Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 21 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Waamuzi 7...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi,
Muumba wa vyote vilivyomo,vinavyoonekana na visivyoonekana..
Mungu wa wote walio hai,Mungu wa wajane,Baba wa yatima,Mungu
mwenye huruma,Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye nguvu..
Mungu wa Abarhamu,Isaka na Yakobo,Baba wa Rehema,Baba wa Upendo,Baba wa Baraka,Muweza wa yote,hakuna lililogumu mbele za
Mungu,Hakuna lisilowezekana mbele zake,Unatosha ee Mungu wetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia Baba wa Mbinguni..!!

Asante kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona
leo hii,si kwa nguvu zetu,wala si kwa akili zetu,si kwamba tumetenda
mema sana, si kwamba sisi ni wazuri mno ni kwa neema/rehema zako
Mungu wetu,ni kwa mapenzi yako Baba wa Mbinguni sisi kuwa hivi
tulivyo leo hii..

Sasa, kwa vile tumefanywa kuwa waadilifu kwa imani, basi tunayo amani naye Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la kushiriki utukufu wa Mungu. Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu tukijua kwamba taabu huleta saburi, nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini. Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha mimina mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
Mungu wetu tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya 
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua Jehovah
nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote
waliotukosea,Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu
Jehovah tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Nguvu za giza,nguvu za mapepo,nguvu za mizimu,nguvu za mpinga Kristo
zishindwe katika jina lililo kuu jina la Bwana wetu Yesu Kristo..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni
tunaomba utufunike kwa damu ya Bwana wetu na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti,kwakuwa yeye aliteseka ili sisi tupate kupona..

Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia, alikufa kwa ajili yetu sisi waovu. Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema. Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu. Kwa kuwa sasa tumefanywa kuwa waadilifu kwa damu ya Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu. Maana, tulipokuwa bado maadui zake, Mungu alitupatanisha naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri zaidi kwamba tutaokolewa kwa uhai wa Kristo. Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu.
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu ukatupe ubunifu,maarifa katika ufanyaji/utendaji
Yahweh tukatende sawasawa na mapezni yako,Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo Baba wa Mbinguni nasi
tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe
kama inavyokupendeza wewe..

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
Familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Baba wa Mbinguni tunaomba
ulinzi wako kwetu na kwavyote tunavyovimiliki,Yahweh ukatupe
neema ya kufuata njia zako,kusimamia Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu,tukanene yaliyo yako,ukatuokoe na kiburi,
majivuno,kujisifu,makwazo na yote yanayokwenda kinyume nawe..
tunakawe wenye Upendo,amani,unyenyekevu,utuwema,fadhili,
kusamehe,kuchukuliana,kuonyana/kuelimishana kwa upendo na amani..
Ukatufanye chombo chema Baba wa Mbinguni nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..

Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa maana wote wametenda dhambi. Kabla ya sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni; lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria. Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi Mungu. Adamu alikuwa kielelezo cha Kristo ambaye alikuja baadaye. Lakini kosa la Adamu haliwezi kulinganishwa na neema ya Mungu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na zawadi zake. Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu na dhambi ya mtu yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe. Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja, kifo kilianza kutawala kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na zawadi hiyo ya kufanywa kuwa waadilifu, watatawala katika uhai kwa njia ya huyo mmoja, yaani Yesu Kristo.

Tazama wenye shida/tabu Baba wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali
Yahweh wagonjwa,wenye njaa,walio katika vifungo mbalimbali vya yule mwovu,waliokata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka,walioanguka/potea,wasiyo ijua kweli na wa taabikao na kuelemewa na mizigo,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako
wenye nguvu,Yahweh wakapate uponyaji wa mwili na roho pia..
Jehovah ukawainue,ukawavushe na ukawasimamishe tena,Yahweh ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe,Mungu wetu ukawape
neema ya kujiombea na kufuata njia zako,amani ikawe nao,Nuru ikaangaze katika maisha yao,Baba wa Mbinguni ukasikie kulia kwao
Jehovah ukawafute machozi ya watoto wako wakuombao kwa bidii,Imani
Ee Baba ukapokee sala/maombi yetu na ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..


Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa binadamu wote, kadhalika kitendo kiadilifu cha mtu mmoja kinawapa wote uadilifu na uhai. Na kama kwa kutokutii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi kuwa waadilifu. Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu; lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi. Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema inatawala kwa uadilifu na kuleta uhai wa milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwa kuwa nami
Mungu akawabariki katika yote,akawalinde na kuwaongoza
msipungukiwe katika mahitaji yenu,Baba wa Mbinguni akawape
sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Gideoni awashinda Wamidiani

1Yerubaali, yaani Gideoni na watu wote waliokuwa pamoja naye waliamka mapema, wakapiga kambi yao bondeni karibu na chemchemi ya Harodi; kambi ya Wamidiani ilikuwa kaskazini mwao bondeni karibu na mlima More.
2Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu ulio nao ni wengi mno kwangu mimi kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Waisraeli wasije wakajisifu mbele yangu na kusema kwamba wamejiokoa kwa nguvu zao wenyewe. 3Sasa watangazie watu wote kwamba mtu yeyote aliye mwoga au anayetetemeka arudi nyumbani kwake.” Basi, Gideoni aliwajaribu, na watu 22,000 wakarudi nyumbani akabaki na watu 10,000.
4Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Watu hao bado ni wengi mno. Sasa wapeleke mtoni, nami nitawajaribu huko. Mtu yeyote nitakayekuambia, ‘Huyu atakwenda nawe, huyo aende nawe. Lakini mtu yeyote nitakayekuambia hatakwenda nawe, huyo asiende nawe.’”
5Basi, Gideoni akawapeleka watu mtoni na Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Watu watakaoramba maji kama mbwa, utawatenganisha na wale watakaopiga magoti kunywa maji.”
6Idadi ya waliokunywa maji kwa kuchota kwa mikono yao na kuramba kama mbwa ilikuwa 300. Lakini wengine wote waliobaki walipiga magoti kunywa maji.
7Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 waliokunywa kwa kuramba kama mbwa, nitawaokoa Waisraeli na kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Lakini wale wengine wote warudi makwao.”
8Basi, Gideoni akachukua vyakula vya wale waliokuwa wanaondoka na tarumbeta, akawaaga waende makwao. Yeye akabaki na wale watu 300. Kambi ya Wamidiani ilikuwa bondeni upande wao wa chini.
9Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Nenda ukawashambulie kambini mwao, maana nimewatia mikononi mwako. 10Lakini kama unaogopa, nenda pamoja na mtumishi wako Pura. 11Huko utasikia wanayosema, nawe utapata nguvu za kuweza kwenda kuwashambulia.” Basi, Gideoni akaenda pamoja na mtumishi wake Pura mpaka kwenye vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani.
12Wamidiani, Waamaleki na watu wote wa Mashariki walilala bondeni, wengi kama nzige, na ngamia wao wasiohesabika, wengi kama mchanga wa pwani.
13Gideoni alipofika, akamsikia mtu mmoja akimsimulia mwenzake ndoto yake hivi: “Niliota ndoto. Niliona mkate wa shayiri ukivingirika hadi kambini mwa Wamidiani, ukalipiga hema na kulipindua chini juu. Hema likalala chini.”
14Mwenzake akamjibu, “Hiyo inamaanisha tu upanga wa yule Mwisraeli Gideoni mwana wa Yoashi ambaye mikononi mwake Mungu amewatia Wamidiani pamoja na jeshi lote.”
15Gideoni aliposikia masimulizi hayo ya ndoto na tafsiri yake, alimwabudu Mungu. Kisha alirudi kwenye kambi ya Waisraeli, akasema, “Amkeni twende; maana Mwenyezi-Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”
16Basi akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawapa tarumbeta na magudulia yenye mienge. 17Akawaambia, “Mniangalie na kufanya sawa kama nitakavyofanya wakati nitakapofika kambini. 18Nitakapopiga tarumbeta, mimi pamoja na kundi langu, nyote pigeni tarumbeta kutoka kila upande na kusema kwa sauti kubwa, ‘Kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!’”
19Ilipokaribia usiku wa manane, Gideoni na kundi lake la watu mia moja mara tu baada ya kufika mwisho wa kambi, mwanzoni mwa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu walikaribia kambi ya adui. Wakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia waliyokuwa nayo.
20Makundi yote matatu kwa pamoja yakapiga tarumbeta na kuvunja magudulia yao. Katika mikono yao ya kushoto walishika mienge na kwa mikono yao ya kulia tarumbeta na kuzipiga, huku wakisema kwa sauti kubwa, “Upanga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu na kwa ajili ya Gideoni!”
21Wakasimama kila mmoja mahali pake kuizunguka kambi. Jeshi lote la adui likatawanyika huku likipiga mayowe.
22Watu wa Gideoni walipopiga tarumbeta zao 300, Mwenyezi-Mungu aliwafanya Wamidiani waanze kuuana wao kwa wao kambini. Waliosalia wakatoroka hadi Serera panapoelekea Beth-shita, hadi mpakani mwa Abel-mehola karibu na Tabathi.
23Waisraeli wa kabila la Naftali, Asheri, na Manase, wote waliitwa, wakawafuatia Wamidiani. 24Gideoni akatuma wajumbe kote katika nchi ya milima ya Efraimu watangaze: “Teremkeni kuwakabili Wamidiani na kuwazuia kwa kuteka vijito na mto Yordani mpaka Beth-bara.” Basi, wanaume wote wa Efraimu wakaja na kuuteka mto Yordani mpaka Beth-bara. 25Wakachukua mateka viongozi wawili wa Midiani, yaani Orebu na Zeebu. Wakamuua Orebu katika mwamba wa Orebu, naye Zeebu wakamuua katika shinikizo la Zeebu, wakiwa wanawafuatia Wamidiani. Wakamletea Gideoni vichwa vya Orebu na Zeebu, ngambo ya mto Yordani.


Waamuzi 7;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: