Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 5 February 2018

Kikombe Cha Asubuhi ; 2 Samueli 5...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana...

 Ni siku/wiki nyingine tena Mungu wetu ametuchagua na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii..
Si kwamba sisi ni wema sana wala si kwa nguvu zetu,si kwa uwezo wetu wala si kwa utashi wetu,si kwamba sisi ni wazuri mno wala si kwa akili zetu..
Ni kwa neema/rehema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo hii..
Tumshukuru Mungu wetu kwa wema na fadhili zake kwetu...
Tumsifu Mungu na kumtukuza daima..
Unastahili sifa na kutukuzwa Mungu wetu,Unastahili kuabudiwa Baba wa Mbinguni,Unastahili kuhimidiwa Yahweh,Unatosha Jehovah..
Neema yako yatutosha Mungu wetu,Mtendo yako ni makuu sana,Mtendo yako ni ya ajabu Mungu wetu..!!


Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, nawaandikia nyinyi watu wa Mungu huko Efeso, mlio waaminifu katika kuungana na Kristo Yesu. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Maana, katika kuungana na Kristo ametubariki kwa kutujalia zawadi zote za kiroho mbinguni. Kabla ya kuumbwa ulimwengu, Mungu alituteua tuwe wake katika kuungana na Kristo ili tuwe watakatifu na bila hitilafu mbele yake. Kwa sababu ya upendo wake, Mungu alikuwa ameazimia tangu zamani kutuleta kwake kama watoto wake kwa njia ya Yesu Kristo. Ndivyo alivyopenda na kunuia. Basi, tumsifu Mungu kwa sababu ya neema yake tukufu ambayo ametujalia katika Mwanae mpenzi!



Yahweh tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako....
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Yahweh nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe wale wote waliotukosea..
Baba wa Mbinguni tunaomba utuepushe katika majaribu 
Yahweh utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote..
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Mungu wetu utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona...



Maana kwa damu yake Kristo sisi tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa. Ndivyo ulivyo ukuu wa neema yake aliyotukirimia bila kipimo! Kwa hekima na ujuzi wake wote Mungu alitekeleza kile alichonuia, akatujulisha mpango wake uliofichika, ambao alikuwa ameazimia kuutekeleza kwa njia ya Kristo. Mpango huo ambao angeutimiza wakati utimiapo ni kukusanya pamoja viumbe vyote, kila kitu mbinguni na duniani, chini ya Kristo. Katika kuungana na Kristo, sisi tumerithishwa wokovu kama tulivyopangiwa kadiri ya azimio lake Mungu atekelezaye kila kitu kulingana na uamuzi na matakwa yake. Basi, sisi tuliotangulia kumtumainia Kristo tunapaswa kuusifu utukufu wa Mungu! Nanyi pia watu wa mataifa mengine, mliusikia ujumbe wa kweli yaani Habari Njema iliyowaletea wokovu, mkamwamini Kristo; naye Mungu, ili kuonesha kuwa nyinyi ni wake, akawapiga mhuri kwa kuwapeni yule Roho Mtakatifu aliyetuahidia. Huyu Roho ni dhamana ya kupata yote yale Mungu aliyowaahidia watu wake, na jambo hili latuhakikishia kwamba Mungu atawakomboa kabisa wote walio wake. Tuusifu utukufu wake!



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Yahweh tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Baba wa Mbinguni tunaomba nasi ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji..
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Jehovah ukatupe kama inavyokupendeza wewe..


Mafalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka..
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh ukatamalaki na kutuatamia,Mungu wetu ukatubariki tuingiapo/tutokapo Yahweh ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Baba wa Mbinguni tunaomna ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo..
Jehovah tukawe salama moyoni Mungu wetu ukatupe macho ya rohoni na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii..
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Yahweh kusimamia Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu..
Jehovah ukatupe hekima,busara,amani,utuwema,fadhili.huruma na tukatende yote yanayokupendeza wewe..
Yahweh ukatuokoe na choyo,kiburi,unafiki,ubinafsi,ugombanishi,makwazo na vyote vinavyokwenda kinyume nawe..
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu,Mungu wetu ukawe nasi popote tupitapo Jehovah na ikajulikane kwamba upo Baba wa mbinguni..
amani ikatawale na upendo ukadumu kati yetu..
Ukatufanye chombo chema Mungu wetu nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi..



Kwa sababu hiyo, tangu niliposikia juu ya imani yenu kwa Bwana Yesu, na mapendo yenu kwa watu wote wa Mungu, sijaacha kamwe kumshukuru Mungu kwa ajili yenu. Ninawakumbuka katika sala zangu, ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mtukufu, awajalieni Roho wake atakayewapa hekima na kuwafunulieni Mungu mpate kumjua. Namwomba Mungu aifunue mioyo yenu iweze kuuona mwanga wake, mpate kutambua lile tumaini alilowaitieni na utukufu mkuu wa zawadi alizowawekea watu wake, mpate kutambua jinsi uwezo wake ulivyo mkuu mno kwa ajili yetu sisi tunaoamini. Uwezo huo unaofanya kazi ndani yetu ni sawa na nguvu ile kuu mno aliyomfufua nayo Kristo kutoka kwa wafu, akamketisha upande wake wa kulia mbinguni. Huko, Kristo anatawala juu ya kila tawala, mamlaka, enzi na ukuu; anatawala juu ya kila cheo kiwezacho kutajwa katika ulimwengu huu na katika ulimwengu ujao. Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake, akamkabidhi kwa kanisa akiwa mkuu wa vitu vyote. Kanisa ni mwili wa Kristo, na ukamilifu wake yeye anayekamilisha vitu vyote kila mahali.


Yahweh tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu wenye shida/tabu,wagonjwa,wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,walio kata tamaa,walio kataliwa,wenye hofu na mashaka,waliokatika vifungo vya yule mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,walioanguka/potea na wote waliokwenda kinyume nawe na wakatubu na kukurudia Mungu wetu ukawaokoe na kuwaongoza
Baba wa Mbinguni ukawasamehe na kuwainua,Mungu wetu ukawaponye na kuwapa chakula,Yahweh ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako nazo ziwaweke huru,Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Yahweh ukaonekane katika maisha yao Mungu wetu tunaomba ukapokee na kusikia kuomba kwetu,Yahweh tunaomba ukajibu maombi/sala zetu na  ukawatendee sawasawa na mapenzi yako..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina..!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami/kunisoma
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye
Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo ikawe nanyi daima..
Nawapenda.


Daudi awa mfalme wa Israeli na Yuda

(1Nya 11:1-9; 14:1-7)

1Kisha makabila yote ya Israeli yalimwendea Daudi huko Hebroni, na kumwambia, “Tazama, sisi ni mwili na damu yako. 2Hapo awali, Shauli alipokuwa mfalme wetu wewe ndiwe uliyewaongoza Waisraeli vitani, na Mwenyezi-Mungu alikuambia ‘Utakuwa mchungaji wa watu wangu Israeli na utakuwa mkuu juu ya Israeli.’” 3Basi, wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme Daudi huko Hebroni; naye akafanya agano nao mbele ya Mwenyezi-Mungu, halafu wakampaka Daudi mafuta awe mfalme wa Israeli. 4Daudi alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoanza kutawala, na alitawala kwa muda wa miaka arubaini. 5Huko Hebroni, alitawala watu wa Yuda kwa muda wa miaka saba na miezi sita, na huko Yerusalemu alitawala watu wa Israeli pamoja na Yuda kwa muda wa miaka thelathini na mitatu.
6Baadaye mfalme na watu wake walikwenda Yerusalemu kuwashambulia Wayebusi waliokuwa wenyeji wa nchi hiyo. Lakini wao wakamwambia, “Hutaingia mjini humu, kwani vipofu na vilema watakufukuzia mbali.” Walimwambia hivyo kwani walifikiri kuwa Daudi asingeweza kuingia mjini humo. 7Hata hivyo, mfalme Daudi aliiteka ngome ya Siyoni, yaani mji wa Daudi.
8Siku hiyo, Daudi alisema, “Mtu yeyote atakayewapiga Wayebusi na apitie kwenye mfereji wa maji ili kuwashambulia vilema na vipofu ambao roho yangu inawachukia.” Ndio maana watu husema, “Vipofu na vilema hawataingia nyumbani.”5:8 makala ya Kiebrania si dhahiri.
9Daudi alikaa kwenye ngome hiyo, nao mji akauita, “Mji wa Daudi.” Daudi aliujenga mji kuuzunguka, akianzia Milo5:9 Milo: Sehemu iliyojazwa na mfalme Daudi mjini Yerusalemu mahali ambapo hekalu lilijengwa. kuelekea ndani. 10Naye Daudi akazidi kuwa maarufu zaidi kwa sababu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye.
11Kisha, mfalme Hiramu wa Tiro alituma wajumbe kwa Daudi; alimpelekea pia mierezi, maseremala na waashi ambao walimjengea Daudi ikulu. 12Hivyo, Daudi akatambua kwamba Mwenyezi-Mungu amemwimarisha awe mfalme wa Israeli, na kwamba ameukuza ufalme wake kwa ajili ya watu wake wa Israeli.
13Daudi alijitwalia masuria na wake zaidi wa huko mjini Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni. Hao, wakamzalia watoto zaidi wa kiume na wa kike. 14Yafuatayo ndiyo majina ya watoto wa kiume, wake zake waliomzalia huko Yerusalemu: Shamua, Shobabu, Nathani, Solomoni, 15Ibhari, Elishua, Nefegi, Yafia, 16Elishama, Eliada na Elifeleti.

Ushindi juu ya Wafilisti

(1Nya 14:8-17)

17Wafilisti waliposikia kwamba Daudi amepakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli, wote walitoka kwenda kumtafuta, lakini yeye alipata habari, akaingia ndani ya ngome. 18Wafilisti walifika na kujitawanya kwenye Bonde la Refaimu. 19Basi, Daudi alimwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwangu?” Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Daudi, “Nenda, maana hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” 20Basi, Daudi akafika Baal-perasimu, na kuwashinda Wafilisti; halafu akasema, “Mwenyezi-Mungu amepita katikati ya adui zangu kama mafuriko ya maji yaendayo kasi.” Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Baal-perasimu.5:20 Baal-perasimu: Kiebrania maana yake, “Bwana apitaye katikati”. 21Wafilisti waliziacha sanamu zao za miungu mahali hapo, naye Daudi na watu wake wakazichukua.
22Kwa mara ya pili, Wafilisti walifika tena na kujitawanya kwenye bonde la Refaimu. 23Daudi alipomwomba Mwenyezi-Mungu shauri, Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiwashambulie kutoka hapa ulipo, bali zunguka na kuwashambulia kutoka mkabala wa miti na miforosadi. 24Na mara mtakaposikia vishindo vya gwaride kwenye vilele vya miforosadi hiyo, hapo jipe moyo kwani nitakuwa nimetoka ili kukutangulia kulipiga jeshi la Wafilisti.” 25Daudi alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu, naye akawapiga Wafilisti kutoka Geba hadi Gezeri.



2Samweli5;1-25

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: