Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 13 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 4..



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa vyote..
Baba wa upendo,Baba wa Baraka,Baba wa  yatima..
Mungu wa Abrahamu Isaka na Yakobo..
Muweza wa yote,wewe ni mwanzo na wewe ni mwisho..
Utukuzwe Baba wa Mbinguni,Usifiwe Mungu wetu,Uhimidiwe Yahweh,Uabudiwe daima,Unatosha ee Mungu wetu,Hakuna kama wewe ee
Jehovah nissi,Jehovah Jireh,Jehovah Shammah,Jehovah Rapha,Jehova Raah, Emanuel -Mungu pamoja nasi..!!


Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako wakati wote..
Asante kwakutuchagua na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Baba wa Mbinguni si kwamba sisi ni wema sana,wala si kwa nguvu/utashi
wetu sisi kuwa wazima na kuwatayari kuendelea na majukumu yetu..
Mungu wetu ni kwa neema/rehema zako,ni kwa mapenzi yako sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..

Yesu alisema nao tena kwa kutumia mifano: “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme aliyemwandalia mwanawe karamu ya harusi. Basi, akawatuma watumishi kuwaita walioalikwa waje harusini, lakini walioalikwa hawakutaka kufika. Akawatuma tena watumishi wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa: Karamu yangu iko tayari sasa; fahali wangu na ndama wanono wamekwisha chinjwa; kila kitu ni tayari; njoni harusini.’ Lakini wao hawakujali, wakaenda zao; mmoja shambani kwake, mwingine kwenye shughuli zake, na wengine wakawakamata wale watumishi wakawatukana, wakawaua. Yule mfalme akakasirika, akawatuma askari wake wakawaangamize wauaji hao na kuuteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumishi wake: ‘Karamu ya harusi iko tayari kweli, lakini walioalikwa hawakustahili. Basi, nendeni kwenye barabara na wowote wale mtakaowakuta waiteni waje harusini.’ Wale watumishi wakatoka, wakaenda njiani, wakawaleta watu wote, wabaya na wema. Nyumba ya harusi ikajaa wageni. “Mfalme alipoingia kuwaona wageni, akamwona mtu mmoja ambaye hakuvaa mavazi ya harusi. Mfalme akamwuliza, ‘Rafiki, umeingiaje hapa bila vazi la harusi?’ Lakini yeye akakaa kimya. Hapo mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni miguu na mikono mkamtupe nje gizani; huko atalia na kusaga meno.’” Yesu akamaliza kwa kusema, “Wengi wamealikwa, lakini wachache wameteuliwa.”

Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya..
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya
kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu kwa Damu ya mwanao mpedwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Kisha, Mafarisayo wakaenda zao, wakashauriana jinsi ya kumnasa Yesu kwa maneno yake. Basi, wakawatuma wafuasi wao pamoja na wafuasi wa kikundi cha Herode. Wakamwuliza, “Mwalimu, tunajua kwamba wewe ni mtu mwaminifu, na kwamba wafundisha njia ya Mungu kwa uaminifu; humwogopi mtu yeyote, maana cheo cha mtu si kitu kwako. Haya, tuambie maoni yako. Je, ni halali au la, kulipa kodi kwa Kaisari?” Lakini Yesu alitambua uovu wao, akawaambia, “Enyi wanafiki mbona mnanijaribu? Nionesheni fedha ya kulipia kodi.” Nao wakamtolea sarafu ya fedha. Basi, Yesu akawauliza, “Sura na chapa hii ni ya nani?” Wakamjibu, “Ni ya Kaisari.” Hapo Yesu akawaambia, “Basi, ya Kaisari mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu.” Waliposikia hivyo wakashangaa; wakamwacha, wakaenda zao.
Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda...
Baba wa Mbinguni tukatende kama inavyokupendeza wewe
Mungu wetu ukavitakase na kuvibariki vyote tunavyoenda kutumia/kugusa ukavifunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo...
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo..
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
 kuwabariki wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Yahweh ukatupe sawasawa na mapenzi yako..


Siku hiyo, baadhi ya Masadukayo wasemao wafu hawafufuki walimwendea Yesu. Basi, wakamwambia, “Mwalimu, Mose alisema mtu aliyeoa akifa bila kuacha watoto, lazima ndugu yake amwoe huyo mama mjane, ili ampatie ndugu yake watoto. Basi, hapa petu palikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa kisha akafa bila kujaliwa watoto, akamwachia ndugu yake huyo mke wake mjane. Ikawa vivyo hivyo kwa ndugu wa pili, na wa tatu, mpaka wa saba. Baada ya ndugu hao wote kufa, akafa pia yule mama. Je, siku wafu watakapofufuka mama huyo atakuwa mke wa nani miongoni mwa wale ndugu saba? Maana wote saba walikuwa wamemwoa.” Yesu akawajibu, “Nyinyi mmekosea kwa sababu hamjui Maandiko Matakatifu wala nguvu ya Mungu. Maana wafu watakapofufuka hawataoa wala kuolewa; watakuwa kama malaika mbinguni. Lakini kuhusu kufufuka kwa wafu, je, hamjasoma yale aliyowaambieni Mungu? Aliwaambia, ‘Mimi ni Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo!’ Basi, yeye si Mungu wa wafu, bali ni Mungu wa walio hai.” Ule umati wa watu uliposikia hivyo ukayastaajabia mafundisho yake.
Mfalme wa Amani tunaomba amani yako,Upendo,Furaha
vikatawale katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Baba ukatubariki na ukatupe hekima,busara,utu wema, huruma na kuchukuliana...
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu na ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu....
Yahweh ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Mafarisayo waliposikia kwamba Yesu alikuwa amewanyamazisha Masadukayo, wakakutana pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza Yesu kwa kumjaribu, “Mwalimu, ni amri ipi iliyo kuu katika sheria?” Yesu akamjibu, “ ‘Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote na kwa akili yako yote’. Hii ndiyo amri kuu na ya kwanza. Ya pili inafanana na hiyo: ‘Mpende jirani yako kama unavyojipenda wewe mwenyewe’. Sheria yote ya Mose na mafundisho ya manabii vinategemea amri hizi mbili.”
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu wote wanaotaabika na kuelemewa na mizigo,wagonjwa,wenye shida/tabu,wenye njaa, waliokatika majaribu/mapito,waliokatika vifungo vya yule mwovu na wote walikata tamaa..
Mungu wetu ukawaponye na kuwaweka huru,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako,
Baba ukawasamehe wale waliokwenda kinyume nawe Mungu wetu ukawakomboe na kuwasimamisha tena
wote walioanguka,Baba wa mbinguni ukaonekane katika mapito yao, Mungu wetu ukapokee sala/maombi yao wote wakuombao na wakutafutao kwa Imani ukawaongoze na ukawape Amani na  Nuru ikaangaze  katika maisha yao..

Mafarisayo walipokusanyika pamoja, Yesu aliwauliza, “Nyinyi mwaonaje juu ya Kristo? Je, ni mwana wa nani?” Wakamjibu, “Wa Daudi.” Yesu akawaambia, “Basi, inawezekanaje kwamba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu Daudi anamwita yeye Bwana? Maana alisema: ‘Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia, mpaka niwaweke maadui zako chini ya miguu yako.’ Basi, ikiwa Daudi anamwita Kristo ‘Bwana,’ anawezaje kuwa mwanawe?” Hakuna mtu yeyote aliyeweza kumjibu neno. Na tangu siku hiyo hakuna aliyethubutu tena kumwuliza swali.
Mungu wetu tunayaweka haya yote mikononi mwako
tukishukuru na kuamini Mungu wetu u pamoja nasi
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa/waungwana asanteni sana kwakunisoma/kuwa nami
Mungu mwenye upendo na baraka aendelee kuwabariki katika yote yampendezayo,msipungukiwe katika mahitaji yenu,Baba akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Mawe ya ukumbusho kumi na mawili

1Taifa zima lilipokwisha vuka mto Yordani, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, 2“Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa hao Waisraeli, yaani mtu mmoja kutoka kila kabila, 3uwaagize hivi, ‘Chukueni mawe kumi na mawili kutoka hapa katikati ya mto Yordani, kutoka hapa ilipo miguu ya makuhani, muyachukue mawe hayo, mkayaweke mahali pale ambapo mtalala leo hii.’”
4Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili ambao alikuwa amewateua miongoni mwa Waisraeli, kila kabila mtu mmoja, 5akawaambia, “Litangulieni sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpaka katikati ya mto Yordani. Kila mmoja wenu achukue jiwe begani mwake, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli. 6Jambo hilo litakuwa ishara kati yenu; na watoto wenu watakapowauliza siku zijazo ‘Je, mawe haya yana maana gani kwenu?’ 7Nyinyi mtawaambia, ‘Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipopitishwa mtoni Yordani, maji ya mto huo yalizuiliwa yasitiririke!’ Kwa hiyo mawe haya yatakuwa ukumbusho kwa Waisraeli milele.”
8Wale wanaume wakafanya kama walivyoamriwa na Yoshua, wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya mto Yordani, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Yoshua, wakaenda nayo hadi mahali pale walipolala, wakayaweka huko. 9Yoshua akasimika pia mawe kumi na mawili katikati ya mto Yordani, mahali pale ambapo nyayo za makuhani waliobeba lile sanduku la agano zilisimama. Mawe hayo yako huko mpaka hivi leo.
10Wale makuhani waliobeba sanduku la agano, walisimama katikati ya mto Yordani mpaka watu walipomaliza kutekeleza kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Yoshua awaambie watu; Yoshua alifanya yote ambayo Mose alikuwa amemwamuru. Watu wakaharakisha kuvuka mto, 11na watu wote walipokwisha vuka, wale makuhani wakawatangulia na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. 12Wanaume wa kabila la Reubeni na la Gadi na nusu ya kabila la Manase waliwatangulia Waisraeli wakiwa na silaha zao, kama vile walivyoagizwa na Mose. 13Watu wapatao 40,000 wakiwa na silaha tayari kwa vita walipita mbele ya Mwenyezi-Mungu wakielekea bonde la mji wa Yeriko. 14Katika siku hiyo Mwenyezi-Mungu akamtukuza Yoshua mbele ya Waisraeli wote, nao wakamheshimu Yoshua maisha yake yote kama walivyomheshimu Mose maishani mwake.
15Kisha Mwenyezi-Mungu alimwambia Yoshua, 16“Waamuru makuhani wanaobeba sanduku la maamuzi, watoke mtoni Yordani.” 17Basi, Yoshua akawaamuru wale makuhani, “Tokeni mtoni Yordani.” 18Hao makuhani waliokuwa wamebeba lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu walipotoka katikati ya mto Yordani, na kukanyaga ukingo wa mto, maji ya mto Yordani yakaanza kutiririka tena, na kufurika kama kwanza. 19Waisraeli walivuka mto Yordani katika siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi huko mjini Gilgali, mashariki ya Yeriko. 20Yoshua akayasimika yale mawe kumi na mawili ambayo waliyachukua kutoka mtoni Yordani, huko Gilgali. 21Kisha Yoshua akawaambia Waisraeli, “Watoto wenu watakapowaulizeni siku zijazo, ‘Je, mawe haya yana maana gani?’ 22Mtawaambia hivi: ‘Taifa la Israeli lilivuka mto huu wa Yordani mahali pakavu.’ 23Mtawaambia kuwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili yenu mpaka mkavuka, kama alivyokausha bahari ya Shamu, kwa ajili yetu tukavuka, 24ili watu wote wa dunia wajue kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu una nguvu; nanyi mpate kumcha Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, milele.”


Yoshua 4;1-24

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: