Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Tuesday, 27 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 17...



Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Mungu wetu yu mwema sana tumshukuru katika yote..

Mungu wetu, Baba yetu,Muumba wetu,Muumba wa Mbingu na Nchi
Mungu mwenye nguvu,Mungu wa walio hai,Mungu mwenye huruma
Mungu mwenye kuponya,Mungu mwenye kusamehe,Mungu mwenye
Baraka,Mungu wetu ni muweza wa yote,Mungu mwenye Upendo
Mungu wa Abrahamu,Isaka na Yakobo...!!

Asante Mungu wetu kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa Ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwa kutuchagua tena na kutupa kibali cha kuendelea
kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwa tayari kwa majukumu yetu
Sifa na Utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu....


Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika kuungana na Bwana. Sichoki kurudia yale niliyokwisha andika pale awali, maana yatawaongezeeni usalama. Jihadharini na hao watendao maovu, hao mbwa, watu wanaosisitiza kujikata mwilini. Watu waliotahiriwa kikweli ni sisi, si wao; kwani sisi twamwabudu Mungu kwa njia ya Roho wake, na kuona fahari katika kuungana na Kristo Yesu. Mambo ya nje tu hatuyathamini. Mimi pia ningeweza kuyathamini hayo mambo ya nje; na kama yupo mtu anayefikiri kwamba anaweza kuyathamini hayo mambo ya nje, mimi ninayo sababu kubwa zaidi ya kufikiri hivyo:

Jehovah tunakuja mbele zako tukijinyenyekeza,tukijishusha na
kujiachilia mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,kwakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea
Yahweh usitutie majaribuni Mungu wetu tunaomba utuokoe
na yule mwovu na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa Mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi wetu
Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi tupate kupona......

Mimi nilitahiriwa siku ya nane baada ya kuzaliwa kwangu; mimi ni wa taifa la Israeli, kabila la Benyamini, Mwebrania halisi. Kuhusu kuizingatia sheria mimi nilikuwa Mfarisayo, na nilikuwa na bidii sana hata nikalidhulumu kanisa. Kuhusu uadilifu unaopatikana kwa kuitii sheria, mimi nilikuwa bila hatia yoyote. Lakini hayo yote ambayo ningeweza kuyafikiria kuwa ni faida, nimeyaona kuwa ni hasara, kwa ajili ya Kristo. Naam, wala si hayo tu; ila naona kila kitu kuwa ni hasara tupu, kwa ajili ya jambo bora zaidi, yaani kumjua Kristo Yesu Bwana wangu. Kwa ajili yake nimekubali kutupilia mbali kila kitu; nimeyaona hayo yote kuwa ni takataka, ili nimpate Kristo na kuunganishwa naye kabisa. Mimi sitaki tena uadilifu unaotokana na kuitii sheria. Sasa ninao ule uadilifu unaopatikana katika kumwamini Kristo; uadilifu utokao kwa Mungu na ambao unategemea imani. Ninachotaka tu ni kumjua Kristo na kuiona nguvu ya ufufuo wake, kushiriki mateso yake na kufanana naye katika kifo chake, nikitumaini kwamba nami pia nitafufuliwa kutoka kwa wafu.

Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Mungu wetu tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika utendaji
Jehovah nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Mungu wetu tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Yahweh nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki wenye kuhitaji,Baba wa Mbinguni tusipungukiwe katika mahitaji yetu
Mungu wetu ukatupe kama inavyokupendeza wewe....

Mungu wetu tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Baba wa Mbinguni tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,
watoto,wazazi wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatamalaki na kutuatamia
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Yahweh tunaomba ukabariki vyote tunavyoenda kugusa/kutumia
Mungu wetu  ukavitakase na kuvifunika kwa Damu ya Bwana wetu
Yesu Kristo...
Jehovah tukawe salama rohoni Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe
macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuata njia zako
Baba wa Mbinguni tukasimamie Neno lako amri na sheria zako
siku zote za maisha yetu....
Jehovah ukatuguse kwa mkono wako wenye nguvu Mungu wetu
ukaonekane popote tupitapo na ikajulikane kwamba upo
Baba wa Mbinguni,Neema yako na Nuru yako ikaangaze katika maisha yetu,Ukatufanye chombo chema ee Mungu wetu nasi tukatumike
kama inavyokupendeza wewe..
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na kutawe na kiasi....

Sijidai kwamba nimekwisha faulu au nimekwisha kuwa mkamilifu. Naendelea kujitahidi kupata lile tuzo ambalo kwalo Kristo amekwisha nipata mimi. Ama kweli, ndugu zangu, sidhani kuwa nimekwisha pata tuzo hilo; lakini jambo moja nafanya: Nayasahau yale yaliyopita na kufanya bidii kuyazingatia yale yaliyo mbele. Basi, nimo mbioni kuelekea lengo langu, ili nipate lile tuzo, ambalo ni mwito wa Mungu kwa maisha ya juu kwa njia ya Kristo Yesu. Sisi sote tuliokomaa tunapaswa kuwa na msimamo huohuo. Lakini kama baadhi yenu wanafikiri vingine, basi, Mungu atawadhihirishieni jambo hilo. Kwa vyovyote, tusonge mbele katika njia hiyohiyo ambayo tumeifuata mpaka hivi sasa. Ndugu zangu, fuateni mfano wangu. Tumewapeni mfano mwema, na hivyo wasikilizeni wale wanaofuata mfano huo. Nimekwisha waambieni jambo hili mara nyingi, na sasa narudia tena kwa machozi: Watu wengi wanaishi kama maadui wa msalaba wa Kristo. Mwisho wao ni kuangamia, kwani tumbo lao ndilo mungu wao; wanaona fahari juu ya mambo yao ya aibu, hufikiria tu mambo ya kidunia. Lakini sisi ni raia wa mbinguni, na twatazamia kwa hamu kubwa Mwokozi aje kutoka mbinguni, Bwana Yesu Kristo. Yeye ataibadili miili yetu dhaifu na kuifanya ifanane na mwili wake mtukufu, kwa nguvu ile ambayo kwayo anaweza kuviweka vitu vyote chini ya utawala wake.

Yahweh tunawaweka mikononi mwako wenye shida/tabu,wagonjwa,
wenye njaa,wanaopitia magumu/majaribu mbalimbali,waliokataliwa,
waliokata tamaa,wenye hofu na mashaka,walio katika vifungo vya yule
mwovu,walio magerezani pasipo na hatia,waliokwama kibiashara,
waliokwama kimasomo,wanaotafuta kazi,wafiwa ukawe mfariji wao,
Na wote wanaokutafuta kwa bidii na imani Mungu wetu tunaomba
ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu,Yahweh ukawaponye kimwili
na kiroho pia,Mungu wetu ukabariki mashamba yao na vyanzo vyao
Yahweh ukawape ubunifu na maarifa katika maisha yao,
Mungu wetu ukawaweke huru na haki ikatendeke,Baba wa Mbinguni
ukaonekane na ukawatendee kila mmoja kwa hitaji lake
Jehovah ukawasamehe pale walipokwenda kinyume nawe
Mungu wetu ukawape neema ya kujiombea,kufuata njia zako na 
kusimamia Neno lako nalo likawaweke huru
Neema yako ikawe nao baraka na amani vikatawale katika
maisha yao,Yahweh Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Baba wa Mbinguni tunaomba ukasikie,ukapokee sala/maombi yetu
Mungu wetu ukawatendee sawasawa na mapenzi yako
kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na Utufu hata Milele..
Amina..!!

Wapendwa katika Kristo Yesu asanteni sana kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza yeye,Amani ya Kristo Yesu ikawe nanyi daima..
Nawapenda.





Ukame: Ujumbe wa Mungu watekelezwa

1Basi Elia wa kijiji cha Tishbe huko Gileadi, akamwambia mfalme Ahabu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli aliye hai ambaye mimi ninamtumikia: Hakutakuwa na umande wala mvua mpaka nitakapotoa amri.” 2Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Elia: 3“Ondoka hapa uelekee mashariki, ukajifiche penye kijito cha Kerithi kilichoko mashariki ya mto Yordani. 4Huko, utapata maji ya kunywa katika kijito hicho tena nimewaamuru kunguru wakuletee chakula.” 5Basi, Elia akatii agizo la Mwenyezi-Mungu, akaenda kukaa kwenye kijito cha Kerithi kilichoko mashariki ya mto Yordani. 6Kunguru wakawa wanamletea mkate na nyama, asubuhi na jioni; akapata na maji ya kunywa katika kijito hicho. 7Lakini, baada ya siku chache kijito kikakauka kwa sababu hapakunyesha mvua nchini.

Elia na mama mjane wa Sarefathi

8Hapo, neno la Mwenyezi-Mungu, lilimjia Elia: 9“Ondoka uende mjini Sarefathi, karibu na Sidoni, ukae huko. Nimemwamuru mwanamke mmoja mjane akupatie chakula huko.” 10Basi, Elia akaondoka, akaenda Sarefathi. Alipofika penye lango la mji, alimkuta mwanamke mmoja mjane anaokota kuni. Elia akamwita mwanamke huyo na kumwambia “Niletee maji ninywe.” 11Yule mwanamke alipokuwa anaondoka, Elia akamwita tena na kumwambia, “Niletee na kipande cha mkate pia.” 12Huyo mwanamke akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, sina mkate hata kidogo. Nilicho nacho ni konzi ya unga katika chungu na mafuta kidogo katika chupa. Nimefika hapa kuokota kuni, kisha niende nyumbani kupika chakula hicho, mwanangu na mimi tule, kisha tufe.” 13Elia akamwambia, “Usiogope. Nenda ukafanye kama ulivyosema. Lakini nitengenezee mimi kwanza na kuniletea andazi dogo, kisha jitengenezee wewe na mwanao chakula. 14Maana, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Unga ulioko chunguni mwako hautapungua wala mafuta yaliomo ndani ya chupa hayataisha, mpaka hapo mimi Mwenyezi-Mungu nitakaponyesha mvua nchini.’” 15Basi, huyo mwanamke mjane akaenda akafanya kama alivyoambiwa na Elia hata mama huyo, jamaa yake na Elia wakapata chakula kwa siku nyingi. 16Unga chunguni haukupunguka, wala mafuta katika chupa hayakwisha sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilomwambia Elia aseme.

Elia anamfufua mtoto wa mama mjane

17Baada ya hayo, mwana wa mwanamke huyo mwenye nyumba akaugua, na hali yake ikazidi kuwa mbaya, hata mwishowe akafariki. 18Huyo mwanamke akamwambia Elia, “Ewe mtu wa Mungu, una kisa gani nami? Kumbe ulikuja kwangu kuzifichua dhambi zangu na kusababisha kifo cha mwanangu?” 19Elia akamwambia, “Nipe mwanao.” Basi, Elia akamtwaa mtoto kifuani pa mama yake, akamchukua juu chumbani mwake, akamlaza juu ya kitanda chake. 20Kisha akamsihi Mwenyezi-Mungu akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, je, hata mwanamke huyu mjane ambaye ninakaa kwake, naye ananitunza, unamletea balaa kwa kumwua mwanawe?” 21Kisha Elia akajinyosha juu ya mtoto huyo mara tatu na kumwomba Mwenyezi-Mungu, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, mrudishie mtoto huyu roho yake!” 22Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi la Elia; mtoto akaanza kupumua tena. 23Elia akamrudisha mtoto chini kwa mama yake, akamwambia, “Tazama! Mwanao yu hai.” 24Huyo mwanamke mjane akamwambia Elia, “Sasa najua kwa hakika kwamba wewe ni mtu wa Mungu, na maneno aliyokupa Mwenyezi-Mungu uyaseme ni ya kweli.”




1Wafalme17;1-24


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: