Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 6 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 20...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah tumshukuru Mungu wetu katika yote..!
Ni wiki/siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na
kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwa nguvu/utashi wetu,wala si kwamba tumetenda mema sana
zaidi ya wengine waliotangulia/kufa, na wengine wana hali mbaya
wagonjwa,wamekata kauli na hata hawawezi kutubu...
Tumempa nini  Mungu?Hapana ni kwa neema/rehema zake
Ni kwa  mapenzi yake Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo..
Tumshukuru Mungu wetu kwa pumzi/uzima,afya na kusimama
tukiwa tayari kwa kufuata majukumu yetu..
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Utukuzwe Mungu wetu,Usifiwe ee Mungu wetu,uhimidiwe Baba wa Mbinguni,Uabudiwe Mungu wetu,Neema yako yatutosha Mungu wetu,
Kwa Neema ya Mungu tumekombolewa kwa njia ya imani...
Mungu wetu amejaa Neema na huruma,hakasiriki upesi..


Yote haya ni kwa faida yenu, hata neema ya Mungu inapowafikia watu wengi zaidi na zaidi, shukrani nazo ziongezeke zaidi, kwa utukufu wa Mungu. Kwa sababu hiyo hatufi moyo; na hata kama maumbile yetu ya nje yataoza, lakini kwa ndani tunafanywa wapya siku kwa siku. Taabu tunayopata ni kidogo, tena ya muda tu; lakini itatupatia utukufu upitao matazamio yote, utukufu ambao hauna mwisho. Hivyo tunatazamia kwa makini si vitu vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Maana vinavyoonekana ni vya muda tu; lakini vile visivyoonekana ni vya milele.
Tunakuja mbele zako ee Mungu wetu,tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Jehovah..
Tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya kwakuwaza,
kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh tunaomba nasi utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea,Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu
Baba wa Mbinguni utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..



Nyinyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu. Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu. Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu. Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika,

Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh tunaomba
utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..



hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu nyinyi mmeokolewa. Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni. Ndivyo alivyopenda kuonesha kwa watu wa nyakati za baadaye ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu. Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu. Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu. Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu,maarifa katika kufanya/kutenda
tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji,Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe sawasawa na mapenzi yako...


Mfalme wa Amani tunaomba amaini yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote
wanaotuzunguka,Mungu wetu amani ikawe nasi daima..
Upendo ukadumu kati yetu,huruma na kusaidia,tukachukuliane,
tukaelimishane/kuonyana kwa upendo,Baba tunaomba ulinzi wako,
furaha ikatawale,Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Baba ukatupe
neema ya kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za
maisha yetu,tukanene yaliyo yako,ukatupe macho ya rohoni,Yahweh
ukatupe masikio na tukasikie sauti yako,Mungu wetu ukaonekane
katika maisha yetu na ukatutendee sawasawa na mapenzi yako..
Ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Nyinyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine – mnaoitwa, “Wasiotahiriwa” na Wayahudi ambao hujiita, “Waliotahiriwa,” (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao) – kumbukeni mlivyokuwa zamani. Wakati ule nyinyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu katika yale maagano aliyoahidi Mungu. Mlikuwa bila matumaini na kama watu wasiomjua Mungu hapa duniani. Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, nyinyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo. Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui. Aliiondoa ile sheria pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani. Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu. Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu nyinyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu. Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba kwa Roho mmoja. Basi, nyinyi si wageni tena, wala si watu wa nje. Nyinyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu. Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi. Yeye ndiye mwenye kuliunganisha jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya Bwana. Katika kuungana naye, nyinyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.

Tazama wenye shida/tabu Mungu wetu,waliokata tamaa,waliokatika vifungo vya yule mwovu,waliokataliwa,wagonjwa,wenye njaa,
wote wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali...
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,yahweh
tunaomba ukabariki mashamba yao,biashara na ukawape ubunifu na maarifa,Mungu wetu ukawaponye kimwili na kiroho,Yahweh ukawafungue
na kuwakweka huru,Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao,Jehovah ukawainue na
kuwasimamisha wote walio anguka,Mungu wetu ukawape neema ya kurudi wale wote waliopotea..Yahweh ukapokee sala/maombi ya watoto wako
wanaokuomba na kukutafuta kwa bidii,imani na kuamini....
Sifa na utukufu tunakurudishia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!

Wapendwa katika Bwana asanteni sana kwa kuwa nami..
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yake
Neema ya Kristo iwe nanyi daima..
Nawapenda...

Miji ya kukimbilia usalama

(Hes 35:9-34; Kumb 19:1-13)
1 Taz Hes 35:6-32; Kumb 4:41-43; 19:1-13 Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, 2awaambie Waisraeli hivi: “Jichagulieni miji ambamo mtu aweza kukimbilia usalama ambayo nilimwambia Mose akueleze. 3Mtu yeyote akimuua mtu bila kukusudia anaweza kukimbilia katika mji mmojawapo na hivyo kumkwepa yule mtu aliye na jukumu la kulipiza kisasi cha damu. 4Mwuaji atakimbilia katika mji mmojawapo na kusimama mlangoni mwa mji na kuwaeleza wazee wa mji huo kesi yake. Wazee watampokea ndani na kumpa mahali pa kuishi pamoja nao. 5Yule mwenye kulipiza kisasi akimwandama mpaka mjini, wazee wa mji huo hawaruhusiwi kumtoa mwuaji huyo kwa yule mwenye kulipiza kisasi, maana alimuua mwenzake kwa bahati mbaya, kwa vile hapakuwa na uadui kati yao hapo awali. 6Mwuaji ataendelea kuishi humo mpaka hapo atakapohukumiwa mbele ya jumuiya nzima ya Israeli na pia mpaka hapo yule kuhani mkuu ambaye alikuwa na madaraka wakati huo amefariki. Baada ya hapo mtu huyo ataweza kurudi nyumbani kwake katika mji ule alikotoroka.”
7Basi, kwa ajili hiyo wakaitenga miji ya Kedeshi katika Galilaya kwenye milima ya Naftali, Shekemu katika milima ya Efraimu na Kiriath-arba (yaani Hebroni) katika nchi ya milima ya Yuda. 8Katika ngambo ya mto Yordani, mashariki ya mji wa Yeriko, walichagua mji wa Bezeri ulio kwenye nyika tambarare na ambao mji wenyewe ni wa eneo la kabila la Reubeni. Pia walichagua Ramothi huko Gileadi ambao ni mji wa kabila la Gadi na Golani huko Bashani katika eneo la kabila la Manase. 9Hii ndiyo miji iliyotengwa kwa ajili ya watu wote wa Israeli na wageni walioishi miongoni mwao, ili mtu yeyote atakayemuua mwenzake bila kukusudia akimbilie huko asije akauawa na mwenye jukumu la kulipiza kisasi cha damu, hadi hapo atakapohukumiwa mbele ya jumuiya nzima.


Yoshua 20;1-9

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: