Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 25 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 12...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Mungu wetu Baba yetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima, afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Tunakushukuru ee Mungu wetu,tunakusifu Jehovah,tunakuabudu Baba wa Mbinguni...
Tunakuhimidi,Tunakutukuza Jehovah,Tunakurudishia sifa na Utukufu ni wako Mungu wetu..


Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu, ulimwengu wote! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu na kulisifu jina lake. Tangazeni kila siku matendo yake ya wokovu. Yatangazieni mataifa utukufu wake, waambieni watu wote matendo yake ya ajabu. Maana Mwenyezi-Mungu ni mkuu, anasifika sana; anastahili kuheshimiwa kuliko miungu yote. Miungu ya mataifa mengine si kitu; lakini Mwenyezi-Mungu aliziumba mbingu. Utukufu na fahari vyamzunguka; nguvu na uzuri vyalijaza hekalu lake. Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima, enyi jamii zote za watu; naam, kirini utukufu na nguvu yake. Lisifuni jina lake tukufu; leteni tambiko na kuingia hekaluni mwake. Mwabuduni Mwenyezi-Mungu katika patakatifu pake; tetemekeni mbele yake ee dunia yote! Yaambieni mataifa: “Mwenyezi-Mungu anatawala! Ameuweka ulimwengu imara, hautatikisika. Atawahukumu watu kwa haki!” Furahini enyi mbingu na dunia! Bahari na ivume pamoja na vyote vilivyomo! Furahini enyi mashamba na vyote vilivyomo! Ndipo miti yote misituni itaimba kwa furaha, mbele ya Mwenyezi-Mungu anayekuja; naam, anayekuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa kwa uaminifu wake.
Tukuja mbele zako Yahweh tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majiribu na utuokoe na
yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa mbinguni ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji..
Jehovah tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba wa Mbinguni
ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Basi, tuyaache nyuma yale mafundisho ya mwanzomwanzo juu ya Kristo, tusonge mbele kwa yale yaliyokomaa, na sio kuendelea kuweka msingi kuhusu kuachana na matendo ya kifo, na juu ya kumwamini Mungu; mafundisho juu ya ubatizo na kuwekewa mikono; ufufuo wa wafu na hukumu ya milele. Hilo tutafanya, Mungu akipenda. Maana watu waliokwisha kuangaziwa, wakaonja zawadi za mbinguni, wakashirikishwa Roho Mtakatifu na kuonja wema wa neno la Mungu na nguvu za ulimwengu ujao, kisha wakaiasi imani yao, haiwezekani kuwarudisha hao watubu tena. Hao wanamsulubisha tena Mwana wa Mungu kwa makusudi na kumwaibisha hadharani. Ardhi ambayo huipokea mvua inayoinyeshea mara kwa mara na kuotesha mimea ya faida kwa mkulima imebarikiwa na Mungu. Ardhi ikiota miti ya miiba na magugu, haina faida; karibu italaaniwa na Mungu na mwisho wake ni kuchomwa moto. Ingawa twasema namna hii, wapenzi wetu, tuna uhakika wa kupewa mambo mema zaidi: Yaani wokovu. Mungu hakosi haki; yeye hataisahau kazi mliyoifanya au upendo mliyoonesha kwa ajili yake katika huduma mliyowapa na mnayowapa sasa watu wake. Hamu yetu ni kwamba kila mmoja wenu aoneshe bidii hiyohiyo mpaka mwisho, ili yale mnayotumainia yapate kutimia. Hivyo msiwe wavivu, bali muwe kama wale wanaoamini na wenye uvumilivu, wakapokea yale aliyoahidi Mungu.


Mungu wetu tunaomba ukabariki Ngumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale,upendo ukadumu,
Tunaomba ulinzi wako katika maisha yetu,Baba ukatamalaki na
kutuatamia,Yahweh ukatupe neema ya kusimamia Neno lako
Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukatufanye barua njema nasi tukasomeke kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote tukapate
kutambua/kujitambua, tukanene yaliyo yako na tukawe na kiasi..

Mungu alipompa Abrahamu ahadi, aliapa kwa jina lake mwenyewe, maana hakuna aliye mkuu kuliko Mungu ambaye kwa huyo angeweza kuapa. Mungu alisema: “Hakika nitakubariki na nitakupa wazawa wengi.” Abrahamu alisubiri kwa uvumilivu na hivyo akapokea kile alichoahidiwa na Mungu. Watu wanapoapa, huapa kwa mmoja aliye mkuu kuliko wao, na kiapo husuluhisha ubishi wote. Naye Mungu aliimarisha ahadi yake kwa kiapo; na kwa namna hiyo akawaonesha wazi wale aliowaahidia kwamba hatabadili nia yake. Basi, kuna vitu hivi viwili: Ahadi na kiapo, ambavyo haviwezi kubadilika na wala juu ya hivyo Mungu hawezi kusema uongo. Kwa hiyo sisi tuliokimbilia usalama kwake, tunapewa moyo wa kushikilia imara tumaini lililowekwa mbele yetu. Tunalo tumaini hilo kama nanga ya maisha yetu. Tumaini hilo lapenya mpaka mahali patakatifu mbinguni. Yesu mwenyewe ametangulia kuingia humo kwa ajili yetu na amekuwa kuhani mkuu milele, kwa utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawabariki na kuwagusa kwa
mkono wako wenye nguvu wote wakutafutao kwa imani na bidii
ukawaponye wagonjwa,wenye njaa ukawabariki na kuwatendea
katika utafutaji wao,kilimo,kazi,biashara na ukawape ubunifu
na akili ya utendaji,wavunapo wakavune vyakutosha sawasawa
na mapenzi yako,wafiwa ukawe mfarji wao..

Kwa imani tunayaweka haya yote mikononi mwako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na Amani ya Bwana wetu
Yesu Kristo iwe nanyi daima..
Nawapenda.

Wafalme walioshindwa na Waisraeli

1Wafuatao ndio wafalme ambao Waisraeli waliwashinda na kuchukua nchi yao yote iliyokuwa mashariki ya mto Yordani kutoka bonde la mto Arnoni mpaka mlima Hermoni na nchi yote ya Araba upande wa mashariki: 2Mfalme Sihoni wa Waamori aliyeishi huko Heshboni na kutawala kutoka makao yake makuu huko Aroeri, mji uliokuwa kandokando ya bonde la Arnoni. Alitawala pia kuanzia katikati ya bonde hadi mto Yaboki ambao ulikuwa mpaka wa nchi ya Waamoni, yaani nusu ya nchi ya Gileadi. 3Vilevile, alitawala nchi yote ya Araba, kutoka bahari ya Kinerethi, upande wa mashariki, mpaka Beth-yeshimothi kwenye Bahari ya Chumvi na kuendelea mpaka chini ya mlima Pisga.
4Mwingine ni mfalme Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala Bashani na alikaa Ashtarothi au Edrei. 5Utawala wake ulienea huko kwenye mlima Hermoni, huko Saleka, Bashani yote mpaka mipaka ya Wageshuri na Wamaaka, nusu ya Gileadi hadi mpakani mwa nchi ya mfalme Sihoni wa Heshboni. 6Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, pamoja na Waisraeli aliwashinda wafalme hao, akayapatia nchi hizo makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase ziwe mali yao kabisa.
7Kisha Yoshua pamoja na Waisraeli waliwashinda wafalme wote wa eneo lote lililoko magharibi ya mto Yordani, kuanzia Baal-gadi katika bonde la Lebanoni mpaka mlima uliokuwa mtupu wa Halaki kusini karibu na Seiri. Yoshua akayagawia makabila ya Israeli nchi hizo ziwe mali yao kabisa. 8Nchi hizo zilikuwa pamoja na maeneo ya milima, nchi tambarare, eneo la Araba, miteremko ya milima, maeneo ya nyika, na eneo la Negebu; nchi zilizokuwa za Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. 9Wafalme waliowashinda walikuwa, mmojammoja: Mfalme wa Yeriko, mfalme wa Ai mji ulioko karibu na Betheli, 10mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, 11mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi, 12mfalme wa Egloni, mfalme wa Gezeri, 13mfalme wa Debiri, mfalme wa Gederi, 14mfalme wa Horma, mfalme wa Aradi, 15mfalme wa Libna, mfalme wa Adulamu, 16mfalme wa Makeda, mfalme wa Betheli, 17mfalme wa Tapua, mfalme wa Heferi, 18mfalme wa Afeka, mfalme wa Lasharoni, 19mfalme wa Madoni, mfalme wa Hazori, 20mfalme wa Shimron-meroni, mfalme wa Akshafi, 21mfalme wa Taanaki, mfalme wa Megido, 22mfalme wa Kedeshi, mfalme wa Yokneamu mji ulioko kwenye mlima Karmeli, 23mfalme wa Dori katika mkoa wa Nafath-dori, mfalme wa Goiimu huko Gilgali na 24mfalme wa Tirza. Jumla ya wafalme hao ni thelathini na mmoja.


Yoshua 12;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: