Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 8 November 2017

Kikombe Cha Asubuhi ;Yoshua 22...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?
Tumshukuru Mungu wetu katika yote..
Mtakatifu..!Mtakatifu..!Mtakatifu..! Baba wa mbinguni..
Mungu wetu,Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo..
Muweza wa yote,Jehovah..!Yahweh..!Elohim..!El Olam..!
El Qanna.!El Elyon..!El Shaddai..!Adonai..!Emanuel-Mungu pamoja nasi..!
Utukuzwe ee Mungu wetu,Uhimidiwe Baba wa Mbinguni,Usifiwe Jehovah,
Uabudiwe Yahweh,Unatosha Mungu wetu,Matendo yako ni makuu mno..!

Msifuni Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mungu katika patakatifu pake; msifuni katika mbingu zake kuu. Msifuni kwa sababu ya matendo yake makuu; msifuni kwa ajili ya utukufu wake mkuu. Msifuni kwa mlio wa tarumbeta; msifuni kwa zeze na kinubi! Msifuni kwa ngoma na kucheza; msifuni kwa filimbi na banjo! Msifuni kwa kupiga matoazi. Msifuni kwa matoazi ya sauti kubwa. Kila kiumbe hai kimsifu Mwenyezi-Mungu! Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii..
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..


Msifuni Mwenyezi-Mungu! Mwimbieni Mwenyezi-Mungu wimbo mpya; msifuni katika kusanyiko la waaminifu! Furahi ee Israeli kwa sababu ya Muumba wako, wakazi wa Siyoni shangilieni kwa sababu ya Mfalme wenu. Lisifuni jina lake kwa ngoma, mwimbieni kwa ngoma na zeze. Maana Mwenyezi-Mungu hupendezwa na watu wake; yeye huwapamba wanyonge kwa ushindi. Watu waaminifu wafurahi kwa fahari; washangilie hata walalapo.
Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha
na kujiachilia mikononi mwako Mungu wetu..
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Jehovah nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale
wote waliotukosea..
Mungu wetu tunaomba utuepushe katika majaribu Baba utuokoe na 
yule mwovu na kazi zake zote..
Yahweh tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Jehovah utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti,yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Sikia maombi yangu mimi mtumishi wako na ya watu wako Israeli wanapoomba wakielekea mahali hapa. Usikie maombi kutoka huko mbinguni; na ukisha sikia, utusamehe. “Mtu akimkosea mwenzake, naye akaletwa apate kuapa mbele ya madhabahu yako katika nyumba hii, naye akiapa, tafadhali wewe usikie kutoka huko mbinguni, uchukue hatua na kuwahukumu watumishi wako. Aliye na hatia umwadhibu kadiri ya makosa yake, asiye na hatia umwachilie na kumpatia tuzo kadiri ya uadilifu wake. “Ikiwa watu wako Waisraeli, wameshindwa na adui zao kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kulikiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii, basi, uwasikie kutoka huko mbinguni, uwasamehe watu wako Israeli dhambi zao, halafu uwarudishe katika nchi uliyowapa babu zao. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao unapowaonya, tafadhali, uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi za watumishi wako, watu wako Israeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu; ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yako.

Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu..
Mungu wetu ukatupe ubunifu/maarifa katika kufanya/kutenda
Jehovah tukatende kama inavyo kupendeza wewe..
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah
ukatupe sawasawa na mapenzi yako..

Heri mtu anayewajali maskini; Mwenyezi-Mungu atamwokoa wakati wa shida. Mwenyezi-Mungu atamlinda na kumweka hai, naye atafanikiwa katika nchi; Mungu hatamwacha makuchani mwa maadui zake. Mwenyezi-Mungu atamsaidia awapo mgonjwa, atamponya maradhi yake yote.

Mfalme wa Amani tuyaweka maisha yetu mikononi mwako..
Baba tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,
familia/ndugu na wote wanaotuzunguka,Mungu wetu tunaomba amani
yako ikatawale,Upendo wetu ukadumu,ukatupe neema ya kusimamia
Neno lako Amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Mungu wetu ukaonekane katika maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatupe neema ya hekima,busara na tukatende na  tukanene
yaliyo yako,Mungu wetu ukatufanye barua njema nasi tukasome
kama inavyo kupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuomngoze katika yote na tukawe na kiasi..


Mwanangu, ukiyakubali maneno yangu, na kuyathamini maagizo yangu; ukitega sikio lako kusikiliza hekima, na kuuelekeza moyo wako upate ufahamu; naam, ukiomba upewe busara, ukisihi upewe ufahamu; ukiitafuta hekima kama fedha, na kuitaka kama hazina iliyofichika; hapo utaelewa ni nini kumcha Mwenyezi-Mungu, utafahamu maana ya kumjua Mungu. Maana Mwenyezi-Mungu huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. Huwawekea wanyofu akiba ya hekima safi, yeye ni ngao kwa watu waishio kwa uaminifu. Huilinda mienendo ya watu watendao haki, na kuzihifadhi njia za waaminifu wake. Ukinisikiliza utafahamu uadilifu na haki, utajua jambo lililo sawa na jema. Maana hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yataipendeza nafsi yako. Busara itakulinda, ufahamu utakuhifadhi; vitakuepusha na njia ya uovu, na watu wa maneno mapotovu; watu waziachao njia nyofu, ili kuziendea njia za giza; watu wafurahiao kutenda maovu, na kupendezwa na upotovu wa maovu; watu ambao mienendo yao imepotoka, nazo njia zao haziaminiki. Hekima itakuwezesha kumkwepa mwanamke mwasherati, mwanamke malaya wa maneno matamu; mwanamke amwachaye mwenzi wa ujana wake, na kulisahau agano la Mungu wake. Nyumba yake yaelekea kuzimu, njia zake zinakwenda ahera. Yeyote amwendeaye kamwe harudi, wala hairudii tena njia ya uhai. Kwa hiyo utafuata mfano wa watu wema, na kuzingatia mienendo ya waadilifu. Maana wanyofu wataipata nchi, na waaminifu watadumu ndani yake. Lakini waovu wataondolewa nchini, na wenye hila watangolewa humo.

Mungu wetu ukawaguse kwamkono wako wenye nguvu,Wagonjwa
ukawaponye,wenye njaa ukawape chakula na ukabariki mashamba yao
mavuno yao yakawe mengi wakapate na akiba..
walio katika magumu.majaribu mbalimbali Mung wetu ukawavushe
walio katika vifungo vya yule mwovu Mungu wetu ukawafungue..
Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Sifa na Utukufu tunakurushia Mungu wetu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!
Asanteni sana wapendwa/waungwana kwakuwa nami
Mungu Baba akawabariki na msipungukiwe katika mahitaji
yenu na Mungu akawape sawasawa na mapenzi yake..
Nawapenda.

Makabila ya mashariki yanarudi nyumbani

1Basi, Yoshua akawaita watu wa kabila la Reubeni, la Gadi na watu wa nusu ya kabila la Manase 2Taz Hes 32:20-32; Yosh 1:12-15 akawaambia, “Nyinyi mmefuata yale yote Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliyowaamuru na mmetii maagizo niliyowaamuru. 3Wala hamkuwaacha ndugu zenu muda huo wote mrefu mpaka leo, bali mmefuata kwa makini amri ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. 4Sasa Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu amewapa ndugu zenu amani, kama vile alivyoahidi, basi, rudini kwenu katika nchi ambayo mlipewa na Mose mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, iwe mali yenu, yaani ngambo ya mto Yordani. 5Muwe waangalifu kutii amri na sheria ambazo Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, aliwaamuru: Kumpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mfuate anachotaka na kushika amri zake; mkae pamoja naye na kumtumikia kwa moyo wote na roho yote.” 6Basi, Yoshua akawabariki na kuwaruhusu waende zao akawaambia, 7,8“Rudini makwenu na utajiri mwingi; ng'ombe wenu wote, fedha, dhahabu, shaba, chuma na mavazi mengi. Gawaneni na ndugu zenu nyara zote mlizoziteka kutoka kwa maadui zenu.” Mose alikuwa ameyapa nusu ya kabila la Manase sehemu yao huko Bashani. Naye Yoshua akaipatia nusu ya pili ya kabila hilo sehemu yao huko magharibi ya mto Yordani kama alivyoyapa makabila yale mengine.

Madhabahu karibu na Yordani

9Basi, watu wa Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase wakaachana na watu wa makabila mengine ya Israeli huko Shilo, nchini Kanaani, wakarudi kwao katika nchi ya Gileadi, nchi yao wenyewe waliyoimiliki kwa amri ya Mwenyezi-Mungu kama alivyomwagiza Mose.
10Walipofika kwenye mto Yordani wakiwa bado katika nchi ya Kanaani, wakajenga madhabahu kubwa sana karibu na mto huo. 11Basi, habari zikawafikia watu wa makabila mengine ya Israeli kwamba makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase yalikuwa yamejenga madhabahu kubwa karibu na mto Yordani katika nchi ya Kanaani, yaani ndani ya eneo lao. 12Waliposikia hivyo, Waisraeli walikusanyika wote huko Shilo kwenda kupigana vita na hayo makabila ya mashariki.
13Basi, watu wa Israeli wakamtuma Finehasi, mwanawe kuhani Eleazari, huko Gileadi kwa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase. 14Finehasi akaondoka pamoja na wakuu kumi, kila mmoja akiwa mkuu wa jamaa katika kabila lake. 15Nao wakawaendea watu wa makabila ya Reubeni, Gadi na nusu ya kabila la Manase huko Gileadi wakawaambia, 16“Jumuiya nzima ya Mwenyezi-Mungu inauliza hivi: ‘Ni udanganyifu gani huu mmemfanyia Mungu wa Israeli? Mbona mmemwasi Mwenyezi-Mungu kwa kujenga madhabahu hii? 17Je, dhambi tulizotenda huko Peori hazitoshi? Hamwoni kwamba bado hatujajitakasa na kwamba mateso yake bado yanaisumbua jumuiya ya Mwenyezi-Mungu? 18Kwa nini, basi, mmeacha kumfuata Mwenyezi-Mungu? Mkimwasi Mwenyezi-Mungu leo, kesho ataikasirikia sana jumuiya nzima ya Israeli. 19Haya, ikiwa nchi yenu si najisi, njoni katika nchi ya Mwenyezi-Mungu ambako hema yake iko na kujichukulia sehemu huko pamoja nasi; ila tu msimwasi Mwenyezi-Mungu na kutufanya sisi sote waasi kwa kujijengea nyinyi wenyewe madhabahu isiyo ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. 20Je, Akani mwana wa Zera alipokosa uaminifu katika vitu vitakatifu, ghadhabu haikuangukia jumuiya nzima ya Israeli? Tena Akani hakufa tu yeye peke yake kwa sababu ya uovu wake.’”
21Hapo watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase wakawajibu viongozi wa jamaa za Israeli, 22“Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Yeye anajua kwa nini tumefanya hivyo. Na Waisraeli wote watajua pia! Kama huu ni uasi au ni ukosefu wa imani kwa Mwenyezi-Mungu basi, yeye aache kutuokoa leo. 23Kama tumemwacha Mwenyezi-Mungu tukajenga madhabahu yetu wenyewe ili tutoe sadaka za kuteketezwa, za nafaka au za amani, basi Mwenyezi-Mungu na atulipize kisasi. 24Lakini sivyo ilivyo. Tuliijenga kwa kuogopa kwamba huenda katika siku zijazo watoto wenu watawaambia watoto wetu, ‘Nyinyi mna uhusiano gani na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli? 25Hamwoni kwamba Mwenyezi-Mungu ameweka mto wa Yordani kuwa mpaka kati yenu na sisi? Nyinyi makabila ya Reubeni na kabila la Gadi hamna fungu lolote lenu kwa Mwenyezi-Mungu.’ Hivyo watoto wenu wangeweza baadaye kusababisha watoto wetu waache kumwabudu Mwenyezi-Mungu. 26Ndiyo maana tuliamua kujenga madhabahu hii, lakini si kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka wala tambiko, 27bali tulitaka madhabahu hii iwe ushuhuda kati yetu na nyinyi na vizazi vyetu vijavyo kwamba sisi tunayo haki ya kumtumikia Mwenyezi-Mungu kwa sadaka zetu za kuteketezwa na tambiko zetu, na kwa sadaka zetu za amani, ili watoto wenu wasije wakawaambia watoto wetu kwamba hawana fungu lolote lao kwa Mwenyezi-Mungu. 28Tena tulifikiri kwamba ikiwa jambo kama hilo litasemwa juu yetu au juu ya wazawa wetu katika siku zijazo, tutasema, ‘Tazameni mfano wa madhabahu ya Mwenyezi-Mungu ambayo wazee wetu waliijenga; sio kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka au tambiko bali kama ushuhuda kati yetu na nyinyi’. 29Sisi hatukuwa na nia ya kumwasi sasa Mwenyezi-Mungu hata kidogo na kumwacha kwa kujenga madhabahu ya kutolea sadaka za kuteketezwa au sadaka za unga au za tambiko. Hatupendi kutolea sadaka mahali pengine isipokuwa juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu iliyo mbele ya maskani yake.”
30Kuhani Finehasi, viongozi wa jumuiya nzima na wakuu wa jamaa za Israeli waliokuwa pamoja naye waliposikia maneno hayo ya watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, wakaridhika. 31Naye Finehasi mwana wa kuhani Eleazari, akayaambia makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase, “Leo tumejua kwamba Mwenyezi-Mungu yumo miongoni mwenu maana hamkumfanyia Mungu uasi. Sasa mmewaokoa Waisraeli wasiadhibiwe na Mwenyezi-Mungu.” 32Basi, Finehasi mwana wa kuhani Eleazari pamoja na viongozi wenzake wakawaaga watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaondoka nchini Gileadi, wakarudi Kanaani kwa Waisraeli na kuwapa habari hizo. 33Taarifa hiyo ikawafurahisha Waisraeli, wakamshukuru Mwenyezi-Mungu na kuacha mipango yao ya vita na lengo lao la kuharibu kabisa nchi iliyokuwa ya makabila ya Reubeni na Gadi. 34Watu wa makabila ya Reubeni na Gadi wakaiita ile madhabahu ya “Ushuhuda,” kwani walisema, “Madhababu hii ni ushahidi wetu kwamba Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu.”


Yoshua 22;1-34

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: