Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 7 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 21...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi..
Muweza wa yote,Mponyaji wetu,Kimbilio letu,Msaada wetu watoka
kwa Mwenyezi-Mungu,Tunajua Mungu ni msaada wetu,Mwenyezi-Mungu
hutegemeza maisha yetu,Msaada wetu watoka kwa Mwenyezi-Mungu aliyeumba Mbingu na  dunia ..



Mwenyezi-Mungu ni mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Hunipumzisha kwenye malisho mabichi; huniongoza kando ya maji matulivu, na kuirudishia nafsi yangu nguvu mpya. Huniongoza katika njia sawa kwa hisani yake. Nijapopita katika bonde la giza kuu la kifo, sitaogopa hatari yoyote, maana wewe ee Mwenyezi-Mungu u pamoja nami; gongo lako na fimbo yako vyanilinda. Umeniandalia karamu mbele ya maadui zangu; umenipaka mafuta kichwani pangu; kikombe changu umekijaza mpaka kufurika. Kweli wema wako na fadhili zako zitakuwa pamoja nami, siku zote za maisha yangu; nami nitakaa nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu milele.

Utukukuzwe ewe Mungu wetu,Uhimidiwe milele na milele,Uabudiwe Jehovah,usifiwe Baba wa Mbinguni,Unatosha Mungu wetu...
Asante kwa wema na fadhili zako kwetu Mungu wetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote...
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu..!!

Baba wa Mbinguni tazama jana imepita leo ni siku mpya kesho ni siku
nyingine Jehovah..!
Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia
mikononi mwako Mungu wetu..
Baba wa Mbinguni tunaomba utusamehe makosa yetu yote
tuliyoyafanya kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Yahweh tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote..




Wapenzi wangu, msimsadiki kila mtu asemaye kwamba ana Roho wa Mungu, bali chunguzeni kwa makini kama huyo mtu anaongozwa na Roho wa Mungu au la, maana manabii wengi wa uongo wamezuka ulimwenguni. Hii ndiyo njia ya kujua kama mtu anaongozwa na Roho wa Mungu: Kila anayekiri kwamba Kristo alikuja, akawa binadamu, mtu huyo anaye Roho wa Mungu. Lakini mtu yeyote asiyemkiri Kristo hivyo, hana huyo Roho atokaye kwa Mungu. Mtu huyo ana roho ambaye ni wa mpinzani wa Kristo; nanyi mlikwisha sikia kwamba anakuja, na sasa tayari amekwisha wasili ulimwenguni! Lakini nyinyi, watoto, ni wake Mungu na mmekwisha washinda hao manabii wa uongo; maana Roho aliye ndani yenu ana nguvu kuliko roho aliye ndani ya hao walio wa ulimwengu. Wao husema mambo ya ulimwengu, nao ulimwengu huwasikiliza kwani wao ni wa ulimwengu. Lakini sisi ni wake Mungu. Mtu anayemjua Mungu hutusikiliza, mtu asiye wa Mungu hatusikilizi. Basi, kwa njia hiyo tunaweza kutambua tofauti kati ya Roho wa ukweli na roho wa uongo.

Mungu wetu tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Jehovah
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo wa Nazareti
yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..




Wapenzi wangu, tupendane, maana upendo hutoka kwa Mungu. Kila mtu aliye na upendo ni mtoto wa Mungu, na anamjua Mungu. Mtu asiye na upendo hamjui Mungu, maana Mungu ni upendo. Na Mungu alionesha upendo wake kwetu kwa kumtuma Mwanae wa pekee ulimwenguni, ili tuwe na uhai kwa njia yake. Hivi ndivyo upendo ulivyo: Si kwamba sisi tulikuwa tumempenda Mungu kwanza, bali kwamba yeye alitupenda hata akamtuma Mwanae awe sadaka ya kutuondolea dhambi zetu.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu,
Baba tunaomba ukatupe ubunifu/maarifa na tukafanye/tukatende kama inavyokupendeza wewe..
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo...
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Mungu wetu tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe
sawasawa na mapenzi yako..

Mfalme wa Amani tunaomba amani yako ikatawale katika
nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako,Baba tunaomba baraka zako,Yahweh
upendo wetu ukadumu,Mungu wetu tunaomba utupe neema ya kusimamia
Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu..
Jehovah ukatamalaki na kutuatamia,Baba wa Mbinguni ukaonekane
katika maisha yetu,ukatupe macho ya rohoni,masikio ya kusikia sauti yako..Mungu wetu ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Hakuna mtu aliyekwisha mwona Mungu kamwe; lakini kama tukipendana, Mungu anaishi katika muungano nasi, na upendo wake unakamilika ndani yetu. Tunajua kwamba tunaishi katika umoja na Mungu, naye Mungu anaishi katika umoja nasi, kwani yeye ametupa Roho wake. Sisi tumeona na kuwaambia wengine kwamba Baba alimtuma Mwanae awe Mwokozi wa ulimwengu. Kila mtu anayekiri kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu anaishi katika muungano na mtu huyo, naye anaishi katika muungano na Mungu. Basi, sisi tunajua na tunaamini upendo alio nao Mungu kwetu sisi. Mungu ni upendo, na kila mtu aishiye katika upendo, anaishi katika muungano na Mungu, na Mungu anaishi katika muungano naye. Upendo umekamilika ndani yetu kusudi tuweze kuwa na ujasiri siku ile ya hukumu; kwani maisha yetu hapa duniani ni kama yale ya Kristo. Palipo na upendo hapana woga; naam, upendo kamili hufukuza woga wote. Basi, mtu mwenye woga hajakamilika bado katika upendo, kwani woga huhusikana na adhabu. Sisi tuna upendo kwa sababu Mungu alitupenda kwanza. Mtu akisema kwamba anampenda Mungu, hali anamchukia ndugu yake, huyo ni mwongo. Maana mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hamwoni. Basi, hii ndiyo amri aliyotupa Kristo: Anayempenda Mungu anapaswa pia kumpenda ndugu yake.

Mungu wetu ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wote wanopitia magumu/majaribu mbalimbali,wagonjwa,wenye njaa,waliokatika vifungo vya yule mwovu,Mungu wetu ukawaponye kimwili na kiroho,ukawatendee
na kuwaokoa,ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako ili
wakapate kuwa huru..eee Mungu wetu tunaomba upokee sala/maombi yetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa katika Bwana kwa kuwa nami..
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi daima..
Nwapenda.

Miji ya Walawi

1Walipokuwa huko Shilo katika nchi ya Kanaani viongozi wa koo za Walawi wakawaendea kuhani Eleazari na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila yote ya Waisraeli, 2Taz Hes 35:1-8 wakawaambia, “Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose tupewe miji ya kuishi na mbuga za malisho ya wanyama wetu.” 3Basi, kulingana na amri ya Mwenyezi-Mungu, Waisraeli walichagua kutoka katika maeneo ya nchi zao, miji na vijiji vya malisho, wakawapa Walawi iwe sehemu yao.
4Kura ya kwanza ilizipata jamaa za ukoo wa Kohathi. Miongoni mwao wazawa wa kuhani Aroni walipewa kwa kura, miji iliyokuwa katika maeneo ya makabila ya Yuda, Simeoni, na Benyamini. Jumla ya miji waliyopewa ni kumi na mitatu.
5Watu wa ukoo wa Kohathi waliosalia walipewa miji kumi iliyoko katika maeneo ya makabila ya Efraimu, Dani na katika eneo la nusu ya kabila la Manase.
6Watu wa ukoo wa Gershoni walipewa kwa kura miji kumi na mitatu katika maeneo ya makabila ya Isakari, Asheri, Naftali na katika eneo la nusu ya kabila la Manase huko Bashani.
7Jamaa za ukoo wa Merari walipewa miji kumi na miwili katika maeneo ya makabila ya Reubeni, Gadi na Zebuluni.
8Waisraeli waliwapa Walawi miji hiyo pamoja na vijiji vya malisho yao, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwagiza Mose.
9Yafuatayo ni majina ya miji kutoka kwenye maeneo ya kabila la Yuda na Simeoni ambayo ilitolewa kwa 10wazawa wa kuhani Aroni, waliokuwa jamaa za ukoo wa Kohathi ambaye alikuwa wa kabila la Lawi. Sehemu yao walipata kwanza kwani kura yao ilitokea kwanza. 11Walipewa Kiriath-arba yaani Hebroni (Arba alikuwa baba yake Anaki) katika milima ya Yuda, pamoja na mbuga zilizoizunguka. 12Lakini mashamba ya mji huo pamoja na vijiji vilivyouzunguka alikuwa amekwisha pewa Kalebu mwana wa Yefune viwe mali yake.
13Licha ya kuwapa wazawa wa kuhani Aroni mji wa Hebroni ambao pia ulikuwa umetengwa kuwa mji wa kukimbilia usalama, waliwapa miji ya Libna pamoja na mbuga zake za malisho, 14Yatiri pamoja na mbuga zake za malisho, Eshtemoa pamoja na mbuga zake za malisho, 15Holoni pamoja na mbuga zake za malisho, Debiri pamoja na mbuga zake za malisho, 16Aini pamoja na mbuga zake za malisho, Yuta pamoja na mbuga zake za malisho na Beth-shemeshi pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji hiyo iliyo katika maeneo ya makabila hayo mawili ni tisa. 17Katika eneo la kabila la Benyamini walipewa miji mingine: Gibeoni pamoja na mbuga zake za malisho, 18Anathothi pamoja na mbuga zake za malisho, Almoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. 19Miji yote ya wazawa wa Aroni ambao walikuwa makuhani, ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho.
20Watu waliosalia wa ukoo wa Kohathi, ambao pia ni jamaa za kabila la Lawi walipewa miji katika eneo la kabila la Efraimu. 21Walipewa Shekemu, mji ambao ulikuwa pia mji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho katika nchi ya milima ya Efraimu, na Gezeri pamoja na mbuga zake za malisho, 22Kibzaimu pamoja na mbuga zake za malisho na Beth-horoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. 23Katika eneo la kabila la Dani walipewa Elteke pamoja na mbuga zake za malisho, Gibethoni pamoja na mbuga zake za malisho, 24Aiyaloni pamoja na mbuga zake za malisho na Gath-rimoni pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. 25Katika eneo la nusu ya kabila la Manase walipewa Taanaki pamoja na mbuga zake za malisho na Gath-rimoni pamoja na malisho yake. Jumla ya miji waliyopewa ni miwili. 26Basi, miji ambayo walipewa jamaa za Kohathi zilizosalia ilikuwa kumi pamoja na mbuga zao za malisho.
27Jamaa za Walawi za ukoo wa Gershoni, walipewa miji miwili katika nusu ya eneo la kabila la Manase: Golani, huko Bashani, mji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho, na Beesh-tera pamoja na malisho yake. 28Katika eneo la kabila la Isakari, walipewa Kishioni pamoja na mbuga zake za malisho, Daberathi pamoja na mbuga zake za malisho, 29Yarmuthi pamoja na mbuga zake za malisho na En-ganimu pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. 30Katika eneo la kabila la Asheri walipewa Mishali pamoja na mbuga zake za malisho, Abdoni pamoja na mbuga zake za malisho, 31Helkathi pamoja na mbuga zake za malisho na Rehobu pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla ya miji waliyopewa ni minne. 32Katika eneo la kabila la Naftali walipewa Kedeshi, mji wa kukimbilia usalama ulioko huko Galilaya pamoja na mbuga zake za malisho, Hamoth-dori pamoja na mbuga zake za malisho na Kartani pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji mitatu. 33Jumla ya miji ya jamaa mbalimbali za ukoo wa Gershoni ilikuwa kumi na mitatu pamoja na mbuga zao za malisho.
34Walawi wengine waliobaki, yaani wazawa wa Merari, walipewa miji katika eneo la kabila la Zebuluni. Nayo ni Yokneamu pamoja na mbuga zake za malisho, Karta pamoja na mbuga zake za malisho, 35Dimna pamoja na mbuga zake za malisho na Nahalali pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji minne. 36Katika eneo la kabila la Reubeni walipewa Bezeri pamoja na mbuga zake za malisho, Yahazi pamoja na mbuga zake za malisho, 37Kedemothi pamoja na mbuga zake za malisho na Mefaathi pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji minne. 38Katika eneo la kabila la Gadi walipewa Ramothi wa Gileadi, mji wa kukimbilia usalama, pamoja na mbuga zake za malisho, Mahanaimu pamoja na mbuga zake za malisho, 39Heshboni pamoja na mbuga zake za malisho na Yazeri pamoja na mbuga zake za malisho. Jumla miji minne. 40Miji yote waliyopewa wazawa wa Merari, yaani jamaa za Walawi zilizobaki, ilikuwa kumi na miwili.
41Jumla ya miji yote ambayo Walawi walipewa katika maeneo ya Waisraeli ilikuwa arubaini na minane pamoja na mbuga zao za malisho. 42Kila mmoja kati ya miji hii ulizungukwa na mbuga za malisho.
43Basi, Mwenyezi-Mungu aliwapa Waisraeli nchi yote ambayo alikuwa amewaahidi wazee wao. Nao wakaimiliki na kuishi humo. 44Mwenyezi-Mungu akawapa amani kila mahali nchini kama alivyowaapia wazee wao. Hakuna adui yeyote aliyethubutu kuwakabili kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa amewatia adui hao mikononi mwao. 45Hakuna hata ahadi yoyote njema ambayo Mwenyezi-Mungu aliiahidi Israeli ambayo haikutimia. Ahadi zote zilitimia.


Yoshua 21;1-45

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: