Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Friday, 16 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 10...

Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah Mungu wetu yu mwema sana
Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Mungu wetu Baba yetu,Muumba wetu Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu mwenye huruma,Mungu mwenye kuponya
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo,Mungu wa walio hai
Baba wa Upendo,Baba wa faraja,Baba wa Yatima,Mume wa Wajane
Muweza wa yote Alfa na Omega...!!!


Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Chonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza, nami nitayaandika maneno yale yaliyokuwa katika vile vibao vya kwanza ulivyovivunja. Uwe tayari kesho asubuhi, uje kukutana nami mlimani Sinai. Mtu yeyote asije pamoja nawe, wala asionekane popote mlimani; wala kondoo au ng'ombe wasilishwe karibu yake.” Basi, Mose akachonga vibao viwili vya mawe kama vile vya kwanza. Akaondoka asubuhi na mapema, akapanda mlimani Sinai, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru, akiwa na vile vibao viwili vya mawe mikononi mwake. Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu, akasimama pamoja na Mose, akalitaja jina lake, “Mwenyezi-Mungu.” Kisha Mwenyezi-Mungu akapita mbele ya Mose akitangaza tena, “Mwenyezi-Mungu; mimi Mwenyezi-Mungu, ni Mungu mwenye huruma na neema; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa fadhili na uaminifu. Mimi nawafadhili maelfu, nikiwasamehe uovu, makosa na dhambi; lakini kwa vyovyote vile sitaacha kumwadhibu mwenye hatia; nawapatiliza watoto na wajukuu uovu wa baba na babu zao, hata kizazi cha tatu na nne.” Mose akainama chini mara, akamwabudu Mungu. Kisha akasema, “Ee Bwana wangu, kwa vile umenijalia fadhili mbele zako, nakuomba uende pamoja nasi. Watu hawa ni wenye vichwa vigumu, lakini utusamehe uovu wetu na dhambi yetu, utupokee kama watu wako mwenyewe.”

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Neema yako yatutosha ee Baba wa Mbinguni...
Sifa na Utukufu tunakurudishia Mungu wetu...!!!

Baba wa Mbinguni tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,
tukijishusha na kujiachilia mikononi mwako
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua..
Mungu wetu tunaomba nasi ukatupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Baba wa Mbinguni usitutie katika majaribu Mungu wetu tunaomba
utuokoe na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovaha tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu Yahweh
utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo
wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona.....


Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Sasa ninafanya agano na watu wako. Nitatenda maajabu mbele yao ambayo hayajapata kutendwa duniani kote, wala katika taifa lolote. Na watu wote mnaoishi kati yao wataona matendo yangu makuu. Maana nitafanya jambo la ajabu kwa ajili yako. “Shikeni amri ninazowapa leo. Nitawafukuza mbele yenu Waamori, Wakanaani, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi. Jihadharini msije mkafanya agano na wakazi wa nchi mnayoiendea, maana hilo litakuwa mtego miongoni mwenu. Lakini mtazibomoa madhabahu zao na kuzivunja nguzo zao za ibada na sanamu zao za Ashera. Msiabudu mungu yeyote mwingine, maana mimi Mwenyezi-Mungu najulikana kwa jina: ‘Mwenye Wivu,’ mimi ni Mungu mwenye wivu. Msifanye mikataba yoyote na wakazi wa nchi hiyo, maana watakapoiabudu miungu yao ya uongo na kuitambikia, watawaalikeni, nanyi mtashawishiwa kula vyakula wanavyoitambikia miungu yao, nao wavulana wenu wakaoa binti zao, na hao binti wanaoabudu miungu yao, wakawashawishi wavulana wenu kufuata miungu yao. “Msijifanyie miungu ya uongo ya chuma. “Mtaiadhimisha sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu. Kwa muda wa siku saba mtakula mikate isiyotiwa chachu wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, kama nilivyowaamuru, kwa sababu katika mwezi huo wa Abibu mlitoka Misri. Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume ni wangu, pamoja na wazaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wako wote, wa ng'ombe na wa kondoo. Mzaliwa wa kwanza wa punda utamkomboa kwa kunitolea kondoo. Kama hutamkomboa utamvunja shingo. Watoto wenu wote wa kiume ambao ni wazaliwa wa kwanza mtawakomboa. Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu. “Siku sita mtafanya kazi zenu, lakini siku ya saba mtapumzika, hata ikiwa ni wakati wa kulima au kuvuna. Mtaadhimisha sikukuu ya majuma mwanzoni mwa majira ya mavuno ya ngano, na sikukuu ya kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka. Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakusanyika mbele yangu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli. Nitayafukuza mataifa mengine mbele yenu na kuipanua mipaka yenu. Hakuna mtu yeyote atakayeitamani nchi yenu wakati mnapokusanyika kuniabudu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu mara tatu kila mwaka. “Msinitolee damu ya tambiko yangu pamoja na chachu; wala tambiko ya sikukuu ya Pasaka isibakizwe mpaka asubuhi. “Mazao ya kwanza ya ardhi yako utayaleta nyumbani kwangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako. “Usimchemshe mwanakondoo au mwanambuzi katika maziwa ya mama yake.” Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Andika maneno haya, maana kulingana na maneno haya, ninafanya agano nawe na watu wa Israeli.” Mose alikaa huko mlimani pamoja na Mwenyezi-Mungu siku arubaini, mchana na usiku; hakula chakula wala kunywa maji. Aliandika maneno yote ya agano na zile amri kumi.



Yahweh tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji...
Yahweh tusipungukiwe katika mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba amani yako ikatawale katika nyumba/ndoa zetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Mungu wetu tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Yahweh tunaomba ukatamalaki  na kutuatamia Baba wa Mbinguni
tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo Mungu wetu tunaomba
ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia Jehovah tunaomba
ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana  wetu Yesu Kristo..
Mungu wetu tunaomba tukawe salama rohoni  Jehovah tunaomba
ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba
upo Baba wa Mbinguni..
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako Mungu wetu
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Yahweh neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu
Baba wa Mbinguni ukatufanye chombo chema Yahweh nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....


Mose alipokuwa anashuka mlimani Sinai akiwa na vile vibao viwili vyenye maneno ya agano mikononi mwake, hakujua kuwa uso wake ulikuwa unangaa kwa sababu alikuwa ameongea na Mwenyezi-Mungu. Aroni na watu Waisraeli wote walipomwona waliogopa kumkaribia, kwani uso wake ulikuwa unangaa. Lakini Mose alimwita Aroni na viongozi wa jumuiya ya Waisraeli waende karibu naye, kisha akazungumza nao. Baadaye Waisraeli wote wakaja karibu naye, naye akawapa amri zote ambazo Mwenyezi-Mungu alimpa kule mlimani Sinai. Mose alipomaliza kuzungumza na watu aliufunika uso wake kwa kitambaa. Lakini ikawa kwamba kila mara Mose alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu katika hema la mkutano, alikiondoa kile kitambaa mpaka alipotoka nje. Na alipotoka nje aliwaambia Waisraeli mambo yote aliyoamriwa, nao Waisraeli waliuona uso wake unangaa. Ndipo Mose alipoufunika tena uso wake kwa kitambaa mpaka alipokwenda kuongea na Mwenyezi-Mungu.

Mungu wetu tunawaweka mikononi mwako watoto wako
wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
kila mmoja na mahitaji yake,Mungu wetu ukaonekane katika shida/tabu
zao Baba wa Mbinguni ukawape neema ya kujiombea na kufuata njia zako
Yahweh wakasimamie Neno lako nalo likawaweke huru
Mungu wetu tunaomba ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Jehovah ukatamalaki na kuwaatamia,Mungu wetu ukasikie kulia kwao
Baba wa Mbinguni ukawafute machozi yao na kuwaongoza
Yahweh ukawape neema ya kutambua mema na mabaya
Mungu wetu ukawaokoe katika maisha yao na ukawatunze, Yesu Kristo ukawe ndani
yao nao wakawe ndani yako..Jehovah tunaomba ukawafariji  wafiwa
Mungu wetu ukawaguse na kuwapa nguvu na amani moyoni
Ee Baba tunayaweka haya yote mikononi mwako tukiamini  Mungu wetu
yu hai na yote yanawezekana kupitia yeye atutiaye nguvu..
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza
yeye..
Nawapenda.



Ziara ya malkia wa Sheba

(2Nya 9:1-12)

1Malkia wa Sheba aliposikia sifa za Solomoni, kwa sababu ya jina la Mwenyezi-Mungu, alimwendea Solomoni ili kumjaribu kwa maswali magumu. 2Aliwasili akiwa amefuatana na msafara wa watu pamoja na ngamia waliobeba manukato, zawadi nyingi sana na vito vya thamani. 3Naye Solomoni akayajibu maswali yote; hapakuwa na swali lolote lililomshinda. 4Malkia wa Sheba alishangaa sana alipoiona hekima yote ya Solomoni, na nyumba aliyokuwa ameijenga; 5tena alipoona chakula kilicholetwa mezani mwake, jinsi maofisa walivyoketi mezani, jinsi watumishi walivyohudumu na walivyovalia, pia wanyweshaji wake na sadaka za kuteketezwa ambazo alizitoa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, aliduwaa na kushangaa mno.
6Basi, akamwambia mfalme, “Mambo yote niliyosikia nchini kwangu kuhusu kazi zako na hekima yako ni kweli! 7Lakini sikuweza kuamini habari hizo mpaka nilipofika na kujionea mwenyewe. Kumbe sikuambiwa hata nusu yake; hekima yako na fanaka zako vimepita habari nilizopewa. 8Wana bahati wake zako! Wana bahati hawa watumishi wako ambao wanakuhudumia daima na kusikiliza hekima yako! 9Asifiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ambaye amependezwa nawe, akakuweka juu ya kiti cha enzi cha Israeli! Kwa sababu Mwenyezi-Mungu alipenda Israeli milele, amekuweka wewe uwe mfalme, ili udumishe haki na uadilifu.”
10Kisha malkia akampa mfalme zaidi ya kilo 4,000 za dhahabu, kiasi kikubwa cha manukato na vito vya thamani. Manukato kiasi kikubwa kama hicho alichomtolea mfalme Solomoni hakijapata kamwe kuletwa tena.
11Tena, msafara wa meli za Hiramu ulioleta dhahabu kutoka Ofiri, ulileta kwa wingi miti ya msandali na vito vya thamani. 12Naye mfalme aliitumia miti hiyo ya msandali kwa ajili ya nguzo za nyumba ya Mwenyezi-Mungu, na za ikulu na pia kwa kutengenezea vinubi na vinanda vya waimbaji. Kiasi cha miti ya msandali kama hicho hakijaonekana tena mpaka leo.
13Mfalme Solomoni naye alimpatia malkia wa Sheba kila kitu alichotamani na alichotaka; pamoja na vitu vingine ambavyo Solomoni alimpa kutokana na ukarimu wake wa kifalme. Basi malkia akarudi nchini kwake pamoja na watumishi wake.

Utajiri wa mfalme Solomoni

(2Nya 9:13-28)

14Kila mwaka, Solomoni alipelekewa dhahabu kilo 22,000. 15Kiasi hicho si pamoja na dhahabu aliyopata kwa wafanyabiashara na wachuuzi, kwa wafalme wote wa Arabia na wakuu wa mikoa ya Israeli.
16Mfalme Solomoni alitengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa; kila ngao kilo 7 za dhahabu. 17Alitengeneza ngao ndogondogo 300 kwa dhahabu iliyofuliwa, kila ngao kilo 1.5; halafu mfalme akaziweka katika jengo lililoitwa Nyumba ya Msitu wa Lebanoni.
18Vilevile mfalme alitengeneza kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakipaka dhahabu safi kabisa. 19Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita. Sehemu ya juu ilikuwa imeviringwa na kiliwekewa mahali pa kuegemeza mkono pande zake mbili; na sanamu za simba wawili zimesimama moja kando ya mahali hapo pa kuegemeza mkono. 20Kulikuwa pia na sanamu kumi na mbili za simba zimesimama, moja mwishoni mwa kila ngazi. Kiti kama hicho hakijawahi kutengenezwa katika ufalme wowote ule.
21Vyombo vyote vya kunywea divai vya mfalme Solomoni vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vilivyokuwa katika Nyumba ya Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi; hakuna kilichotengenezwa kwa madini ya fedha kwani madini ya fedha haikuthaminiwa kuwa kitu wakati huo. 22Kwa kuwa mfalme Solomoni alikuwa na msafara wa meli za Tarshishi zilizokuwa zikisafiri pamoja na meli za Hiramu, kila mwaka wa tatu meli hizo za Tarshishi zilimletea mfalme dhahabu, fedha, pembe, nyani na tausi.
23Hivyo, mfalme Solomoni aliwapita wafalme wote duniani kwa mali na hekima. 24Watu wa nchi zote walikuwa na hamu ya kumwendea Solomoni ili kusikiliza hekima yake ambayo Mungu10:24 Mungu: Septuaginta: Mwenyezi-Mungu, au Bwana. alikuwa amemjalia. 25Kila mmoja wao alimletea zawadi: Vyombo vya fedha, vya dhahabu, mavazi, manemane,10:25 manemane: Au silaha. manukato, farasi na nyumbu. Zawadi hizi alizipokea kila mwaka.
26Solomoni alikusanya magari ya farasi na wapandafarasi, alikuwa na magari ya farasi 1,400 na wapandafarasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji yenye vituo vya magari ya farasi, na huko Yerusalemu. 27Basi, Solomoni alifanya madini ya fedha katika Yerusalemu kuwa kitu cha kawaida kama mawe, na mbao za mierezi zilikuwa nyingi kama mbao za mikuyu ya Shefela. 28Solomoni aliagiza farasi kutoka Misri, na pia kutoka Kilikia ambako wafanyabiashara wake waliuziwa na watu wa Kilikia. 29Gari moja la kukokotwa liliweza kununuliwa huko Misri kwa fedha ipatayo kilo 7, na farasi mmoja aliweza kugharimu fedha kilo 2. Wafanyabiashara wa mfalme walisafirisha magari na farasi hao na kuwauzia wafalme wote wa Wahiti na wa Wasiria.




1Wafalme10;1-29


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: