Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 16 October 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 5..



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah..!Mungu wetu yu mwema sana..
Tumshukuru Mungu kwa kila jambo.
Mtakatifu..!Mtakatifu..!,Mtakatifu..!Baba wa Mbinguni..
Mungu wetu,Muumba wetu, Muumba wa Mbingu na Nchi..
Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu wa Abarahamu,Isaka na Yakobo,Muweza wa yote..
Mume wa wajane,Baba wa Yatima,Baba wa upendo..
Baba wa Baraka,Baba wa Huruma,Kimbilio letu..
Msaada wetu,Mwanga wetu,Nuru ya maisha yetu..
Hakuna kama wewe,Hakuna wa kufanana nawe..
Unatosha ee Mungu wetu,Matendo yako ni ajabu..
Matendo yako ni makuu Mno..!
Utukuzwe Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni..
Unastahili sifa Mungu wetu,Unasahili kuabudiwa Jehovah..
Sifa na Utukufu ni wako Mungu wetu..!

Yesu alipomaliza kuwapa wanafunzi kumi na wawili maagizo, alitoka hapo, akaenda kufundisha na kuhubiri katika miji yao. Yohane Mbatizaji akiwa gerezani alipata habari juu ya matendo ya Kristo. Basi, Yohane akawatuma wanafunzi wake, wamwulize: “Je, wewe ni yule anayekuja, au tumngoje mwingine?” Yesu akawajibu, “Nendeni mkamwambie Yohane mambo mnayoyasikia na kuyaona: Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wanahubiriwa Habari Njema. Heri mtu yule ambaye hana mashaka nami.”
Asante kwa wema na fadhili zako Yahweh
Asante kwa ulinzi wako  wakati wote Mungu wetu
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii Mungu wetu..
Asante kwa pumzi/uzima na tukiwa tayari kwa majukumu yetu..
Ni kwa neema/rehema zako,ni kwa mapenzi yako Jehovah sisi kuwa hivi tulivyo,si kwa nguvu/utashi wetu,si kwamba sisi tumetenda mema sana zaidi ya wengine waliotangulia/kufa na wengine wakiwa taabani vitandani..
Tunakushukuru ee Mungu wetu..

Basi, hao wajumbe wa Yohane walipokuwa wanakwenda zao, Yesu alianza kuyaambia makundi ya watu habari za Yohane: “Mlikwenda kutazama nini kule jangwani? Je, mlitaka kuona mwanzi unaotikiswa na upepo? Basi, mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona mtu aliyevaa mavazi maridadi? Watu wanaovaa mavazi maridadi hukaa katika nyumba za wafalme. Lakini, mlikwenda kuona nini? Nabii? Naam, hakika ni zaidi ya nabii. “Huyu ndiye anayesemwa katika Maandiko Matakatifu: ‘Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu akutangulie, ambaye atakutayarishia njia yako’. Kweli nawaambieni, miongoni mwa watoto wote wa watu, hajatokea aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji. Hata hivyo, yule aliye mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni, ni mkubwa kuliko yeye. Tangu wakati wa Yohane Mbatizaji mpaka leo hii, ufalme wa mbinguni unashambuliwa vikali, na watu wakali wanajaribu kuunyakua kwa nguvu. Mafundisho yote ya manabii na sheria mpaka wakati wa Yohane yalibashiri juu ya nyakati hizi. Kama mwaweza kukubali basi, Yohane ndiye Elia ambaye angekuja.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha,tukijiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Tunaomba utusamehe makosa yetu yote tuliyoyafanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Baba wa Mbinguni tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nzareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Kisha Yesu akaanza kuilaumu miji ambayo, ingawaje alifanya miujiza mingi humo, watu wake hawakutaka kutubu: “Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwisha vaa mavazi ya gunia kitambo na kujipaka majivu kutubu. Hata hivyo, nawaambieni, siku ya hukumu, nyinyi mtapata adhabu kubwa kuliko ya Tiro na Sidoni. Na wewe Kafarnaumu, je, utajikweza mpaka mbinguni? Utaporomoshwa mpaka kuzimu! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika kule Sodoma, mji huo ungalikuwako mpaka hivi leo. Lakini nawaambieni, siku ya hukumu wewe utapata adhabu kubwa kuliko ya Sodoma.”

Mwenyezi-Mungu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Biashara,Masomo na vyote tunavyoenda kufanya/kutenda Baba
tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Yahweh ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Baba nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Jehovah ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale katika Nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Upendo wako ukawe nasi daima,Baraka zako zitufuate,
wema na fadhili zako ziwe nasi,furaha na shangwe ziwe nasi,Hekima,Busara ziwe nasi,huruma na kusaidia wengine,tukaonyane na kuelimisha kwa upendo, tukachukuliane na kusameheana..
Baba wa Mbinguni tukanene yaliyo yako,ukatupe macho ya kuona,masikio ya kusikia sauti yako..
Mungu wetu ukatupe neema ya kusimamia Neno lako Amri na Sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
wagonjwa, wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye shida/tabu,waliokatika vifungo vya yule mwovu na wote wataabikao na kuelemewa na mizigo
Mungu wetu tunaomba ukawabariki na kuwaponya kimwili na kiroho...
Baba ukaonekane na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako..
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea,
kufuata njia zako,nuru yako ikaangaze katika maisha yao..

Wakati huo Yesu alisema, “Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, maana umewaficha wenye hekima na wenye elimu mambo haya, ukawafunulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza. “Baba yangu amenikabidhi vitu vyote. Hakuna amjuaye Mwana ila Baba, wala amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anapenda kumfunulia. Njoni kwangu nyinyi nyote msumbukao na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jifungeni nira yangu, mkajifunze kwangu, maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, nanyi mtatulizwa rohoni mwenu. Maana, nira niwapayo mimi ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Baba wa mbinguni ukasikie kulia kwao na ukawafute machozi yao wote wanokuomba na kuamini
kwamba wewe ni Mungu wao na wewe ndiye mponyaji mkuu,Mungu wetu ukapokee sala/maombi yao,Baba ukawaweke huru na ukawafunike kwa
Damu ya mwanao mpendwa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo..
Wafiwa ukawe mfariji wao..
Jehovah tunayaweka haya yote mikononi mwako
 tukishukuru na tukiamini Mungu wetu u pamoja nasi jana,leo na hata Milele..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwaongoza katika yote
Msipungukiwe katika mahitaji yenu,Baba wa Mbinguni
akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda. 

1Wafalme wote wa Waamori walioishi ngambo ya magharibi ya Yordani, na wafalme wote wa Wakanaani waliokuwa pwani ya bahari ya Mediteranea, waliposikia kwamba Mwenyezi-Mungu aliyakausha maji ya mto Yordani kwa ajili ya Waisraeli mpaka walipokwisha vuka, wakafa moyo; wakaishiwa nguvu kabisa kwa kuwaogopa Waisraeli.

Kutahiriwa kwa Waisraeli huko Gilgali

2Wakati huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Tengeneza visu vya jiwe gumu ili uwatahiri Waisraeli.” 3Basi, Yoshua akatengeneza visu hivyo vya jiwe gumu na kuwatahiri Waisraeli huko Gibea-haaralothi.5:3 Gibea-haaralothi: Maana yake mlima wa magovi. 4Sababu ya kuwatahiri Waisraeli ni hii: Waisraeli wote, wanaume, waliotoka Misri ambao walikuwa na umri wa kwenda vitani, wote walifariki safarini jangwani baada ya kutoka nchini Misri. 5Hao wote waliotoka Misri walikuwa wametahiriwa, lakini wale wote waliozaliwa safarini huko jangwani baada ya kutoka Misri, walikuwa bado hawajatahiriwa. 6Taz Hes 14:28-35 Waisraeli walisafiri kwa muda wa miaka arubaini nyikani hata wanaume wote waliokuwa na umri wa kwenda vitani wakaangamia kwa kuwa hawakusikiliza aliyosema Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu alikuwa amewaapia watu hao kwamba hawataiona nchi ile inayotiririka maziwa na asali ambayo yeye aliwaapia baba zao kuwa atawapa. 7Kwa hiyo ilikuwa ni watoto wa watu hao ambao Mwenyezi-Mungu aliwakuza badala yao, hao ndio Yoshua aliwatahiri, kwani hawakuwa wametahiriwa wakati ule walipokuwa safarini jangwani.
8Wanaume wote walipokwisha tahiriwa walikaa katika sehemu zao humo kambini mpaka walipopona. 9Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Leo hii nimewaondoleeni ile aibu ya Misri.” Hivyo mahali hapo pakaitwa Gilgali5:9 Gilgali: Linasikika kama neno lenye maana “kuondolewa”. mpaka hivi leo.
10Waisraeli walipokuwa wamepiga kambi huko Gilgali waliadhimisha sikukuu ya Pasaka jioni ya siku ya kumi na nne ya mwezi katika tambarare za Yeriko. 11Kesho yake, yaani baada ya Pasaka, walikula mikate isiyotiwa chachu na bisi kutokana na mazao ya nchi ile. 12Taz Kut 16:35 Basi, tangu siku hiyo walipokula mazao ya nchi hiyo Waisraeli hawakupata mana tena. Tangu mwaka huo Waisraeli walikula mazao ya nchi ya Kanaani.

Yoshua na kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu

13Siku moja Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, ghafla aliona mtu mmoja amesimama mbele yake na upanga uliofutwa mkononi mwake. Yoshua akamwendea, akamwuliza, “Je, wewe ni wetu au ni wa adui zetu?” 14Naye akamjibu; “Wala wenu wala wa adui zenu! Ila mimi ni kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu, na sasa nimewasili.” Yoshua akainama chini akasujudu, kisha akamwuliza, “Bwana wangu, mimi mtumishi wako, unataka nifanye nini?” 15Huyo kamanda wa jeshi la Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Vua viatu vyako kwa maana mahali unaposimama ni patakatifu.” Yoshua akafanya hivyo.



Yoshua 5;1-15

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: