Wimbo wa ushindi wa Daudi
1Daudi alimwimbia Mwenyezi-Mungu maneno ya wimbo ufuatao siku ile Mwenyezi-Mungu alipomkomboa mikononi mwa adui zake, na mkononi mwa Shauli. 2Alisema,
“Mwenyezi-Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu, na mkombozi wangu.
3Mungu wangu, mwamba wangu, ninayemkimbilia usalama;
ngao yangu, nguvu ya wokovu wangu,
ngome yangu na kimbilio langu.
Mwokozi wangu; unaniokoa kutoka kwa watu wakatili.
4Namwita Mwenyezi-Mungu astahiliye sifa anisaidie,
nami naokolewa kutoka kwa adui zangu.
5“Maana mawimbi ya kifo yalinizingira,
mafuriko ya maangamizi yalinivamia;
6kamba za kuzimu zilinizinga,
mitego ya kifo ilinikabili.
7“Katika taabu yangu, nilimwita Mwenyezi-Mungu;
nilimwita Mungu wangu.
Toka hekaluni mwake aliisikia sauti yangu,
kilio changu kilimfikia masikioni mwake.
8“Hapo, dunia ikatetemeka na kutikisika,
misingi ya mbinguni ikayumbayumba na kuruka,
kwani Mungu alikuwa amekasirika.
9Moshi ulifuka kutoka puani mwake,
moto uunguzao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yalilipuka kutoka kwake.
10Aliinamisha anga, akashuka chini;
na wingu jeusi chini ya miguu yake.
11Alipanda kiumbe chenye mabawa22:11 kiumbe chenye mabawa; Kiebrania: Kerubi. na kuruka,
alionekana juu ya mabawa ya upepo.
12Alijizungushia giza pande zote,
kifuniko chake kilikuwa mawingu mazito na mkusanyiko wa maji.22:12 makala ya Kiebrania si dhahiri.
13Umeme ulimulika mbele yake,
kulilipuka makaa ya moto.
14Mwenyezi-Mungu alinguruma kutoka mbinguni,
Mungu Mkuu akatoa sauti yake.
15Aliwalenga adui mishale, akawatawanya,
alirusha umeme, akawatimua.
16Mwenyezi-Mungu alipowakemea,
kutokana na pumzi ya puani mwake,
vilindi vya bahari vilifunuliwa,
misingi ya dunia ikaonekana.
17“Mungu alinyosha mkono wake toka juu, akanichukua,
kutoka kwenye maji mengi alininyanyua.
18Aliniokoa kutoka kwa adui yangu mwenye nguvu,
aliniokoa kutoka kwa hao walionichukia
maana walikuwa na nguvu nyingi kunishinda.
19Walinivamia nilipokuwa taabuni,
lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa kinga yangu.
20Alinileta, akaniweka mahali pa usalama,
alinisalimisha, kwani alipendezwa nami.
21“Mwenyezi-Mungu alinipa tuzo kadiri ya uadilifu wangu;
alinituza kwa vile mikono yangu haina hatia.
22Maana, nimefuata njia za Mwenyezi-Mungu,
wala sikujitenga na Mungu wangu kwa uovu.
23Nimeshika maagizo yake yote,
sikuacha kufuata masharti yake.
24Mbele yake sikuwa na hatia,
nimejikinga nisiwe na hatia.
25Mwenyezi-Mungu amenituza kadiri ya uadilifu wangu,
yeye anajua usafi wangu.
26“Wewe ni mwaminifu kwa walio waaminifu,
mwema kwa wale walio wema.
27Wewe ni mkamilifu kwa walio wakamilifu,
lakini mkatili kwa watu walio waovu.
28Wewe wawaokoa walio wanyenyekevu,
lakini wawaangalia wenye majivuno kuwaporomosha.
29Ee Mwenyezi-Mungu, wewe u taa yangu,
Mungu wangu, unayefukuza giza langu.
30Kwa msaada wako, wakishambulia kikosi;
wewe wanipa nguvu ya kuruka kuta zake.
31Anachofanya Mungu hakina dosari!
Ahadi ya Mwenyezi-Mungu ni ya kuaminika;
yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia.
32“Nani aliye Mungu isipokuwa Mwenyezi-Mungu?
Nani aliye mwamba wa usalama ila Mungu wetu?
33Mungu huyu ndiye kimbilio langu imara,
na ameifanya njia yangu iwe salama.22:33 makala ya Kiebrania si dhahiri.
34Ameiimarisha miguu yangu22:34 yangu: Au yake. kama ya paa,
na kuniweka salama juu ya vilele.
35Hunifunza kupigana vita,
mikono yangu iweze kuvuta upinde wa shaba.
36Umenipa ngao yako ya kuniokoa;
msaada wako umenifanya mkuu.
37Umenirahisishia njia yangu;
wala miguu yangu haikuteleza.
38Niliwafuatia adui zangu na kuwaangamiza,
sikurudi nyuma mpaka wameangamizwa.
39Niliwaangamiza, nikawaangusha chini
wasiweze kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40Wewe ulinijalia nguvu ya kupigana vita;
uliwaporomosha adui chini yangu.
41Uliwafanya adui zangu wakimbie,
na wale walionichukia niliwaangamiza.
42Walitafuta msaada, lakini hapakuwa na wa kuwaokoa,
walimlilia Mwenyezi-Mungu, lakini hakuwajibu.
43Niliwatwanga na kuwaponda kama mavumbi ya nchi,
nikawaponda na kuwakanyaga kama matope barabarani.
44“Wewe uliniokoa na mashambulizi ya watu wangu,22:44 sehemu ya aya hii makala ya Kiebrania si dhahiri.
umenifanya mtawala wa mataifa.
Watu nisiowajua walinitumikia.
45Wageni walinijia wakinyenyekea,
mara waliposikia habari zangu walinitii.
46Wageni walikufa moyo;
wakaja kutoka ngome zao wakitetemeka.22:46 wakitetemeka: Kiebrania: Wamejifunga wenyewe.
47“Mwenyezi-Mungu yu hai!
Asifiwe mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu wangu, mwamba wa wokovu wangu.
48Yeye ameniwezesha kulipiza kisasi
na kuyatiisha mataifa chini yangu.
49Ameniokoa kutoka adui zangu.
Ee Mwenyezi-Mungu, ulinikuza juu ya wapinzani wangu
na kunisalimisha mbali na watu wakatili.
50“Kwa hiyo, nitakutukuza kati ya mataifa,
ee Mwenyezi-Mungu, nitaliimbia sifa jina lako.
51Mungu humjalia mfalme wake ushindi mkubwa;22:51 Mungu … mkubwa: Au yeye ni mnara wa wokovu.
humwonesha fadhili zake huyo aliyemweka wakfu,
naam, humfadhili Daudi na wazawa wake milele.”
2Samweli22;1-51
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)
"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.
No comments:
Post a Comment