Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Monday, 26 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 16...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Haleluyah ni siku nyingine tena Mungu wetu ametuchagua
na kutupa kibali cha kuendelea kuiona leo hii
Si kwa nguvu zetu wala si kwa uwezo wetu,Si kwa kwamba sisi
tumetenda mema sana wala si kwamba sisi ni wazuri mno
Si kwa akili zetu wala utashi wetu sisi kuwa hivi tulivyo leo
Ni kwa rehema/neema zake ni kwa mapenzi yake Mungu wetu
Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa 
majukumu yetu...
Sifa na utukufu tunakurudishia ee Baba wa Mbinguni...!!


Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee. Nao waliposikia habari hizo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, “Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na dunia, bahari na vyote vilivyomo! Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, baba yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: ‘Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure? Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, dhidi ya Bwana na dhidi ya Kristo wake.’


Tazama jana imepita Mungu wetu leo ni siku mpya  na kesho ni 
siku nyingine...
Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
Kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza kuwasamehe
wale wote waliotukosea
Mungu wetu usitutie katika majaribu Baba wa Mbinguni utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Yahweh ukatufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tutape kupona.....


“Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye ulimweka wakfu. Naam, walikutana ili wafanye mambo yale uliyokusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako. Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari. Nyosha mkono wako ili uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu.” Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila woga.



Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika
utendaji Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Jehovah tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhutaji..
Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe...

Mfalme wa amani tunaomba amani yako ikatawale katika 
nyumba/ndoa zetu
Mungu wetu tunaomba ukabariki watoto,wazazi wetu,familia/ndugu
na wote wanaotuzunguka,Yahweh ukatubariki tuingiapo/tutokapo Jehovah tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyo
vimiliki,Mungu wetu tunaomba ukavibariki vyote tunavyoenda kugusa/tumia Yahweh tunaomba ukavitakase na kuvifunika
kwa Damu ya Bwana  wetu Yesu Kristo...
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Mungu wetu tukawe salama rohoni Jehovah tunaomba ukatupe
macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Yahweh ukaonekane katika maisha yetu Mungu wetu popote
tupitapo na ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Jehovah tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako 
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu,Neema yako na Nuru yako ikaangaze
katika maisha yetu,Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe
Neema ya kutambua mema na mabaya ...
Jehovah ukatufanye chombo chema nasi tukatumike kama
inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi...


Jumuiya yote ya waumini ilikuwa na moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo. Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi. Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake. Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita Barnaba (maana yake, “Mtu mwenye kutia moyo”). Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.

Yahweh tazama watoto wako wanaokutafuta/kukuomba kwa
bidii na imani,Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono
wako wenye nguvu Jehovha tunaomba ukawatendee kila mmoja
na hitaji lake Mungu wetu ukaonekane katika shida/tabu zao
Baba wa Mbinguni ukawasamehe wale wote walikwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na
kusimamia neno lako nalo likawaweke huru
Yahweh ukasikie kulia kwao Mungu wetu ukawafute machozi yao
Baba wa Mbinguni amani yako ikatawale katika maisha yao
Jehovah ukawaponye kimwili na kiroho pia Mungu wetu 
tunaomba ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utukufu hata Milele..
Amina...!!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwa nami
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea
Msipungukiwe katika mahitaji yenu Baba wa Mbinguni akawape 
kama inavyompendeza yeye..
Nawapenda.



1Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yehu mwana wa Hanani, dhidi ya Baasha: 2“Wewe Baasha, mimi nilikuinua kutoka mavumbini, nikakufanya kiongozi wa watu wangu Israeli. Wewe umemwiga Yeroboamu, ukawafanya watu wangu Israeli watende dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. 3Haya! Sasa, nitakufutilia mbali wewe na jamaa yako; nitaitendea jamaa yako kama nilivyoitendea jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati. 4Yeyote wa jamaa yako atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.”
5Matendo mengine ya Baasha na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. 6Hatimaye, Baasha alifariki, akazikwa huko Tirza; mwanawe Ela akatawala mahali pake. 7Tena neno la Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha na jamaa yake, lilimjia Yehu mwanawe Hanani kwa sababu ya maovu aliyotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu. Baasha alimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yake; alimwiga Yeroboamu na jamaa yake na kuiletea jamaa yake maangamizi.

Ela, mfalme wa Israeli

8Mnamo mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha, alianza kutawala huko Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka miwili. 9Mtumishi wake Zimri ambaye alisimamia nusu ya kikosi cha magari yake ya kukokotwa, alikula njama juu yake. Siku moja, mfalme Ela alipokuwa huko Tirza nyumbani kwa Arsa aliyekuwa msimamizi wa ikulu, alikunywa, akalewa. 10Basi, Zimri akaingia ndani, akamuua. Kisha akatawala mahali pake. Huu ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda.
11Mara tu alipoanza kutawala, Zimri aliwaua watu wote wa jamaa ya Baasha; hakumwachia hata mwanamume mmoja wa jamaa yake wala wa rafiki zake; 12ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha, kwa njia ya nabii Yehu. 13Mambo haya yalifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda Baasha na mwanawe Ela. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kutenda dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa sanamu za miungu yao. 14Matendo mengine ya Ela, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

Zimri, mfalme wa Israeli

15Zimri alitawala huko Israeli kutoka Tirza kwa muda wa siku saba. Huo ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Basi, watu wa Israeli walikuwa wamepiga kambi kuuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, 16na majeshi ya watu wa Israeli waliposikia kwamba Zimri alikuwa amekula njama, akamuua mfalme, wote wakamtawaza Omri, amiri jeshi wao, kuwa mfalme wa Israeli siku hiyohiyo. 17Omri na majeshi yake akaondoka Gibethoni, akaenda na kuuzingira mji wa Tirza. 18Zimri alipoona kwamba mji umezingirwa, aliingia ngomeni, ndani ya ikulu, akaichoma moto, naye akafia humo. 19Jambo hilo lilifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda alifanya maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. 20Matendo mengine ya Zimri na njama aliyokula, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

Omri, mfalme wa Israeli

21Watu wa Israeli, sasa, waligawanyika makundi mawili: Kundi moja lilimtambua Tibni mwana wa Ginathi kuwa mfalme, na kundi la pili lilimtambua Omri. 22Hatimaye watu wa kundi lililomtambua Omri, wakawazidi nguvu wale waliomtambua Tibni mwanawe Ginathi; Tibni akafa na Omri akawa mfalme. 23Omri alianza kutawala mnamo mwaka wa thelathini na mmoja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na miwili; miaka sita alikuwa anatawala kutoka mjini Tirza. 24Alinunua mlima wa Samaria kwa vipande 6,000 vya fedha kutoka kwa mtu mmoja aitwaye Shemeri, akajenga ngome juu yake, na mji. Mji wenyewe akauita Samaria, kwa heshima ya Shemeri aliyeumiliki mlima huo hapo awali.
25Omri alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; alifanya maovu zaidi ya wale wote waliomtangulia. 26Kwa sababu alimwiga Yeroboamu mwana wa Nebati, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa kuabudu sanamu za miungu. 27Matendo mengine ya Omri na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. 28Hatimaye, Omri alifariki, akazikwa huko Samaria; mwanawe Ahabu akatawala mahali pake.

Ahabu, mfalme wa Israeli

29Mnamo mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri, alianza kutawala Israeli. Alitawala huko Samaria kwa muda wa miaka ishirini na miwili. 30Ahabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kuliko wafalme wote waliomtangulia. 31Tena, licha ya kuiga mwenendo mbaya wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Ahabu alimwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni; akamtumikia na kumwabudu Baali. 32Alimjengea Baali hekalu huko Samaria, na ndani yake akatengeneza madhabahu ya kumtambikia. 33Hali kadhalika, alitengeneza sanamu ya Ashera mungu wa kike. Ahabu alitenda maovu mengi, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu Mungu wa Israeli zaidi ya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. 34Wakati wa utawala wake, Hieli kutoka Betheli, aliujenga upya mji wa Yeriko. Na sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilonena kwa njia ya Yoshua mwana wa Nuni, Hieli alifiwa na mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, wakati wa kuiweka misingi ya Yeriko, akafiwa pia na mwanawe mdogo Segubu, wakati wa kuyaweka malango yake.



1Wafalme16;1-34


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: