kitu kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alivyoamuru. 41Yoshua aliwashinda watu wote kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na kutoka Gosheni mpaka Gibeoni. 42Aliweza kuitwaa nchi hii yote kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliwapigania Waisraeli. 43Basi, Yoshua akarudi mpaka kambini huko Gilgali pamoja na Waisraeli wote.


Yoshua 10;1-43

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: