Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 23 January 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1Samueli27...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu kwa kila wakati..

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu..
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote..
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu..
Utukuzwe Mungu wetu,Muumba wetu,Mungu mwenye nguvu,
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa walio hai..
Mungu mwenye huruma,Mungu wa Wajane,Mungu wa Yatima,Mungu unayeponya,Mungu unayebariki,Mungu usiyeshindwa,Mungu wetu ni muweza wa yote,Neema yako yatutosha Baba wa mbinguni..


Lakini wewe unapaswa kuhubiri mafundisho sahihi. Waambie wanaume wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu. Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema, ili wawazoezeshe kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto, wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa. Kadhalika, wahimize vijana wawe na kiasi. Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako. Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili maadui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu. Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao, au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu. Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote. Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa, tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema. Basi, sema mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.


Tunakuja mbele zako Mungu wetu tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako Baba wa Mbinguni..
Jehovah tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya 
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutujua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu
Yahweh tunaomba utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Baba wa Mbinguni
tunaomba utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona..

Mfalme wa amani tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika ufanyaji/utendaji
Baba wa Mbinguni nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhutaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu Yahweh tunaomba ukatupe kama inavyokupendeza wewe..

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Jehovah tunaomba ukatamalaki na kutuatamia,Yahweh tukawe salama moyoni,Mungu wetu ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii,Jehovah tukanene yaliyoyako,Baba wa Mbinguni ukatuongoze tutokapo/tuingiapo Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo Yahweh na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni..
Jehovah Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu Baba wa Mbinguni tunaomba utupe neema ya kufuata njia zako Yahweh tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..


Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema. Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikilizano, wawe daima wapole kwa kila mtu. Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukachukiana. Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu ulipofunuliwa, alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji. Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu, ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uhai wa milele tunaotumainia. Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, yaani mambo mazuri na ya kuwafaa watu. Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu. Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye. Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.
Baba wa Mbinguni tazama wenye shida/tabu Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Mungu wetu tunaomba ukawaponye wagonjwa Jehovah ukawape uvumilivu na imani wale wanaowauguza..
Yahweh ukawaokoe wale walio katika vifungo vya yule mwovu Baba wa Mbinguni tunaomba ukawatete wale walio magerezani pasipo na hatia na haki ikatendeke..
Mungu wetu ukawe tumaini kwa walio kata tamaa,waliokataliwa,wenye hofu na mashaka..
Baba wa Mbinguni tunaomba ukawavushe salama wale wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,Mungu wetu ukawape chakula wenye njaa Baba ukabariki mashamba/vyanzo vyao wakapate chakula cha kutuosha,kuweka akiba na kusaidia wengine..
Mungu wetu utunaomba ukawasamehe wale wote walikwenda kinyume nawe nao wakatubu na kukurudia wewe..
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao..
Yahweh tunayaweka haya yote mikononi mwako,Mungu Baba  tunaomba ukasikie kuomba kwetu Baba wa Mbinguni tunaomba ukapokee maombi/sala zetu Yahweh  tunaomba ukafute machozi ya watoto wako wanaokutafuta na kukuomba kwa bidii na imani..
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..


Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi. Jitahidi kumsaidia mwanasheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao, na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji. Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa. Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu aendelee kuwabariki na amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi daima..
Nawapenda.

Daudi miongoni mwa Wafilisti

1Daudi akajisemea moyoni, “Siku moja, Shauli ataniangamiza. Jambo jema kwangu ni kukimbilia katika nchi ya Wafilisti. Shauli atakata tamaa kunitafuta ndani ya mipaka ya nchi ya Israeli, nami nitakuwa salama kutoka mikononi mwake.” 2Hivyo, mara moja Daudi na watu wake 600 wakaenda kwa Akishi mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi. 3Daudi na watu wake pamoja na jamaa yake wakaishi na Akishi huko Gathi. Daudi alikuwa na wake wawili: Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali kutoka mji wa Karmeli. 4Shauli aliposikia kwamba Daudi amekimbilia Gathi, hakumfuata tena.
5Siku moja, Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali mbele yako nakuomba unipe mji mmoja nchini mwako ili uwe mahali pangu pa kuishi. Hakuna haja kwangu kuishi nawe katika mji huu wa kifalme.” 6Siku hiyo, Akishi akampa mji wa Siklagi. Hivyo, tangu siku hiyo mji wa Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda.
7Daudi aliishi katika nchi ya Wafilisti kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne. 8Katika muda huo, Daudi na watu wake waliwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki, ambao walikuwa wenyeji wa nchi hiyo tangu zamani. Aliwashambulia katika nchi yao mpaka Shuri, mpakani na Misri. 9Daudi aliipiga nchi hiyo asimwache hai mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, akateka kondoo, ng'ombe, punda, ngamia na mavazi; kisha akarudi na kufika kwa Akishi. 10Akishi alipomwuliza, “Leo mashambulizi yako yalikuwa dhidi ya nani?” Daudi alimwambia, “Dhidi ya Negebu ya Yuda” au “Dhidi ya Negebu ya Wayerameeli” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.” 11Daudi hakumwacha mtu yeyote hai awe mwanamume au mwanamke ili aletwe Gathi; alifikiri moyoni: “Wanaweza wakaeleza juu yetu na kusema, ‘Daudi alifanya kitendo hiki na kile.’” Hivyo ndivyo Daudi alivyozoea kutenda wakati wote alipoishi katika nchi ya Wafilisti. 12Kwa hiyo, Akishi alimsadiki Daudi, akifikiri, “Wananchi wenzake Waisraeli hawampendi kabisa; kwa hiyo, atanitumikia maisha yake yote.”


1Samweli27;1-12

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: