Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Thursday, 12 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 3..




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..! mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Asante Baba wa Mbinguni,Mungu wetu,Muumba wetu..
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Mfalme wa Amani,Muweza wa yote,Mungu mwenye huruma ,Mungu mwenye kusamehe,Baba wa Upendo,Baba wa Baraka..
Baba wa Yatima,Mume wa wajane,Matendo yako ni makuu mno..
Hakuna kama wewe,Hakuna wa kufanana nawe..
Unastahili sifa,Unastahili kusifiwa,Unastahili kuabudiwa..
Unastahili kuhimidiwa,Unastahili Mungu wetu..


Mfalme wa wa amani tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako...
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe dhambi zetu zote
 tulizozifanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Jehovah tunaomba utuepushe katika majaribu na utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote...
Nguvu za giza,nguvu za mizimu,nguvu za mapepo,nguvu za mpinga Kristo zishindwe katika jina lililo kuu
kupita majina yote jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..

Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba tunaomba
utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda
Mungu wetu tukatende sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu
ziingiazo/zitokazo,Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya
kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Baba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani ikatawale katika nyumba/ndoa
zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,Baraka,Baba wa Mbinguni
ukatamalaki na kutuatamia,ukatuongoze katika kunena na kutenda
Baba tukanene/kutenda yanatokupendeza wewe..
Mungu wetu ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na
Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Tukawe barua njema nasi tukasomeke kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na
 tukawe na kiasi...


Mwenyezi-Mungu asema: “Piga kelele, wala usijizuie; paza sauti yako kama tarumbeta. Watangazie watu wangu makosa yao, waambie wazawa wa Yakobo dhambi zao. Siku hata siku wananijia kuniabudu, wanatamani kujua mwongozo wangu, kana kwamba wao ni taifa litendalo haki, taifa lisilosahau sheria za Mungu wao. Wananitaka niamue kwa haki, na kutamani kukaa karibu na Mungu. “Nyinyi mnaniuliza: ‘Mbona tunafunga lakini wewe huoni? Mbona tunajinyenyekesha, lakini wewe hujali?’ “Ukweli ni kwamba wakati mnapofunga, mnatafuta tu furaha yenu wenyewe, na kuwakandamiza wafanyakazi wenu! Mnafunga, na kugombana na kupigana ngumi. Mkifunga namna hiyo maombi yenu hayatafika kwangu juu. Mfungapo, nyinyi mnajitaabisha; mnaviinamisha vichwa vyenu kama unyasi, na kulalia nguo za magunia na majivu. Je, huo ndio mnaouita mfungo? Je, hiyo ni siku inayokubaliwa nami? “La! Mfungo ninaotaka mimi ni huu: Kuwafungulia waliofungwa bila haki, kuziondoa kamba za utumwa, kuwaachia huru wanaokandamizwa, na kuvunjilia mbali udhalimu wote! Mfungo wa kweli ni kuwagawia wenye njaa chakula chako, kuwakaribisha nyumbani kwako maskini wasio na makao, kuwavalisha wasio na nguo, bila kusahau kuwasaidia jamaa zenu. “Mkifanya hivyo mtangara kama pambazuko, mkiwa wagonjwa mtapona haraka. Matendo yenu mema yatawatangulia, nami nitawalindeni kutoka nyuma kwa utukufu wangu. Ndipo mtakapoomba, nami Mwenyezi-Mungu nitawaitikia; mtalia kwa sauti kuomba msaada, nami nitajibu, ‘Niko hapa!’ “Kama mkiiondoa dhuluma kati yenu, mkiacha kudharau wengine na kusema maovu, mkiwapa chakula kwa ukarimu wenye njaa, mkitosheleza mahitaji ya wenye dhiki, mwanga utawaangazia nyakati za giza, giza lenu litakuwa kama mchana. Mimi Mwenyezi-Mungu nitawaongozeni daima, nitatosheleza mahitaji yenu wakati wa shida. Nitawaimarisha mwilini, nanyi mtakuwa kama bustani iliyomwagiliwa maji, kama chemchemi ya maji ambayo maji yake hayakauki kamwe. Magofu yenu ya kale yatajengwa; mtajenga upya juu ya misingi iliyoachwa zamani. Nanyi mtaitwa watu waliotengeneza upya kuta, watu waliozifanya barabara za mji zipitike tena.
Yahweh tazama wenye shida/tamu,wagonjwa,wenye njaa/dhiki
walio dhulumiwa,waliokata tamaa,waliokatawaliwa,
wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio katika
vifungo vya yule mwovu na wote wataabikao na kuelemewa
na mizigo,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu,Baba ukawape uponyaji wa mwili na roho..
Yahweh tunaomba ukawafungue na ukawape neema ya kuweza
kujiombea,Mungu wetu ukawasamehe wale waliokwenda kinyume nawe
Baba wa Mbinguni tunaomba usikie kulia kwao na ukawafute machozi yao,Jehovah tazama wanaokumba na kuamini Baba ukasikie kuomba kwao ukapokee maombi/sala zao..
Baba ukaonekane katika mapito yao na ukawabariki..
Neema zako,Baraka zako,Huruna yako na uponyaji wako vikawafuate watoto wako...

“Kama ukiacha kufanya kazi siku ya Sabato, ukaacha shughuli zako siku yangu hiyo takatifu; kama ukiifanya siku yangu kuwa ya furaha, ukaiheshimu siku hiyo takatifu ya Mwenyezi-Mungu, ukaacha na shughuli zako na kupiga domo, utapata furaha yako kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, nitakupatia ushindi katika kila pingamizi nchini, nitakulisha mali ya Yakobo, babu yako. Mimi, Mwenyezi-Mungu, nimesema.”

Asante Baba wa Mbinguni tunayaweka haya yote mikononi
mwako tukiamini Mungu wetu u pamoja nasi..
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Baba wa neema/rehema aendelee kuwaneemesha katika
yote yampendezayo,Baraka na amani ziwafuate..
Nawapenda.


Waisraeli wanavuka mto Yordani
1Asubuhi na mapema Yoshua pamoja na watu wote wa Israeli walianza safari kutoka Shitimu. Walipoufikia mto Yordani, walipiga kambi hapo kwa muda kabla ya kuvuka. 2Baada ya siku tatu, viongozi walipita katikati ya kambi hiyo, 3wakawaambia watu, “Mtakapoliona sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, limebebwa na makuhani Walawi, mtaondoka na kulifuata; 4ndivyo mtakavyojua njia ya kupita maana hamjapita huku kamwe. Lakini msilikaribie mno sanduku la agano; muwe umbali wa kilomita moja hivi.”
5Yoshua akawaambia watu, “Jitakaseni kwa kuwa kesho Mwenyezi-Mungu atatenda maajabu kati yenu.” 6Kisha akawaambia makuhani, “Chukueni sanduku la agano, mtangulie nalo mbele ya watu.” Nao wakalichukua na kutangulia mbele ya watu.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua: “Leo hii, nitaanza kukutukuza mbele ya watu wote wa Israeli ili wajue kwamba, kama vile nilivyokuwa pamoja na Mose, ndivyo pia nitakavyokuwa pamoja nawe. 8Utawaamuru hao makuhani wanaobeba sanduku la agano wasimame karibu na ukingo wa mto Yordani wakati watakapofika huko.”
9Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli: “Njoni karibu mpate kusikia maneno ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” 10Yoshua akaendelea kusema, “Sasa mtajulishwa kabisa kwamba Mungu aliye hai yu miongoni mwenu na kwamba atawafukuza mbele yenu Wakanaani, Wahiti, Wahivi, Waperizi, Wagirgashi, Waamori na Wayebusi, bila kushindwa. 11Tazameni, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote, liko karibu kupita mbele yenu kuelekea mtoni Yordani. 12Sasa, chagueni watu kumi na wawili kutoka makabila ya Israeli, kila kabila mtu mmoja. 13Wakati nyayo za makuhani wanaobeba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Bwana wa dunia yote, zitakapoingia katika maji ya mto Yordani, maji ya mto huo yataacha kutiririka. Na yale yatakayokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yatajikusanya pamoja kama rundo.”
14Basi, watu waliondoka katika kambi zao ili kwenda kuvuka mto Yordani, nao makuhani wakiwa wamebeba sanduku la agano wanawatangulia watu. 15Na mara tu hao waliobeba sanduku la agano walipofika Yordani na nyayo zao zilipokanyaga ukingoni mwa mto huo (mto Yordani hufurika wakati wa mavuno), 16maji yaliyokuwa yanatiririka kutoka upande wa juu yalisimama na kurundikana mpaka huko Adamu kijiji kilicho karibu na mji wa Sarethani. Maji yaliyokuwa yanateremka kwenda bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yalitoweka kabisa, watu wakavuka mbele ya Yeriko. 17Wakati Waisraeli walipokuwa wanavuka makuhani waliokuwa wanalibeba sanduku la agano walisimama mahali pakavu katikati ya mto Yordani mpaka taifa lote likavuka.


Yoshua 3;1-17

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: