Swahili na Waswahili

Swahili na Waswahili
Waswahili na Mswahili Rachel Siwa...Pamoja Daima!!

Wednesday, 28 March 2018

Kikombe Cha Asubuhi ;1 Wafalme 18...




Shalom,Habari za Asubuhi,Hamjambo,Mmeamkaje?

Tumshukuru Mungu wetu katika yote...

Asante Baba wa Mbinguni kwa wema na fadhili zako kwetu
Asante kwa ulinzi wako kwetu wakati wote
Asante kwakutuchagua tena na kutupa kibali cha 
kuendelea kuiona leo hii
Asante kwa pumzi/uzima,afya na kuwatayari kwa majukumu yetu
Utukuzwe ee Baba wa  Mbinguni,Unastahili sifa Mungu wetu
Unastahili kuabudiwa Jehovah,Unastahili kuhimidiwa Yahweh
Matendo yako ni makuu sana,Matendo yako ni ya ajabu,
Matendo yako ni ya kutisha,Neema yako yatutosha Mungu wetu
Sifa na utukufu tunakurudishia ee Mungu wetu...!!



Hapo mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu. Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu. Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye. Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu. Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.


Tazama jana imepita Baba wa mbinguni leo ni siku mpya Jehovah
kesho ni siku nyingine Mungu wetu
Yahweh tunaomba utusamehe dhambi zetu zote tulizozifanya
kwakuwaza,wakunena,kwakutenda,kwakujua/kutojua
Baba wa Mbinguni nasi tunaomba utupe neema ya kuweza
kuwasamehe wale wote waliotukosea
Mungu wetu usitutie majribuni Yahweh utuokoe na yule mwovu
na kazi zake zote
Jehovah tunaomba ututakase miili yetu na akili zetu
Baba wa mbinguni utufunike kwa Damu ya Bwana na Mwokozi
wetu Yesu Kristo wa Nazareti yeye aliteseka kwanza ili sisi
tupate kupona,kwakupigwa kwakwe sisi tumepona


Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane, ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini. Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote. Basi, Neno alikuwako ulimwenguni, na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua. Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea. Lakini wale waliompokea, wale waliomwamini, aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu, ambao walizaliwa si kwa maumbile ya kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala mapenzi ya mtu, bali kutokana na Mungu mwenyewe.

Mungu wetu tunaomba ukabariki kazi za mikono yetu
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe ubunifu na maarifa katika
utendaji,Mungu wetu nasi tukatende sawasawa na mapenzi yako
Yahweh tunaomba ukabariki ridhiki zetu ziingiazo/zitokazo
Mungu wetu nasi tunaomba ukatupe neema ya kuweza kuwabariki
wenye kuhitaji
Jehovah tusipungukiwe katka mahitaji yetu Mungu wetu ukatupe
kama inavyokupendeza wewe....

Mfalme wa amani tunayaweka maisha yetu mikononi mwako
Mungu wetu tunaomba ukabariki nyumba/ndoa zetu,watoto,wazazi
wetu,familia/ndugu na wote wanaotuzunguka
Yahweh tunaomba ulinzi wako kwetu na kwa vyote tunavyovimiliki
Mungu wetu tunaomba ukatubariki tuingiapo/tutokapo
Jehovah ukatamalaki na kutuatamia Mungu wetu tukawe salama rohoni
Baba wa Mbinguni tunaomba ukatupe macho ya kuona na masikio ya kusikia sauti yako na kuitii
Mungu wetu tunaomba ukatupe neema ya kufuta njia zako Yahweh
tukasimamie Neno lako amri na sheria zako siku zote za maisha yetu
Jehovah ukaonekane katika maisha yetu popote tupitapo na 
ikajulikane kwamba upo Baba wa Mbinguni
Yahweh ukatuguse na mkono wako wenye nguvu Mungu wetu amani
yako ikatawale katika maisha yetu,furaha na upendo ukadumu
kati yetu Baba wa Mbunguni ukatufanye chombo chema Mungu wetu
nasi tukatumike kama inavyokupendeza wewe
Roho Mtakatifu akatuongoze katika yote na tukawe na kiasi....



Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli. Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, “Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: ‘Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.’” Kutokana na ukamilifu wake sisi sote tumepokea neema kupita neema. Maana Mungu alitoa sheria kwa njia ya Mose, nayo neema na kweli vimetujia kwa njia ya Yesu Kristo. Hakuna mtu aliyemwona Mungu kamwe. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.

Yahweh tunawaweka mikononi mwako watoto wako 
wanaokutafuta/kukuomba kwa bidii na imani
Mungu wetu tunaomba ukawaguse kwa mkono wako wenye nguvu
Baba wa Mbinguni ukawatendee kila mmoja kwa hitaji lake
Jehovah ukaonekane katika maisha yao Mungu wetu ukawasamehe
pale walipokwenda kinyume nawe Yahweh ukawape neema
ya kujiombea kufuata njia zako na kusimamia Neno lako
nalo likawaweke huru,Neema na Nuru yako ikaangaze katika maisha yao
Baba wa Mbinguni ukasikie kulia kwao Mungu wetu ukawafute machozi
yao Yahweh ukawabariki na kuwatendea sawasawa na mapenzi yako
Kwakuwa Ufalme ni wako Nguvu na utukufu hata Milele...
Amina....!

Asanteni sana wapendwa katika Kristo Yesu kwakuwanami/kunisoma
Mungu Baba aendelee kuwabariki na kuwatendea kama inavyompendeza
yeye,Amani ya Bwana wetu Yesu  Kristo na upendo
wa Mungu Baba vikawe nanyi Daima.....
Nawapenda.

Elia amkabili mfalme na manabii wa Baali

1Ikawa baada ya siku nyingi, mnamo mwaka wa tatu wa ukame, neno hili la Mwenyezi-Mungu likamjia Elia: “Nenda ukajioneshe kwa mfalme Ahabu, halafu nitanyesha mvua nchini.” 2Basi, Elia akaenda kujionesha kwa Ahabu.
Wakati huo, njaa ilikuwa kali sana huko Samaria. 3Basi, Ahabu akamwita Obadia msimamizi wa ikulu. (Obadia alikuwa mtu amchaye Mwenyezi-Mungu sana, 4na wakati Yezebeli alipowaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, Obadia aliwachukua manabii 100, akawaficha hamsinihamsini pangoni, akawa anawapelekea chakula na maji). 5Kisha, Ahabu akamwambia Obadia, “Labda tutapata majani na hapo tutawaokoa baadhi ya farasi na nyumbu wetu.” 6Basi, wakagawana nchi ili wapate kuipitia yote; Ahabu akaenda upande mmoja na Obadia upande mwingine.
7Obadia alipokuwa njiani, alikutana na Elia; naye Obadia alipomtambua Elia, aliinama chini na kusema, “Kumbe! Ni wewe bwana wangu Elia?” 8Elia akamwambia, “Naam! Ni mimi Elia. Nenda ukamwambie bwana wako kwamba niko hapa.”
9Obadia akasema, “Nimekosa nini hata utake kunitia hatarini ili niuawe na mfalme Ahabu? 10Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu, Mungu wako aliye hai, kwamba mfalme amekuwa akikutafuta duniani kote. Na mfalme yeyote akisema kwamba hujaonekana huko, Ahabu alimtaka huyo mfalme aape na watu wake kwamba kweli hupo. 11Na sasa, wataka niende kumwambia kwamba wewe uko hapa! 12Ninahofia kwamba mara nitakapoondoka, Roho ya Mwenyezi-Mungu itakunyakua na kukupeleka mahali nisipopajua! Nikienda kumwambia Ahabu kwamba uko hapa, naye akikutafuta asikupate, ataniua mimi, ingawaje mimi mtumishi wako nimemcha Mwenyezi-Mungu tangu ujana wangu. 13Je, huna habari kwamba Yezebeli alipokuwa akiwaua manabii wa Mwenyezi-Mungu, mimi niliwaficha manabii 100, watu hamsinihamsini pangoni, nikawa nawapa chakula na maji? 14Sasa waniambia ati niende kumwambia bwana wangu kwamba wewe Elia uko hapa! Ahabu ataniua.” 15Elia akamwambia, “Nakuapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa Majeshi, aishivyo ambaye ninamtumikia: Leo hii nitajitokeza mbele ya mfalme.”
16Basi, Obadia akaenda kwa mfalme Ahabu, akampa habari hizo. Naye Ahabu akaenda kukutana na Elia. 17Ahabu alipomwona Elia, alisema, “Kumbe kweli ni wewe, mtaabishaji wa Israeli?” 18Elia akamjibu, “Mtaabishaji wa Israeli si mimi, bali ni wewe na jamaa ya baba yako. Nyinyi mmekiuka amri za Mwenyezi-Mungu na kuabudu Mabaali. 19Sasa, uwakusanye watu wote wa Israeli mbele yangu huko mlimani Karmeli. Hali kadhalika, wakusanye wale manabii 450 wa Baali, na manabii 400 wa Ashera mungu wa kike, ambao huhifadhiwa na malkia Yezebeli.”
20Basi, Ahabu akawaita watu wote wa Israeli, akawakusanya na manabii wote kule mlimani Karmeli. 21Kisha, Elia akawakaribia watu hao, akawaambia, “Mtasitasita na kuyumbayumba mioyoni mpaka lini? Ikiwa Mwenyezi-Mungu, ndiye Mungu mfuateni; lakini ikiwa Baali ni Mungu, basi, mfuateni yeye.” Lakini watu hawakumjibu neno lolote. 22Hapo, Elia akawaambia, “Mimi tu ndiye peke yangu nabii wa Mwenyezi-Mungu niliyebaki, lakini manabii wa Baali wapo 450. 23Haya! Leteni fahali wawili; manabii wa Baali wajichagulie fahali mmoja, wamchinje, wamkate vipandevipande na kumweka juu ya kuni, bila kuwasha moto. Nami pia nitamtwaa huyo fahali mwingine, nitamchinja na kumweka juu ya kuni bila kuwasha moto. 24Kisha, wao watamwomba mungu wao, nami nitamwomba Mwenyezi-Mungu. Mungu atakayejibu kwa kuleta moto, huyo ndiye Mungu wa kweli.” Na hapo umati wote ukasema, “Naam! Na iwe hivyo.”
25Kisha, Elia akawaambia manabii wa Baali, “Nyinyi ni wengi; basi anzeni. Jichagulieni fahali, mtayarisheni na kumwomba mungu wenu, lakini msiwashe moto.” 26Hao manabii wakamtwaa fahali wao waliyepewa, wakamtayarisha, kisha wakaanza kumlilia Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakirukaruka na kuyumbayumba kuizunguka madhabahu waliyotengeneza wakisema: “Ee Baali, utusikie!” Lakini hapakutokea sauti yoyote, wala hakuna aliyewajibu.
27Ilipofika saa sita mchana, Elia akaanza kuwadhihaki akisema, “Ombeni kwa sauti kubwa zaidi! Yeye ni mungu ati! Huenda ikawa amezama katika mawazo yake, amekwenda haja, au yumo safarini! Labda amelala, mnapaswa kumwamsha!” 28Manabii hao wakapiga kelele zaidi, wakajikatakata kwa visu na simi, kufuatana na desturi yao, hata wakabubujika damu. 29Wakaendelea kupiga makelele na kufanya kama wendawazimu hadi alasiri wakati wa kutoa tambiko; lakini hakuna aliyewajibu wala kuwajali.
30Basi, Elia akawaambia watu, “Sogeeni karibu nami.” Wao wakamkaribia. Kisha Elia akaijenga upya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu iliyokuwa imebomolewa. 31Alitwaa mawe kumi na mawili, hesabu ya makabila kumi na mawili yaliyopewa majina ya wana wa Yakobo ambaye Mwenyezi-Mungu alimwambia “Jina lako litakuwa Israeli.” 32Kwa mawe hayo, Elia alimjengea Mwenyezi-Mungu madhabahu, akachimba na mtaro kuizunguka madhabahu hiyo; mtaro uwezao kuchukua kama debe moja na nusu la nafaka. 33Kisha akapanga kuni vizuri, akamkata vipandevipande yule fahali, akaviweka juu ya kuni. Kisha akawaambia watu, “Jazeni mitungi minne maji mkaimwagie tambiko hii ya kuteketezwa pamoja na kuni.” Wakafanya hivyo. 34Kisha akawaambia, “Rudieni tena.” Nao wakafanya hivyo mara ya pili. Naye akawaambia, “Fanyeni hivyo tena mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo. 35Maji yakatiririka chini pande zote za madhabahu, hata yakajaa mtaroni.
36Mnamo alasiri, wakati wa kutoa tambiko, nabii Elia aliikaribia madhabahu, akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, waoneshe watu leo hii kwamba wewe ndiwe Mungu wa Israeli, na kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya kwa amri yako. 37Unijibu, ee Mwenyezi-Mungu; unijibu ili watu hawa wajue kuwa wewe Mwenyezi-Mungu ndiwe Mungu, na kwamba umeigeuza mioyo yao wakurudie.” 38Mara, Mwenyezi-Mungu akashusha moto, ukaiteketeza tambiko hiyo ya kuteketezwa, kuni, mawe na vumbi, na kuyakausha maji yote mtaroni. 39Watu walipoona hivyo, walianguka kifudifudi na kusema, “Mwenyezi-Mungu, ni Mungu; Mwenyezi-Mungu, ni Mungu!”
40Ndipo Elia akawaambia, “Wakamateni manabii wote wa Baali. Msimwache hata mmoja wao atoroke!” Basi, watu wakawakamata wote, naye Elia akawapeleka mtoni Kishoni, akawaulia huko.

Mwisho wa ukame

41Baada ya hayo, Elia akamwambia mfalme Ahabu, “Nenda ukale na kunywa. Nasikia kishindo cha mvua.” 42Basi, Ahabu akaenda zake kula na kunywa; naye Elia akapanda juu ya kilele cha mlima Karmeli, na huko akainama hadi chini na kuuweka uso wake katikati ya magoti yake. 43Kisha akamwambia mtumishi wake, “Sasa, nenda utazame upande wa baharini.” Mtumishi akaenda, akatazama, kisha akarudi akasema, “Hamna kitu.” Elia akamwambia, “Nenda tena mara saba.” 44Mara ya saba, huyo mtumishi akarudi, akasema, “Naona wingu dogo kama mkono wa mtu linatoka baharini.” Elia akamwambia, “Nenda umwambie mfalme Ahabu atayarishe gari lake la kukokotwa, ateremke, asije akazuiliwa na mvua.”
45Muda haukupita mrefu mbingu zikatanda mawingu mazito, upepo ukavuma, pakanyesha mvua kubwa. Ahabu naye akapanda gari lake la kukokotwa, akarudi Yezreeli. 46Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Elia, naye akajifunga na kukaza joho lake, akakimbia na kumtangulia Ahabu kuingia mjini Yezreeli.



1Wafalme18;1-46


Biblia Habari Njema kwa Watu Wote(BHN)

"Swahili Na Waswahili"Mbarikiwe.

No comments: