Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..Mtakatifu..Mtakatifu Baba wa Mbinguni.. Mungu wetu,Muumba wetu,Muumba wa Nchi na Mbingu Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Baba wa Upendo Baba wa amani, Muweza wa yote,Baba wa Yatima,Mume wa wajane Utukuzwe ee Mungu wetu,Unastahili sifa,Unastahili kuabudiwa, Unastahili kuhimidiwa,Unastahili ee Mungu wetu.. Unatosha Baba wa Mbinguni,Matendo yako ni ya ajabu, Matendo yako ni makuu mno,Hakuna kama wewe Mungu wetu..
Mfalme Yehoshafati wa Yuda alirejea salama katika ikulu yake mjini Yerusalemu. Lakini mwonaji Yehu mwana wa Hanani, alikwenda kumlaki mfalme, akamwambia, “Je, unadhani ni vema kuwasaidia waovu na kuwapenda wamchukiao Mwenyezi-Mungu? Mambo uliyofanya yamekuletea ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Walakini, kuna wema fulani ndani yako. Umekwisha ziondoa sanamu zote za Ashera, mungu wa kike, na umejitahidi sana kumtafuta Mungu kwa moyo wote.”
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu.. Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote.. Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Mungu wetu.. Asante kwa pumzi/uzima,afya na tukiwa tayari kwa majukumu yetu.. Si kwamba sisi ni wema sana,si kwamba sisi ni wazuri mno, si kwa nguvu/utashi wetu sisi kuwa hivi tulivvyo Mungu wetu.. Ni kwa Neema/rehema zako,ni kwa mapenzi yako Jehovah.. Sifa na utukufu tunakurudishia wewe Mungu wetu..
Mfalme Yehoshafati alikaa Yerusalemu, lakini hata hivyo, mara kwa mara aliwatembelea watu wa Beer-sheba kusini, mpaka milima ya Efraimu, upande wa kaskazini. Alifanya hivyo ili kuwavutia watu wamrudie Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. Aliteua waamuzi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, akawaambia, “Muwe waangalifu sana wakati mnapoamua, kwa maana hukumu mtoayo hamwitoi kwa amri ya binadamu, bali kwa amri itokayo kwa Mwenyezi-Mungu, naye yu pamoja nanyi mnapotoa uamuzi. Basi, sasa mwogopeni Mwenyezi-Mungu, muwe waangalifu katika kila jambo mtakalotenda kwa sababu Mwenyezi-Mungu wetu hatavumilia upotoshaji wa haki, wala upendeleo wala ulaji rushwa.” Mjini Yerusalemu, Yehoshafati aliteua Walawi kadhaa, waamuzi na baadhi ya wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi wa magomvi yahusuyo uvunjaji wa sheria za Mwenyezi-Mungu, au ugomvi baina ya wakazi wa mji. Akawaamuru akisema; “Tekelezeni wajibu wenu mkimwogopa Mwenyezi-Mungu, kwa uaminifu na kwa moyo wote. Kila mara ndugu zenu kutoka katika mji wowote ule wanapowaletea shtaka lolote kuhusu uuaji, uvunjaji wa sheria, amri, kanuni au maagizo, washaurini vema ili wasije wakamkosea Mwenyezi-Mungu. Msipofanya hivyo, nyinyi pamoja na ndugu zenu mtapatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini mkiutekeleza wajibu wenu, hamtakuwa na hatia. Amaria, kuhani mkuu, ndiye atakayesimamia mambo yote yanayomhusu Mwenyezi-Mungu, naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, gavana wa Yuda atasimamia mambo yote ya utawala, na Walawi watakuwa maofisa. Jipeni moyo muyatekeleze masharti haya, naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nao walio wema.”
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza, tukijishusha na tukijiachilia mikononi mwako Yahweh.. Tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua.. Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea.. Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti.. Yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..
Baada ya muda, majeshi ya Moabu na Amoni pamoja na baadhi ya Wameuni, waliivamia Yuda. Watu kadhaa walikuja wakamwambia mfalme Yehoshafati, “Jeshi kubwa limekuja kukushambulia kutoka Edomu, ngambo ya Bahari ya Chumvi. Tayari wamekwisha teka Hasason-tamari.” (Hili ni jina lingine la Engedi). Yehoshafati akashikwa na woga, akamwomba Mwenyezi-Mungu amwongoze. Akatangaza watu wote nchini Yuda wafunge. Watu wakaja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakakusanyika ili kumwomba Mwenyezi-Mungu awasaidie. Yehoshafati akasimama katikati ya kusanyiko la watu wa Yuda na Yerusalemu mbele ya ua mpya wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu, akaomba kwa sauti akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zetu, wewe ndiwe Mungu uliye mbinguni! Wewe unazitawala falme zote duniani; unao uwezo na nguvu, wala hakuna awezaye kukupinga.
Jehovah tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Mungu wetu tukatende kama inavyokupendeza wewe.. Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji.. Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu,Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanotuzunguka,Mungu wetu tunaomba ulinzi wako Baba tunaomba nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Yahweh upendo wetu ukadumu,Furaha,utuwema,fadhili... Baba wa mbinguni tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako,Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu,Jehovah tukanene yaliyo yako,tukapate kutambua/kujitambua na tukashirikiane katika shida na raha ukatupe neema ya hekima,busara, kuchukuliana na kuonyana/kuelimishana kwa upendo,upole na amani.. Ukatufanye chombo chema Jehovah nasi tukatumike sawasawa na mapenzi yako.. Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..
Ni wewe ee Mungu wetu, uliyewafukuza wenyeji wa nchi hii wakati watu wako Israeli walipoingia katika nchi hii, ukawapa wazawa wa Abrahamu rafiki yako, iwe yao milele. Nao wamekaa humu, na kukujengea hekalu kwa heshima ya jina lako, wakijua kwamba wakipatwa na maafa yoyote, vita, maradhi mabaya, au njaa, basi watakuja na kusimama mbele ya nyumba hii mbele yako, wakulilie katika shida zao, nawe utawasikiliza na kuwaokoa. Sasa watu wa Amoni, Moabu na wa mlima Seiri, ambao hukuwaruhusu babu zetu washambulie nchi zao walipotoka Misri, wakapitia kandokando wasiwaangamize, tazama, jinsi wanavyotulipa. Wanakuja kututoa katika nchi yako uliyotupa iwe mali yetu. Wewe ndiwe Mungu wetu! Waadhibu, kwani sisi hatuna uwezo wowote mbele ya jeshi kubwa kama hili linalotujia. Hatujui la kufanya ila tunatazamia msaada kutoka kwako.” Wanaume wote wa Yuda, pamoja na wake zao na watoto wao, walikuwa wamesimama hapo mbele ya Mwenyezi-Mungu. Ndipo Roho wa Mwenyezi-Mungu akamjia mmoja wa Walawi aliyekuwa hapo, jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, wa ukoo wa Asafu. Yahazieli akasema, “Sikilizeni watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu na mfalme Yehoshafati, Mwenyezi-Mungu awaambia hivi: Msiogope wala msihangaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. Kesho washambulieni wakati watakapokuwa wakipanda Bonde la Sisi. Mtawakuta mwisho wa bonde, mashariki mwa jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita hivi. Nyinyi jipangeni tu halafu mngojee, na mtaona Mwenyezi-Mungu akiwashinda kwa niaba yenu. Enyi watu wa Yuda na Yerusalemu, msiogope wala msifadhaike. Nendeni vitani, naye Mwenyezi-Mungu atakuwa pamoja nanyi!” Hapo mfalme Yehoshafati akasujudu pamoja na watu wote wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu wakamsujudu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu. Walawi wa ukoo wa Kohathi na Kora, wakasimama na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa sauti kubwa sana. Kesho yake, wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda mpaka katika jangwa la Tekoa. Walipokuwa wanaondoka, Yehoshafati alisimama, akawaambia, “Nisikilizeni, enyi watu wa Yuda na wakazi wa Yerusalemu! Mwaminini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, nanyi mtakuwa imara. Muwe na imani na manabii wake, nanyi mtafaulu.” Baada ya kushauriana na watu, mfalme alichagua wanamuziki fulani, akawaagiza wajivike mavazi yao rasmi kisha watangulie mbele ya jeshi, wakiimba: “Mshukuruni Mwenyezi-Mungu, maana fadhili zake zadumu milele!” Wakati walipoanza kuimba na kusifu, Mwenyezi-Mungu aliwavuruga akili wanajeshi wa Amoni, Moabu na wa Mlima Seiri waliokuja kupigana na Yuda. Na wanajeshi hao wakashindwa. Watu wa Amoni na wa Moabu wakawashambulia wenyeji wa mlima Seiri, na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kuwaangamiza wakazi wa mlima Seiri wakaanza kushambuliana wao kwa wao, wakaangamizana. Jeshi la Yuda lilipofika penye mnara wa ulinzi huko jangwani, waliangalia upande wa maadui, wakaona maiti zimetapakaa kila mahali. Hakuna mtu yeyote aliyenusurika. Yehoshafati na wanajeshi wake wakaenda kuchukua nyara wakakuta ng'ombe wengi, mali, nguo na vitu vingine vya thamani. Iliwachukua muda wa siku tatu kusomba nyara hizo, na hata hivyo, hawakuzimaliza kwani zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Sifa, na kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa yote aliyowafanyia. Ndio maana bonde hilo linaitwa Bonde la Sifa hadi hivi leo. Kisha Yehoshafati akawaongoza wanajeshi wake mpaka Yerusalemu kwa shangwe, kwa sababu Mwenyezi-Mungu aliwashinda maadui zao. Walipofika Yerusalemu, walikwenda moja kwa moja hadi nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakipiga vinanda, vinubi na tarumbeta. Falme zote ziliingiwa na hofu ziliposikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyowashinda maadui za Israeli. Basi, Yehoshafati akatawala kwa amani, na Mungu akampa amani pande zote.
Tazama wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wote wanaopitia magumu/majaribu,waliokata tamaa,walio katika vifungo vya yule mwovu,waliopotea/walioanguka na wote wataabikao na kuelemewa na mizigo,Mungu wetu tunaomba ukawape neema ya kujiombea,wakapate kutambua Mungu muweza wa yote upo na unayaweza yote, Mponyaji wa kweli upo, Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaponye kimwili na kiroho pia,Yahweh ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Jehovah ukaonekane kwenye mapito yao na ukasikie kulia kwao Mungu wetu ukawafute machozi yao Baba wa Mbinguni ukawasimamshe na kuwasamehe
wale wote walikwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukapokee sala/maombi ya watoto wako wote wanokutafuta na kukuomba kwa imani na bidii.. Baba ukawape amani ya moyo,mwanga katika maisha yao, macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako..
Tunayaweka haya yote mikononi mwako Mungu wetu tukiamini Mungu wetu u pamoja nasi jana,leo na hata Milele.. Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Miele Amina..!
Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami Baba wa upendo aendelee kuwatendea sawasawa na mapenzi yake Nawapenda. |
No comments:
Post a Comment